Rafiki yangu mpendwa,

Bidhaa zote za kielektroniki pamoja na huduma zake, huwa zinakuja kwa matoleo. Linatoka toleo la kwanza, kisha linakuja la pili ambalo ni bora kuliko la kwanza, linaenda la tatu ambalo ni bora zaidi na mlolongo unaenda hivyo. Najua unatumia simu na unajua hili vizuri, kwamba simu uliyotumia miaka 5 au 10 iliyopita, haiwezi kabisa kuwa na uwezo sawa na simu unayotumia sasa.

Hiki ndiyo kinatufanya tusizichoke bidhaa na huduma hizi za kielektroniki, kwa sababu kila wakati kuna toleo jipya ambalo ni bora kuliko toleo lililopita. Kama makampuni ya simu au kompyuta yangekuwa yanatoa toleo lile lile la bidhaa yao kila mwaka, yasingeweza kufanikiwa, tusingesukumwa kununua simu mpya na maisha yetu yasingekuwa bora kwa namna yanavyoendelea kuwa.

evolution-phone-min

Lakini sisi wenyewe tumekuwa tunayachoka maisha yetu na kuona hayana jipya kwa sababu tumekuwa hatujibadili na kuwa toleo jipya kila mara. Tumekua tunaishi maisha yale yale, kufikiri kwa namna ile ile na kutegemea kupata matokeo ya tofauti. Hii ni sawa na kulazimisha simu ya kawaida ifanye kama simu janja kwa sababu tu umekaa nayo muda mrefu.

Rafiki, kitu kikubwa nilichojifunza kwenye maisha yangu mpaka sasa ni hiki; ili kufanikiwa nje lazima kwanza ufanikiwe ndani. Mafanikio ya nje ni matokeo ya mafanikio ya ndani. Hivyo kama ulipo sasa siyo unapotaka kuwa, lazima kwanza ubadilike ndani yako ndiyo mabadiliko hayo yaweze kutokea nje yako.

Na hili ndiyo limekuwa kikwazo kikubwa kwa wengi, wengi wamekuwa wanakazana kubadilika nje kabla hawajabadilika ndani, kitu ambacho kimekuwa hakiwaletei matokeo wanayotegemea.

MAKIRITA 3.1

Kwa msingi huu wa kuwa toleo jipya kila wakati, nimekuwa nachukulia kila mwaka wangu mpya wa maisha hapa duniani kama kipindi cha kuwa mpya, nakuwa toleo jipya la mimi mwenyewe.

Leo tarehe 28/05/2019 ni siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwangu. Siku kama ya leo mwaka 1988 ndipo nilizaliwa, hivyo leo nimetimiza miaka 31 ya kuwa hapa duniani.

SAMSUNG CAMERA PICTURES
Kwenye semina ya KISIMA CHA MAAARIFA 2018

Kwa miaka hii 31 ya kuwa hapa duniani, naweza kusema nimebahatika kujifunza mengi, kujaribu mengi na hata kukutana na wengi ambao wamekuwa sehemu ya mimi kujifunza na kupiga hatua zaidi.

Katika kuwa bora zaidi kwenye maisha yangu, na kwa kutumia utaratibu wa bidhaa na huduma za kielektroniki, nimekuwa najitathmini kila ninapoelekea kuingia kwenye mwaka mpya wa maisha yangu.

Nimekuwa naangalia kila ambacho ninakifanya kwenye maisha yangu, naangalia matokeo yake na thamani yake kwangu na kwa wengine pia na kisha kuja na mpango wa mabadiliko au maboresho ili kufanya kwa ubora zaidi. Na hapa ndipo ninapokuwa toleo jipya la mimi mwenyewe.

Katika mwaka wangu huu mpya wa 31 kwenye maisha, nimeupa namba ya toleo ambayo ni 3.1 (tatu nukta moja). Huu utakwenda kuwa mwaka bora na wa kipekee sana kwangu, kwa sababu nimejiandaa kuwa wa tofauti kabisa na nilivyokuwa huko nyuma.

Nakukaribisha sana kwenye toleo hili jipya la maisha yangu, twende pamoja, tukijifunza, kuhamasika na kuchukua hatua ili maisha yetu yaweze kuwa bora sana.

MALENGO YANGU MAKUBWA MAWILI.

Rafiki yangu mpendwa, kama umekuwa na mimi kwa muda sasa unayajua malengo yangu makubwa mawili, kwa sababu nimekuwa nayasema mara kwa mara bila ya hofu wala wasiwasi.

Nina malengo makubwa mawili kwenye maisha yangu, ambayo najitoa kila siku kuhakikisha nayafikia malengo hayo.

Lengo la kwanza ni kuwa bilionea mpaka kufikia mwaka 2028. Hili ni lengo kubwa la kwanza, ambapo nategemea kuwa bilionea. Na njia pekee ya kufika kwenye lengo hili ni kutoa thamani zaidi kwa wengine kupitia yale ninayofanya. Nimekuwa nakuambia kwamba sijaweka lengo hili kwa sababu ya fedha, bali nimeliweka kama lengo la kunisukuma zaidi niweze kutumia uwezo wote uliopo ndani yangu na pia niweze kuwagusa watu wengi zaidi. Sina wasiwasi juu ya mimi kufikia lengo hili.

Lengo la pili ni kuwa raisi wa Tanzania mwaka 2040. Hili ni lengo la pili kubwa sana ambalo nalifanyia kazi. Naipenda sana nchi yangu Tanzania na ninawapenda sana wananchi wenzangu wa Tanzania. Na ndiyo maana sehemu kubwa ya maarifa ninayoandaa na kutoa kila siku yanapatikana bure kabisa kwenye mtandao wa AMKA MTANZANIA. Pamoja na juhudi ambazo zimekuwa zinafanywa na viongozi mbalimbali ambao tunawapata, ninaamini kuna kitu kimoja kinakosekana kwa Watanzania ili tuweze kupiga hatua kubwa kama taifa. Na kitu hicho ni mabadiliko makubwa ya kifikra na kimtazamo ya mtu mmoja mmoja. Nimekuwa naona jinsi ambavyo wachache wanaokutana na kazi zangu wanabadili maisha yao baada ya kubadili fikra na mitazamo yao. Watu ambao wamekuwa kwenye madeni miaka mingi na kuamini vipato hakitoshelezi na hivyo hawawezi kuweka akiba, wameweza kutoka kwenye madeni na kuwa na akiba. Watu walioamini hawawezi kuanzisha biashara kwa sababu hawajui, hawana mtaji au hawana muda, wameweza kuanzisha biashara na kufanikiwa sana. Hivyo ninaamini nikipata nafasi ya juu kabisa ya uongozi kwenye nchi yetu, yaani kuwa Raisi, nitaweza kuchoche mabadiliko haya kutokea kwa watu wengi zaidi.

Rafiki, hayo ndiyo malengo yangu makubwa mawili, ambayo nayatumia kuchuja kila ambacho ninapanga kufanya na kila fursa ambayo inakuja mbele yangu. Sifanyi kitu ambacho hakinisogezi karibu na malengo hayo, na pia sifanyi kitu ambacho kitanizuia kufikia malengo hayo.

Nimekuwa nakusihi na wewe rafiki yangu uwe na malengo makubwa sana ya maisha yako, malengo ambayo mtu yeyote wa karibu yako akiyasikia atashtuka na kukuambia hayawezekani, na hapo upate msukumo wa kuyafanyia kazi zaidi. Kama una malengo ambayo hayamstui mtu yeyote, jua malengo hayo ni madogo sana na hayatakufikisha mbali.

KAZI YANGU NI WEWE.

Rafiki yangu, nina ahadi moja kubwa sana kwako kwenye toleo langu jipya la MAKIRITA 3.1. Kama nilivyokuambia, kila mwaka wangu mpya ni toleo jipya la maisha yangu na ninakuwa mpya kabisa kwenye yale ninayofanya na hatua ninazochukua.

Kwenye toleo hili la 3.1 ahadi yangu kwako ni hii; KAZI YANGU KUU NI WEWE.

Ndiyo rafiki yangu, pamoja na majukumu makubwa niliyonayo kila siku, kipaumbele changu cha kwanza ni wewe. Wewe ndiye jukumu langu kuu la kwanza kwenye maisha yangu, wewe ndiye unayeniamsha mapema zaidi kila siku, wewe ndiye unayenisukuma nitafute maarifa bora zaidi kila siku.

Kwa kipindi ambacho nimekuwa naendesha kazi hii ya uandishi, ushauri na ukocha, nimeweza kuona watu wengi wakibadilika sana kwenye maisha yao. Nimepokea shuhuda nyingi mno za jinsi ambavyo watu wamebadilika, kutoka hali za chini sana na kwenda hali za juu zaidi.

Hivyo kwenye toleo jipya la maisha yangu nakwenda kuweka nguvu zaidi kuhakikisha maisha yako wewe rafiki yangu yanakuwa bora sana. Nitakwenda kukuandalia maarifa bora sana na kukusaidia kujijengea misingi imara sana kwako kufanikiwa zaidi.

MABADILIKO MAKUBWA YA KISIMA CHA MAARIFA.

Moja ya mabadiliko makubwa ninayokwenda kufanya kwenye toleo jipya la maisha yangu ni kwenye KISIMA CHA MAARIFA.

Kwanza hapa ndipo ninapokwenda kuweka sehemu kubwa sana ya nguvu zangu, kwa sababu nimeona kupitia KISIMA CHA MAARIFA watu wengi wameweza kupiga hatua sana.

Lakini kwa miaka mitano sasa KISIMA CHA MAARIFA kimekuwa kinaendeshwa kwa njia ya mtandao pekee. Tumekutana mtandaoni, tunajifunza mtandaoni na hata ushirikiano tunaotengeneza umetegemea mtandao zaidi.

Nimekuwa natafakari kwa kina, na kuona mabadiliko makubwa yanayoendelea kwenye teknolojia na kugundua chochote kinaweza kutokea kwenye mitandao hii na kikaleta madhara makubwa kwenye huduma hii ambayo ndiyo bora kabisa kwa mtu yeyote anayetaka kujikwamua kimaisha.

Hivyo jukumu kubwa ninalokwenda kufanyia kazi ni hili; KUTOA KISIMA CHA MAARIFA MTANDAONI NA KUKILETA KWENYE UHALISIA, KWENYE MAISHA YETU YA KILA SIKU.

Hapa simaanishi kwamba hatutakuwa tena na mafunzo ya mtandaoni, mafunzo hayo yataendelea kuwepo, tena kwa ubora wa hali ya juu sana.

Lakini pia tutakwenda kutengeneza mtandao huu wa mafanikio nje ya mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii.

Tunakwenda kuwa na Klabu za KISIMA CHA MAARIFA ambazo kwa kuanza zitakuwa kwa ngazi ya mikoa. Yaani kila mkoa ambapo kuna wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, wanatengeneza klabu yao ambapo watakuwa wanakutana ana kwa ana, kujifunza, kuhamasishana na kusimamiana ili kuweza kupiga hatua zaidi.

Klabu hizi zitakuwa na utaratibu wa uendeshaji, kukutana na hata shughuli nyingine ambazo wanachama watazifanya kwa pamoja. Lengo kuu likiwa ni moja, kumsukuma kila mwanachama kuweza kupiga hatua zaidi.

Mimi kama Kocha na kiongozi mkuu wa KISIMA CHA MAARIFA, nitapata nafasi ya kutembelea kila klabu na kukutana na wanachama ana kwa ana, kuona maendeleo ya kila mwanachama na klabu kwa ujumla na kuweka mipango na mikakati ya kupiga hatua zaidi kwa kila mwanachama na kwa klabu pia.

Klabu hizi zitakuwa na nguvu kubwa sana ya kumsukuma kila mtu kupiga hatua, kwa sababu unapozungukwa na wengine wanaopiga hatua, na ambao watakuhoji kama hupigi hatua, basi utajilazimisha kupiga hatua.

Klabu hizi pia zitakuwa mchango kwa maendeleo ya jamii zinazotuzunguka kupitia shughuli mbalimbali ambazo zitafanywa na kila klabu. Klabu hizi zitajihusisha na shughuli mbalimbali za kijamii kama sehemu ya kutoa mchango kwa jamii inayotuzunguka.

Hii ni kazi kubwa iliyopo mbele yetu kwa mwaka huu 2019/2020 na nina imani tutashirikiana vizuri katika kuitekeleza.

Naomba maoni na ushauri wako wa namna gani tunaweza kuzifanya klabu hizi kuwa bora zaidi. Tayari nina mipango mizuri ya jinsi klabu hizi zitakuwa, lakini kwa kuwa ni kitu chetu sote, naomba na wewe rafiki yangu uchangie namna unavyopendekeza klabu hizi ziwe. Niandikie maoni na ushauri wako kwa email kwenda amakirita@gmail.com au kwa wasap kwenda namba 0717396253.

HATUA KUBWA YA WEWE KUCHUKUA ILI TUWE PAMOJA KWENYE TOLEO HILI LA 3.1

Rafiki yangu mpendwa, nimeshakueleza nia yangu kubwa ya mwaka wangu huu mpya wa maisha, nia ya kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Kwa sababu nimegundua ndipo uwezo wangu mkubwa ulipo, lakini pia ndiyo kitu pekee kitakachoniwezesha kufikia malengo yangu makubwa mawili.

Ili niwe bilionea, ninahitaji kuwatengeneza mabilionea wengi zaidi. Hivyo nimejitoa kuhakikisha wewe unakuwa bilionea, kwa sababu ndiyo njia pekee ambayo na mimi nitakuwa bilionea.

Na pia nikishawatengeneza mabilionea wengi, ambao wanagusa maisha ya wengi, ni rahisi kwa lengo langu jingine la kuwa raisi kufikiwa, kwa sababu kadiri ambavyo ninakuwa sehemu ya kuwagusa wengi, ndivyo inavyokuwa rahisi kwa wengi hao kunipa nafasi ya kuwaongoza zaidi.

Hivyo rafiki yangu mpendwa, kama upo tayari twende pamoja kwenye safari hii, kuna hatua moja pekee ambayo unapaswa kuichukua sasa.

Hatua hiyo ni kuwa mwanachama wa kudumu wa KISIMA CHA MAARIFA. Kama bado hujawa mwanachama kabisa, fanya uwezalo uwe mwanachama sasa, usikubali chochote kile kikuzuie kuwa mwanachama, kwa sababu kwa sasa siyo tu utapata mafunzo mtandaoni, bali pia utapata nafasi ya kukutana na wengine wanaotaka kufanikiwa, wanaopatikana kwenye mkoa ambao upo.

Kama tayari wewe ni mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, basi hakikisha kwa namna yoyote ile hutoki, hakikisha umepiga kambi na hakikisha una ndoto kubwa sana unazozifanyia kazi kwenye maisha yako. Tuendelee kuwa pamoja kwenye safari hii, ninaamini sana kwako wewe kupiga hatua, na ukishapiga hatua, na mimi nitapiga hatua zaidi.

Kwa wale ambao hawajajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, ada kwa kipindi hiki ni shilingi laki moja (100,000/=) ambayo ni ada ya mwaka mzima inayokuwezesha kuwa kwenye KISIMA CHA MAARIFA na kujifunza kila siku. Lipa sasa ada yako kwa namba 0717396253 au 0755953887 kisha tuma ujumbe kwa wasap kwenda namba 0717396253 na utaunganishwa na KISIMA CHA MAARIFA.

HUDUMA NYINGINE NINAZOTOA.

Rafiki, pamoja na KISIMA CHA MAARIFA kuwa huduma kuu ninayoshauri kila mtu mwenye kutaka kupiga hatua awepo, zipo huduma nyingine muhimu sana ninazotoa ambazo nashauri uweze kunufaika nazo pia.

  1. Uchambuzi wa kina wa vitabu kupitia channel ya telegram ya TANO ZA JUMA. Hapa kila juma unapata uchambuzi wa kina wa vitabu. Kujiunga na channel hii ni bure kwa wiki moja na baada ya hapo unalipa elfu moja kila wiki. Kujiunga tuma ujumbe sasa kwa njia ya telegram app wenye maneno TANO ZA JUMA kwenda namba 0717396253 na utaunganishwa.
  2. Usimamizi wa karibu wa wewe kupiga hatua zaidi kupitia huduma ya UKOCHA BINAFSI. Huwa nafanya kazi na mtu mmoja mmoja kumwezesha kuondoka pale alipokwama na kuweza kupiga hatua zaidi. Nina huduma ya ukocha binafsi ambapo nafanya kazi kwa karibu na mtu anayetaka kupiga hatua zaidi. Kupata huduma hii niandike ujumbe kwa wasap kwenda namba 0717396253.
  3. Vitabu vya mafanikio na hamasa, kupata vitabu hivi fungua hapa; https://amkamtanzania.com/vitabu/
  4. Huduma za ukocha wa pamoja. Hapa huwa ninakuwa na vikundi vidogo vidogo ambavyo huwa navikochi kwa pamoja. Kuna kikundi cha wafanyabiashara ambao ninawakochi kwa pamoja na pia kikundi cha wanaofanyia kazi malengo yao makubwa. Pia zipo huduma kama GAME CHANGERS ambapo watu wanajisukuma kupiga hatua zaidi kwenye maisha yao. Nafasi za kujiunga na huduma hizi huwa zinatolewa pale huduma fulani inapoanza. Hivyo kama tutakuwa pamoja kwenye KISIMA CHA MAARIFA utapata nafasi ya kunufaika zaidi na huduma hizi.
  5. Semina ya ana kwa ana kila mwaka. Kila mwaka nimekuwa naandaa semina kubwa ya kukutana ana kwa ana na kujifunza pamoja wanamafanikio wote. Hii ni njia ya kujifunza, kuhamasika na hata kukuza mtandao wa mafanikio yako. Hii ni semina ambayo yeyote anayetaka mafanikio hapaswi kuikosa. Kwa kuwa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA unapata taarifa kuhusu semina hii na kuweza kushiriki.
  6. Bila ya kusahau huduma za mafunzo ya bure kabisa ninayoshirikisha kupitia mtandao wa AMKA MTANZANIA pamoja na mfumo wetu wa EMAIL. Kila siku tembelea amkamtanzania.com kujifunza. Pia hakikisha umejiandikisha kwenye mfumo wetu wa email na kila siku tembelea email yako kujifunza kupitia masomo yanayotumwa kwenye email yako. Kujiandikisha fungua hapa; https://amkamtanzania.com/jiunge/

Rafiki, nichukue nafasi hii kukukaribisha sana kwenye toleo hili jipya la maisha yangu, toleo la 3.1. Naamini wewe ndiye utakayeniwezesha mimi kufikia malengo makubwa mawili niliyojiwekea kwenye maisha yangu, na ndiyo maana nimejitoa sana kuhakikisha wewe unakuwa bora sana.

Kauli kuu ambayo nimekuwa ninaiishi kila siku ni kutoka kwa aliyekuwa mwandishi na mhamasishaji bora kabisa Zig Zigler ambaye alisema; unaweza kupata chochote unachotaka kwenye maisha, kama utawasaidia watu wengi zaidi kupata kile wanachotaka.

Nimetoa nguvu zangu zote kukusaidia wewe upate unachotaka, kwa sababu najua ukishakipata, na mimi pia nitapata ninachotaka. Niseme karibu sana tuwe pamoja kwenye safari hii.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge