Rafiki yangu mpendwa,

Mwaka huu 2019 tunaongozwa na maneno matatu makuu ambayo ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA. Haya ni maneno matatu yanayowakilisha maeneo matatu muhimu sana kwenye maisha yetu.

Kwenye makala ya leo, tunakwenda kujifunza eneo la afya, na inapokuja kwenye afya, changamoto kubwa inaanzia kwenye ulaji.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia yameleta mabadiliko makubwa sana kwenye ulaji na hata maisha kwa ujumla. Kazi zetu zimebadilika sana na hata aina ya vyakula tunavyokula imebadilika sana.

Changamoto kubwa kwenye ulaji zimekuwa ni tatu, moja tunakula vitu ambavyo siyo vyakula, yaani vimetengenezwa mno kiasi kwamba ule uhalisia wa chakula unakuwa umepotea, kwa kifupi tunakula sumu nyingi kuliko vyakula. Mbili tunakula kupitiliza na tatu tunakula vyakula ambavyo vinatokana na wanyama zaidi kuliko mimea.

eat-healthy.-live-healthy.-its-a-choice.

Katika makala hii, tunakwenda kujifunza kanuni kuu ya ulaji ambayo kwa kuifuata tutaweza kuwa na afya bora sana kwa mwaka huu 2019 na kuendelea.

KULA CHAKULA.

Msingi wa kwanza kwenye ulaji ni kuhakikisha unakula chakula. Na hii ni sentensi rahisi kusoma lakini ngumu kuelewa.

Watu wengi tunakula vitu ambavyo siyo vyakula, bali bidhaa zilizotengenezwa kutokana na vyakula. Vyakula vingi tunavyokula ambavyo vimeandaliwa viwandani siyo bora kwa afya zetu. Vinakuwa vimewekwa kemikali mbalimbali ambazo kwenye miili yetu zinakuwa sumu.

Hivyo hakikisha unakula chakula, na kipimo kizuri cha kujua kama ni chakula au la jiulize je bibi yako anaweza kutambua kile unachokula kama chakula? Kama hawezi kutambua kama ni chakula, basi usile.

Hapa utaondokana na vyakula vilivyotengenezwa na kuhifadhiwa kwa kemikali mbalimbali. Utakula vyakula ambavyo vinajulikana kabisa, hizi ni mboga, huu ni mchele, hii ni nyama ya kuku na kadhalika.

Hakikisha unakula chakula, ni msingi muhimu kwenye kuimarisha afya yako.

SOMA; Maeneo Matatu Muhimu Ya Kudhibiti Kinachoingia Kwenye Maisha Yako Ili Kuweza Kuwa Na Maisha Bora Na Ya Mafanikio Makubwa.

USILE CHAKULA KINGI.

Ipo kauli ya kiingereza inaema “we are eating ourselves to death” ikiwa na maana kwamba tunajiua kwa kula.

Chakula tunachokula ni kingi mno ukilinganisha na uhitaji halisi wa miili yetu.

Iko hivi, ukishakuwa mtu mzima, ukuaji wako siyo mkubwa tena, hivyo sehemu kubwa ya chakula unachokula ni kwa ajili ya kuupa mwili nguvu na kutengeneza kinga.

Sasa kama kazi zako siyo nzito, chakula unachokula hakitumiki kwa wingi kuzalisha nguvu na hivyo kinahifadhiwa kama mafuta, kitu ambacho kinaongeza uzito wa mwili.

Unapaswa kula kiasi kidogo cha chakula, hasa vyakula vya wanga na kula zaidi mboga mboga na matunda.

Vyakula vya wanga kama ugali, wali na ndizi vinameng’enywa haraka na kuhifadhiwa kwenye mwili kama mafuta. Mbogamboga na matunda vinameng’enywa kidogo sana, sehemu kubwa vinatoka kama uchafu.

Protini na mafuta pia yanameng’enywa taratibu na kile kinachochukuliwa kinatumika kwa sehemu kubwa na siyo kuhifadhiwa.

Hivyo tunaweza kusema adui wetu mkubwa kwenye ulaji ni vyakula vya wanga na sukari. Ukipunguza hivi kwa asilimia kubwa, afya yako itakuwa imara sana.

KULA MIMEA ZAIDI.

Kitu kingine muhimu sana kwenye ulaji ni kuhakikisha sehemu kubwa ya chakula chako ni mimea, hasa majani na matunda kuliko wanyama au mazao ya mimea.

Nusu mpaka robotatu ya sahani yako ya chakula inapaswa kuwa mimea, yaani majani na matunda. Na sehemu inayobaki ndiyo unaweka vyakula vinavyotokana na wanyama na mazao ya mimea, kama nyama, mafuta na wanga.

Ninaposema mazao ya mimea namaanisha mahindi, mchele, ndizi na kadhalika. Haya yanapaswa kuliwa kidogo kama nilivyoeleza hapo juu.

Zingatia misingi hii mitatu muhimu sana kwenye ulaji na utaweza kuwa na afya bora sana. KULA CHAKULA, SIYO KINGI SANA NA ZAIDI MIMEA.

Je kuna ugumu kwenye hilo? Kama upo niulize kwenye sehemu ya maoni hapo chini na nitakujibu njia bora ya kutekeleza hili.

Kila la kheri.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge