Mpendwa rafiki,

Familia ndiyo eneo ambalo kila mmoja wetu ametokea, baada ya kutoka kwenye majukumu yetu huwa tunarudi nyumbani  na kukutana na familia. Familia ndiyo sehemu ambayo watu huwa wanapumzika baada ya kuchoshwa na mizunguko ya siku nzima. Mara nyingi huwa tukitoka maeneo ya kazi au biashara zetu huwa tunakimbilia nyumbani  kupumzika na kuonana na wanafamilia.

Ziko familia ambazo ni bora na ziko familia ambazo ni bora familia tu. Msingi wa familia bora unajengwa na waasisi wa familia ambao ni baba na mama. Ukiona familia imetulia kuanzia chini ujue nguvu kubwa imetumika kujenga, kujenga kitu chochote ni kazi na siyo kila mtu anaweza kujenga kitu bora.

Familia bora zinajengwa kwa misingi imara, sasa namna bora ya kuendesha familia zetu kwa mafanikio makubwa ni kuziendesha familia zetu kwa mfumo.

Serikali yoyote inaendeshwa kwa mfumo, raisi huwa hafanyi kila kitu yeye, bali anatoa madaraka kwa watu wengine kufanya kazi fulani kwa niaba yake. Ndivyo ilivyo hata katika familia,siyo kila kitu afanye baba au mama.

Kuna takiwa kuwe na mfumo ndani ya familia, na kila mwanafamilia anatakiwa awe na majukumu yake ya kufanyia kazi. Mwanafamilia anapoamka anajua ni nini anakwenda kufanya, wako ambao wanaamka hawajui hata nini wanakwenda kufanya. Wengine hawana hata mfumo wa kula, utasikia wanaamka asubuhi leo tunakula nini.

Unatakiwa kama mzazi uweke mfumo katika familia, hata kupangilia kabisa ratiba siku fulani chakula ni moja mbili, ukienda mashuleni huwezi ukakuta wapishi wa shule wanafika shuleni na kujiuliza eti leo tunapika nini? Bali uko mfumo unao waongoza kufanya kitu fulani. Kuna ratiba ya chakula kama ni wali na maharage au ugali na maharage.

Familia ikiwa na mfumo inajiendesha vizuri, kama huna biashara basi sehemu moja muhimu ya kuanzia kuendesha taasisi  yako kama mfumo wa biashara vile.  Katika ngazi ya familia yajulikane majukumu ya baba ni yapi, ya mama ni yapi, watoto nakadhalika. Kila mtu ajue yeye anafanya nini katika familia, badala ya kuulizana familia inakufanyia nini jiulize utaifanyia nini familia yako?

Familia inakuwa bora kama kila mmoja akiwajibika katika nafasi yake, watoto wakijua majukumu yao wanayatekeleza vizuri. Ukisema baba ufanye kila kitu au wewe ndiyo uwe kila kitu utachoka na utashindwa kufanya mambo mengine.

SOMA; Hiki Ndiyo Kitu Kibaya Katika Malezi Ya Watoto Ambacho Wazazi Wanapaswa Kukiepuka

Tawanya madaraka, siyo kila kitu unatakiwa kufanya wewe, una wasaidizi wako, mpe kila mtu majukumu apambane nayo na wewe usiwe ndiyo unafanya kila kitu na huo utakua ni mfumo wa uongozi mbaya wa kukumbatia madaraka.

Weka ratiba inayoingoza familia kwenye kila kitu, familia iwe na mfumo kuanzia kulala na kuamka, muda wa kuamka ni saa ngapi na kila mtu aende kwenye majukumu yake. Siyo watu wanalala mpaka usingizi uishe wenyewe, familia ikiendeshwa kwa mfumo mambo mengi yanaenda vema. Kuwe na muda ambao familia inakuwa inasoma vitabu, ina Sali pamoja na siyo kila mtu anafanya lake, watawa wanaishi wengi katika eneo moja lakini wanaendesha mambo yao kwa mfumo, muda wa kusali wako wote, muda wa kuamka ni kwa wote sasa sembuse familia?

Hatua ya kuchukua leo;  weka mfumo wa kuiendesha familia yako, weka ratiba ya familia mtakayokuwa mnaifuta kila siku katika majukumu ya nyumbani. Kila mtu awe na majukumu yake na siyo mtu mmoja kushughulika na kila kitu.

Kwahiyo, majukumu ya kila mtu yakiwa wazi, inasaidia kutoleta lawama au uzembe kutokea, kazi fulani inajulikana wazi ni ya fulani hivyo asipoweka mambo vizuri atapata aibu. Familia bora inajengwa kwa misingi imara.

Makala hii imeandikwa na

Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo, vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net

Asante sana