Rafiki yangu mpendwa,

Zipo siri muhimu za mafanikio kwenye biashara ambazo huwa hazifundishwi kwenye shule ya biashara na hata vitabu vingi vya biashara na mafanikio vimekuwa havigusii siri hizo.

Mara nyingi watu wanapokwenda kujifunza biashara vyuoni au wanaposoma vitabu vinavyohusu biashara, huwa wanafundishwa zaidi kuhusu maeneo muhimu ya biashara kama bidhaa, masoko, mauzo na kadhalika.

Lakini yapo maeneo mengine muhimu kwenye biashara kama mahusiano, furaha, malengo, siasa za ofisini na kuchukua hatua za hatari ambayo ni muhimu sana kuyajua ili kufanikiwa kwenye kazi na biashara. Lakini mambo hayo muhimu yamekuwa hayafundishwi kwenye shule za biashara na hata vitabu vya biashara.

Mwandishi na mshauri wa mambo ya biashara Chris Haroun kupitia kitabu chake kinachoitwa  101 Crucial Lessons They Don’t Teach you in Business School anatushirikisha siri hizo 101 za kufanikiwa kwenye biashara ambazo zimekuwa hazifundishwi na kupewa uzito.

101 crusial

Chris amejifunza siri hizi kupitia wafanyabiashara na wajasiriamali wenye mafanikio makubwa sana. Katika kazi zake za ushauri, Chris ameweza kukutana na watu wenye mafanikio makubwa kama Warren Buffett, Bill Gates, Marc Benioff na wakurugenzi wakuu wa makampuni makubwa ya teknolojia.

Hapa nakwenda kukushirikisha siri hizo 101 ili na wewe uweze kuzifanyia kazi na kufanikiwa sana kwenye biashara yako.

Zifuatazo ni siri 101 za mafanikio kwenye biashara ambazo hazifundishwi shuleni.

SEHEMU YA KWANZA; MAHUSIANO NI MUHIMU KULIKO BIDHAA.

  1. Ipo njia moja ya kupata chochote unachotaka na njia hiyo ni kuomba. Ombeni na mtapewa ni siri muhimu ya mafanikio kwenye biashara. Kama kuna kitu unataka, omba, na wengine watakuwa tayari kukupa. Huwezi kupata kitu bila kuomba.
  2. Unapoomba kazi, badala ya kutuma maombi kama wengine wanavyofanya, tafuta mikutano na wahusika wa eneo unalotaka kufanya kazi. Kwa kutumia mtandao wa kijamii wa LinkedIn, unaweza kukutana na mtu yeyote na ukaongeza nafasi zako za kupata kazi unayotaka.
  3. Biashara ni watu, haijalishi unajua nini, bali unamjua nani na nani anakujua wewe. Hivyo kazana kukuza zaidi mtandao wako wa watu unaowajua na wanaokujua.
  4. Mchukulie kila mtu unayekutana naye kama mtu mashuhuri, jua ni mtu muhimu, muoneshe umuhimu na watu watapenda kukutana na wewe. Ili kufanikiwa kwenye biashara unahitaji kutengeneza marafiki wengi.
  5. Kutana na watu, furahia na jifunze. Weka kipaumbele chako katika kujenga mahusiano imara kwenye biashara yako na kazi yako, fanya kile ambacho unapenda ukiwa umezungukwa na watu unaowapenda. Pia jifunze kupitia wale ambao unafanya nao kazi na wanaokuzunguka.
  6. Kuwa mtu wa shukrani, kila unapokutana na mtu, au mtu anapokufanyia kazi, chukua muda wa kumwandikia ujumbe wa shukrani, inaimarisha zaidi mahusiano yako.
  7. Wale uliosoma nao shule moja au chuo kimoja ni watu muhimu sana kwenye mafanikio yako. Kuwa nao karibu na tengenezeni mahusiano bora, kila mtu anaweza kunufaika kupitia kazi za wengine. Kama hakuna umoja wa wale mliosoma pamoja, una fursa nzuri ya kuuanzisha.
  8. Wafuatilie watu baada ya kukutana nao. Unapokutana na kujuana na mtu mara ya kwanza, endelea kuwafuatilia kwa mawasiliano, hili linaimarisha mahusiano mnayokuwa mmeanzisha.

SEHEMU YA PILI; TAMAA YA MUDA MREFU.

  1. Kuwa na mtazamo wa muda mrefu, usiwe mtu wa kutaka mafanikio ya haraka, bali kuwa na subira ukijua mafanikio ya muda mrefu ndiyo yanayodumu. Ukitaka mafanikio ya haraka utafanya makosa ambayo yatakugharimu sana baadaye. Fikiria miaka 5, 10, 20 na hata 30 ijayo.
  2. Jifunze, pata, rudisha. Jifunze kuongeza kipato chako, hili litapelekea kipato kuongezeka na kikishaongezeka kirudishe kwa jamii yako. Unapaswa kuwa mtu wa kutoa kwa wale wenye uhitaji, hili linakuwezesha kufanikiwa zaidi.
  3. Jinsi unavyofanya kazi kwa juhudi, ndivyo unavyoongeza bahati yako. kama kuna bahati kwenye kazi na biashara basi inatokana na kujituma sana kwenye kile unachofanya. Wale unaoona wana bahati, ni kwamba wanajituma kuliko wengine.
  4. Uwekezaji bora kuliko wote unaoweza kufanya kwenye maisha yako ni kuwekeza ndani yako mwenyewe. Kuwa tayari kulipa gharama za kupata mafunzo na ushauri sahihi, maarifa yatakusaidia sana kufanikiwa. Soma vitabu, hudhuria mafunzo, semina na kuwa na makocha na mamenta ambao wanakusaidia kufanikiwa zaidi.
  5. Jifunze ni vitu gani hupaswi kufanya. Watu huwa wanajifunza vitu gani vya kufanya, lakini wanasahau somo muhimu la vitu gani vya kuepuka kufanya. Angalia makosa ambayo wengine wamefanya, halafu wewe usiyarudie makosa hayo.

SEHEMU YA TATU; EPUKA UCHOVU UNAOTOKANA NA KUFANYA KAZI SANA.

  1. Tenga muda wa kufanya kazi sana na kisha tenga muda wa mapumziko. Tenga juma moja la kupumzika kila baada ya miezi sita. Na unapotoka kwenye mapumziko, tenga tarehe ya mapumziko yanayofuata. Kadiri unavyofanya kazi sana ndivyo mwili wako unahitaji mapumziko pia, la sivyo utapata uchovu mkubwa utakaokukwamisha.
  2. Msongo utakuua. Epuka sana msongo kwenye maisha yako. Msongo unatokana na hofu ambazo mtu anakuwa amejijengea, ondokana na hofu ulizonazo na hutakuwa na msongo. Jua kila kitu kitakwenda vizuri kama utachukua hatua sahihi.
  3. Unapogundua una msongo mkali, jipe siku ya mapumziko, hata kama huumwi. Mapumziko haya yatapunguza msongo kwa kujiweka mbali na kazi. Lakini pia yatakuepusha kufanya makosa pale unapofanya maamuzi ukiwa na msongo.
  4. Fuata amri kumi za Mungu, kufanya kazi siku sita na ya saba kupumzika. Tengeneza utaratibu mzuri wa kupata siku moja ya kupumzika kila juma, itakuondoa kwenye msongo na kuupa mwili utulivu.

SEHEMU YA NNE; JIJENGEE KUJIAMINI.

  1. Hakuna kinachoweza kukuzuia wewe kufanikiwa ila wewe mwenyewe. Jiamini kwamba unaweza kuwa chochote unachotaka, weka juhudi na utakuwa. Kama unafikiri unaweza na kama unafikiri huwezi, uko sahihi.
  2. Glasi imejaa mara zote. Ipo njia ya kupima mtazamo wa mtu, kwa kuweka maji nusu glasi kisha kumuuliza mtu aeleze glasi na maji. Wenye mtazamo chanya wanasema glasi imejaa nusu, wenye mtazamo hasi wanasema glasi iko tupu nusu. Wenye mtazamo wa kujiamini wanaona glasi imejaa mara zote. Mara zote chukulia kile unachokutana kwa mtazamo chanya na jiulize unawezaje kunufaika nacho zaidi.
  3. Maisha yenye mlinganyo yanaleta ufanisi mkubwa kwenye biashara. Tumia vizuri muda wako, kuwa na vipaumbele sahihi kwako na usiahirishe yale muhimu. Fanya yale muhimu tu na mengine achana nayo. Una muda wa kufanya kila kitu kama utautumia vizuri.
  4. Sehemu kubwa ya hofu ulizonazo unajidanganya mwenyewe. Akili zetu zipo vizuri sana kwenye kutengeneza hofu, huwa zinatabiri mambo yatakuwa mabaya zaidi. Lakini mara zote mambo huwa hayawi mabaya kama tunavyotegemea. Hivyo usisikilize sana hofu zako.
  5. Epuka sana watu waliokata tamaa, watu ambao hawakazani kufanikiwa, watu wanaolalamika na kulaumu wengine. Watu wa aina hii watanyonya nguvu zako za mafanikio na hutaweza kupiga hatua.
  6. Usijilinganishe na mtu mwingine yeyote, wewe ndiye mtu bora kabisa kuwahi kutokea hapa duniani, hakuna ambaye amewahi kuwepo na wala hatakuja kuwepo. Jua wewe ni wa kipekee na muhimu, hivyo usijilinganishe na yeyote. Jua utofauti wako na utumie huo.
  7. Hakuna mtu mwenye akili kukuzidi wewe. Vitu vyote vikubwa unavyoona vimefanywa, vimefanywa na watu ambao hawajakuzidi sana akili. Hii ina maana na wewe ukiweka juhudi utaweza kufanya makubwa pia.

SEHEMU YA TANO; KUWA NA MAADILI.

  1. Uwazi unajenga uaminifu. Kwa kila unachofanya, kuwa na uwazi wa asilimia 100. Usifiche kitu chochote kwenye biashara yako, mweleze mteja ukweli kuhusu kile unachomuuzia. Ukimdanganya kuna siku atakuja kujua na utaharibu kabisa mahusiano yenu ya kibiashara.
  2. Usiwaamini watu ambao siyo waaminifu. Usifanye biashara na watu ambao wanawasaliti wapenzi au wenza wao. Kwa sababu kama wanaweza kuwasaliti watu wa karibu kwao, hawatashindwa kukusaliti wewe kwenye mambo muhimu ya biashara. Pia usiwaamini watu ambao wanawasema wengine vibaya kwako, jua wakienda kwa wengine wanakusema wewe vibaya pia.
  3. Njia nne za kujua kama mtu anadanganya;

Moja; anatoa maelezo marefu kwa swali linalohitaji jibu la ndiyo au hapana.

Mbili; hakuangalii machoni wakati anaongea.

Tatu; anaweka mkono wake mdomoni wakati anaongea.

Nne; anatikisa mguu wake wakati anaongea.

  1. Unaweza kujenga jina lako kwa miaka 30, halafu ukalivunja kwa sekunde 30 tu. Kuwa makini na kila unachofanya, hasa kwenye mitandao ya kijamii, unaweza kufanya kitu kidogo na kikawa na madhara makubwa sana kwako.

SEHEMU YA SITA; UNASHINDA VITA KABLA HATA HUJAINGIA KWENYE MAPAMBANO.

  1. Weka maandalizi makubwa kwenye chochote unachofanya. Kama mshindani wako anatumia masaa 5 kujiandaa kwa kitu, wewe tumia masaa 50. Mara zote weka maandalizi makubwa kwenye chochote unachofanya kuliko wengine wanavyoweka na hilo litakupa nafasi kubwa ya mafanikio.
  2. Zoezi rahisi la kupata wafanyakazi bora au wewe mwenyewe kuwa mfanyakazi bora. Zoezi hili lina maswali manne, ambapo kama majibu ni ndiyo kwenye maswali yote basi mtu huyo ni bora. Kama kuna jibu la hapana, mtu huyo siyo bora. Maswali hayo ni kama ifuatavyo;

Moja; je anafurahia kufanya kazi kwenye kampuni hiyo?

Mbili; je mtu anatumia muda mwingi kusikiliza kuliko kuongea?

Tatu; je wanauliza wengine maswali zaidi na kuwasikiliza wakijieleza?

Nne; je ni watu wanaoaminika?

  1. Usipite njia ya mkato ambayo hujawahi kupita wakati una haraka. Unapokuwa na haraka, utafanikiwa kwa kupita njia sahihi kuliko kupita njia ya mkato. Njia za mkato mara zote huwa na madhara, hasa unapokatisha kwenye ubora wa kile unachofanya ili kukamilisha kwa wakati au kwa gharama kidogo.

SEHEMU YA SABA; KUWEKA MALENGO.

  1. Fanya kile ambacho unahofia kufanya, hapo ndipo penye mafanikio yako makubwa. Jua kile unachohofia wewe kufanya ndiyo pia washindani wako wanahofia kufanya, hivyo unapokifanya unakuwa umejitofautisha nao.
  2. Jua pengo lililopo kwa pale ulipo sasa na kule unakotaka kufika, kisha weka juhudi kwenye kuziba pengo hilo. Usiwe tu mtu wa kuweka malengo na kuyasahau, jua pengo unalopaswa kuziba kisha lifanyie kazi.
  3. Kuyaandika malengo yako kunakupa nafasi kubwa ya kuyafikia kuliko kutokuyaandika. Utafiti uliofanywa kwenye chuo cha Yale uligundua hilo. Andika malengo yako kila siku na utayafikia.
  4. Kuhusu kuongeza elimu ya darasani, ongeza elimu pale tu ambapo ina msaada kwako kufanya kazi bora zaidi. Lakini usirudi shule kwa sababu unataka ulipwe zaidi, kama unataka kulipwa zaidi soma vitabu na fanyia kazi yale unayojifunza.
  5. Kila unapofikia lengo ambalo umejiwekea, weka lengo kubwa zaidi. Usirishike na kupumzika kwa sababu umefikia lengo, badala yake weka lengo kubwa zaidi na kila wakati utakuwa unajisukuma zaidi.

SEHEMU YA NANE; FURAHA NI…

  1. Usiwe na kazi, kuwa na unachopenda kufanya. Furaha ni matokeo ya kufanya kile unachopenda kufanya. Hivyo unapaswa kupenda unachofanya na hapo hutafanya kazi kabisa. Kama unachofanya unakiona ni kazi tu, basi tayari unakosea.
  2. Furahia kushindwa kwako. Hakuna mtu aliyewahi kufanikiwa sana bila ya kushindwa. Hivyo unaposhindwa furahia, kwa sababu ni njia ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa.
  3. Fedha siyo sawa na furaha. Lengo lako kuu kwenye kile unachofanya lisiwe fedha, bali anza kwa kupenda kile unachofanya na kutoa mchango wako kwa wengine. Na furaha unayoweza kuipata kwenye fedha ni kuwasaidia wengine.
  4. Shukrani inaleta furaha. Unapokuwa mtu wa kushukuru, unakuwa na furaha. Kila siku orodhesha vitu unavyoshukuru kuwa navyo kwenye maisha yako na utakuwa na maisha yenye furaha.
  5. Utajiri hauwezi kununua afya, hivyo weka kipaumbele cha kwanza kwenye afya yako. Wengi wanasahau afya zao kwa kukimbizana na utajiri, halafu wakishaupata wanautumia kuboresha afya zao, huo ni ujinga. Zingatia afya yako, kula vizuri, fanya mazoezi na pata muda wa kupumzika.
  6. Wakati sahihi kwako kubadili kazi au biashara ni pale kila unapoamka asubuhi hujisikii kabisa kwenda kwenye kazi au biashara yako. Unapoanza kujiona unafanya kazi, hapo umeshapotea. Kumbuka, kufanikiwa hupaswi kufanya kazi, bali unapaswa kufanya unachopenda.

SEHEMU YA TISA; MAMBO MUHIMU YA KISHERIA KUZINGATIA.

  1. Ilinde familia yako kwa kusajili biashara yako kama kampuni. Biashara inapofilisika, mali zako ninafsi hazifilisiwi. Lakini unapoendesha biashara kama mtu binafsi, biashara ikifilisika mali zako binafsi zinafilisiwa pia.
  2. Kuwa na mwanasheria anayekusaidia kwenye mikataba mbalimbali unayoingia na watu wengine. Usiwaamini wale wanaoandaa mikataba, wanajali maslahi yao kuliko yako. Hivyo kuwa na mwanasheria wako anayepitia kwanza mikataba kabla hujakubaliana nayo.
  3. Jikinge na matatizo kwenye eneo la kazi au biashara, jua mipaka ya mawasiliano na mahusiano eneo la kazi. Mfano epuka kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mtu mnayefanya kazi eneo moja, inaharibu ufanisi wa kazi.

SEHEMU YA KUMI; MBINU BORA ZA UONGOZI.

  1. Sifia hadharani, kosoa faraghani. Unapokuwa kiongozi, mtu akifanya vizuri msifie mbele ya wengine na anapofanya vibaya mkosoe akiwa peke yake. Hili linawafanya watu kufanya vizuri na kutohofia kuadhirikia mbele ya wengine.
  2. Usiweke hisia kwenye biashara. Ukishaweka hisia kwenye biashara, unafanya maamuzi ya tamaa na yatakayokugharimu sana. Mara zote tumia fikra, na unapogundua hisia zipo juu, jizuie sana kufanya maamuzi.
  3. Kitu kimoja muhimu unachopasa kuangalia kwenye uwekezaji ni uwepo wa timu bora ya uendeshaji. Biashara bora ni ile ambayo inaendeshwa na timu bora na siyo inayomtegemea mtu mmoja. Unapotaka kuwekeza kwenye biashara, angalia timu inayoendesha biashara hiyo.
  4. Ajiri taratibu, fukuza haraka. Unahitaji kuchukua muda mpaka kumwajiri mtu, kumfuatilia kwa karibu na kumjua vizuri. Na inapotokea umegundua kwamba mtu haendani na biashara yako, unapaswa kumfukuza haraka kwa sababu kadiri anavyokaa kwa muda mrefu ndiyo anavyotengeneza madhara makubwa.
  5. Gusa kitu mara moja na malizana nacho. Muda umekuwa tatizo kwa wengi kwa sababu hawana mpangilio mzuri. Jiwekee sera ya kugusa kitu mara moja na kuachana nacho, hasa kwenye mawasiliano. Mfano kama umetenga muda wa kusoma email, kila email unayofungua isome na kuchukua hatua hapo hapo, usijiambie naihifadhi nije kuifanyia kazi baadaye, hapo unapoteza muda. Hivyo pia kwenye barua na kazi nyingine unazofanya, gusa mara moja na malizana nacho.

SEHEMU YA KUMI NA MOJA; JINSI YA KUVUKA SIASA ZA OFISINI.

  1. Andika ujumbe na uhifadhi. Mtu anaweza kukuudhi kweli kweli, na ukamwandikia ujumbe, labda kwa siku, au email. Kabla hujatuma ujumbe huo, uhifadhi mpaka kesho yake, kisha njoo usome tena kabla hujautuma. Mara nyingi utajikuta siyo ujumbe sahihi kutuma. Somo ni usiwe unajibu unapokuwa na hasira, jipe muda wa kutulia na utaona hatua sahihi za kuchukua.
  2. Dini na siasa ni aina mbili za mijadala unayopaswa kuiepuka sana eneo lako la kazi au biashara. Hii ni mijadala inayowagawa watu sana. Unaofanya biashara inayohusisha watu wa aina mbalimbali, usiweke wazi msimamo wako wa kidini au kisiasa, haitakusaidia chochote zaidi ya kukupunguzia wateja.
  3. Wale wanaokukosoa wanakusifia. Hakuna mtu anayekosolewa ambaye hafanyi kitu kikubwa. Hivyo usiogope kukosolewa, jua hizo ni sifa kwamba kuna kitu kikubwa na cha tofauti ambacho unakifanya.
  4. Kamwe usimseme mtu ambaye hayupo, kama mtu amekuja kwako na habari za mtu mwingine, mwambie subiri tumwite mtu huyo asikie unavyomsema. Na unapowakuta watu wanamsema mtu mwingine, sema kitu chanya kuhusu mtu huyo au ondoka hapo haraka. Chochote kibaya unachosema kuhusu wengine, jua kitawafikia.
  5. Angalia wengine wanafanyaje kisha na wewe fanya kama wao. Unapoenda kwenye mazingira mapya ya kazi au biashara, haitasaidia kama utaonekana ni mtu wa tofauti kabisa. Jua utamaduni wa eneo husika kisha nenda nao. Kile unachofanya fanya kwa ubora kabisa, lakini usivunje utamaduni uliozoeleka.
  6. Kwenye kazi kama unataka kupandishwa cheo, lazima uwe mtiifu kwa wale walio juu yako. Lazima uwe tayari kunyenyekea hata pale ambapo unaonewa kabisa. Wale wanyenyekevu na watiifu ndiyo wanapata nafasi za kupanda juu. Kama huwezi kunyenyekea hata pale wa juu yako anapokosea, basi ingia kwenye biashara, kwenye kazi itakuwa vigumu sana kwako kupanda juu.
  7. Kwenye kazi, kadiri unavyoonekana ndivyo unavyochukuliwa kama mchapakazi. Hivyo ili kupata nafasi za kupanda vyeo kwenye kazi, hajalishi unafanya kazi kiasi gani, unatakiwa ujioneshe kwa watu sahihi pia kwamba unafanya kazi. Kwa kifupi maigizo yanahusika sana ili kupandishwa cheo kwenye kazi. Kama huwezi maigizo basi ingia kwenye biashara, kazi itakuwa ngumu sana kwako.
  8. Usimwamini mtu yeyote. Kwenye kazi na biashara, kila mtu anaweza kuwa adui yako muda wowote ule, kwa sababu kila mtu anaangalia maslahi yake zaidi ya wengine. Hivyo mara zote kuwa makini, mara zote fanya kile kilicho sahihi na usimwamini mtu yeyote, kila mtu ana ajenda zake binafsi.
  9. Watu wanapaswa kuyajua mafanikio yako, na wewe ndiye unayepaswa kuwaambia. Kama unakaa kimya na mafanikio yako ukiamini watu watayajua, jua unajizuia kupiga hatua zaidi. Watu wana mambo mengi yanayowavuruga, unahitaji kuwakumbusha kuhusu mafanikio yako ili wajue wewe ni mtu sahihi wa kufanya nao kazi.
  10. Kila mara chukua maoni ya ufanisi wako. Ni rahisi kujiona unafanya kilicho sahihi wakati unapotea. Njia rahisi ya kujua kama unachofanya ni sahihi ni kuwauliza wale wanaokuzunguka kukupa maoni yao. Wafanye wawe huru kutoa maoni, hata kama siyo mazuri, kwa njia hiyo utajua kama unafanya vizuri au la.
  11. Njia pekee ya kupandishwa cheo na kuongezewa kipato ni kuomba. Ukisubiri mpaka watu waone unastahili kupandishwa cheo au kuongezewa kipato unajichelewesha. Mfuate mtu anayehusika kisha omba nafasi ya kupewa majukumu zaidi na kuongezewa kipato pia. Kumbuka, ombeni nanyi mtapewa.
  12. Kabla hujacha kazi, ongea na bosi au mwajiri wako. Kama umepata kazi eneo jingine ambayo inakulipa zaidi, kabla hujaacha kazi unayofanya sasa, ongea na bosi au mwajiri wako kuhusu kazi mpya uliyopata na manufaa yake. Kama wewe ni mfanyakazi mzuri, atakuwa tayari kukupa kile unachokwenda kupata kwenye kazi mpya ili asikupoteze.
  13. Kwenye sherehe au mikutano ya kikazi au kibiashara, epuka sana kutumia kilevi cha aina yoyote ile, hata kama kila mtu anatumia. Ni bora utumie kinywaji cha kawaida kinachofanana na kilevi, lakini usitumie kilevi. Unapolewa, una nafasi ya kufanya mambo ambayo yatakuharibia kazi au biashara yako.
  14. Kwenye kazi, usitake kumzidi bosi wako, hasa kwa kufanya mambo ambayo yanakuonesha wewe ni bora kuliko yeye. Yeyote aliyepo juu yako anapopata hisia kwamba unafanya kuliko yeye, atakuweka kila kikwazo ili usifanikiwe.
  15. Onekana mtu wa kawaida na asiye na madhara. Kwenye eneo la kazi, usitake kuonekana wewe ndiye mjanja na unajua kila kitu. Ukijiweka wazi hivyo unatengeneza maadui wengi. Onekana mtu wa kawaida na asiye na madhara, hakuna atakayesumbuka na wewe na utakuwa na muda mzuri wa kujijenga na kuwa bora zaidi.
  16. Kamwe usilalamike. Usilalamike wala kumlaumu yeyote, usiwe mtu wa kuwa na mtazamo hasi. Mtazamo hasi na kuwa mtu wa kulalamika hakutakusaidia chochote.

SEHEMU YA KUMI NA MBILI; CHUKUA USHAURI KWA WATU WALIOFANIKIWA PEKEE.

  1. Unahitaji kuwa na mamenta, watu ambao wameshafika kule unakotaka kufika wewe. Watu hawa watakushirikisha uzoefu wao, lakini pia watakurekebisha pale unapokosea. Chagua watu sahihi ambao watakusukuma kufanikiwa zaidi.
  2. Jifunze kwa watu waliofanikiwa sana kwa kusoma vitabu vinavyoelezea historia za maisha yao. Wafuatilie wale waliofanikiwa zaidi kwenye mitandao ya kijamii, utajifunza mengi zaidi kupitia watu hao.
  3. Hakuna mtu aliyefanikiwa sana ambaye ana mtazamo hasi. Hii ni siri moja ya kujifunza kutoka kwa wale waliofanikiwa na kuiishi kila siku kwenye maisha yako. Mara zote kuwa na mtazamo chanya na jiamini wewe mwenyewe na amini kwenye malengo yako.
  4. Kwenye uwekezaji, wekeza kule ambapo wawekezaji wenye mafanikio makubwa wanawekeza. Usitumie hisia zako kuwekeza kwa kufikiri umepata fursa ambayo wengine hawajaiona. Wawekezaji wenye mafanikio makubwa wana uzoefu mzuri kwenye uwekezaji, wafuate wao na utafanikiwa.

SEHEMU YA KUMI NA TATU; WENYE WASIWASI NDIYO WANAOPONA.

  1. Wanasema wasiwasi akili, kuwa na wasiwasi ambao unakutaka uthibitishe kwanza kitu kabla ya kufikia maamuzi, unasaidia. Mfano kabla hujatuma ujumbe wowote, rudia kwanza kuusoma na hapo utaona kama kuna makosa yoyote. Kadhalika kwenye matumizi yako ya mitandao ya kijamii, kuwa makini na mwangalifu sana.
  2. Mipango yako binafsi ya baadaye inapaswa kuwa siri yako. Kwenye kazi, kama una mpango wa kuja kuacha kazi hiyo siku za mbeleni, hilo linapaswa kuwa siri yako na mtu yeyote asijue. Kwa sababu inapotokea changamoto na watu wakahitaji kupunguzwa, utaanza kupunguzwa wewe ambaye umeshaonesha kwamba siku zijazo utakuja kuondoka, na hilo litaweza kuharibu mipango yako ya baadaye.
  3. Mara zote kuwa na mpango mbadala. Usitegemee mpango mmoja pekee, unaposhindwa utakwama.
  4. Hoji ajenda iliyo nyuma ya kile ambacho watu wanafanya. Kila ambacho watu wana fanya, kuna ajenda imejificha nyuma yake, ambayo huwa hawaiweki wazi. Unapaswa kujua ajenda ya kila mtu kabla hujakubaliana naye.

SEHEMU YA KUMI NA NNE; KUCHUKUA HATUA ZA HATARI.

  1. Shindwa haraka na shindwa mapema. Chochote unachofanya kwenye kazi au biashara, hutaweza kufanikiwa kama unafanya kawaida. Unahitaji kuchukua hatua ambazo zinaonekana ni za hatari. Hivyo unahitaji kushindwa haraka na kushinda mapema, kwa kujaribu vitu hatari. Kwa kushindwa huko, utakuwa umejifunza mapema na kujua kilicho sahihi kufanya.
  2. Tumia fedha za watu wengine. Unapotaka kukuza zaidi biashara yako, njia bora ni kutumia fedha za wengine. Na fedha nzuri kutumia ni kutafuta watu wa kuwekeza kwenye biashara yako. Mikopo siyo mizuri, hasa biashara inapokuwa changa. Lakini kuwa na wawekezaji kunakupa uhuru wa kukuza zaidi biashara yako.
  3. Usiwekeze kwenye biashara ambayo waanzilishi wake wameshaondoka. Biashara huwa zinakua na kuwa na ubunifu pale ambapo waanzilishi wa biashara hizo wanakuwepo kwenye biashara hizo. Kwa sababu wao ndiyo wenye maono makubwa ya biashara hiyo. Wakishaondoka hao kinachobaki ni siasa tu, na kuangalia faida zaidi ya ukuaji. Kampuni nyingi huanza kuanguka pale waanzilishi wanapoondoka.

SEHEMU YA KUMI NA TANO; MBINU BORA ZA MAUZO.

  1. Fanya vitu vichache kwa ufanisi mkubwa kuliko kufanya vitu vingi kwa ukawaida. Uza vitu vichache vyenye ubora wa juu badala ya kuuza vitu vingi vyenye ubora wa kawaida. Kwenye mauzo yako, sema maneno machache na muhimu.
  2. Ongea kwa mapenzi na hamasa. Pale unapoongelea bidhaa au biashara yako, ongea kwa mapenzi na hamasa kubwa. Kadiri unavyopenda na kuhamasika na kile unachouza, ndivyo unavyoweza kuwashawishi wengine kukubaliana na wewe. Kama unaongea kwa kutokujiamini, kwa sauti ya chini na kukata tamaa, hutaweza kumuuzia mtu yeyote.
  3. Ukishajua mtu anataka kununua kitu, kaa kimya. Wakati wa kumshawishi mtu kununua kitu, wauzaji wengi hujikuta wanaongea sana mpaka mtu anaahirisha kununua kitu. Ondokana na hilo kwa kuongea maneno machache na muhimu, na pale mtu anapoonesha nia ya kununua, kaa kimya, usiendelee kuongea tena. Hapo mtu atafanya maamuzi na kununua.
  4. Wateja wadogo wanahitaji kazi kuliko wateja wakubwa. Kwenye biashara yako, chagua kuwahudumia wateja wakubwa na utaweza kufanikiwa zaidi. Ukikazana kukimbizana na wateja wadogo, watakupa kazi kubwa sana. Kwanza watataka punguzo kwa sababu bajeti yao ni ndogo na pili watahitaji sana msaada wako hata baada ya kununua. Wateja wakubwa wanakuwa na bajeti kubwa na wana timu ya watu wa kufanyia kazi vitu hivyo hawatakutegemea sana wewe.
  5. Usisikie neno hapana. Unapowashawishi watu kununua kitu, watakuwa na mapingamizi mengi. Kama utayasikia mapingamizi hayo na kukubaliana nao, hutaweza kuuza kamwe. Wewe endelea kuwashawishi watu wanunue na kadiri unavyong’ang’ana ndivyo wanavyokuwa tayari kukubali.
  6. Anza na mazungumzo binafsi kabla ya mazungumzo ya biashara. Unapokutana na mteja kabla hujaingia kwenye mazungumzo ya biashara, anza kwanza na mazungumzo binafsi, hili linajenga mahusiano mazuri lakini pia linakupa kujua kinachowasukuma wateja na kukusaidia kwenye mauzo.
  7. Njia bora ya kupata mkutano na mtu yeyote ni kutumia mtandao wa kijamii wa LinkedIn, kuangalia kitu ambacho mnacho kwa pamoja na mtu unayetaka kukutana naye, labda mnatokea eneo moja, au mmesoma shule au chuo kimoja, kisha mtumie ujumbe ukijitambulisha na kueleza kile kinachowaunganisha na omba mkutano. Wengi watakuwa tayari kukupa nafasi.
  8. Kujiamini kunaleta ubobezi. Jiamini sana kwenye kile unachofanya na watu watakuamini na kukuona ni mbobezi kwenye kile unachofanya. Unapojiamini unauza zaidi kwa sababu watu wengi zaidi wanakuamini. Jiamini lakini usiwe na kiburi.
  9. Michezo ni moja ya mazungumzo ambayo kila mtu anaweza kuendana nayo. Unapokutana na mtu, jua anapendelea mchezo gani na anashabikia timu gani, hapo mnaweza kuwa na mazungumzo mazuri yanayojenga mahusiano mazuri kabla hamjaingia kwenye mazungumzo ya kibiashara.
  10. Mchezo wa gofu ni mchezo mzuri unaokukutanisha na watu wenye vyeo vya juu kwenye makampuni na biashara kubwa. Jifunze na kushiriki mchezo huu na utakutana na watu wengi waliofanikiwa.
  11. Vaa kama mtu ambaye tayari ameshafanikiwa. Watu wanakuhukumu kwa mavazi na mwonekano wako. Hivyo mara zote kuwa na mwonekano mzuri, vaa kama mtu aliyefanikiwa. Mara zote vaa kama ambavyo wale unaotaka kufikia mafanikio yao wanavyovaa. Kama umeajiriwa, vaa kama anavyovaa bosi wako au mkurugenzi wa kampuni hiyo.
  12. Tumia vizuri vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Hizi ni fursa za kuitangaza biashara yako na kuwafikia wengi bure kabisa au kwa gharama ndogo. Pata nafasi za kushiriki na kuhojiwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari na hilo litawafanya wengi zaidi wajue kuhusu wewe na biashara yako.

SEHEMU YA KUMI NA SITA; FIKIRI TOFAUTI.

  1. Nenda kinyume na kundi la wengi na utafanikiwa zaidi. Kitu kinapofanywa na wengi, wewe fanya kinyume nao, na utafanikiwa sana. mara nyingi kinachofanywa na wengi siyo kitu sahihi. Mfano kwenye uwekezaji wakati kila mtu anauza, wewe nunua, na wakati kila mtu ananunua, wewe uza.
  2. Endesha biashara yako kama kampuni ndogo mara zote. Kampuni ikishakuwa kubwa urasimu unakuwa mwingi na ugunduzi na ubunifu unapungua. Unapoendesha biashara yako, hata kama ni kubwa kiasi gani, iendeshe kama biashara ndogo, maamuzi muhimu yafanywe na watu wachache na yafanywe haraka.
  3. Fikiri akwa akili yako kabla hujafanya maamuzi. Kuna watu wengi ambao wanashauri vitu vingi kuhusu biashara na uwekezaji. Lakini kamwe usifanye kitu kwa sababu ya ushauri wa wengine, kaa chini na fikiri kwa akili yako na ufanye maamuzi ambayo ni sahihi kwako.
  4. Chukua muda wa kufanya matembezi. Unapokua umekwama kwenye jambo lolote, au una msongo, au unataka kufanya maamuzi muhimu, fanya matembezi. Kupitia matembezi utaweza kufikiri tofauti na kufanya maamuzi bora.
  5. Tengeneza jukwaa. Mfumo wa biashara umebadilishwa kwa kasi sana na ujio wa mtandao wa intaneti. Njia bora ya kuwa na biashara yenye mafanikio ni kuifanya biashara yako kuwa jukwaa ambali watu wanakutana. Na hata unapowekeza, wekeza kwenye kampuni ambazo ni jukwaa. Kampuni kubwa ya Amazon ni jukwaa ambalo wauzaji na wanunuzi wanakutana. Mitandao ya kijamii ni majukwaa ambayo yanakusanya watu na kuuza matangazo. Tengeneza jukwaa na utaweza kufanikiwa sana.
  6. Usiheshimu mazoea, heshimu ugunduzi na ubunifu. Biashara nyingi zinakufa kwa sababu ya kufuata mazoea hata pale mambo yanapobadilika. Usiwe mtu wa kufuata mazoea, badala yake fuata ubunifu na ugunduzi mpya, kila kitu kinabadilika, biashara yako pia inapaswa kubadilika.

SEHEMU YA KUMI NA SABA; KUWA WEWE.

  1. Kuwa mwaminifu na ongea kutoka ndani ya moyo wako. Unapokuwa unaongea na mtu yeyote, ongea ukweli na ongea kutoka ndani ya moyo wako. Kwa njia hii utaaminika na kuwashawishi wengi zaidi. Unapoongea kutoka ndani ya moyo wako watu wanajua wewe ni mtu halisi na siyo mwigizaji.
  2. Msikilize mwenza wako, huyu ni mtu anayekujua kwa undani kuliko watu wengine. Ndiye anayepaswa kuwa mshauri wa kwanza kwako. Omba ushauri na maoni kutoka kwa mwenza wako na atakueleza ukweli ambao utakusaidia sana.
  3. Usitoe nafasi kwa watu au mawazo hasi kwenye akili yako. Usiruhusu kabisa hali ya kushindwa au kukata tamaa iingie ndani yako. Usipokuwa makini, wewe mwenyewe utakuwa ndiyo kikwazo kwa mafanikio yako, kwa kujikosoa sana mwenyewe. Ondokana na mawazo hasi na ya kukatisha tamaa na usiyape nafasi kabisa kwenye akili yako.
  4. Jipe muda wa kuwa na wewe peke yako. Huwa tunatoa muda wetu kwa kila mtu kasoro sisi wenyewe. Hakikisha unatenga muda wa kuwa wewe peke yako, kuyatafakari maisha yako, kuangalia unakotoka, uliko na unakokwenda na hata muda wa kupumzika pia. Wewe ndiye mtu muhimu kwako, jipe muda wa kuwa peke yako na kujisikiliza.
  5. Hujachelewa kuanza chochote. Kwa zama tunazoishi sasa, unaweza kuanza kitu chochote kwenye umri wowote na bado ukafanikiwa. Kama ulichelewa kuanza, usijikatishe tama kwamba huwezi kuanza sasa. Kwenye umri wowote ule, unaweza kuanza chochote unachotaka kuanza na ukafanikiwa. Iwe ni biashara au ujuzi fulani, unachohitaji ni mapenzi na kuwa tayari kujifunza.
  6. Kuvurugwa kunaleta ugunduzi mpya. Kuvurugwa kwenye kazi na hata biashara ni hali ya kawaida. Kuna wakati unafika na kuona kila unachofanya hakieleweki au kuchoshwa na namna mambo yanavyofanywa. Hapo ndipo pazuri kwa sababu unakuwa kwenye hatua nzuri ya kuja na ugunduzi mpya. Unapojikuta kwenye hali ya kuvurugwa, fikiria njia mpya na bora ya kufanya kile unachofanya.

Rafiki, hizo ndiyo siri 101 za mafanikio kwenye biashara ambazo hazifundishwi maeneo mengi. Weka mafunzo haya kwenye matendo na hutabaki hapo ulipo sasa.

Rafiki, nikukaribishe kwenye SEMINA YA KUTENGENEZA MFUMO WA BIASHARA YENYE MAFANIKIO, ambayo itafanyika kwa njia ya wasap kupitia kundi la KISIMA CHA MAARIFA. Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, nitumie ujumbe sasa hivi wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717396253. Karibu sana usikose semina hii ya kukuwezesha kufanikiwa sana kwenye biashara unayofanya au unayokwenda kuanza.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge