Rafiki yangu mpendwa,

Vipo vikwazo viwili vikubwa kwenye ukuaji wa biashara. Vikwazo hivyo ni fedha na rasilimali watu. Biashara nyingi zinashindwa kukua na hata nyingine kufa kwa sababu uwekezaji wa fedha haufanyiki kwenye biashara hizo. Pia pale ambapo kunakosekana rasilimali watu, biashara haiwezi kukua.

Pamoja na umuhimu wa rasilimali watu kwenye ukuaji wa biashara, watu hao huwa wanakuja na changamoto zao ambazo usipokuwa makini zinaweza kupelekea biashara kufa.

Kwa mfano pale unapoajiri watu ambao siyo waaminifu, wanapelekea biashara kufa. Pia kama watu utakaowaajiri watakuwa hawajitumi, ni wazembe na wavivu, watarahisisha sana kuiua biashara yako.

Swali ni je unawezaje kuajiri wafanyakazi ambao ni waaminifu na wanaojituma kwenye majukumu yao? Hili ndiyo tunakwenda kujifunza leo kwenye makala hii ya changamoto.

Msomaji mwenzetu Ephraim, alituandikia hivi kuhusiana na changamoto hii;

Changamoto kubwa ni kupata msimamizi wa biashara ambaye anaweza kufanya kazi kwa uaminifu na kwa juhudi. Wengi wanakuwa siyo waaminifu. – Ephraim M. K.

Zoezi la kuajiri siyo rahisi, ili uweze kuwapata watu sahihi, lazima utapita kwa watu wengi ambao siyo sahihi.

Yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia kwenye kuajiri ili kuweza kupata wasaidizi waaminifu na wanaojitua.

  1. Chukua ushauri wa Warren Buffet.

Warren Buffet, bilionea mwekezaji na mmoja wa matajiri wakubwa sana duniani, anasema unapoajiri angalia vitu vitatu, UADILIFU, AKILI NA NGUVU. Lakini kama mtu hana hicho cha kwanza, basi hivyo viwili vitakumaliza. Na yupo sahihi sana, mfanyakazi unayemwajiri anapaswa kuwa mwadilifu, anapaswa kuwa na akili kuhusiana na kazi anayokwenda kufanya na pia anahitaji kuwa na nguvu. Lakini kama uadilifu haupo, akili na nguvu vitatumika vibaya na biashara yako itaumia.

Angalia sana tabia binafsi za mtu kabla hata hujamwajiri. Kama kuna hali ya kukosekana kwa uadilifu kwa mtu, achana naye mara moja. Usijidanganye kwamba mtu atabadilika, hata kama anakuambia atabadilika. Tabia huwa hazibadiliki kirahisi, utaishia kuumia.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

  1. Angalia vitu vingine ambavyo mtu amewahi kufanya kwenye maisha yake, bila ya kutumwa au kusimamiwa.

Kila mtu akitumwa au kusimamiwa kufanya kitu, anaweza kufanya. Lakini kuna watu ambao huwa wanafanya vitu vikubwa kwa maamuzi yao wenyewe. Hawa ndiyo watu unaowahitaji sana kwenye biashara yako, kwa sababu hawahitaji kusukumwa sana ili kutimiza majukumu yao.

Unapoajiri, angalia mtu amewahi kufanya nini kwenye maisha yake ambacho ni msukumo kutoka ndani yake mwenyewe. Labda kuna mradi wowote ambao amewahi kufanya, hiyo inakupa picha kwamba ni mtu wa kujituma.

  1. Jua msukumo wa mtu kutaka kazi, ukiacha fedha.

Kama mtu unayemwajiri anachoangalia ni fedha pekee, atakuingiza kwenye matatizo. Unahitaji mtu ambaye anaangalia zaidi ya fedha. Ndiyo fedha ni muhimu na lazima mtu apate, lakini pia mtu anapaswa kuwa na msukumo mwingine ndani yake ukiacha fedha pekee.

Ukipata mtu anayependa ile aina ya biashara unayoifanya, itakuwa rahisi sana kwako kwa sababu atafanya kwa moyo. Kama mtu hapendi ile biashara unayofanya, achana naye.

Na hii pia inaenda kwa matumizi, kama mtu anapingana na biashara unayofanya au haiamini, usimwajiri. Kama unauza pombe, huhitaji kuajiri mtu ambaye anapinga kabisa matumizi ya pombe. Kwa sababu atafukuza wateja kwa kujua au kutokujua.

SOMA; Mitazamo Hii Mitano (05) Kuhusu Kipato Ndiyo Inakufanya Uingie Kwenye Matatizo Ya Kifedha, Ijue Na Hatua Za Kuchukua Ili Kuondoka Kwenye Umasikini.

  1. Majukumu ya kazi yawe yanaeleweka na yanapimika.

Kitu kingine muhimu sana kwenye kuajiri ni kuhakikisha mtu anakuwa na majukumu yake ya kazi yanayoeleweka na yanayopimika. Hii itakuwa rahisi kwako kupima ufanisi wake na kujua kama anatimiza kile anachopaswa kutimiza au la.

Mtu anapoyajua majukumu yake, anawajibika kwa majukumu hayo. Lakini kama mtu hana majukumu maalumu, atakazana kukwepa kila majukumu yanayojitokeza.

  1. Kuwa tayari kulipa vizuri.

Kosa kubwa sana ambalo wengi wanafanya kwenye kuajiri ni kutafuta watu ambao watawalipa fedha kidogo. Na kama ilivyo kwenye maisha, unapata kile unacholipia. Kama upo tayari kulipa mshahara kidogo, utapata watu ambao wapo tayari kupokea mshahara kidogo, ambao pia siyo bora kwenye ufanyaji wa kazi.

Ili kupata wachapaji wazuri wa kazi, lazima uwe tayari kulipa fedha ya juu kidogo. Hapo utapata wanaojituma, na hata mtu anapolipwa kiasi cha juu, yeye mwenyewe atajisukuma kufanya zaidi kwa sababu anajua siyo sehemu nyingi ataweza kulipwa vizuri kama unavyomlipa wewe.

Muhimu sana rafiki ni unapoajiri ni sawa na wewe unakuwa mlezi, hivyo wale unaowaajiri unawalea kwenye kukuza biashara yako. Hivyo lazima uwe nao karibu, lazima ujue nini kinaendelea kwenye maisha yao na pia uwasaidie kutatua changamoto mbalimbali wanazokutana nazo kwenye kuiendesha biashara yako.

Na mwisho, upo msingi muhimu sana kwenye kuajiri ambao unaitwa AJIRI TARATIBU, FUKUZA HARAKA. Watu wengi wamekuwa wanafanya kosa la kuajiri haraka pale wanapokutana na mtu, lakini wakigundua hafanyi vizuri, inawachukua muda sana kuwafukuza, wanawapa muda wakiamini watabadilika. Mwandishi mmoja amewahi kusema, wanaoua biashara yako siyo wale unaowafukuza, bali wale unaowaacha kwenye biashara yako. hivyo fuata msingi huo, ajiri taratibu, mfuatilie mtu kwa muda kabla hujamwajiri. Na baada ya kuajiri, kama mtu umegundua hafai kwenye biashara yako, unahitaji kumfukuza mara moja. Kwa sababu kadiri unavyomwacha kwenye biashara yako, ndivyo anavyozidi kutengeneza madhara makubwa kwenye biashara hiyo.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog