Rafiki yangu mpendwa,

KISIMA CHA MAARIFA ni kundi maalumu kwa wale ambao wamejitoa kweli kwa ajili ya kufikia mafanikio makubwa. Ni kundi la wale ambao wameamua kuweka sababu pembeni na kuweka juhudi ili waweze kufika pale wanapotaka kufika.

Kwa kuwa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA kuna baadhi ya vitu unapaswa kuvifanya ili uendelee kupata nafasi ya kuwa kwenye KISIMA. Baadhi ya vitu hivyo ni kuwa na mifereji mingi ya kipato, kuweka akiba, kuwekeza na kujifunza zaidi kwa kujisomea vitabu.

Kwa mwaka 2018, wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA wameweza kusoma vitabu vingi sana. Hata wale ambao hawakuwa wamewahi kusoma vitabu kwenye maisha yao, kwa kuwa ndani ya KISIMA wameweza kujijengea tabia ya kusoma vitabu na wananufaika nayo sana.

Hapa nimekushirikisha vitabu 117 ambavyo vimesomwa na wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA kwa mwaka 2018. Hapa kuna vitabu na kile ambacho mtu alijifunza na kufanyia kazi.

Soma makala hii kwa kina na utaondoka na mengi sana ya kufanyia kazi kwenye maisha yako ili yawe bora zaidi.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

Na kama utapenda kujijengea tabia za mafanikio, kama unapenda kufanikiwa zaidi ya ulipo sasa, na kama ungependa kupata baadhi ya vitabu hivyo vya kusoma, karibu sana ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Kupata maelekezo ya kujiunga tuma ujumbe kwa njia ya wasap kwenda namba 0717396253 wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA.

Vivuatavyo ni vitabu 117 pamoja na yale ambayo watu walijifunza kupitia vitabu hivyo;

  1. The Law of Success – Napoleon Hill. Nimejifunza na nafanyia kazi suala la kuweka lengo kuu la maisha (definite chief aim).
  2. You’re born an original, don’t die a copy – John Mason. Kubwa ninalofanyia kazi kutoka kitabu hiki ni namna ya kufanya maamuzi sahihi kwa wakati sahihi wakati wote. Mason anasema hatma ya mwanadamu imo katika maamuzi anayoyafanya
  3. Goals – Brian Tracy. Ananifundisha kuwa, malengo lazima uyaandike kila siku bila kuacha hata siku moja. Pia kuwa na dira (vision) ya maisha yangu. Yaani ule kutazama miaka mingi mbele kwa yale unayotaka yatokee na kufanya vitu fulani sasa vinavyokupeleka kwenye ile picha kubwa ya maisha unayoyajenga.
  4. Timiza Malengo Yako – Joel Arthur Nanauka. Nanauka ananifundisha kuwa, kwenye uwekaji malengo, pamoja na kuhakikisha kwamba yako SMART na yameandikwa, lakini lazima lengo kubwa kiasi cha kwamba ukiwaamba watu wakucheke, wahisi umechanganyikiwa. Kama hujachekwa na kushangawa, lengo bado halijawa kubwa ipasavyo. Pia lengo lazima liwekewe mpango wa utekezaji
  5. The magic of thinking $uccess – Dr. David J. Schwartz. Kitabu hiki kinanifundisha kuwa, mafanikio katika jambo lolote yanaanza kwanza kwa kujua kwa hakika kwamba ni nini unahitaji kwenye jambo hilo. Kama hujui unakokwenda, huwezi kufika wala huwezi kupotea. Safari pia haitakuwa na maana. Ndiyo maana lazima kwanza ujue unachohitaji, kisha mengine yafuate.
  6. A setback is a setup for a comeback – Willie Jolley. Katika kitabu hiki, nilijifunza kuwa, fursa yoyote ile imefungashwa kwenye changamoto. Hakuna fursa ya waziwazi, zote zinafikiwa kwa kuingilia mlango unaotwa changamoto.
  7. The impossible is possible – John Mason. Mason katika kitabu hiki ananifundisha kujipambanua. Yale wengine wanayosema hayawezekani, mimi nayafanya. Ni marufuku kufuata mkumbo. Tai huruka peke yao, lakini kunguru huruka katika makundi.
  8. The Power of your subconscious mind – Dr. Joseph Murphy. Nilijifunza kuwa, subconscious mind (akili isiyofikika) ni kama shamba. Usipopanda mazao ya kuliwa, yataota magugu au mimea mwitu. Subconscious mind haiwezi kukaa bure. Kwa hiyo kila mwanadamu (kwa kujua ama kutokujua; kwa kukusudia au kutokukusudia) anapanda mbegu (mawazo) kwenye subconscious mind yake kila siku kwa kadri ya mwelekeo wa tabia zake kimawazo. Hivyo apandacho mtu (kwenye subconscious mind yake), ndicho avunacho kwenye matokeo ya nje. Ili subconscious mind ituhudumie kwa usahihi, lazima tuilishe kwa usahihi pia. Mbegu zetu sasa (mawazo) na ziwe amani, furaha, matendo ya haki, nia njema na mafanikio.
  9. As a man thinketh – James Allen. Namheshimu sana Allen. Kwa ufupi kabisa, nimejifunza kuwa Hali ya nje ya mtu kimazingira, ni dhihiriko la hali yake ya ndani kimawazo. nakazana kuwaza kwa usahihi na najifunza kila siku ili kuboresha hali yangu ya ndani kwanza ili nichochee ubora wa hali yangu ya nje kimazingira.
  10. The science of getting rich – Wallace D. Wattles. Huu ni msaafu wangu wa kuongoza maisha. Ujumbe nilionao kutoka kwenye kitabu hiki ni kuwa, utajiri unapatikana kwa sayansi kamili kama zilivyo sayansi zingine – siyo ajali, bahati wala uchawi wowote. Kikubwa ni kuwaza kwa namna Fulani na kuweka mawazo hayo kwenye vitendo. Dunia haijawahi kupungukiwa na chochote. Hivyo yatupasa tuwaze katika utele, siyo katika uhaba. Fursa za mafanikio hazina kikomo, hakuna mtu mmoja (na pengine hatatokea) wa kumzuia mwingine kufanikiwa.
  11. The secret code of success – Noah ST. John. Kinachowanyima watu mafanikio ni kushindwa kutekeleza (ACTION) matumaini yao halisi, ndoto, na matarajio. Linapokuja suala la mafanikio, akili ya kufikika (conscious mind) si mahali sahihi kuanzia. Sehemu muafaka ya kuanzia ni kwenye subconscious mind maana 90% ya tabia zetu zinatoka huku.
  12. Secrets of the Millionaire Mind – T. Harv Eker. Mafanikio katika jambo lolote yanahitaji kubadili hali ya ndani kwanza kimtazamo ili kubadili matokeo kwa nje kimazingira. Waliofanikiwa kifedha wana picha ya tofauti sana ndani mwao kuhusu fedha ukilinganisha na picha walizo nazo watu maskini na wenye kipato cha kati.
  13. Acres of Diamonds – Russell H. Conwell. Najifunza kupitia simulizi ya jamaa aliyeamua kuuza shamba lake na kusafiri nchi za mbali kwenda kutafuta almasi – bahati mbaya hakuzipata na alifia huko. Huku nyuma, jamaa aliyenunua shamba lake, aligundua lile shamba lilikua limejaa almasi na alichimba akapata nyingi sana. Kwa hiyo, mtu ukiwa na ndoto ya mafanikio, nirahisi kuangalia nje kwa kuamini huko ndiko ndoto yako itatimia, lakini ukweli ni kwamba lazima tuanzie pale tulipo, akilini mwetu, mazingira yetu, na vile tulivyonavyo.
  14. Tatizo si raslimali zilizopotea – Godius Rweyongeza. Huyu Mtanzania kijana ananifundisha kuwa thamani ya mtu inapimwa kwa kile anachotoa si kile unachopokea. Kila mwanadamu angejijua mipaka ya uwezo wake, hakika tusingekuwa hapa leo.
  15. I can, I must, I will – Reginald Abraham Mengi. Kutoka kwa mzee Mengi, napigana Kukataa Hofu ya kushindwa. Hii ni moja ya vitu vikuu vya awali kabisa vinayotufanya watanzania wengi kushindwa kuingia kwenye Biashara. Mengi anasema, tunakosa the “I can” attitude.
  16. Why “A” students work for “C” students and “B” students work for the government – Robert T. Kiyosaki. Nimejifunza kuwa, tunakoelekea watakaoimudu dunia ni wale watakaokuwa na taarifa sahihi, na kuwa tayari kubadirika kadri dunia inavyobadirika na siyo kukinzana na mabadiriko.
  17. Before you quit your job – Robert T. Kiyosaki. Kiyosaki katika kitabu hiki ananifundisha mambo ya kuzingatia kabla ya kuanza safari ya ujasiriamali. Kuna habari ya dhamira, uongozi na timu ya watu. Hizi nguzo tatu, zinabeba ndani mambo matano: mtiririko wa fedha, mawasiliano, mifumo, masuala ya kisheria, na bidhaa. Mtu anapaswa kuwa tayari kwa changamoto zote zijazo. Japo anasema ujasiriamali siyo wa kila mtu, lakini anasisitiza kuwa mtu yeyote anaweza kuwa mjasiriamali.
  18. Increase your financial IQ – Robert T. Kiyosaki. Akili ya fedha si tu kuzalisha fedha zaidi, lakini pia kuzilinda zisipotee, kuzibajeti, kuifanya fedha izae kwa kuwekeza n.k., na kuhakikisha una taarifa sahihi za fedha wakati wote.
  19. Kuna uhusiano kati ya fedha yako na hali yako ya kiroho – Christopher Mwakasege. Fedha ina nguvu kuliko roho kwa mujibu wa maandiko ya biblia kwenye Matayo 6: 21 yanayosema, “Maana pale ilipo hazina yako ndipo utakapokuwa moyo wako”. Mwakasege ananifundisha kuwa, haiwezekani kuapata uhuru wa kiroho vizuri pasipo kwanza kuwa na uhuru wa kifedha. Kwa hiyo, fedha/utajiri ni muhimu sana ili kustawi kiroho.
  20. How to Raise your Own Salary – Napoleon Hill. Hapa najifunza kuwa, watu wenye mafanikio daima wanafanya kazi wanayopenda kufanya. Masaa si kitu kwao. Wanaona furaha katika kufanya kazi yao. Umaskini ni tabia. Mtu yeyote akikubali hali ya umaskini, hali hii ya akili inakuwa tabia. Mtu anakubali umasikini kwa kutokuweka mpango wa kupata utajiri.

Mafanikio ni tabia. Paradiso na umasikini havichanganyiki!

  1. The Monk who sold his Ferrari – Robin Sharma. Katika kitabu hiki, Sharma ananifundisha kuwa mafanikio ya nje hayana maana ikiwa mafanikio ya ndani (i.e. mwili, roho, na nafsi) hayajakaa sawa. Pia siri ya furaha si ngumu. Ni kutafuta kile unachokipenda kukifanya, kisha elekeza nguvu na maisha yako yote katika kukifanya hicho tu. Ukijijua, umeyajua maisha.
  2. How to live on 24 hours a day – Arnold Bennett. Jamaa huyu ananifundisha kuwa, muda wa ziada kufanikisha mipango ya mafanikio unaweza kupatikana: mwanzoni mwa siku, kwa kuamka mapema, njiani kuelekea kazini, njiani kurudi nyumbani baada ya kazi, masaa ya jioni, mwisho wa wiki.
  3. Who Moved My Cheese? – Spencer Johnson. Kitabu kinaeleza kwa njia ya simulizi njia ya ajabu ya kushughulika na mabadiliko katika kazi na katika maisha. Kwa hiyo, mkao sahihi kwenye maisha ni kukubali kwamba mabadiliko yapo, yatarajie, fuatilia mabadiliko, endana na mabadiliko, badilika na yafurahia mabadiliko.
  4. The Law of Success – Napoleon Hill. Ni hizi sarafu ndogondogo tunazozidharau na kuzipuuza zingeweza kutuletea uhuru wa kifedha kama tungedumu katika tungeziweka akiba na kuwekeza. “The nickels, dimes and pennies which the average person allows to slip through his fingers would, if systematically saved and properly put to work, eventually bring financial independence.”
  5. How to achieve total success in life – Dr. C.S. Chopra. Kwa habari ya mafanikio, Chopra naye anakazia umuhimu wa kuanza na picha ya mwisho unakotaka kufika kisha kujenga mfumo wa kufika huko.
  6. PRINCIPLES AND POWER OF VISION.

Kutekeleza maono makubwa niliyonayo ni lazima nitambue kuwa nitakutana na changamoto hivyo mara zote ninapaswa kujiandaa kukabiliana na changamoto zozote ambazo zinaweza kujitokeza.

  1. HOW TO THINK LIKE LEONARDO DAVINCI

Kuna mengi ya kujifunza kupitia njia ya kujiuliza maswali, Na kwa kuanza niliandaa maswali yangu 101 na baada ya kuyafanyia tathimini na kuyachambua kwa kina nilibakiwa na maswali 11 ambapo maswali hayo kwa kweza kuyajibu naweza sema msingi mkuu wa maisha yangu sambamba na  maono makubwa maishani yaliyokana na kuweza kuyajibu maswali hayo muhimu.

  1. THE SOCRATES WAY.

Kila kitu kina mwisho waka hakuna ambacho kinaweza kuishi milele, mimi pia nitaondoka hapa Duniani  hivyo kama ninataka kuacha urithi bora ninapaswa kujiuliza ni kitu gani nitaweza kukiacha katika akili na mioyo ya marafiki na wale niwapendao.

  1. THE COSMIC ENERGIZER MIRACLE POWER OF THE UNIVERSE.

Wivu juu ya maendeleo ya wengine ni kikwazo kikubwa sana mwa sisi kupata mambo mazuri. Na kulalamika au kuilaani fedha kunaifanya fedha iote mbawa. Hivyo tunapaswa kutambua kuwa wivu ni kupoteza nguvu na ni hatari kwa sababu huharibu mafanikio yetu.

  1. FROM PASSION TO PEACE.

Ili kufikia furaha na amani ya kweli kuna hatua muhimu za kupitia  ni wazi utakutana na mateso, majaribu matumaini kisha unafika katika maisha ya furaha na utulivu.

  1. A GIFT TO MY CHILDREN.

Katika mafanikio yenye maana mambo muhimu tunapaswa kuyaishi na kuyafanyia kazi ambayo kuweka akiba na kuwekeza, kutoruhusu wengine wafikiri kwa niaba yangu, kuwa mtu wa maadili , kujifunza falsafa na kutambua kuwa mabadiliko yapo na yataendelea kuwepo hivyo sipaswi kupingana nayo.

  1. THE 80/20 PRINCIPLE

Uchache wa jitihada au visababishi ndio huleta matokeo makubwa. Yaani asilimia 80 ya kile nilichofanikisha  kinatokana  asilimia 20 ya nguvu na muda unaotumia kwa hiyo ili kufanya mambo makubwa ninapaswa kuchagua maeneo machache ambayo nitaweka  nguvu zote huko.

  1. 177 MENTAL TOUGHNES SECRETS OF THE WORLD CLASS.

Hakuna watu wa kawaida wote tupo sawa isipokuwa kuna wale ambao wanafanya kazi zao kikawaida yaani kwa mazoea na hupata matokeo ya kawaida. Kwa hiyo utofauti upo katika namna wanavyofanya kazi na kupata matokeo.

  1. SELF IMPROVEMENT 101

Ni muhimu kuwa na watu ambao utajifunza mengi kupitia wao (mamenta).

  1. THE BUFFERT REPORT

Katika kuwekeza kwenye soko la hisa ni muhimu kuwekeza katika biashara ambayo unaijua na inatoa bidhaa ambayo unaiamini, Kwa kufanya hivyo kunapunguza vihatarishi.

  1. THE 1-2-3 MONEY PLAN.

Kamwe nisiwekeze katika maeneo ambayo siyaelewi, kama uwekezaji ninaotaka kuufanya siwezi kuuelezea kwa mtoto mdogo au bibi ambaye ni mzee na akaniekewa  basi sipaswi kuwekeza huko.

  1. THE 5 LOVE LANGUAGES.

Katika mahusiano kuna lugha muhimu za upendo lugha na vile ambavyo mweza hupenda kufanyiwa na ndipo huhisi kupendwa hivyo ni muhimu kujua lugha ya upendo ya upendo wa mwenzio.

  1. MEGALIVING.

Mafanikio ya nje huanzia na mafanikio ya ndani na kama kweli nataka kuboresha ubora wangu wa nje basi ninapaswa kuanza kuboresha hali yangu ya ndani na namna bora ya kuboresha kwa undani ni kuhakikisha kila siku ninatafuta ushindi mdogo mdogo ambao hupelekea ushindi mkubwa.

  1. Think and Grow Rich – Napoleon Hill. Kitu kimoja nilichojifunza na kukifanyia kazi ni jinsi ya kutumia ubongo wetu wa ndani (suconcious mind) katika kufanikisha ndoto zetu. Kitu tunachotakiwa kufanya ni kuushirikisha ubongo wetu wa ndani kile ambacho tunakitaka na kwa kutumia nguvu zilizo nje ya uwezo wetu hutupatia kile tunachokitaka.
  2. Why forgiveness cha Deogratius kessy. Kitu kimoja nilichojifunza na kukifanyia kazi ni Kwa nini tunatakiwa kusamehe na sio kuvumilia. Unapovumilia unaendelea kubaki na uchungu ndani ya moyo ambao unaendelea kukutafuna, unaendelea kuteseka, kuijeruhi nafsi yako na kuendelea kuongeza majeraha ndani ya moyo wako. Unaposamehe unaachilia uchungu na kuiweka huru nafsi yako.
  3. ‘Eat That Frog’ – Brian Tracy.

Kitu kimoja nilichojifunza na kukifanyia kazi ni jinsi ya  kutumia njia ya ABCD kila wakati katika kuweka vipaumbele vya kazi zako. Katika njia hii mwandishi anatuhimiza kuzipanga kazi zetu katika makundi matano ABCDE kulingana na umuhimu wake. Kazi za kundi A ni zile ambazo ni muhimu na zinazoleta matokeo chanya unapozifanya au matokeo hasi usipozifanya, mara zote tunahimizwa kuanza na kumaliza kufanya kazi za kundi A kabla hatujafanya kazi za makundi mengine. Kazi za kundi B ni za umuhimu wa wastani ambazo hata usipozifanya hazina athari kubwa na sheria inatutaka kutofanya kazi za kundi la B kama au kabla hatujamaliza za kundi A. Kazi za kundi C hazina athari kabisa kwako zisipofanywa ingawa ni kitu kizuri kufanya kama vile kumpigia simu rafiki au kufanya kazi binafsi muda wa kazi. Kazi za kundi D, ni kazi ambazo unaweza kumpa mwingine afanye na sheria inatutaka kuwapa wengine kazi zote ambazo wengine wanaweza kufanya ili kupata muda zaidi wa kufanya kazi za kundi la A ambazo mara nyingi lazima ufanye mwenyewe. Kazi za kundi E ni zile ambazo unaweza kuziacha kabisa na zisilete tofauti yoyote. Ni vile vitu ambavyo tunafanya kwa mazoea au kwa sababu vinatufurahisha. Kila dakika unayotumia kwenye kazi za kundi la E ni muda ambao unapoteza kufanya kazi za kundi la A.

  1. Mambo 55 ya kuzingatia kabla ya kuanzisha biashara – Godius Rweyongeza Kitu kimoja nilichojifunza na kukifanyia kazi ni muda gani mzuri wa kukata tama. Mwandishi anatuambia muda mzuri wa kukata tamaa ni pale unapokuwa umekamilisha kile ulichokianzisha. Kwa maana nyingine hakuna kukata tamaa katika mbio za mafanikio
  2. Wherever you go, There you are – Jon Kabat Zinn. Kitu kimoja nilichojifunza na kukifanyia kazi ni kuhusu fikra zetu, hiki ni kitu pekee ambacho tunaudhibiti wa asilimia mia moja, watu wanaweza kufanya kila kitu kwenye vitu vingine vinavyotuzunguka lakini sio fikra zetu , tunaporuhusu kuumizwa hadi kufikia hatua ya kukata tamaa, kuchanganyikiwa au kufikiria kulipiza kisasi, tunaruhusu watu wengine watawale hadi fikra zetu kitu ambacho sio kizuri.
  3. Procrastinate on Purpose – Rory Vaden; Kitu kimoja nilichojifunza na kukifanyia kazi – Ili kupata muda zaidi wa kufanya mambo makubwa kuna vitu tunatakiwa kuviacha, kuna kazi tunatakiwa kuzitengenezea mfumo maalumu wa kuzifanya, kuna kazi tunatakiwa kuwapa wengine watusaidie kufanya na kuna kazi tunatakiwa kuzihairisha kwa muda kusubiri wakati muafaka wa kuzifanya.
  4. 365 Ways to Live Cheap – Trent Hamm. Katika kitabu hiki mwandishi amezungumzia njia 365 za kuishi kwa gharama nafuu akitumia maeneo 19 muhimu yanayogusa kila nyanja ya maisha yetu ya kila siku kuanzia vifaa tunavyotumia, jinsi ya kuwafurahisha watoto na familia kwa ujumla hadi jinsi ambavyo tunaweza kwenda kwenye mapumziko kirahisi. Pamoja na hizo ametushirikisha vidokezo 10 vya kuishi kwa gharama nafuu na mbinu 10 za kuendelea kuwa na maisha ya gharama nafuu. Kitu kimoja nilichojifunza na kukifanyia kazi ni njia ya 12 ambayo inatutaka kuangalia ubora wa vitu tunavyonunua na siyo bei. Kwenye manunuzi ya vitu, ubora ni kitu cha msingi sana ambacho tunatakiwa kukizingatia. Kununua kitu kizuri kwa bei kubwa kidogo ni bora kuliko kununua kitu chenye ubora wa chini kwa bei ndogo.
  5. Nisaidie ninaogopa cha Joyce Meyer. Kitu kimoja nilichojifunza na kukifanyia kazi  ni kwamba Hofu, mashaka, wasiwasi vyote ni mpango wa shetani kututisha ili aendelee kututawala na kutukosesha vitu vizuri au mambo mazuri ambayo Mungu ametuandalia. Shetani ni kama simba mzee, hawezi kutushinda bila kutumia vitisho kwa sababu anafahamu hana nguvu za kutosha hivyo silaha pekee aliyonayo ni kutufanya tuogope ndipo atudhuru au atushambulie. Hofu haitoki kwa Mungu, mwandishi anatuambia sitaivumilia au kuiacha hofu itawale maisha yangu, nitaikabili, kwa sababu ni roho kutoka kuzimu ambayo imekuja kunitesa, nasi nyakati zote tunapaswa kujiambia hivyo
  6. Jinsi ya kuibua ubunifu uliopo ndani yako- Godius Rweyongeza. Kitu kimoja nilichojifunza na kukifanyia kazi ni mbinu ya kutumia dakika 30 kila siku kuendeleza kipaji au kitu unachopenda kufanya hii ni kwa sababu ubunifu unahitaji kujifunza  kila siku lakini pia kufanya marudio ya kile ulichojifunza ili ukielewe vizuri.
  7. The Richest Man in Babylon – George Clason Kitu kimoja nilichojifunza na kukifanyia kazi ni jinsi gani unaweza kuanguka ikiwa utaacha kuifuata misingi au sheria 5 za dhahabu na kusimama tena endapo utairudia na kuanza kuifuata tena misingi au sheria 5 za dhahabu. Katika kitabu tunaona jinsi mtoto wa Arkad (Tajiri wa Babylon) aitwaye Nomasir alivyoanguka baada ya kushindwa kuzifuata sheria tano za dhahabu na alipozikumbuka na kuanza kuzifuata, aliweza kurudi kwenye mstari na kurudisha dhahabu yote aliyokuwa ameipoteza.
  8. Born to Win cha Zig Ziglar; jambo kubwa nililojifunza kwenye kitabu hiki ni kwamba kila mtu amezaliwa mshindi, na ili uwe mshindi kwenye maisha haya lazima nipange kushinda, nijiandae kushinda na nitegemee kushinda.
  9. Midas Touch cha Donald Trump; kutojiruhusu kwa namna yoyote kukaa kenye confort zone, yani natakiwa kuingia kwenye maisha halisi ya mafanikio, na maisha halisi ya mafanikio makubwa kama mjasiriamali ni kujua kuna changamoto na kuhakikisha pamoja na changamoto zote zitakazotokea natakiwa kutimiza malengo yangu makubwa.
  10. Ten Commitment to Your Success cha Steve Chandler; nilichojifunza hapa ni nidhamu na kujitoa, hata kama kuna tabia mbaya kiasi gani mwandishi anatuambia kama utajijengea nidhamu na kujitoa utaibadili tabia hiyo, na mafanikio kwenye maisha yanahitaji nidhamu na kujitoa.
  11. The Glory of Living cha Dr. Myles Munroe; kitu kimoja nilichojifunza hapa ni kwamba tumeumbwa tukiwa na vitu vingi ndani yetu ambavyo kama tutavitoa au kuvitumia tutaibariki sana dunia na huo ndio utukufu (glory), kwamba lengo kuu la sisi kuishi ni ili tuutoe utukufu ambao upo ndani yetu, na pia lengo kuu la kuishi ni ili tufe tukiwa tupu yaani empty.
  12. Releasing Your Potential cha Dr. Myles Munroe; kikubwa sana nilichojifunza katika kitabu hiki ni kwamba njia pekee ya kutoa uwezo mkubwa uliojificha ndani yangu ni kufanya kazi, (You must work to mine your hidden potential). Usipofanya kazi hutajua unaweza nini na hata una kipaji gani, kazi ni baraka.
  13. Overcoming the Crisis cha Dr. Myles Munroe; katika kitabu hiki mwandishi anatuambia faida za majanga, changamoto na dhoruba kwenye maisha; nimejifunza Mungu huwa anapenda sana crisis ili awe na watu imara, wanaojua kubeba vitu vizito na wanaoaminika. Nimejifunza pia Mungu anaruhusu crisis kwenye maisha ili kutujua vizuri na ana nia nzuri kabisa.
  14. The Secret cha Rhoda Byrne; katika kitabu hiki nimejifunza nguvu ya mawazo ambayo tunayo, kupitia mawazo tunaweza kuyafanya maisha yetu kuwa bora na mazuri kwa kuvutia na kuwaza vitu vizuri, vitu chanya.
  15. The Principle and Power of Kingdom Citizenship cha Dr. Myles Munroe; hapa nimejifunza mengi kuhusu ufalme wa Mungu, na kwamba sisi binadamu tuna uraia wa aina mbili, wa hapa duniani na mbinguni, hivyo asili yetu ni mbinguni na dunia ni koloni la mbinguni hivyo tupo hapa kama mabalozi wa ufalme wa Mungu kwa ajili ya kueneza mapenzi na makusudi ya Mfalme Mkuu ambaye ni Mungu.
  16. Think Like a Champion cha Donald Trump; hapa nimejifunza kuwa usipokuwa na utamaduni wa kujiambia vitu vikubwa na vizuri hakuna atakayefanya hivyo, hivyo ni vizuri sana tukajikubali na kujiona kama washindi siku zote ili tufanikiwe kwenye maisha.
  17. Saa 72 za kufa na Kupona cha Japhet Nyang’oro; hiki ni kitabu cha riwaya ambacho kinaeleza sana visa vya kijasusi, hapa nimejifunza kwenye maisha tunatakiwa kufanya mambo yetu kwa umakini mkubwa, pia hakuna muda wa kuchezea, wakati tunapoteza muda kuna wenzetu wanatumia muda kujiandaa, kujipanga, wengine hata hawalali kuhakikisha wanafanikiwa, umakini, umahiri, ujasiri ni muhimu sana katika maisha.
  18. Becoming a Leader cha Dr. Myles Munroe; katika kitabu hiki nimejifunza misingi ya uongozi na namna ya kuwa kiongozi bora, nimejifunza kuwa kiongozi wa kweli na bora ni kuwa tayari kuwa peke yako, kutembea peke yako, kuamua peke yako hadi pale watu watakapokuona kuwa una kitu kizuri ambacho wanakihitaji kutoka kwako na hapo ndipo unapoanza kuwapa vitu hivyo. huo ndio uongozi na sio kutafuta watu kwa nguvu na kuwalazimisha wakufuate na wakuone au wakuite kiongozi.
  19. Mindfulness Meditation cha John Kobat Zinn; Hapa nimejifunza namna ya kuituliza akili yangu, kingia ndani yangu na kufanya tahajudi, nimejifunza kuwa bora, kuwa mwanga kwangu mwenyewe na hapa ni lazima nifanye tahajudi, kuwa na kutambua kuwa natakiwa kuishi.
  20. The Miracle Morning for Writters cha Hal Elrod and Steve Scott; hapa nimejifunza mengi kuhusu uandishi, nimejifunza uandishi sio kazi nyepesi lakini ni kazi ya thamani sana, kujitoa kwa ajili ya kuboresha maisha ya wengine kupitia maandishi yangu.
  21. Incharge cha Dr. Myles Munroe: hapa nimejifunza mengi sana kuhusu uongozi. Lakini kubwa zaidi uongozi sio kutoa amri au watu kukutumikia, uongozi ni kuwa mtumwa kwa kuwatumikia wengine kwa kipaji ulichonacho, mwandishi ametoa mfano wa Bwana Yesu kuwa hakuja duniani kutumikiwa bali kutumika kwa ajili ya kuboresha na kuokoa maisha ya wengi.
  22. Final Down Over Jerusalem cha John Hagee; ni kitabu cha kinabii na kinaeleza kwa kina historia ya Wayahudi na makusudi yao hapa duniani. Nimejifunza kuwa tukilibariki taifa la Israel Mungu atatubariki pia, na tukililaani Mungu atatulaani, pia kwa mifano nimejifunza watu walioibariki Isreal au Wayahudi walivyobarikiwa, mfano taifa la Marekani limewatunza sana Wayahudi na ndio maana ndio taifa lenye mafanikio mengi sana.
  23. 2 Minutes Wisdom cha Mike Murdock; ni kitabu kifupi sana lakini nimejifunza mengi na ya muhimu sana, nimejifunza kutambua na kuwalinda na kuheshimu zawadi ya kuwa na mtu ambaye ananihamasisha, ananijali, na kunilinda.
  24. Ishinde Tabia ya Kughairisha Mambo cha Joel Nanauka; hapa kwenye kitabu hiki kifupi nimejifunza nisiahirishe mambo muhimu kwenye maisha yangu hata kama ni magumu, pia nimejifunza kanuni ya dakika 2, naweza kujiambia kuliko niache kufanya jambo hili hembu nilifanye hata kwa dakika mbili tu, na hapo ndipo nitakapopata hamasa ya kuendelea kulifanya jambo hili hadi mwisho.
  25. Adili na Nguguze cha Shaban Robart; sikujua kitabu hiki cha riwaya kama kina mafunzo muhimu sana kama niliyojifunza humo, nimejifunza kuwa “asiye matendo hula uvundo na kula uhondo kwataka matendo”. Nimejifunza sana kauli hizi matendo ndio husikiwa zaidi, mfalme Rasi alikuwa na falsafa yake kuwa yeye amechagua kufanya matendo na maneno amewaachia wengine waseme, yeye atatenda wengine watasema, na watu wataamka kwenye usingizi wa uvivu wao sio kwa kuishia tu kuwaambia bali kwa kutenda matendo sahihi ndio wataamka na kuwa wachapakazi.
  26. The Jewish Phenomenon cha Steven Silbiger; hiki pia ni kitabu cha ajabu sana ambacho kinaonyesha jinsi taifa la Isreali au Wayahudi walivyofanikiwa sehemu yoyote wanapokwenda duniani. Nimejifunza siri nyingi sana za mafanikio yao kwenye nyanja mbali mbali kama elimu, kilimo, sheria, biashara, utabibu nk. Kwa Wayahudi wanaamini sana katika elimu na ni wasomaji wakubwa sana wa vitabu, na pia ndio wanaoongoza kwa kusoma hata kama wamekuwa wazee, takwimu zinaonyesha wanaohudhuria madarasa ya jioni kwa taifa la Marekani wengi ni wayahudi wazee, kwa wastani myahudi mmoja anakadiriwa kusoma vitabu 64 kwa mwaka, pia wanaamini katika utajiri na kusaidia wengine kwa misaada. Mwandishi anasema “The Jewish community is very tough audience to please because there so many successful students from successful families.
  27. Your First 100 Milion cha Dan Pena; ni kitabu kigumu kuwahi kusoma, lakini pia sikukimaliza chote, ila hapa nimejifunza jambo kuu kuhusu mafanikio makubwa, kama nataka mafanikio makubwa natakiwa kuacha kujihurumia na kutoa sababu, mafanikio ni kama kwenda vitani kupambana ili kushinda vita kwa namna yoyote ile, kupambana kama vile sina ukomo wa nguvu nilizo nazo, mafanikio ni kujitoa na hakuna kuona aibu kwenye hilo.
  28. Ishi Ndoto Yako cha Joel Nanauka; hiki ni kitabu kizuri sana kinaelezea kwa mifano namna ambayo ndoto niliyonayo inaweza kutimia. Nimejifunza kufanya kila ninaloweza kuhakikisha ndoto niliyonayo naitimiza na sitakufa na kwenda na ndoto yangu kaburini.
  29. Rich dad cash flow quadrant, nimejifunza nilichojifunza na kuanza kufanyia kazi ni kuchukua jukumu la kuyabeba maisha yangu Mara baada ya kuhitimu nilijifunza kila quadrant faida zake na namna ya kuanza kuhama kutoka kwenye quadrant moja kwenda nyingine hivyo najitahidi sana nisiingie E quadrant na nibaki kwenye S quadrant kwa muda mfupi iwezekanavyo ili niweze kuhamia B na I quadrant haraka iwezekanavyo ila sio kwa papala bali kwa juhudi, subira, na uvumilivu wa hari ya juu sana.
  30. Buying customer; hapa nimejifunza juu ya namna bora ya kumuhudumia mteja hapa mwandishi umenifunza kwamba kila gharama tunayowekeza kwenye biashara ni gharama ya kununua wateja ,mwandishi umenifunza namna ya kutumia wateja niliokuwa nao kuniletea wateja wapya kwamba iwe ndio njia ya kwanza na ya kuipa kipaumbele na kweli nimeona matunda yake yaani mteja anatakiwa kuwa zaidi ya mteja yaani awe rafiki pia kweli mwandishi amenisaidia sana .
  31. Rich dad poor dad , hapa mwandishi amenifundisha mengi lakini moja kati ya mengi niliofanyia kazi ni juu ya fedha na mahusiano yake na shule hapa amenifundisha namna mpya ya kufikiri kuhusu shule na hatima yangu baada ya shule na nimelifanyia kazi kuhakikisha nafuta kabisa hari ya kufikiri kwamba shule ndio kila kitu kuelekea mafanikio ya kiuchumi kumbe kuna njia nyingine nyingi nzuri kuliko shule hasa( BIASHARA NA UWEKEZAJI)
  32. The perfect day formula ,hapa mwandishi amenifundisha namna ya kuianza na kuimaliza siku yangu vyema na hapa nimeweza kubadili namna ya kulala, kuamka, na kupangilia mambo na nimekuwa na matokeo mazuri .
  33. How Rich People Think By Steve

Kushindwa hutokana pia na kufanya mambo mengi kwa kiwango kidogo. Huwa nachagua mambo machache ya kukamilisha kila siku ambayo najua yatakuwa na mchango mkubwa kwenye mafanikio yangu

  1. Rich Dad Guide to Investiment

Wawekezaji wakubwa wana vitu vitatu mhimu; Elimu , Uzoefu na Fedha nyingi. Lengo langu ni kuwa mwekezaji mkubwa, nafanya bidii kuwa hivyo vitu vitatu muhimu. Najifunza sana kuhusu uwekezaji kupitia kusoma vitabu ili kupata elimu. Nimeshaanza kuwekeza katika Nyanja mbalimbali ili kupata uzoefu, na naamini kupitia biashara na matumizi ya fedha vitanipa fedha za kutosha kwa ajili ya kuwa mwekezaji mkubwa

  1. Rich Dad Guide To Financial Freedom by Robert kiyosaki

Tusiishi maisha kwa kutafuta fedha tu; bali tuwe na fedha kwa ajili ya kusaidia maisha. Natengeneza mfumo wa kufanya kazi si kwa ajili ya kupata fedha bali kwa kuweka kipaumbele cha kuweka dhamani kwa wengine ili wanipe fedha na kusaidia maisha yaende kwa uhuru

  1. Tajirika kwa Ufugaji wa kuku na Frank Mapunda

Magonjwa ndio kilio cha wafugaji Magonjwa ya kuku ndiyo yamekuwa yakiwakatisha tamaa wafugaji. Nimesoma namna ya kukabiliana na magonjwa ya kuku na hii itanirahisishia kukabiliana nayo kwa awamu hii ya ufugaji

  1. The Millionare Mind set by Gerry Robert

Huwezi kufanikiwa bila ya kuwa na ndoto. Ndoto uliyonayo ndiyo dira ya kukuelekeza unakotaka kwenda. Nina ndoto ya kuwa huru kifadha na msaada kwa watu wengine

  1. The power of positive thinking by Norman Peale.

Nguvu ya mwili inategemea hali ya akili. Akili ikichoka na mwili pia huchoka. Hivyo huwa nahakikisha siichoshi akili yangu kwa mambo yasiyo na msingi.

  1. Be a Sells Superstar by Brian Tracy.

Ubora hauna mwisho. Kuna nafasi ya kuendelea kuboresha tunayoyafanya kila siku. Nitatumia maarifa haya kuendelea kuboresha ufugaji wa kuku ninaoufanya. Nitaboresha “packing” ya kuku ninaowafuga na kuongeza thamani zaidi kwa wateja wangu.

  1. Your infinity power to be rich by Joseph Murphy

Akili ni chanzo cha utajiri wote. Ili uwe upate mafanikio yoyote yale akili yako lazima iyakubali kwanza kabla hayajatokea. Nafikiri mara kwa mara na kuyaamini yale ninayotaka yatokee maishani mwangu.

  1. Retire Young Retire Rich by Robert Kiyosaki.

Nguvu ya Leverage. Kwa kuwa na uzoefu, maarifa na mipango mizuri unaweza kutumia fedha za watu wengine kupiga hatua kubwa za kiuchumi. Nimeanza kutumia mikopo mizuri katika uwekezaji ninaoufanya.

  1. The business of the 21st century na R Kiyosaki. Hatuwezi kutajirika kwa mfumo wa ‘mapinduzi ya viwanda’ hizi ni zama za maarifa na taarifa. Ukifanyia kazi maarifa na taarifa sahihi utapata mafanikio.
  2. Pata Masaa Mawili Ya Ziada Kila Siku. Hiki kimeandikwa na Dr. Makirita Amani.

Katika kitabu hiki moja kati ya mambo ambayo nimejifunza na ninayafanyia kazi katika maisha yangu, ni kudhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii, kitu ambacho nimejifunza katika kitabu hiki ni kudhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii niliamua kujiondoa kwenye mitandao ya kijamii kama facebook, twitter, instagram, pamoja na kupunguza makundi ya WhatsApp ambayo hayachagui kitu chochote kwenye maisha yangu zaidi ya kunipotezea muda. yapo mengi ambayo nimeweza kujifunza nmekushirikisha japo jambo moja.

  1. Kitabu, Mimi ni mshindi, pia kimeandikwa na Dr. Makirita Amani.

Katika kitabu hiki mambo ambayo nimejifunza na yapo katika matendo ni kutambua kubwa maisha yangu ni jukumu langu, kushindwa kwangu kwenye maisha yangu huwa kunatokana na mimi mwenyewe, kwa sababu mimi mwenyewe ninatakiwa kufanya jitihada kubwa sana ili nifanikiwe kwa sababu hakuna miujiza kwenye mafanikio lazima nijitoe.

  1. Kitabu, cha mbinu 12 zinazoleta mafanikio, pia hiki kitabu kimeandikwa na Joel Nanauka. Katika kitabu hiki nimejifunza mbinu zinazoleta mafanikio na baadhi tayari nazifanyia kazi kwenye maisha yangu. Kufanya maamuzi bila woga katika kujifunza mbinu hizi kumi na mbili nimejifunza kufanya maamuzi bila woga, hata mwandishi Ralph Waldo aliwahi kusema kwamba mara unapofanya maamuzi basi ulimwengu mzima huanza kufanya kila kitu ili ukusaidie uweze kukamilisha kile ulichoamua kukifanya. na nilivyo leo ni matokeo ya maamuzi ambayo niliyafanya huko nyuma na vile nitakavyokuwa kesho yatakuwa ni matokeo ya maamuzi ambayo nimeyafanya leo.
  2. Kitabu, cha mbinu za kukuza na kuimarisha familia ya kikristu kitabu hiki kimeandikwa na Fr, Cleophas A.M.Sukary katika kitabu hiki father ameeleza mbinu mbalimbali za kukuza na kuimarisha familia za kikristo moja ya mbinu ambayo nazifanyia kazi ni hii kubwa na uvumilivu, kusamehe na kusahau. Katika maisha ya familia yapo magumu na matatizo yanayoweza kutokea, magumu na matatizo haya husababishwa na watu walio nje ya familia au yanatokana na wanafamilia wenyewe lakini uvumilivu katika magumu haya ndio silaha ya kuimarisha familia zetu uvumilivu wa aina yeyote ile katika jambo lolote gumu huishia kubwa na furaha iliyo kubwa sana ndio maana Yesu Kristu alivumilia mateso na hatimaye alifikia utimilifu wa ukombozi wetu, kwa ujumla hali yeyote ya uvumilivu huleta furaha mwishoni.

Kusamehe ni kuacha kuwapa na kinyongo kwa jambo baya ambalo umetendewa, pia msamaha ni rehema, huruma na neema ambayo mkosaji hupewa bure na yule mwenye wajibu wa kumhukumu. Katika familia zetu mambo haya huenda sambamba kuvumiliana magumu, kuwasamehe wale wanayoleta hayo magumu miongoni na kusahau.

  1. Money Master the Game, 7 Simple Steps to Financial Freedom cha Tony Robbins. Katika kitabu hiki nimejifunza kuhusu kuweka akiba na kuwekeza hata kama kipato tunachopata ni kidogo hadi kufikia uhuru wa kifedha.
  2. What Winner’s Do To Win cha Nicki Joy. Katika kitabu hiki nimejifunza kuwa washindi wanajua umuhimu wa mafanikio na ndiyo maana wanapambana kwa hali zote kuhakikisha wanayafikia mafanikio hayo.
  3. Who Took My Money cha Robert T. Kiyosaki. Katika kitabu hiki nimejifunza kuwa uwekezaji bora ni ule unaleta fedha kila siku.
  4. JINSI YA KUNUFAIKA NA MABADILIKO YANAYOTOKEA KWENYE MAISHA. kitabu kinasemea na kuhamasisha umakini Mkubwa Wa kuyajua mabadiliko na kuwa tayari kuyapokea kabla hayajaathiri mfumo wako Wa kimaisha kinataka ujiandae na kuyatambua uwepo Wa mabadiliko katika dunia tunayoishi..
  5. IJUE BIASHARA YA MTANDAO. manufaa makubwa yanayopatikana kutokana na biashara ya mtandao na ubaya na uzuri Wa biashara ya mtandao na kutofautisha utapeli na biashara ya mtandao na hata kujua inavyofanya kazi mpaka MTU kulipwa kitabu kimeeleza kwa undani na nimenufaika na yaliyomo mule maana wakati naisikia biashara ya mtandao nilijua ni kazi ndogo sana kuifanya na ni rahisi lakini baada ya kusoma kitabu hiki niligundua inahitaji kazi na muda mwingi kuifanya tofauti na walivyokuwa wanasema wanataka nijiunge nayo.
  6. SIRI SABA ZA KUWA HAI LEO. upo hai kwa dhumuni maalum hujaja duniani kuwa tu hai unatakiwa kuishi na kuijenga dunia kuna deni unadaiwa na dunia ndio maana upo hai kitabu kimetaja mengi na sababu nyingi za kukusukuma MTU uchukue hatua Leo na sio kesho kufanya makubwa ili ukifa dunia iwe imenufaika na uwepo wako.
  7. KUTOKA SIFURI MPAKA KILELENI. umhimu Wa kujijua na kujitathimini mambo ya msingi unapotaka kutoka sifuri mpaka kifikia kilele cha mafanikio yepi ya kuzingatia na kuyatumia na kufikia kilele mwandishi ametaja mengi ya kumsaidia MTU kufikia kilele cha mafanikio.
  8. Nyuma ya ushindi kuna kushindwa. By Godius Rweyongeza.

Ni kitabu kizuri kinakuongezea kujiamini na kuamini unaweza mfano nilizaliwa kuishinda, mimi ni mshindi ukitumia mbinu za ushindi lazima ulete mabadiliko yako ya maisha.

  1. Boron latters:- unapoamka asubuhi fanya zoezi kujenga mwili wako na zoezi zuri unaweza kuanza kwa kutembea mwendo wa lisaa limoja na usile chochote isipokuwa matunda tu haswa ndizi mbivu mpaka mchana saa sita.
  2. Epictetus handbook:- msongo wa mawazo mwingi kwa mwanadamu ni pale unapojibebesha mambo ambayo hayapo chini ya udhibiti wako chagua mambo utakayojihusisha nayo na ili kuwa na furaha jihusishe na yale yaliyo ndani ya uwezo wako yale yaliyo nje ya uwezo wako usiyoweza kuyaathiri achana nayo
  3. Make today count:- mafanikio ni tabia unayoishi kila siku jinsi unavyopangilia siku yako moja angalia tabia unazozifanya kila siku rekebisha siku yako unayoishi kila siku.
  4. Goal setting mastery: malengo unayojiwekea kila mara hakikisha yanapimika una njia za kufikia na jipe ukomo wa muda katika malengo yako uliyojiwekea usiendeshe maisha bila kujua unatakiwa kukamilisha lini kuwa na mpango wa ukomo wa muda.
  5. Enjoy your life and your job: usikimbilie kufanya kazi kwa sababu ya kipato tu au mshiko penda kazi unayoifanya kwanza ndani yako ipende ni mateso kufanya kitu usichokipenda
  6. A mans guide to mastering the challenges of women: katika suala la mapenzi wengi suala la hisia zipo juu kuliko kufikiri kwa akili ya kawaida haswa wanawake ,mwanaume mjue mwanamke wako sana jua ni kipi kinachoweza kumuondolea raha na furaha yake
  7. 67steps of easy way of life: kila unachokifanya na wengine wanachokifanya jitahidi kuwa tofauti na wengi wewe ukiwa katika nafasi ya kukifanya kwa ubora zaidi na thamani bora zaidi
  8. Millionaire next door: sifa mojawapo ya milionea anajua kanuni za kipato na matumizi na siri yao nyingi ni matumizi kuwa chini kuliko kipato na kila matumizi kuwa na rekodi umetumia aje na ni kiasi gani imegharimu na akiba na uwekezaji.
  9. A guide to the goodlife ancient art of stoic joy; thamini sana ulicho nacho sasa lakini jua ipo siku hutakuwa nacho jenga mtazamo hasi kwa kila ulicho nacho utakapokikosa usiumie.
  10. Real estate investing for dummies. Mwandishi anaeleza misingi muhimu sana katika biashara ya uwekezaji kwenye ardhi na majengo.
  11. From 0 to 130 Properties. Mwandishi anasema kuwekeza ili kupata faida ni uwekezaji usio na manufaa. Kuwekeza kwa kupata kipato endelevu ndio jambo la kupigania
  12. Tenacity of youth and students. Mwandishi anasema kuwa vijana wanapaswa kutegemea na kufanya makubwa. Kila kanuni iko wazi. Anasisitiza kuwa maadili ni jambo litakaloweza kukupatia hata mtaji fedha.
  13. Ugonjwa wa Umaskini na tiba yake. Mwandishi anasema umaskini ni ugonjwa tishio kwa wengi hapa Tanzania na Afrika kwa ujumla. Tiba pekee ya ugonjwa huu ni KUFANYA KAZI KWA BIDII.
  14. The Corporate Property Management. Mwandishi anasema kuwa usimamizi bora wa Ardhi Na majengo unategemea sana juhudi za serikali katika kuboresha huduma ya makazi. Pia anasema biashara yoyote hapa duniani inategemea ardhi na majengo kwa namna moja ama hadi nyingine.
  15. Negotiation Genius. Mwandishi anasisitiza kuwa mazungumzo bora ndio kitovu cha biashara ya kuwekeza kwenye ardhi na majengo. Unaweza kuanza kuwekeza hata bila mtaji ili hali una mbinu za mazungumzo bora.
  16. Sign-Posts On The Road To Success:

Linapokuja suala la  ufanyaji wa mambo, ili kuleta matokeo yenye manufaa zaidi ninatakiwa niwe kiongozi/kufanya watu wanitegemee. kwenye kila jambo ambalo ninafanya hasa yale ya msingi, kwa kulifanya kwa utofauti na mazoea ya wengine iwe ni langu binafsi, au la kuwashirikisha watu.

  1. The 10X rule:

Maendeleo sio kitu cha mara moja kuwa tukishayafikia basi tunaridhika, hapana kufikia mafanikio ni suala moja na kuendelea kubaki kwenye mafanikio ni suala lingine, hivyo basi inatupasa tuweke X 10 kwa kila hatua ya mafanikio tunayoifikia.

  1. You can win:

Katika  kujiletea maendeleo, hamasa ni kitu cha msingi sana. Bila hamasa tunaweza kuishia njiani, kwa kuwa mara zote huwa tunaanza kitu kwa hamasa kubwa sana, lakini kadiri muda unavyozidi kusonga mbele hamasa hupungua na matokeo yake tunapokutana na changamoto hata ndogo, tunakuwa wepesi wa kutoa visingizio na ndio maana  mipango mingi tunayoanzisha inakufa.  Hivyo tunasisitizwa tujihamasishe sisi wenyewe kila siku na bila kuchoka na kuwahamasisha wengine pia.

  1. Change your thinking change your life:

Hivi tulivyo leo ni matokeo ya fikra zetu, matajiri na maskini wanatofautiana kwenye kufikiri, ili tuyafikie mafanikio makubwa hatuna budi kubadili kufikiri kwetu, kuanzia ndani na kufikiri chanya.

  1. The Rules of Money:

Tujifunze jinsi mali zetu zinavyoweza kutufanyia kazi:

Huwa tunamiliki mali za muda mfupi (current asset)  ambazo ni rahisi kuzigeuza kuwa pesa. Na mali za muda mrefu (fixed asset)  ambazo zinachukua muda kuziuza. Anashauri kuwa tusiache mali zetu zikakaa tu bila kutuingizia chochote/kipato.  Mfano Kama ni jengo limekaa tu ni heri upangishe, Kama ni ardhi iko tupu na eneo unaloishi kuna uhaba wa parking ifanye iwe  parking ikuingizie kipato.

  1. How to stop worrying and start living, Dale Carnegie

Hofu ni adui mkuu wa maisha ya mafanikio na ndio inatunyima kuchukua hatua kwenye maisha. Cha ajabu sana hofu nyingi hazina uhalisia na huanzia ndani yetu. Hivyo moja ya njia bora ya kuondokana na hofu ni kuelewa kuwa hofu ni zao LA fikra zetu na hivyo tukiwa na fikra chanya tutaondokana na hofu nyingi.

  1. How to win friends and influence people; Dale Carnegie

Mawasiliano sahihi na ujumbe sahihi utaleta watu sahihi kwako, na jinsi utakavyojihusisha na watu hao, usiwakosoe, usiwalaumu, usilalamike unapotaka kusahihisha jambo. Ukikosea kubali umekosea na jitahidi kuona jambo kutoka upande wa pili sio upande wako mwenyewe.

  1. Imitation is limitation john Mason, nimejifunza adui mkuu wa maisha yangu ni Mimi mwenyewe. Kwa kuwa niliumbwa Mimi kama Mimi lakini cha ajabu nataka niwe kama fulani ambaye sio Mimi. Najitambua sasa na ninaishi Mimi kama Mimi si kufanana na MTU mwingine.

Rafiki, hivyo ndiyo vitabu 117 ambavyo vimesomwa na wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA kwa mwaka 2018. Kama ungependa kujijengea tabia ya kujisomea vitabu pamoja na kuweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako karibu sana ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Kupata maelezo ya kujiunga tuma ujumbe kwa njia ya wasap kwenda namba 0717396253 wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA. Karibu sana.

vitabu softcopy

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge