Kuongea mbele ya kundi kubwa la watu ni moja ya vitu ambavyo watu wengi sana wanavihofia. Baadhi ya tafiti zinaonesha kwamba sehemu kubwa ya watu wako tayari kuzikwa wakiwa hai kuliko kuongea mbele ya kundi kubwa la watu.

Je wewe ni mmoja wa watu ambao kila unapopata nafasi ya kuongea mbele ya wengine unajawa na hofu kubwa sana? Je umekuwa unafika wakati wa wewe kuongea mbele ya wengine na kujikuta unasahau hata kile ulichopanga kuongea?

Kama majibu yako ni ndiyo basi leo unakwenda kupata dawa ya tatizo hilo, leo unakwenda kujifunza jinsi unavyoweza kujijengea kujiamini na kuishinda hofu ya kuongea mbele ya watu.

Kila mmoja wetu anahitaji kuwa na uwezo wa kuongea mbele ya watu wengine. Kwa sababu ni kwa njia hiyo pekee ndiyo tunaweza kuwashawishi wengine wakubaliane na sisi, ndiyo njia bora ya kuuza kile tunachouza na hata kwenye ajira mbalimbali, hitaji la kuongea mbele ya wengine ni kubwa.

Kama kuna kitu kimoja unachoweza kujifunza na kikakupa manufaa makubwa kwenye maisha yako basi ni sanaa ya kuongea mbele ya watu.

public-speaking-fear

Kwenye kitabu kinachoitwa The Art of Public Speaking waandishi Dale Carnegie na J. Berg Esenwein wametushirikisha maarifa na mbinu sahihi za kuweza kuongea mbele ya wengine kwa kujiamini na kwa mafanikio makubwa.

Ni katika kitabu hiki, waandishi wametufundisha jinsi ya kujijengea kujiamini na kuweza kuongea mbele ya wengine bila ya kuwa na hofu.

Yafuatayo ni mambo ya kuzingatia ili kuondokana na hofu ya kuongea mbele ya wengine.

MOJA; NJIA YA KUISHINDA HOFU NI KUFANYA.

Njia pekee ya kuishinda hofu ni kufanya kile kitu ambacho unahofia kufanya.

Hii ndiyo hatua ya kwanza kabisa unayopaswa kuchukua ili kujijengea kujiamini na kuondokana na hofu ya kuongea mbele ya wengine, kwa kuongea zaidi mbele ya wengine.

Lengo lako linapaswa kuwa ni kutafuta fursa zaidi za kuongea mbele ya wengine.

Iko hivi rafiki, hofu huwa ni hali ya kifikra zaidi kuliko uhalisia. Huwa tunatengeneza hofu kwenye fikra zetu kwa kutengeneza picha ambazo hazipo. Lakini tunapofanya kitu matokeo huwa ni tofauti kabisa na picha tuliyokuwa tunajipa awali. Hivyo kwa matokeo tunayopata, hofu inapungua yenyewe.

Mara ya kwanza kufanya kitu chochote huwa tunakuwa na hofu kubwa, lakini kadiri tunavyoendelea kufanya, hofu hiyo inakosa nguvu na kupotea kabisa.

Kinachowafanya wengi kuwa na hofu ya kuongea mbele ya wengine ni kwa sababu hawachukui hatua za kutosha katika kuishinda hofu hiyo.

Wewe anza kuchukua hatua sasa. Kila unapokuwa mbele ya wengine, tafuta nafasi ya kuongea chochote. Anza na vikundi vidogo vidogo kisha nenda kwenye makundi makubwa zaidi.

Kadiri unavyorudia rudia kufanya kitu, ndivyo hofu inavyokosa nguvu na mtu kujiamini zaidi. Tafuta nafasi za kongea zaidi mbele ya watu na utaweza kuishinda hofu ya kuongea mbele za watu.WhatsApp Image 2019-07-13 at 19.06.36

 

MBILI; ZAMA KWENYE SOMO LAKO.

Kitu kikubwa kinachofanya watu kupata hofu wakati wanaongea mbele ya wengine ni kuruhusu mawazo yao kuzurura kwenye mambo yasiyohusiana na kile wanachozungumzia.

Mtu anakuwa anazungumza, lakini mawazo yake yapo kwenye vitu kama watu wanamchukuliaje, je nguo alizovaa zinaonekanaje kwa watu, au akitoka hapo anakwenda kufanya nini.

Kuruhusu mawazo kuzurura ndiyo imekuwa inachochea sana hofu ya kuongea mbele ya wengine na hata kukaribisha makosa mbalimbali katika uongeaji.

Kuondokana na hali hiyo, zama kwenye somo lako, mawazo yako yanapaswa kufikiria kile ambacho unazungumzia pekee. Achana na vitu vingine vyote wakati unapokuwa unaongea na fikiria kile tu ambacho unazungumzia.

Kwa kuweka umakini wako wote kwenye kile unachozungumzia, unaifanya hadhira yako nayo ipeleke umakini wao kwenye unachozungumzia na zile hofu ndogo ndogo zinapotea zenyewe.

Kama tulivyojifunza, hofu huwa inatengenezwa kwenye fikra zetu, hivyo kama utaweka fikra zako kwenye kile unachozungumzia pekee, hutakuwa na nafasi ya hofu kwenye fikra zako.

Unapopata nafasi ya kuzungumza mbele ya wengine jali kitu kimoja tu, ukweli ambao unataka watu hao waujue, mengine yote siyo muhimu kwa wakati ambao unazungumza.

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kuondokana Na Hofu Ya Kuongea Mbele Ya Wengine.

TATU; KUWA NA KITU CHA KUSEMA.

Maandalizi ni muhimu sana katika kuongea mbele ya wengine. Kama unakwenda kuongea mbele ya wengine huku ukiwa huna maandalizi sahihi, hofu itakujaa na utafanya vibaya.

Ni muhimu sana uwe na kitu cha kusema na uwe na maandalizi mazuri katika kusema kitu hicho. Lazima uwe unajua kwa kina kile ambacho unazungumzia, iwe ni kwa kujifunza au kwa uzoefu.

Lakini kujua pekee haitoshi, lazima pia uwe umejiandaa jinsi ya kusema kile unachojua, kwa namba ambayo watu wataelewa na kukupokea. Hivyo lazima ujiandae kwa kujua kile unachokwenda kuzungumzia na pia kujua njia bora ya kukisema kwa wengine.

Unapokuwa unajua kwa kina kile unachosema na kuwa na maandalizi mazuri ya jinsi ya kukiongea, unakuwa unajiamini zaidi na hilo linaondoa kabisa hofu unayokuwa nayo wakati wa kuongea mbele ya wengine.

Ukienda kuongea mbele ya wengine bila ya maandalizi, hofu itakutanda na utasahau hata kile kidogo ambacho ukikuwa nacho.

Wanenaji wenye mafanikio makubwa wamekuwa wanafanya maandalizi makubwa. Kwanza wanajifunza sana kuhusu somo wanalonenea, pili wanafanya mazoezi ya jinsi ya kunena. Wengi wanachukua muda wa peke yao na kusimama mbele ya kioo na kuigiza jinsi wanavyokwenda kuongea mbele ya wengine. Wengi wanarekodi sauti zao na kujisikia jinsi wanavyoongea na kuboresha zaidi.

Ni muhimu sana uwe na maandalizi ya kutosha ili uweze kuishinda hofu ya kuongea mbele ya wengine na uweze kuongea kwa kujiamini.

NNE; TEGEMEA KUFANIKIWA.

Baada ya kuwa na maandalizi mazuri kinachofuata ni kutegemea kufanikiwa. Iko hivi rafiki, kile kinachotokea kwenye maisha yetu ni ambacho tumekuwa tunakitegemea.

Sasa inapokuja kwenye kuongea mbele ya wengine, wengi huwa wanategemea kufanya vibaya. Wanajiambia watasahau, wanajiambia watakosea na mengine mengi. Na haishangazi kwa nini wanapata matokeo hayo kwenye unenaji wao.

Ili ufanye vizuri kwenye kuongea mbele ya wengine, lazima uanze ukiwa unategemea kufanya vizuri. Jione ukiwa unaongea kwa kujiamini na kwa mafanikio makubwa mbele ya wengine. Pata picha ya watu wakiwa wanakusikiliza kwa umakini na kujifunza au kukuelewa.

Na unapokwenda kuongea mbele ya wengine, hicho ndiyo kinachotokea. Tofauti na ukiwa na mategemeo ya kushindwa, kila kitu kitakupeleka kwenye kushindwa.

Kumbuka unapata kile ambacho unategemea kupata, hivyo tegemea kilicho bora na utapata kilicho bora.

TANO; TAWALA HADHIRA YAKO.

Kuihofia hadhira hasa kwa ukubwa wake ndiyo chanzo cha watu wengi kupata hofu ya kuongea mbele ya wengine. Wengi wanapokuwa mbele ya kundi kubwa la watu huwa wanajifikiria zaidi wao wenyewe kuliko wanavyowafikiria watu hao au kile wanachokwenda kuongea.

Ili kujijengea kujiamini na kuondokana na hofu ya kuongea mbele ya wengine, unapaswa kutawala hadhira yako. Wewe unapaswa kuwa ndiyo nguvu kuu ambayo hadhira inafuatilia.

Utaweza kuitawala hadhira yako kwa kujiamini wewe mwenyewe na kuongea kwa mamlaka. Unapoongea kwa mamlaka hadhira inakufuata. Lakini unapoongea kwa hofu na kwa hali ya chini, hadhira inakutawala na hapo utashindwa kuongea vizuri.

Ili kutawala hadhira yako vizuri, unapokuwa mbele ya wengine kongea jali vitu viwili pekee, kile unachoongea na wale ambao unawaongelea. Yaani fikra zako zote zinakua kwenye ukweli ambao unataka watu waujue na watu hao ambao unataka wajue ukweli. Vitu vingine vyote havina umuhimu.

Iko hivi rafiki, kama upo mbele ya wengine na ukaanza kujiuliza iwapo umependeza, hadhira nayo itaanza kufikiria kwa namna hiyo. Lakini unapofikiria kuhusu kile unachoongea, basi hadhira nayo inaufuata kwenye hilo.

Kwa kifupi, unaposimama kuongea mbele ya wengine, simama kama kiongozi na hadhira iwe inakufuata kwa kile unachozungumza.

SITA; USIHARAKISHE.

Unapozungumza mbele ya wengine, usiharakishe kuanza wala kumaliza. Jua muda ulionao kwenye kutoa mazungumzo yako kisha pangilia vizuri mazungumzo yako. Usiwe mtu wa kuharakisha kuanza kuongea au kuharakisha kumaliza kuongea.

Kuharakisha kwenye jambo lolote ni kiashiria kwamba mtu hana udhibiti na maandalizi ya kutosha na kwenye kuongea mbele ya wengine hilo linatosha kuiba hofu kubwa mbele yako.

Ni bora kuongea vitu vichache kwa utulivu ambapo watu wanaelewa, kuliko kuongea vitu vingi kwa haraka ambayo watu hawaelewi wala kuondoka na kitu cha kwenda kufanyia kazi.

SOMA; Mbinu Saba(7) Za Kuondokana Na Hofu Ya Kuongea Mbele Ya Kundi Kubwa La Watu.

SABA; USIOMBE MSAMAHA.

Unaposimama mbele ya wengine usihangaike na kuomba msamaha kwa kitu kidogo ulichofanya ambacho hakihusiani na mazungumzo unayofanya.

Mfano usianze kuwaambia watu wakusamehe kwa sauti yako, au mavazi yako au kuchelewa kwako na kadhalika.

Chochote ambacho unawaomba watu wakusamehe ndipo fikra zao zitakapokwenda na hivyo kuondoka kwenye mada kuu unayozungumzia. Na hata wewe utahama kutoka kufikiria kile unachozungumzia na kufikiria kile ulichoombea msamaha.

Kumbuka, kitu pekee kwako kuzingatia ni kile unachosema na wale ambao unawasemea.

NANE; CHUKULIA KAMA UNAONGEA NA RAFIKI.

Hakuna mtu hata mmoja ambaye huwa anakuwa na hofu ya kuongea na rafiki yake wa karibu. Kila mtu huwa anakuwa huru na kujiamini pale anapoongea na rafiki yake. Lakini inapokuja kwenye kuongea mbele ya watu wengine, hofu kubwa inajengeka.

Hakuna tofauti yoyote kati ya kuongea na rafiki yako wa karibu na kuongea mbele ya kundi kubwa la watu. Bali sisi wenyewe tumekuwa tunajenga fikra za hofu pale namba ya watu inapokuwa kubwa. Kwa kuona kama tutashindwa basi wengi watajua kuhusu kushindwa kwetu.

Kuondokana na hofu ya kuongea mbele ya wengine, chukulia kama unaongea na rafiki wa karibu kwako. Ondoa kabisa ile dhana kwamba unaongea mbele ya kundi kubwa. Wanenaji wengine wamekuwa wanachagua mtu mmoja kwenye kundi ambaye ndiyo kama wanazungumza naye. Kwa njia hii wanazungumza kwa kujiamini na kwa mafanikio makubwa.

Kwa kuwa huna hofu unapozungumza na rafiki, chukulia mazungumzo yako mbele ya wengine kama mazungumzo na rafiki na hapo utaweza kuzungumza kwa kujiamini na kwa mafanikio makubwa.

Haya ndiyo mambo nane muhimu ya kuzingatia ili kuweza kuondokana na hofu ya kuongea mbele ya wengine. Yafanyie kazi haya kwenye kila nafasi ya kuongea mbele ya wengine unayoipata na utaweza kuwa bora zaidi kwenye uongeaji.

Kwenye TANO ZA JUMA hili la 30 la mwaka 2019 tutakwenda kujifunza kwa kina kuhusu SANAA YA UNENAJI, (ART OF PUBLIC SPEAKING) ambapo tutajua njia bora za kuongea vizuri mbele ya wengine, kueleweka na kuwa na ushawishi mkubwa. Kuongea mbele ya wengine ni hitaji muhimu sana kwa mafanikio ya kila mmoja wetu, usikose tano za juma hili ili kujifunza na kuwa mnenaji bora kabisa.

WhatsApp Image 2019-07-13 at 18.40.49

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge