Mpendwa rafiki yangu,

Hivi ukiamka asubuhi kila siku halafu mtu wako wa karibu anakunenea maneno hasi utajisikiaje? Labda ni mke au mume wako anakunenea kila siku maneno hasi labda anakuambia uwe na siku mbovu sana badala ya kukuambia uwe na siku njema? Hivi utajisikiaje?

Hakuna mtu ambaye hapendi kusifiwa kwa kitu chochote kile, kwa kuwa sisi ni viumbe vya hisia basi kila mtu anapenda kuhisi anathaminiwa. Na habari njema ni kwamba hakuna mtu ambaye hafai kwenye kila kitu. kila mtu ana sehemu yake ambayo ana uwezo naye wa kuifanya kwa ubora wake.

Hivyo basi, wazazi wengi siku hizi wamekuwa wanawanenea watoto wao maneno hasi. Kwa mzazi anamwambia mtoto wake wewe ni mjinga wa mwisho, unashindwa hata mdogo wako na matusi mengine mengi ambayo sipaswi kuyaanika hapa.  Mzazi anamporomoshea mtoto wake makombora ya matusi ya kumlaani halafu huku akitegemea mtoto yule aje kubadilika.

Hakika, ukichunguza watoto ambao hawafanyi vizuri shuleni huenda sababu kubwa inaanzia nyumbani hususani kwa wazazi. Wazazi wengi hawawajengi watoto bali wanawabomoa, mzazi unamwambia mtoto wako maneno mabaya kila siku unafikiri atawezaje kufanya mazuri?

Lisha Akili

Unapomwambia yeye hawezi basi moja kwa moja akili yake inasa kuwa yeye hawezi hivyo hata akitak kujituma zaidi yale maneno yanamrudia kwanza ameambiwa yeye hawezi, hana akili ni mjinga sasa kwanini ajisumbue? Basi anajikuta kuacha kwanini ajisumbue wakati ameshaambiwa hwezi?

Kama mtoto wako kila siku unamwambia maneno mazuri lazima atakwenda kufanya vizuri. Wazazi tumepewa uwezo kubariki na kulaani hivyo umepewa mamlaka makubwa unatakiwa kuchunga sana mdomo wako kile unachomwambia mtoto wako.

Kila siku mpe mtoto maneno chanya ya faraja yatakayomfanya akue na kwenda mbele na siyo kumrudisha nyuma. Usimwandalie mtoto mazingira ya hovyo wakati unauwezo wa kumwandalia mazingira mazuri ya kumfanya kuwa bora.

SOMA; Hizi Ndiyo Nguzo Nne Za Malezi Bora

Mtoto ni malezi na malezi ni asubuhi siyo jioni. Hii ina maana kwamba mpatie mtoto msingi wa malezi bora wakati akiwa mdogo, usitegemee kuja kumkunja samaki wakati tayari ameshakauka. Linalowezekana zuri kumfundisha mtoto au watoto wafundishe sasa na kazi yako kubwa ni kuwajenga vizuri kwa kuwatabiria makubwa.

Wazazi wanatakiwa kuwa walinzi wazuri wa watoto wao. Kama mtoto anakosa ulinzi kutoka kwa wazazi wao je unategemea watakwenda kuupata wapi ulinzi? Dunia inawanyanya na wazazi pia hivyo hivyo je watoto watakuwaje? Kama una nguvu zako mlee mtoto wako vizuri usije ukaiachia dunia ikusaidie kulea mtoto wako kwa sababu haina huruma itamlea kikatili sana.

Chunga kondoo uliopewa, kama umeweza kuzaa basi ujue na kulea. Waswahili wanasema kuzaa siyo kazi bali kazi kulea mwana. Jitahidi kumfundisha mtoto yale yaliyo bora na wewe simama imara kumuonesha mtoto njia iliyo bora kwani mtoto akiona anapendwa na kuoneshwa njia bora anafurahi sana.

Mtoto akiwa na hofu hawezi kufanya kitu chochote, hivyo dunia inatia watu hofu na mtu wa kumtoa hofu mtoto wako ni wewe mwenyewe. usipomtoa hofu dunia inaendelea kumshindilia hofu mpaka anakua anaamini mambo hayawezekani.

Kuwa mjanja wa kuishinda dunia, kabla mtoto wako hajaingia katika mambo ya ulimwengu mwandalie silaha kali za kupambana na hii dunia.  Silaha kali za kupambana nah ii dunia ni maarifa pekee, ukimpa mtoto maarifa ataweza kushinda kama siyo kukabiliana na vita vingi. Maarifa ni nguvu kwani yatamwezesha kushinda vita vingi. Weka nguvu ya kumjenga mtoto wako na siyo kumbomoa.

Hatua ya kuchukua leo; mfundishe mtoto wako yale mazuri. Mnenee yale mazuri na mabaya usithubutu kuwambia.

Kwahiyo, jukumu lako ni kumlinda mtoto wako dhidi ya hatari yoyote ile, kama vile kuku anavyolinda vifaranga vyake dhdi ya mwewe vivyo hivyo na wewe unawajibika kufanya hivyo.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki yangu.

Rafiki na mwalimu wako,

Deogratius Kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com , kessydeo@mtaalamu.net

Unaweza kutembelea tovuti yangu kwa kujifunza zaidi kila siku na kupata huduma mbalimbali kama vile vitabu, kwa kutembelea tovuti  hii  hapa  www.mtaalamu.net/kessydeo .

Asante sana na karibu sana!