#TANO ZA JUMA #22 2019; Hujavutiwa Bali Umesukumwa, Falsafa Bora Ya Matumizi Ya Mitandao Ya Kijamii, Jinsi Mitandao Inaharibu Akili Yako, Muda Wako Ni Pesa Kwao Na Gharama Ya Kitu Ni Maisha Unayopoteza.

Rafiki yangu mpendwa,

Hongera kwa juma hili namba 22 ambalo tumekuwa nalo kwa mwaka huu 2019. Naamini limekuwa juma bora sana kwako, juma ambalo umepata maarifa sahihi na kuchukua hatua za tofauti katika shughuli zako na maisha yako kwa ujumla.

Nakuchukua nafasi hii kukukaribisha kwenye makala ya TANO ZA JUMA ambapo nimekuandalia maeneo matano muhimu ya kujifunza kutoka kwenye uchambuzi wa kina wa kitabu cha juma husika.

Juma hili tunakwenda kujifunza kwa kina kuhusu madhara ya simu janja (smartphone) pamoja na mitandao ya kijamii. Ni ukweli usiopingika kwamba maendeleo ya teknolojia, ambayo yametuletea simu janja na mitandao ya kijamii yamekuwa na manufaa sana kwetu. Lakini kama tunavyojua, kila chenye manufaa kina madhara yake pia. Matumizi yasiyo na ukomo ya simu janja pamoja na mitandao ya kijamii yameanza kuonesha madhara makubwa kwenye maisha ya wengi. Tutakwenda kujifunza hapa madhara hayo na hatua za kuchukua ili maisha yetu yaweze kuwa bora zaidi.

digital minimalism

Kitabu tunachokwenda kujifunza kwa kina kuhusu madhara haya ya mitandao ya kijamii kinaitwa Digital Minimalism: Choosing a Focused Life in a Noisy World ambacho kimeandikwa na Cal Newport. Cal ambaye ni Profesa wa chuo kikuu nchini marekani, ambaye pia ana taaluma ya TEHAMA, hajawahi kuwa kwenye mitandao ya kijamii maisha yake yote. Pia amekuwa haweki hadharani barua pepe yake au namba yake ya simu. Njia bora ya kuwasiliana naye ni kumwandikia barua au kumtembelea ofisini kwake. Kwa msimamo huu mkali alionao, ameweza kuwa anapata muda wa kufanya kazi zake za kufundisha, na pia kuandika vitabu bora sana. Vitabu vingine alivyoandika ni DEEP WORK na SO GOOD THEY CAN’T IGNORE YOU.

Katika uandishi wake, Cal amekuwa anaegemea upande wa kufanya kile kilicho bora na kuweka umakini kwenye kile unachofanya. Baada ya vitabu vyake vya awali kusisitiza sana hilo, watu walianza kumlalamikia kwamba mitandao ya kijamii ni usumbufu kwao na hivyo hawawezi kuweka umakini kwenye kazi zao. Na hapo ndipo alipokuja na falsafa bora ya matumizi bora ya mitandao ya kijamii anayoiita DIGITAL MINIMALISM. Tunakwenda kujifunza kwa kina kuhusu falsafa hii na jinsi ya kuitumia kwenye maisha yetu.

Karibu kwenye tano za juma, ujifunze kwa kina, uende ukachukue hatua na kuweza kuwa na maisha bora sana.

#1 NENO LA JUMA; HUJAVUTIWA BALI UMESUKUMWA.

Rafiki yangu, kuna kitu kimoja ambacho hujakijua, na wanaomiliki mitandao ya kijamii hawataki ukijue, lakini kwa sababu mimi nakupenda, lazima ukijue kisha uamue mwenyewe kama utachukua hatua sahihi au utaendelea kutumiwa.

Mitandao ya kijamii inashawishi sana kutumia, ukishaanza kutumia mtandao fulani, ukikaa muda mrefu bila ya kuingia unaona kama kuna vitu unakosa, kuna vitu vinakupita, na hivyo ukipata hata muda kidogo tu unatamani kuchungulia ili uone nini kinachoendelea.

Kwa hali kama hii, ni rahisi kujiambia kwamba mitandao hiyo inakuvutia sana kutembelea, yaani unafikiri kutembelea kwako mitandao hiyo ni maamuzi yako binafsi.

Nasikitika kukuambia kwamba unachofikiri siyo kweli, ushawishi mkubwa unaopata wa kutembelea mitandao ya kijamii muda wote siyo kwa sababu umevutiwa na unaamua kwenyewe, bali ni kwa sababu kuna watu wanakusukuma ili utembelee mitandao hii. Kwa maneno mengine ni kwamba unajikuta kila mara unataka kurudi kutembelea mitandao hiyo, siyo kwa maamuzi yako, bali kwa namna ambavyo umetegwa kuitembelea mitandao hiyo.

Hivyo tunaweza kusema mitandao hii imegeuza watumiaji wake kuwa kama misukule, wanajikuta wanaitembelea muda wote lakini hawajui kwa nini wanaitembelea.

Rafiki, kitu ambacho nimekuambia leo utakijua na ufanye maamuzi sahihi kwako ni hiki, mitandao ya kijamii imeajiri watu wenye elimu ya juu sana ambao kazi yao ni kuteka umakini wako. Watu hawa ambao ni mainjinia wa kuteka umakini (ATTENTION  ENGINEERING) wanatengeneza viroboti ambavyo vinafuatilia matumizi yako ya mitandao ya kijamii, kuangalia vitu gani unafuatilia zaidi na unaletewa vitu hivyo zaidi. Ndiyo maana unapoingia kwenye mitandao hii, kila ukitaka kutoka unaona kitu kingine kizuri zaidi, ukijiambia sasa natoka kinakuja kitu kingine kizuri zaidi.

Wakati wewe unatembelea mitandao hii usiku na mchana ukiamini unaamua hivyo mwenyewe, wapo watu ambao wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha unaendelea kutembelea mitandao hii. Kwa sababu kama nitakavyokuambia kwenye kipengele namba 4, MUDA WAKO = FEDHA ZAO.

Rafiki yangu mpendwa, makampuni haya makubwa ya mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, Twitter na mingineyo siyo marafiki zako, bali wale wanakutumia wewe kama bidhaa yao kwa ajili ya kuwauzia wanaotangaza kwenye huduma zao hizo. Hivyo ili wapate fedha zaidi, lazima wewe utumie muda zaidi kwenye huduma zao, na hapo ndipo wanafanya kila namna kuhakikisha unanasa kwenye mitandao yao na hauchukui muda mrefu kabla hujarudi tena.

Kwenye uchambuzi wa kitabu tutajifunza falsafa bora ya matumizi ya mitandao ya kijamii ili uache kutumiwa kama bidhaa kwa watu kujitajirisha.

Mimi binafsi baada ya kujua madhara haya makubwa ya mitandao ya kijamii, nilijiondoa kwenye mitandao yote tangu mwezi mei 2018 na sijawahi kupata utulivu ambao nimeupata baada ya kuondoka kwenye mitandao hii. Na haya ubora wa kazi zangu umekwenda juu zaidi. Siyo lazima ufanye maamuzi magumu kama yangu ya kuondoka kabisa kwenye mitandao hii, lakini unapaswa kuboresha matumizi yako, ukiendelea kama unavyotumia sasa, hutaweza kupiga hatua kwenye maisha yako.

#2 KITABU CHA JUMA; FALSAFA BORA YA MATUMIZI YA MITANDAO YA KIJAMII.

Rafiki yangu mpendwa,

Tuna bahati ya kuishi kwenye zama ambazo mawasiliano yamerahisishwa sana. Hakuna kipindi ambacho dunia imewahi kupata mapinduzi makubwa kama mapinduzi haya ya taarifa.

Hivyo ilitegemewa mapinduzi haya makubwa ya taarifa kuwa msaada kwa wengi na kuwawezesha kupiga hatua zaidi. Ilitegemea mtandao wa intaneti kurahisisha sana mawasiliano na ufanyaji wa biashara. Ilitegemewa simu janja kutuwezesha kufanya majukumu ya kompyuta kupitia simu tunazotembea nazo mkononi.

Pamoja na kwamba manufaa hayo yanaonekana wazi, lakini pia mapinduzi haya yamekuja na madhara ambayo hakuna mtu aliyatarajia. Mwaka 2000, kabla mitandao ya kijamii na simu janja hazijaingia kwenye maisha ya watu, mtandao ulipewa nafasi ya kufanya makubwa na hakuna aliyeweza kufikiri ungekuja na madhara makubwa kwa watumiaji wake.

Lakini miaka kumi baadaye, 2010, mambo yakawa yamebadilika sana. Simu janja zikawa sehemu ya maisha ya kawaida ya watu na mitandao ya kijamii njia kuu ya mawasiliano na kupashana habari.

Hatari kubwa ambayo imeibuka ni usumbufu mkubwa ambao umeletwa kwenye maisha yetu na simu hizi janja pamoja na mitandao ya kijamii. Imekuwa vigumu sana kupata utulivu na umakini wa kuweka kwenye yale mambo muhimu ya maisha yetu. Kila mara tunapata msukumo wa kuingia kwenye mitandao hii, kushirikisha kuhusu maisha yetu au kuangalia nini kinaendelea kwenye maisha yetu.

Tumefika hatua ambayo sisi binadamu tunajishangaa wenyewe, tuna akili kubwa sana ambayo imeweza kutengeneza kompyuta na hata kwenda mwezini, lakini tunashindwa kujizuia kutumia simu janja na mitandao ya kijamii bila ya ukomo.

Tatizo hili limezidi kukua na sasa madhara yake yanakwenda zaidi kwa vijana wanaokulia katika kizazi hiki, wengi wanakosa muda wa kutengeneza mahusiano imara ya kijamii, ya kuwa na watu ana kwa ana kwa sababu muda wao mwingi wanautumia kwenye mitandao ya kijamii.

Kazi pia zimeathirika sana na mitandao hii, watu wengi wanakiri ufanisi na uzalishaji wao kushuka kutokana na matumizi makubwa ya mitandao hii ya kijamii.

Zipo njia mbalimbali za kutatua changamoto hii ambazo zimependekezwa na watu mbalimbali. Ipo njia ya kuachana kabisa na mitandao ya kijamii na simu janja, lakini hii ni njia ambayo inahitaji maamuzi magumu, na kwa mazingira ya wengi ya maisha na kazi, haiwezekani. Mitandao hii inakusaidia kuwasiliana na watu unaofanya nao kazi na biashara, inakusaidia kuwasiliana na familia ukiwa mbali na pia kupata habari muhimu kutoka kwa watu wa muhimu kwako.

Njia nyingine ambayo imejaribu kutumiwa na wengi katika kukabiliana na changamoto hii ni kujizuia kuingia kwenye mitandao hiyo kila muda. Wapo ambao wamekuwa wanaweka programu za kuwazuia wasitumie mitandao kwa muda fulani. Wengine wameondoa kabisa zile taarifa ambazo zinakuja kwenye simu pale ambapo ujumbe mpya umeingia. Lakini njia hii kwa wengi imeshindwa, kwa sababu kuendelea kuwa na mitandao hiyo kwa ukaribu kwenye simu janja, ni sawa na mtu anayetaka kuacha kutumia pombe kuhifadhi pombe ndani kwake, hawezi kujizuia kutumia.

Mwandishi Cal Newport baada ya kutafakari hili kwa kina amekuja na falsafa bora ya matumizi mazuri ya mitandao hii, ambayo itakuwa na manufaa kwetu na kuondokana na madhara ya mitandao hii. Falsafa hii haibadili kitu kimoja kwenye matumizi yetu ya simu janja na mitandao ya kijamii, bali inabadili mfumo wetu mzima wa maisha na jinsi tunavyoichukulia na kuitumia mitandao hii. Falsafa hii anaiitwa DIGITAL MINIMALISM na ameieleza kwenye kitabu chake ambacho tunakwenda kukichambua kwa kina hapa.

MAANA YA DIGITAL MINIMALISM.

Digital Minimalism ni falsafa ya matumizi ya teknolojia ambapo mtu unaweka mkazo kwenye huduma chache za kidigitali zenye manufaa kwako na zinazoendana na misingi yako na kuchagua kupuuza huduma nyingine zisizokuwa na manufaa kwako.

Kwa falsafa hii, huachi kabisa kutumia simu janja na mitandao ya kijamii, badala yake unaanza na malengo na misingi yako ya maisha, kisha unaangalia ni huduma zipi za kidigitali ambazo zinaweza kuwa na manufaa kwako.

Kwa njia hii, utachagua huduma chache ambazo zina manufaa kwako, lakini pia utazitumia kwa njia ambayo inakuwa na manufaa kwako. Huwi tena kama wale ambao kila mtandao mpya wa kijamii unaokuja wanajiunga, kipa programu mpya inayogunduliwa wanajiunga nayo kwa sababu kila mtu anatumia.

Hii ni falsafa bora sana ya kuitumia kwenye maisha yako na shughuli zako. Mfano kwangu binafsi, licha ya kujitoa kwenye mitandao yote ya kijamii, yaani Facebook, Instagram, Twitter na Linkedin ambayo nilikuwa natumia, nimebaki natumia mitandao mikuu miwili, Whattsapp na Telegram, ambayo hii ina manufaa kwangu kwa sababu naitumia kufundisha watu maarifa haya ninayotoa. Mitandao hii miwili inaendana na malengo na misingi yangu ya maisha ya kujifunza na kufundisha wengine. Kwenye wasap naendesha progamu ya KISIMA CHA MAARIFA ambapo ina mafunzo ya kila siku pamoja na huduma nyingine za ukocha. Kwenye Telegram naendesha channel ya TANO ZA JUMA ambapo kila juma nashirikisha kitabu na uchambuzi wake wa kina. Isingekua kwa huduma hizo, hata mitandao hiyo miwili ningeacha kabisa kuitumia.

MISINGI MITATU YA DIGITAL MINIMALISIM.

Kila falsafa huwa ina misingi yake. Falsafa ya DIGITAL MINIMALISM ina misingi mikuu mitatu.

Msingi wa kwanza; matumizi ya digitali yasiyo na ukomo ni gharama kwako.

Kukosa ukomo kwenye matumizi yako ya huduma za kidigitali kunakugharimu sana. Kuwa kwenye mitandao mingi ya kijamii na muda wote kutumia simu janja yako kunavuruga umakini wako na hivyo inakuwa na madhara kwako kuliko faida.

Msingi wa pili; kuweka vipaumbele ni muhimu.

Kwa kuwa huduma hizi za kidigitali ni nyingi, njia pekee ya kuzuia zisitugharimu ni kuweka vipaumbele katika kuzitumia. Badala ya kutumia kila huduma inayopatikana, unachagua huduma ambazo zinaendana na wewe, zinachangia kwenye kufikia malengo yako na kuendana na misingi yako.

Msingi wa tatu; kuwa na kusudi kunaridhisha.

Kinachofanya huduma hizi za kidigitali kuwa mzigo zaidi kwetu ni pale ambapo tunajikuta hatuwezi kuacha kuzitumia, hapo tunakuwa tumegeuka misikule wa wenye mitandao hiyo. kwa msingi huu wa tatu, unachagua huduma ambayo unataka kuitumia na kwa muda ambao unataka kuitumia na kuepuka matumizi ya utegemezi. Kujua unatumia kitu kwa maamuzi yako kunakupa hali ya kuridhika kuliko unapotumia kwa sababu huwezi kuacha kutumia. Kuchagua mwenyewe ni uhuru, kulazimika kutumia ni utumwa.

FANYA USAFI WA KIDIGITALI.

Hatua ya kwanza ya kuishi kwa falsafa ya DIGITAL MINIMALISM ni kufanya usafi wa kidigitali. Kama umekuwa unatumia teknolojia bila ya kujitathmini basi utakuwa umezoa uchafu mwingi sana na kuujaza kwenye maisha yako ya kidigitali. Utakuwa unatumia mitandao ya kijamii mingi ambayo haina manufaa yoyote kwako, unatumia kwa kuwa wengine wanatumia.

Hatua ya kwanza kabisa kuchukua ni kufanya usafi wa kidigitali ambapo utafuata hatua hizi tatu;

Hatua ya kwanza; tenga siku 30 ambapo utaacha kutumia teknolojia zote ambazo siyo za lazima kwako. Kama teknolojia unayotumia sasa haina ulazima kwamba, yaani kama maisha hayatasimama kwa kuacha kuitumia, basi jipe siku 3o za kutokutumia kabisa teknolojia hiyo. Hapa mitandao mingi ya kijamii unayotumia sasa inaingia kwenye kundi hili. Usihofu, ni jaribio la siku 30 tu, baada ya hapo utakuwa tayari kurudi kwenye matumizi ambayo utayachagua kwa ubora zaidi.

Hatua ya pili; ndani ya siku 30 ambazo umeacha kutumia teknolojia ambazo umekuwa unatumia kila siku, tafuta vitu unavyopenda kufanya. Kutokana na matumizi ya kupitiliza ya teknolojia, wengi tumesahau ni vitu gani tunapenda. Sasa ndani ya siku 30 ambazo hutumii teknolojia, tafuta vitu vya kianalojia unavyopenda kufanya. Inaweza kuwa kuandika, kujisomea, kufanya kazi za mikono, michezo, kupata muda wa kuongea na watu wengine, kuandika na kuimba muziki, kucheza vyombo vya muziki na hata kuwa peke yako. Ni muhimu kujua vile unavyopenda kufanya kwa sababu ndiyo vitachukua muda unaouokoa sasa kwenye kuboresha matumizi yako ya teknolojia.

Hatua ya tatu; baada ya siku 30 kuisha, ambapo hujatumia kabisa teknolojia ambazo hazikuwa za lazima, anza kurudisha teknolojia kwenye maisha, ila tu ziwe zina mchango kwa wewe kupiga hatua zaidi kwenye maisha. Usirudishe kila teknolojia, bali jiulize kwa siku 30 kipi kikubwa umekosa kwa kutokutumia teknolojia hiyo, kama hakuna basi achana nayo moja kwa moja. Unapochagua teknolojia unazorudisha kwenye maisha yako, anza na vile vitu ambavyo umegundua unapenda kuvifanya kwenye hatua ya pili hapo juu, kisha jiulize teknolojia unayoirudisha inachangiaje kwako kupiga hatua zaidi kwenye kile unachopenda kufanya.

Vigezo vya kuzingatia wakati unachagua kurudisha huduma za kidigitali kwenye maisha yako.

Baada ya kufanya zoezi la kuacha huduma za kidigitali zisizo za lazima kwa siku 30, utagundua jinsi ambavyo umekuwa unapoteza maisha yako kwa mambo yasiyo muhimu. Baada ya kumaliza zoezi hilo, usikubali tena kurudi ulikotoka. Badala yake tumia vigezo hivi vitatu kuchagua huduma za kidigitali utakazorudisha kwenye maisha yako.

Kigezo cha kwanza; iwe inachangia kwenye kusudi kuu la maisha yako, iwe inaendana na misimamo yako na kukuwezesha kufikia malengo yako.

Kigezo cha pili; matumizi yake yawe ni bora kwa kusudi ulilonalo, yaani namna utakavyotumia teknolojia hiyo, isiwe kikwazo kwako kuwa na maisha unayotaka.

Kigezo cha tatu; uweze kujiwekea utaratibu wa jinsi ya kuitumia na kwa wakati gani, na siyo kugeuka kuwa kitu unachotumia muda wote. Kulingana na mchango wa teknolojia hiyo kwenye maisha yako, unapaswa kuwa na utaratibu maalumu unaoufuata kwenye kuitumia na usikubali tena kuwa mtumwa wa teknolojia hizi.

USIBONYEZE KITUFE CHA ‘LIKE’.

Wakati mitandao mingi ya kijamii inaanza hakuna mtu aliwahi kufikiri ingefikia utawala iliyonayo sasa kwenye maisha ya wengi. Mfano toleo la mwanzo la mtandao wa Facebook ambao ulikuwa unaitwa thefacebook halikuwa na kitufe cha like. Lakini baadaye walikuja na ugunduzi wa kitufe hicho cha like na ndipo mambo yalibadilika kabisa.

Kwa kufuatilia matumizi ya watu ya mitandao hii, kitufe cha like kimechangia sana watu kuwa watumwa wa mitandao hii. Sasa hivi mtu akiweka ujumbe au picha mtandaoni, kipimo cha umaarufu wa kile alichoweka ni kuangalia ‘likes’ ngapi amepata.

Kubonyeza kitufe cha like ni njia rahisi na ya mkato kuwasiliana na mtu, lakini njia hii ina madhara kwetu kama binadamu. Sisi binadamu tuna ubongo mkubwa ambao una kazi nyingi pale tunapokuwa na mazungumzo na watu, huwa hatusikilizi tu, bali pia tunaangalia matendo ya wale tulionao. Matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii na uwepo wa njia za mkato kama likes unaharibu uwezo mkubwa tulionao.

Kwenye falsafa mpya ya digital minimalism, mwandishi anatoa hoja kwamba tuache kutegemea njia rahisi za mawasiliano na badala yake tujenge utamaduni wa kufanya mazungumzo na wale ambao ni muhimu kwetu. Tunapaswa kuweka vipaumbele kwenye mazungumzo yenye maana badala ya mawasiliano ya haraka yasiyokuwa na mchango katika kuboresha mahusiano yetu.

Katika kufanyia hili kazi, mwandishi anashauri mtu uchukue hatua zifuatazo.

  1. Unapotumia mtandao wa kijamii ambao umechagua kuendelea kuutumia, usibonyeze kabisa kitufe cha like, wala usiweka maoni mafupi kama ‘umependeza’, ‘nzuri’ wala usitumie alama nyingine za mawasiliano (emoji) badala yake kama kuna kitu umeona kwa wengine chukua hatua ya kukifuatilia. Mfano umeona rafiki yako wa karibu kaweka picha mtandaoni kwamba amepata mtoto, badala ya kubonyeza like au kuweka maoni ya hongera, funga safari na nenda kwake kumsalimia na kumpa pongezi. Kama yuko mbali piga simu na mpongeze kwa mazungumzo.
  2. Dhibiti mawasiliano unayowanya kwa ujumbe mfupi. Mawasiliano ya ujumbe mfupi yamekuwa yanaingilia sana umakini wetu. Unafanya kazi yako, mara ujumbe mfupi unaingia halafu unaacha kazi na kuujibu. Ukija kurudi kwenye kazi unakuwa umerudi nyuma sana. Badala ya kuruhusu ujumbe mfupi kuvuruga umakini wako, ondoa kabisa vitaarifu vya ujumbe mfupi kwenye simu yako, kisha weka muda maalumu wa kupitia na kujibu jumbe zilizotumwa. Usijenge tabia ya kuwajibu watu ujumbe hapo hapo, hakuna ujumbe mfupi wa dharura, watu wakiwa na dharura kweli huwa wanapiga simu na siyo kutuma ujumbe. Kwenye simu yako unayotumia tukia kitufe cha DO MOT DISTURB na hapo jumbe hazitakusumbua kabisa. Lakini pia unaweza kuboresha na jumbe za watu muhimu kwako zinaingia moja kwa moja.
  3. Tenga muda unaokuwa huru kwa mawasiliano na mazungumzo. Badala ya kuruhusu mawasiliano kuingilia kazi zako za siku, tenga muda, hasa mwisho wa siku yako ambapo ndiyo utafanya mazungumzo yako yote. Kwa mfano unaweza kutenga jioni baada ya kazi kuwa muda wa kutembelea mitandao, kujibu jumbe na kuzungumza na simu. Mtu anapokutumia ujumbe au kukupigia simu muda wa mchana mwambie akupigie baadaye, labda kuanzia saa 11 au saa 12 jioni utakuwa huru kwa mazungumzo. Kwa kuweka utaratibu huu watu watajua muda sahihi wa kuwasiliana na wewe, na utakuwa na siku tulivu ambayo umakini wako umeweka kwenye kazi zako.

RUDISHA BURUDANI KWENYE MAISHA YAKO.

Maendeleo ya teknolojia yameondoa kabisa mkapa baina ya kazi na maisha. Kabla teknolojia haijakua, mtu alikuwa akitoka kazini, anaziacha kazi zote kazini na akienda nyumbani hajihusishi kabisa na mambo ya kazini. Lakini ukuaji wa teknolojia, ujio wa barua pepe na mitandao ya kijamii, unawafanya watu kwenda na kazi zao nyumbani na kutegemewa kupatikana muda wote.

Hili limefanya maisha kukosa kabisa burudani kwa kutokuwepo mpaka baina ya maisha na kazi. Moja ya vitu ambavyo falsafa ya DIGITAL MINIMALISM inatufundisha jinsi ya kurudisha burudani kwenye maisha yetu.

Ili kurudisha burudani kwenye maisha yetu, kwanza lazima tudhibiti matumizi yetu ya mtandao yasiyo na ukomo, na kujihusisha kufanya vitu ambavyo unapenda kufanya lakini siyo sehemu ya kazi.

Hapa unachagua burudani ambayo inakuhitaji kuweka juhudi fulani, badala ya wengi wanaofikiri mitandao ya kijamii ni sehemu ya burudani.

Mwandishi anasema burudani sahihi kwako kuiweka kwenye maisha yako, inapaswa kuwa na vigezo hivi vitatu;

Kigezo cha kwanza; iwe ni kitu ambacho kinakufanya wewe kuchukua hatua fulani na siyo kukaa tu na kufuatilia.

Kigezo cha pili; iwe ni kitu kinachokutaka kutumia ujuzi kuzalisha matokeo fulani yanayoonekana.

Kigezo cha tatu; kiwe ni kitu ambacho kina mfumo unaoeleweka wa kufanya na kinakuweka pamoja na watu wengine.

Katika kuzingatia vigezo hivyo, mwandishi ameshauri baadhi ya vitu tunavyoweza kufanya katika kuhakikisha tunarudisha burudani kwenye maisha yetu.

  1. Tengeneza kitu fulani kila wiki. Kila wiki, tengeneza kitu ambacho kimeharibika nyumbani kwako au kwenye kazi yako. Badala ya kutegemea mafundi kwenye kila kitu, jifunze kutengeneza na kurekebisha vitu mbalimbali nyumbani kwako. Mfano kubadili tairi za gari mwenyewe, kutengeneza bomba mwenyewe, kama una nyumba za mifugo zinahitaji marekebisho fanya mwenyewe. Unapofanya kazi za mikono kama hivi unajisikia vizuri sana.
  2. Jiunge na kitu. Tafuta kikundi au klabu ambayo unaweza kujiunga nayo ambapo kwa pamoja mnafanya shughuli mbalimbali. Inaweza kuwa klabu ya usomaji wa vitabu ambapo mnakutana na kusoma kwa pamoja au klabu nyingine zinazohusiana na mambo mengine. Unapojiunga na klabu ambayo mnakutana angalau kwa wiki mara moja, unapata muda mzuri wa kushirikiana na wengine na hata kuondoka kwenye usumbufu wa dunia. Hili ni wazo ambalo limenisaidia sana kwenye mpango wa kuanzisha Klabu za KISIMA CHA MAARIFA ambalo nalifanyia kazi sasa. Nina imani utakuwa mmoja wa watakaojiunga na klabu hizi kama moja ya kuondokana na usumbufu wa kidigitali.
  3. Kuwa na mpango wa muda unaotumia kwenye burudani na kwenye kuperuzi mitandao. Usiwe mtu wa kufungua mtandao kila wakati, badala yake kuwa na mpango unaofuata, mfano kwenye muda fulani wa siku yako tenga huo ndiyo wa kutembelea mitandao ya kijamii na tembelea mitandao yote muda huo. Muda ukiisha ndiyo imetoka, hutembelei tena. Kadhalika kwenye shughuli zako za kiburudani, usipozipangilia hutapata muda wa kuzifanya.

Rafiki, hii ndiyo falsafa bora ya matumizi sahihi ya teknolojia mpya kwenye maisha yetu, matumizi yenye manufaa kwetu na yanayochangia kwetu kupiga hatua zaidi badala ya kuwa watumwa wa teknolojia hizi.

Kuna kipengele kimoja muhimu sana cha mwisho kutoka kwenye kitabu hiki, ambacho kina hatua tano za kuchukua ili kurudisha uhuru wako uliochukuliwa na hizi teknolojia mpya, yaani simu janja na mitandao ya kijamii. Nitakushirikisha hatua hizo tano kwenye makala ya #MAKINIKIA ambayo itapatikana kwenye channel ya TANO ZA JUMA kwenye mtandao wa telegram. Hakikisha umejiunga na channel hiyo ili usikose hatua hizo muhimu sana katika kurudisha uhuru ulioupoteza. Maelezo ya kujiunga yapo mwisho wa makala hii.

#3 MAKALA YA JUMA; JINSI MITANDAO INAHARIBU AKILI YAKO.

Madhara makubwa kabisa ya mitandao ya kijamii yanaanzia kwenye akili yako. Kwenye ulaji nilikuambia sukari ni madawa ya kulevya, sasa kwenye teknolojia nakuambia tena, MITANDAO YA KIJAMII NI MADAWA YA KULEVYA.

Mitandao hii ina tabia ya kuleta utegemezi mkubwa kwenye akili zetu, lakini pia kututenga na wengine, lakini kama haitoshi, mitandao hii inatutenga na sisi wenyewe.

Sisi kama binadamu tunahitaji kuwa na muda wa kukaa sisi peke yetu, tukiwa na mawazo yetu bila ya usumbufu wowote. Ni katika hali kama hii ya kuwa peke yako ndiyo unaweza kupata mawazo mapya, kutatua changamoto zinazokukabili, kuzijua na kuzidhibiti hisia zako na hata kujijua wewe mwenyewe.

Lakini matumizi yasiyo ya ukomo ya mitandao ya kijamii, yameondoa kabisa nafasi ya sisi kukaa wenyewe na mawazo yetu. Muda wote tupo na simu zetu, tangu tunapoamka mpaka tunaporudi kitandani.

Kwenye makala ya juma nimekushirikisha jinsi ambavyo mitandao ya kijamii inaharibu akili yako na hatua tatu kwako kuchukua ili kuondoa na kuzia madhara haya.

Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hii ambayo ina mwongozo muhimu sana kwako, isome sasa hapa; Hivi Ndivyo Mitandao Ya Kijamii Imeharibu Akili Za Watu Wengi Na Hatua Tatu Za Kuchukua Ili Kunusuru Akili Yako Isiharibiwe.

Pia endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kila siku uendelee kupata maarifa sahihi yatakayokuwezesha kuchukua hatua sahihi kwa mafanikio tako.

#4 TUONGEE PESA; MUDA WAKO NI PESA KWAO.

Rafiki yangu mpendwa, nimekuwa napenda kukuambia sana kauli hii, HAKUNA KITU CHA BURE. Ukiona mtu anakupa kitu bure, jua kuna namna unalipia ambayo wewe hujui au kuna mtu ameshalipa kwa ajili yako. Huu ni msingi ambao ukiweza kuuishi na kuusimamia kwenye maisha yako, utajiepusha na matatizo mengi mno. Mfano huwezi kutapeliwa kama utaishi kwa msingi kwamba hakuna kitu cha bure.

Sasa tuje kwenye mitandao ya kijamii, orodhesha mitandao yote ya kijamii ambayo unaitumia. Je ni Instagram? Facebook? Whattsapp? Twitter? Snapchat? Na mingine zaidi. Swali ni je umekuwa unalipa kiasi gani ili kutumia mitandao hii ya kijamii?

Ukiacha bando (data) unazonunua ili kuweza kuingia mtandaoni, hulipi hata senti moja kutumia mitandao hii. Lakini unaweza kuitumia muda wowote, masaa 24 kwa siku, siku 7 za wiki.

Swali jingine unalopaswa kujiuliza ni je mitandao hii inapataje fedha za kujiendesha. Maana mitandao hii ina wafanyakazi wengi, na ambao ni wasomi kweli kweli, ina rasilimali nyingi na wamiliki wake ni matajiri wakubwa sana duniani. Ukichukua mfano wa mmiliki wa Facebook na Instagram, ambaye ni bilionea mkubwa duniani, ambaye yupo kwenye watu 10 matajiri zaidi duniani. Hizo fedha wanazitoa wapi?

Kama hujawahi kujiuliza swali hili basi leo unakwenda kupata mwanga, na utakufanya uangalie kwa mtazamo tofauti kabisa mitandao hii ya kijamii.

Mitandao ya kijamii inaingiza kipato kupitia MATANGAZO. Mfumo wao wa biashara uko hivi, kusanya watu wengi watumie huduma yako ya mtandao wa kijamii, kisha nenda kwa mtu mwenye biashara na mwambie unaweza kutangaza biashara yako kwenye mtandao wangu ambao una watumiaji wengi, na wanaotumia huduma hiyo kwa muda wao mwingi wa siku.

Sasa kama unavyojua tabia yetu binadamu, huwa tunafanya zaidi kile tunacholipwa ili kufanya. Kwa kuwa makampuni haya yanapata fedha kwa watu kutangaza kupitia mitandao yao, na kwa sababu wingi wa fedha unaamuliwa na wingi wa watembeleaji na muda ambao watembeleaji wanatumia kwenye mitandao hiyo, basi mitandao hii imekuwa inahakikisha inatumiwa na wengi, na ukishaitumia huachi, kila muda unataka kuitembelea. Kama nilivyokuambia kwenye kipengele namba moja, hujavutiwa kutembelea mitandao hii, umesukumwa kuitembelea kila wakati, kwa sababu unavyoitembelea zaidi, ndivyo wenye mtandao wanatengeneza kipato zaidi.

Hivyo basi, MUDA WAKO = PESA ZAO. Muda unaotumia kwenye mitandao ya kijamii ndiyo fedha ambazo zinawafanya wamiliki wa mitandao hiyo kuwa mabilionea wakubwa.

Swali jingine muhimu sana ni je, kwa matumizi yako makubwa ya mitandao ya kijamii, ni manufaa gani unayapata? Najua wengi mnajiambia naungana na marafiki na kujua yanayoendelea. Kama jibu hilo ni kweli, swali jingine litakuwa je unahitaji zaidi ya masaa mawili kwa siku kutembelea mitandao hii? Je kweli unahitaji kila baada ya nusu saa au saa moja kutembelea tena mitandao hii?

Rafiki, nafikiri unapata picha ni jinsi gani tumechagua kuharibu na kupoteza maisha yetu, kuwafaidisha wengine, huku sisi wenyewe tukibaki hatuna kitu.

Nikuache na mbinu moja ya kupima matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwako. Chukulia hili, kama kila dakika unayotumia kwenye mitandao ya kijamii ulikuwa unailipia shilingi elfu moja, je ungekuwa tayari kulipa shilingi ngapi kwa siku kutembelea mitandao hii?

Je ungekuwa tayari kulipa tsh 120,000/= kila siku ili tu utumie mitandao ya kijamii? (kwa wastani mtumiaji wa mitandao ya kijamii anatumia masaa mawili kila siku). Kama jibu ni hapana basi jua muda unaoweka kwenye mitandao hiyo unaupoteza. Kama kweli unatumia mitandao ya kijamii kuungana na marafiki na kujua yanayoendelea, utahitaji dakika 10 tu kwa siku kwa ajili ya hilo. Muda mwingine utakuwa na manufaa kwako kama utatumia kwenye mambo yenye tija.

Kila unapoingia kwenye mitandao ya kijamii jikumbushe hili, MUDA WAKO = PESA KWAO na jiulize kama kweli unataka kuendelea kuwa bidhaa inayouzwa.

Na mwisho kabisa, pima umuhimu wa mitandao hii kwa kujiuliza kama ungekuwa tayari kulipia ili kuitumia, maana bure inakudanganya na kukupotezea muda wako.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; GHARAMA YA KITU NI MAISHA UNAYOPOTEZA.

“The cost of a thing is the amount of what I will call life which is required to be exchanged for it, immediately or in the long run.” ― Cal Newport

Gharama ya kitu ni kiasi cha maisha unayopoteza ili kupata kitu hicho, iwe ni ndani ya muda mfupi au muda mrefu.

Rafiki, hii ni kauli nzito sana unayopaswa kuielewa kama unataka kufanya tathmini ya uhakika kwenye maisha yako.

Kuna vitu huwa tunavifanya kwa sababu ni bure au rahisi kufanya, lakini huwa hatuangalii madhara yake ya baadaye. Hivyo tumekuwa tunajizuia sisi wenyewe kufanikiwa na kupiga hatua kwa sababu ya kutokufanya tathmini ya vitu tunavyofanya.

Kila kitu ambacho unachagua kufanya, maana yake umeweka muda hapo, muda ambao huwezi kuutumia kwenye vitu vingine kwenye maisha yako. Kama umeamua kuzurura kwenye mitandao ya kijamii, maana yake muda unaoweka hapo huwezi kuutumia tena kwenye kazi zako, huwezi kuutumia kwenye mahusiano yako na wala huwezi kuutumia kuboresha afya yako. Muda huo ukishapita ndiyo umepotea, hautarudi tena.

Chagua sasa kupima umuhimu wa kitu kabla hujakifanya kwa kujiuliza kama kweli kina thamani ya kuchukua maisha yako. Kabla hujaweka muda wako kwenye kitu chochote, jiulize je hicho ndiyo kitu muhimu zaidi kwako kufanya, kitu ambacho kinastahili kuchukua maisha yako? Jiulize kama ingekuwa siku yako ya mwisho hapa duniani, je ungefanya kitu hicho?

Kama majibu ya maswali hayo ni hapana, basi hustahili kufanya kitu hicho. Kitu hicho hakijafikia hadhi ya kuiba muda wa maisha yako, achana nacho na weka muda wako kwenye vitu muhimu zaidi kwenye maisha yako.

Rafiki yangu mpendwa, hizi ndiyo TANO ZA JUMA namba 22 kwa mwaka huu 2019, naamini umepata mwanga mkubwa sana kuhusu mitandao ya kijamii, mwanga ambao wanaonufaika na mitandao hii hawataki uupate, kwa sababu wanajua ukiamka basi wao wanapata hasara. Sasa umeshayapata maarifa, kazi yako ni kuchukua hatua. Kama utachagua kuendelea kuzurura kwenye mitandao hii kila siku, fanya hivyo ukijua kabisa kwamba unapoteza maisha na hakuna kikubwa unachopata. Na kama utaamua kuachana na mitandao hii, au kutumia kwa kiwango kidogo sana basi jua utapata muda mwingi wa kufanya yaliyo muhimu zaidi kwako.

Maisha ni yako na uchaguzi ni wako, wajibu wangu ni kukupa wewe maarifa sahihi, nikiamini unakwenda kufanya uchaguzi sahihi.

Kwenye mafunzo ya ziada kutoka kwenye kitabu hiki (#MAKINIKIA) nitakwenda kukushirikisha hatua tano za kuchukua ili kurudisha uhuru wako kutoka kwenye matumizi mabaya ya simu janja na mitandao ya kijamii. Kwa kufuata hatua hizo tano utaweza kupata muda zaidi kwa yale muhimu kwako, utapata utulivu wa akili yako na utaacha kuwa bidhaa na mtumwa wa makampuni makubwa ya mitandao ya kijamii.

#MAKININIA yanapatikana kwenye channel ya TANO ZA JUMA kwenye mtandao wa telegram, ili usipitwe na mafunzo haya mazuri na mengine mengi, jiunge na channel hii leo. Maelekezo ya kujiunga yako hapo chini.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu