Rafiki yangu mpendwa,

Nimekuwa nasema kitu kimoja, kama umeajiriwa na unalalamika kwamba kipato hakikutoshi au kazi huipendi, basi unapaswa kuwa na biashara ya pembeni wakati unaendelea na ajira yako.

Kama unailalamikia ajira au kipato na huna biashara ambayo unaifanya kwa pembeni, unajipotezea muda mwenyewe na hata wale ambao wanakusikiliza ukiwa unalalamika.

Hakuna malalamiko yatakayokusaidia, hasa inapokuja kwenye kazi na kipato, kitu pekee kitakachokusaidia wewe ni hatua unazochukua kutoka pale ulipo sasa.

Na baada ya kuona hili ni changamoto kwa wengi, niliandika kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA, ambacho kimetoa majawabu ya changamoto ya muda na kipato katika kuendesha biashara ukiwa bado umeajiriwa. Kama hujasoma kitabu hiki hatua ya kwanza unayopaswa kuchukua sasa ni kukisoma, kwa sababu unakwama kwa maarifa haya unayoyakosa.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

Katika makala ya leo, tunakwenda kuangalia kwa kifupi jinsi unavyoweza kufanya biashara kwa mafanikio makubwa ukiwa bado umeajiriwa.

Na msomaji mwenzetu alituandikia kuomba ushauri kama ifuatavyo;

“Mimi ni mwajiriwa nataka kufanya biashara muda wa kuisimamia biashara ni mdogo lakini mtaji pia ni mdogo nina shilingi laki nne tu. Naomba ushauri Wa biashara nitakayoifanya Bila kuathiri ajira yangu na ambayo yaweza kunipa faida asante” – Emmanuel D. C.

Rafiki, nianze kwa kusema biashara yoyote ile unaweza kuifanya ukiwa bado umeajiriwa. Lakini kuna vikwazo viwili ambavyo vitakupa wakati mgumu katika kuamua ni biashara gani ufanye.

Kikwazo cha kwanza ni muda, kama ajira yako inachukua muda wako mwingi, au kama unafanya kazi mbali na unapotaka kufanyia biashara yako, utakwamba kwenye biashara nyingi zinazohitaji usimamizi wa karibu na muda mwingi.

Kikwazo cha pili ni fedha, kiasi cha mtaji unachoweza kuwekeza kwenye biashara kitaamua ni biashara ya aina gani unaweza kufanya. Ukiwa na mtaji mkubwa unaweza kuanzisha biashara yoyote unayotaka na kuweka mifumo ambayo itakusaidia kusimamia biashara hiyo hata ukiwa mbali. Lakini kama mtaji wako ni kidogo, utalazimika kuanza na biashara ndogo ambayo inakutegemea wewe kwenye uendeshaji.

Sasa leo nakwenda kushauri eneo moja; UNA MTAJI KIDOGO NA HUNA MUDA WA KUTOSHA KUSIMAMIA BIASHARA, je unawezaje kufanikiwa kwenye biashara ukiwa umeajiriwa?

Jibu ni kwa kuanzisha biashara ambayo unaweza kuifanya wewe mwenyewe kwa muda mfupi ambao unao.

Na ni vizuri biashara hii ukawa unaifanyia nyumbani kwako au kuwafuata wateja kule walipo badala ya kuingia gharama za kukodi eneo la biashara ambalo hutalitumia kwa muda mwingi.

Kwa zama tunazoishi sasa, mtandao wa intaneti umerahisisha sana ufanyaji wa biashara. Unaweza kutangaza biashara yako kwa wengi na ukaendesha biashara bila hata ya kuwa na eneo la kufanyia biashara hiyo.

Kwa mfano kwa rafiki yetu aliyetuomba ushauri, kwa mtaji wa laki nne huku akiwa hana muda mwingi wa kusimamia biashara yake, nashauri achague huduma au bidhaa ambayo watu wana uhitaji nayo, kisha kuwatangazia watu kupitia mtandao na hata mawasiliano yao, na wale watakaotaka anawapelekea bidhaa au huduma hiyo.

Kwa njia hii unaweza kuuza bidhaa kama mavazi, vyakula na hata vitabu. Kadhalika unaweza kutoa huduma kama za ushauri, kufundisha na hata wakati mwingine kutoa nguvu zako na uzoefu wako kwa wale wenye uhitaji. Kwa mfano kama wewe ni mhasibu ambaye umeajiriwa, kwa muda wako wa ziada unaweza kuwatafuta wafanyabiashara wadogo wadogo na ukawasaidia kuandaa hesabu zao. Kama ni mwanasheria unaweza kuwasaidia watu kuandaa mikataba mbalimbali na hata kuwashauri vyema kwenye hatua wanazokwenda kuchukua, ambazo zinaweza kuwapa changamoto za kisheria.

Ninachokuambua hapa ni hiki kimoja rafiki, unapoanza biashara ukiwa kwenye ajira, huku mtaji ukiwa ni changamoto, unapaswa kukazana kufanya kile ambacho kinakuhusisha wewe moja kwa moja. Lakini kadiri utakavyoendelea kukua zaidi utapata nafasi ya kuwa na watu wa kukusaidia na hata ukawa na eneo la kufanyia biashara yako. Lakini mwanzoni, biashara ni wewe na pale ulipo ndipo biashara yako ilipo, tumia mitandao ya kijamii na mawasiliano uliyonayo katika kuwafikia wateja zaidi.

Chagua leo ni bidhaa au huduma gani unayoweza kuwasambazia watu kwa muda mchache unaokuwa nao kwenye siku yako, na nguvu yako kubwa weka kwenye kujitangaza na kuwafikia watu wengi zaidi.

Na kama bado hujasoma kitabu cha BIAHSARA NDANI YA AJIRA, kipate na ukisome sasa. Gharama yake ni tsh elfu 10 (10,000/=) na kitabu ni softcopy kinatumwa kwa email. Kukipata tuma fedha tsh elfu 10 kwa namba 0717396253 au 0755953887 kisha tuma email yako na utatumiwa kitabu.

Usikubali ajira yako iwe kikwazo kwa mafanikio yako, anza biashara ya pembeni na muda wako wote wa ziada peleka kwenye biashara hiyo, anza na mtaji kidogo au hata bila ya mtaji kabisa na kwa malengo na mipango utaweza kupiga hatua zaidi.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog