Rafiki yangu mpendwa,

Moja ya maeneo muhimu sana ya biashara ni mauzo. Mauzo ndiyo yanaendesha biashara kwa sababu ndiyo yanaingiza fedha kwenye biashara.

Unaweza kuwa na bidhaa au huduma nzuri sana, lakini kama hutaweza kuwashawishi watu kununua, hutaweza kudumu kwenye biashara kwa muda mrefu.

Moja ya ujuzi muhimu ambao kila mtu anapaswa kuwa nao ili kufanikiwa kwenye maisha, ni ujuzi wa kuuza. Kwa sababu kila kitu kwenye maisha yetu ni kuuza, hivyo anayeweza kuuza vizuri ndiye anayepata chochote anachotaka.

Leo nakwenda kukushirikisha njia moja ya uhakika ya kuwashawishi wateja kununua chochote unachouza.

Kwanza nianze kwa kusema siyo njia ulizozoea, kwa sababu kwa zama tunazoishi sasa, njia ambayo wengi wamezoea ni ya kupiga kelele. Kwa sababu kuna watu wengi wanafanya biashara kama ambayo unafanya, njia pekee unayoona rahisi kutumia ni kupiga kelele. Hivyo matangazo yanakuwa mengi sana hasa kwenye mitandao ya kijamii.

Hakuna kosa ambalo wengi wanafanya kama kuwasukumia watu matangazo ya kile wanachofanya. Mtu anaweza kutuma picha nyingi sana za matangazo ya biashara yake akiamini ndiyo njia sahihi ya kuwafikia wateja na kuwafanya wateja wajue yupo. Njia hii inaweza kufanya kazi kwa muda, lakini baadaye kelele zinakuwa nyingi na wateja wanaacha kusikiliza na hata imani yao inapungua.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

Njia nyingine rahisi ambayo wengi wameizoea ni kupunguza bei. Kama wengine wanauza bei fulani basi yeye anashusha na kuuza bei ya chini zaidi. Hilo linawafanya baadhi ya wateja kwenda kununua kwa anayeuza kwa bei ya chini. Lakini njia hii pia huwa ina matatizo yake, tena makubwa. Kwanza unapunguza faida, kitu ambacho kinakupa kazi zaidi kwa malipo kidogo. Pili wengine nao wakiamua kushusha bei utalazimika kushusha zaidi na hapo unaumia zaidi. Na tatu, unapotumia kigezo cha bei rahisi kupata wateja, unapata wateja wanaoangalia bei tu, na siyo kile unachowapa.

Hivyo rafiki, ipo njia moja ya uhakika ya kuwashawishi wateja kununua chochote unachotaka, na ambayo haina madhara kwako wala kwa biashara yako.

Njia hiyo ni kutoa thamani kubwa kuliko mteja anavyotegemea au anavyolipia.

Kama unauza kitu kwa shilingi elfu 10, basi mfanye mteja aone anapata thamani ya shilingi elfu 20. Kwa njia hii, mteja atasukumwa kununua kwa sababu anajua ni kama unampa fedha, yaani kwake yeye ni kama unampa elfu kumi kila anapokuja kwenye biashara yako.

Unapotoa thamani zaidi, unawavutia wateja wanaijali kuhusu thamani na ile biashara unayofanya, na hawa huwa ni wateja bora na waaminifu.

Pia unapotoa thamani zaidi unajitofautisha na wengine na hivyo kujiondoa kwenye ushindani usio na maana. Mteja hatajiuliza mara mbili kwamba anunue wapi, atakuja kwako moja kwa moja kwa sababu anajua atapata thamani kubwa.

Swali ni je unawezaje kutoa thamani zaidi kwenye biashara yako?

Watu wengi huwa wanauliza na kujiuliza swali hili, na wengi huona ni vigumu sana kutoa thamani zaidi kwenye biashara za kawaida ambazo kila mtu anafanya.

Hilo siyo kweli, kwenye kila biashara, kuna nafasi kubwa ya kutoa thamani zaidi kwa wateja.

Lakini ili uweze kutoa thamani zaidi, lazima kwanza uache uvivu, lazima uache kufanya biashara kwa mazoea na lazima ufurahie kutatua matatizo ya wateja wako na siyo kufurahi pale ambapo mteja hana matatizo.

Ili kuongeza thamani zaidi kwa wateja wako, zingatia haya muhimu sana;

  1. Jua tatizo kubwa la wateja wako ambalo biashara yako inatatua, na jua ni kwa jinsi gani biashara hiyo inatatua tatizo la wateja wako. Hii itakuwezesha kuboresha zaidi kile unachofanya ili kutatua matatizo ya wateja kwa ubora zaidi.
  2. Beba jukumu la kutatua matatizo ya wateja wa biashara yako, mteja anapokuja kwako, mfanye kuwa jukumu lako. Usitafute njia ya kukwepa au kuyakataa matatizo yake, badala yake yamiliki matatizo hayo, mfanye mteja ajione ametua mzigo mkubwa wa matatizo yake kwa kufika kwenye biashara yako.
  3. Jali sana kuhusu biashara yako na wateja wako, kuwa tayari kwenda hatua ya ziada katika kutoa huduma bora kabisa kwa wateja wako. Kuwa na msukumo ndani yako wa kufanya zaidi ili kuhakikisha mteja ametatua tatizo lake.
  4. Mpe mteja uhakika wa kile unachomuuzia, mfanye ajisikie kwamba amepata suluhisho na siyo kupoteza fedha zake. Siku zote kutoa fedha kunauma, kwa sababu unapotoa fedha na kulipia kitu, maana yake huna tena fedha hizo kwa matumizi mengine. Jua mteja wako ana matumizi mengine ya fedha zake, hivyo lazima umpe uhakika kwamba atakuwa hajafanya makosa kununua kile unachouza. Na hata kama atapata changamoto, upo tayari kumsaidia na siyo kwamba anakuwa amepoteza fedha zake na hajatatua tatizo lake.
  5. Toa huduma bora sana kwa wateja wako, hichi ndiyo kinaweza kukutofautisha na wengine wote ambao mnafanya biashara zinazofanana. Mfanye mteja ajisikie wa kipekee kufanya biashara na wewe, mpe huduma ambazo hajawahi kupata pengine na mfanye akienda kununua sehemu nyingine ajisikie kuna kitu anakosa, na hivyo kurudi kununua kwako.

Rafiki, kila unapoongeza thamani zaidi kwenye biashara yako, unawafanya wateja wawe tayari kununua zaidi chochote unachouza. Thamani inavyokwenda juu, ndivyo imani ya wateja kwako inakuwa kubwa na utayari wa kununua unakuwa mkubwa zaidi.

Kumbuka wateja wanasukumwa kununua pale wanapoamini na wanapoona wanapata zaidi ya wanacholipia. Hivyo weka kazi katika kujenga imani ya wateja kwako na kutoa thamani zaidi, na hutateseka kutafuta wateja, hutahitaji kupiga kelele na hutafikiria kupunguza bei ili kupata wateja zaidi.

Rafiki, kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018 itakayofanyika tarehe 03/11/2018 tutakwenda kujifunza misingi muhimu sana ya kuanzisha na kukuza biashara yako. Pia tutajifunza mifumo muhimu ya kuiwezesha biashara yako kujiendesha mwenyewe bila ya wewe kuwepo.

Kama ndoto yako ni kuwa mfanyabiashara mwenye mafanikio makubwa sana, basi hii siyo semina ya wewe kukosa. Kwa sababu utajifunza misingi muhimu sana kwa mafanikio ya biashara yako. Maelezo zaidi kuhusu semina hii yapo hapo chini;

KARIBU KWENYE SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018.

Rafiki, tarehe 03/11/2018 ndiyo siku ya SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, semina hii itafanyika kwenye moja ya hoteli zilizopo jijini dar es salaam.

Itakuwa ni semina ya siku nzima, kuanzia saa moja asubuhi mpaka saa moja jioni. Yatakuwa ni masaa 12 ya kujifunza, kujuana na wengine, kuhamasika na kuweka mkakati wa kwenda kufanyia kazi kwa mwaka mzima.

Ada ya kushiriki semina hii ni tshs 100,000/= (laki moja) ada ambayo itajumuisha huduma zote za siku ya semina, kuanzia chai, chakula cha mchana, vitafunwa vya jioni, vijitabu vya kuandikia na kalamu.

Ili kupata nafasi ya kushiriki semina hii, unapaswa kulipa ada yako kabla ya tarehe 31/10/2018, ambayo ndiyo tarehe ya mwisho ya kulipia ada.

Pia nafasi za kushiriki semina hii ni 100 pekee, na zilizobaki ni chache sana. hivyo kama hutaki kukosa nafasi hii, lipa ada yako mapema ili tuweze kuwa pamoja kwenye semina hii.

Nakusubiri kwa hamu sana rafiki yangu kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, kwa sababu yapo mengi mazuri nimekuandalia kwa mafanikio yako kwa mwaka 2018/2019.

Namba za kufanya malipo ili kushiriki semina hii ni MPESA- 0755 953 887 au TIGO PESA/AIRTEL MONEY – 0717 396 253. Majina ya namba hizo ni AMANI MAKIRITA. Ukituma fedha tuma na ujumbe wa kueleza umefanya malipo ya semina, ukiambatana na jina lako na namba yako ya simu kwa ajili ya kupewa taarifa zaidi za semina.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL