#TANO ZA JUMA #36 2019; Usibobee Mapema, Kwa Nini Wasiobobea Wanafanikiwa Zaidi, Kuwa Ndege Lakini Ajiri Vyura, Jinsi Ya Kuepuka Kupotezwa Na Mashine Na Kitu Cha Kufanya Kabla Ya Kutatua Tatizo.

Rafiki yangu mpendwa,

Juma namba 36 la mwaka huu 2019 limeshatuacha, na mwaka nao unaendelea kutuacha taratibu. Ni matumaini yangu kwamba jinsi siku hizi zinavyokwenda kasi, ndivyo na wewe pia unavyokazana kujifunza na kupiga hatua zaidi.

Kumbuka miaka 5 mpaka 10 ijayo utakuwa wewe ulivyo sasa, isipokuwa kwa watu uliokutana nao na vitabu ulivyosoma. Hivyo kwa kuchagua kujifunza kila juma, utaweza kupiga hatua kubwa sana kwenye maisha yako. Japo unapokuwa unajifunza siku moja au juma moja huwezi kuona matokeo makubwa, kadiri miaka inavyokwenda ndivyo unavyoyaona matunda ya kujifunza.

Nichukue nafasi hii kukukaribisha kwenye makala ya TANO ZA JUMA, makala ambayo inakuwa inagusia maeneo matano muhimu kwenye kitabu ninachokuwa nimekisoma kwa kina kwenye juma husika.

Juma hili tunakwenda kujifunza kutoka kwa mwandishi David Epstein kwenye kitabu chake kinachoitwa Range : why generalists triumph in a specialized world. Kwenye kitabu hiki, David ametuonesha jinsi ambavyo hadithi ya kubobea haraka ambayo imekuwa inatumiwa na wengi kama mfano wa mafanikio isivyo sahihi. Ametushirikisha kwa kina jinsi ambavyo kutokubobea kwenye jambo moja kuna manufaa makubwa kwa mtu, hasa kwa maisha na mafanikio ya baadaye.

Range_ Why Generalists Triumph.jpg

Karibu tujifunze kwa kina kuhusu ubobezi na nini cha kufanya ili tusijizuie kufanikiwa sisi wenyewe.

#1 NENO LA JUMA; USIBOBEE MAPEMA.

Ushauri ambao umekuwa unatolewa na wengi, hasa watoto na vijana, ni kubobea mapema. Kwamba kadiri mtu anavyojua mapema nini anachotaka kufanya kwenye maisha yake na kisha kuweka nguvu zake kwenye kitu hicho, ndivyo anavyofanikiwa zaidi.

Na hapa hadithi za watu waliobobea mapema na wakafanikiwa zimekuwa zinatumika sana. Hadithi kama ya Toger Woods ambaye alikuwa mchezaji bora kabisa kwenye mchezo wa golf, alianza kujifunza mchezo huo akiwa na miaka miwili. Na maisha yake yote amecheza mchezo huo mmoja tu.

Licha ya kuwepo kwa hadithi hizi nzuri za watu waliofanikiwa kupitia kubobea kitu kimoja na mapema, hiyo siyo njia sahihi kwa wengi kupita kama wanataka mafanikio makubwa.

Hii ni kwa sababu kuchagua kitu na kubobea mapema kunakunyima kujua nini hasa unachoweza au unachopenda. Tumeona mara nyingi watoto wanalazimishwa kuchagua watakuwa nani wakiwa watu wazima. Wao hujibu kwa vile wanavyojisikia, sasa wakifanya makosa ya kusimamia majibu hayo, wengi wanakuja kuishia kwenye kazi ambazo hawazipendi.

Njia sahihi ya kuchagua kipi cha kufanya kwa mtu ni kujaribu vitu mbalimbali. Kupitia mafanikio na kushindwa ambapo mtu atakutana nako kwenye majaribio hayo, atajijua vizuri na kujua kipi kinachomfaa zaidi.

Lakini pia kubobea kwenye kitu kimoja mapema kunamnyima mtu wigo mpana wa kufikiri na kufanya maamuzi. Tafiti zinaonesha wale wanaojaribu vitu tofauti kabla ya kubobea kwenye kitu kimoja wanakuwa vizuri kwenye kile wanachobobea kuliko wale ambao wanaanza na kitu kimoja mapema.

Hivyo swala siyo kutokubobea kabisa, bali kutokukimbilia kubobea, kujaribu kwanza vitu vingi kabla ya kuchagua kitu kimoja ambacho unataka kubobea.

Pia kama tayari umeshabobea kwenye kitu kimoja, chukua muda wako na kujifunza vitu vingine, tofauti kabisa na kile ambacho umebobea. Kwa kujifunza vitu vingine, utaweza kutumia uzoefu wa eneo moja na kuupeleka kwenye eneo jingine.

Upo usemi kwamba kama kifaa pekee ulichonacho ni nyundo, basi kila tatizo kwako linakuwa ni msumari. Kadhalika, pale unapokuwa umebobea kwenye eneo moja, kila tatizo unalokutana nalo unalifikiria kwa ubobezi wako tu. Lakini kama ungekuwa na uelewa wa mambo mengi, inakuwa rahisi kuliona tatizo katika kona tofauti na kuweza kuona suluhisho rahisi na bora kuliko unapokuwa na ubobezi mmoja pekee.

Na kama umechagua biashara au uwekezaji kuwa ndiyo njia yako kuu ya kukuingizia kipato na ya kukupeleka kwenye mafanikio, basi jua umejiandikisha kwenye darasa la kujifunza kila siku na kujifunza kwa upana. Ili kufanikiwa kwenye maeneo hayo, unapaswa kuwa na uelewa mpana kwenye mambo mbalimbali.

Chagua kuwa mwanafunzi wa maisha, chagua kujifunza kwa upana maeneo mengi kabla hujabobea kwenye eneo moja na hata baada ya kubobea kwenye eneo moja. Kadiri unavyojua kwa upana, ndivyo unavyoweza kufanya maamuzi bora na sahihi kwako na hata kufanikiwa pia.

#2 KITABU CHA JUMA; KWA NINI WASIOBOBEA WANAFANIKIWA ZAIDI.

Hakuna wakati ambao watu wanasisitizwa kubobea kama huu, lakini pia ushauri huo siyo mzuri kwa zama tunazoishi sasa.

Kwa sababu hizi ni zama ambazo maarifa na taarifa zinapatikana kwa urahisi mno. Lakini jinsi ya kutumia maarifa na taarifa hizo ndiyo imekuwa kikwazo kwa wengi.

Mwandishi David Epstein kwenye kitabu chake kinachoitwa Range : why generalists triumph in a specialized world, ametuonesha kupitia tafiti na mifano mbalimbali ya wale waliofanikiwa sana kwamba kubobea kwenye jambo moja ni kikwazo kwa mafanikio makubwa.

Yafuatayo ni mambo muhimu ya kujifunza na kufanyia kazi kutoka kwenye kitabu hicho cha RANGE.

MOJA; WAUMINI WA KUBOBEA MAPEMA.

Kumekuwa na kundi la watu ambao wamekuwa wanaamini sana kwenye kubobea mapema kwenye kile wanachofanya. Hapa mtu anachagua mapema kile anachotaka kufanya kisha anabobea kabisa kwenye kitu hicho.

Uimara wetu binadamu haupo kwenye kubobea eneo moja, bali kuweza kuunganisha maeneo tofauti. Hivyo ni vyema kupata uelewa mpaka kwenye mambo mbalimbali kabla ya kubobea kwenye eneo moja.

Pale ambapo sheria na matokeo yanajulikana na hakuna mabadiliko makubwa, ubobezi unakuwa na manufaa makubwa. Lakini dunia ya kawaida haina uhakika wowote, hivyo kubobea ni kujiweka kwenye mazingira magumu.

Tafiti zinaonesha wanasayansi ambao wamekuwa wanashinda tuzo ya Nobel huwa pia wanajihusisha na mambo mengine nje ya sayansi. Hii inazidi kuonesha kwamba kubobea eneo moja pekee siyo njia nzuri ya kufanikiwa. Unapaswa kuwa na uelewa mpana wa vitu mbalimbali.

MBILI; JINSI DUNIA YA TOFAUTI ILIVYOTENGENEZWA.

Kwa sasa tunaishi kwenye dunia ya tofauti kabisa, dunia isiyotabirika. Kwa kipindi kirefu binadamu wameishi kwenye hali ya kuweza kuitabiri dunia kwa uhakika, iwe ni misimu au hali ya usalama. Na hii ilitoa nafasi nzuri kwa wale walioweza kubobea.

Lakini kwa sasa mambo yamebadilika, hakuna kitu chenye uhakika tena, hivyo hakuna yeyote awezaye kutabiri chochote na kikatokea. Hivyo maandalizi yoyote ambayo mtu anaweza kuwa nayo, bado hayawezi kumtosha kwa sababu matokeo yanakuwa tofauti kabisa na maandalizi hayo.

Katika hali kama hii, njia pekee ni kuwa na uelewa mpana wa maeneo mbalimbali badala ya kubobea kwenye eneo moja.

TATU; KIDOGO KWENYE KITU KIMOJA NI KINGI.

Mkazo wa kubobea mapema umepata umaarufu sana kwa sheria ya masaa elfu kumi. Sheria hii inaeleza kwamba ili mtu kuweza kubobea kitu chochote, inabidi akifanya kwa angalau masaa elfu kumi. Sheria hii imepewa umaarufu na kitabu kinachoitwa Outliers, ambacho kimeonesha jinsi wabobezi wote walivyokuwa wamekifanya kitu walichobobea kwa angalau masaa elfu kumi.

Hivyo mkazo ukawa kwenye urefu wa kufanya na siyo kiwango chakufanya. Kwamba kadiri mtu anavyofanya kitu kimoja kwa muda mrefu ndivyo anavyobobea na kufanikiwa zaidi.

Lakini tafiti zaidi zinaonesha wale wanaobobea siyo wanaofanya kitu kimoja kwa muda mrefu, bali wale wanaofanya vitu vingi. Hivyo mafanikio hayapo kwenye kufanya kitu kimoja kwa wingi, bali kufanya kitu kimoja kwa kiasi na kufanya vitu vingi.

Wazazi wengi wamekuwa wanaua vipaji vya watoto wao kwa kuwawekea masharti makali kwenye kipi wafanye na kipi wasifanye, hilo linawanyima uhuru wa kujaribu vitu mbalimbali na kujua kipi hasa kinachowafaa wao.

NNE; KUJIFUNZA HARAKA NA TARATIBU.

Mfumo unaotumika mashuleni kwenye kufundisha na kujifunza ni wa mwanafunzi kuweza kuelewa haraka. Hivyo anapewa mifano mingi na rahisi inayomwezesha kuelewa dhana inayofundisha. Japo mfumo huu unaleta ufaulu wa haraka, matokeo yake ni mabovu kwa muda mrefu.

Njia bora ya kujifunza ni ile ambayo ni ngumu na ya taratibu. Njia ambayo mtu anachukua muda kukielewa kitu, kuiumiza akili yake kuipata dhana inayofundishwa. Kwa njia hii mtu anakumbuka kwa muda mrefu kile alichojifunza.

Tafiti zinaonesha, wale wanaojifunza kwa haraka wanasahau haraka, wale wanaojifunza kwa ugumu wanakumbuka kwa muda mrefu kile walichojifunza.

Hivyo kwa ule ujuzi ambao ni mgumu na mtu anataka kujijengea kwa namna itakayodumu, njia bora ya kujifunza ni njia ngumu na siyo njia rahisi ya kupitia yale mafunzo yaliyolainishwa. Kwa dunia ya sasa ni muhimu sana kuzingatia hili, maana mafunzo mengi yamerahisishwa kiasi kwamba akili haiteseki kabisa. Hivyo mtu unaweza kujifunza sana, lakini baada ya muda unakuwa umesahau kila kitu.

TANO; FIKIRIA NJE YA UWEZO WAKO.

Tunapokutana na tatizo, huwa tunaanza kufikiria uzoefu tulionao kwenye tatizo hilo, na hii hupelekea kukwama, kwa sababu huwezi kutatua tatizo kwa kufikiri kama ulivyokuwa unafikiri wakati unalitengeneza tatizo hilo.

Hivyo tunapaswa kufikiria nje ya uzoefu wetu, kufikiria kwa picha na mifano tofauti kwa kuangalia vitu vingine jinsi vinavyofanya kazi. Hapa unatumia uzoefu tofauti na ulionao kutatua matatizo uliyonayo sasa.

Kwa kila tatizo unalokutana nalo, ambalo umejaribu kulitatua kwa ujuzi na uzoefu wako na ukashindwa, jaribu kutumia uzoefu wa nje kutaua tatizo hilo. Jaribu kuliangalia tatizo hilo kwa mtazamo wa tofauti, kama vile wewe huna uzoefu ulionao. Kwa njia hii ni rahisi kukutana na jibu zuri na rahisi ambalo linafanya kazi.

SITA; TATIZO LA KUNG’ANG’ANA SANA.

Kwenye ubobezi, ung’ang’anizi unasifiwa na kutukuzwa sana. Kwamba wale wanaong’ang’ana ndiyo wanaofanikiwa. Upo usemi kwamba washindi huwa hawakati tamaa na wanaokata tamaa huwa hawashindi. Japokuwa ni usemi mzuri na wenye nia njema, lakini unakuwa kikwazo kwa wengi kupiga hatua.

Kama jinsi usemi huo unavyoashiria, unapaswa kuanza na kitu kimoja na kung’ang’ana nacho mpaka ufanikiwe. Hii ndiyo kanuni ya ubobezi kwenye kitu kimoja. Lakini kama ambavyo mpaka saa tumeona, ubobezi kwenye kitu kimoja siyo mzuri, hivyo ni bora mtu kujaribu vitu mbalimbali na kuona kipi kinachomfaa zaidi.

Sasa unapojaribu vitu mbalimbali, hutaki kung’ang’ana na kila ulichoanza mpaka ukimalize. Bali unapaswa kuwa tayari kuacha kile ambacho unaona hakikufai na kwenda kwenye kingine.

Hauna ubaya wowote kwenye kuanza na kuacha vitu, muhimu ni kupata uelewa mpana kwenye mambo mengi kabla hujatulia na kubobea kwenye eneo moja au machache.

SABA; MVUTANO WA NAFSI NYINGI ZILIZOPO NDANI YAKO.

Kufikia maamuzi kwako mwenyewe ni tatizo kwa sababu ndani yako kuna nafasi nyingi, hivyo kunakuwa na mvutano kwa kila maamuzi unayotaka kufanya. Hivyo njia bora ya kushinda hili siyo kuendeleza mvutano, bali kuwa tayari kuchagua nafsi moja utakayoisikiliza na kwenda nayo kwa wakati huo.

Lakini ili uweze kutumia hili vizuri, lazima kwanza uondokane na ile dhana ya kuchagua kitu kimoja unachotaka kufanya maisha yako yote. Badala yake kuyaendesha maisha yako kama mradi, kwa kuchukua hatua sahihi kwa kila wakati ambapo fursa zinajitokeza mbele yake.

Yaani badala ya kujiambia utakuwa mtu fulani pekee kwenye maisha, unayapeleka maisha yako kwa kufanya maamuzi kulingana na fursa unazokuwa umekutana nazo kwenye maisha yako. Kama ni kitu unachoweza kukifanyia kazi na kunufaika nacho basi unachukua hatua.

Utu na haiba zetu huwa zinabadilika kadiri umri unavyokwenda. Kuchagua mapema kwamba utakuwa nani, kunakuweka kwenye wakati mgumu pale utu na haiba yako inapobadilika. Hivyo ni vyema kuchagua kuwa wazi wakati wowote kutumia kila fursa inayojitokeza mbele yako, inayokuwezesha kupiga hatua zaidi.

NANE; TUMIA MSAADA WA NJE.

Kadiri watu wanavyobobea kwenye kitu kimoja, ndivyo inavyokuwa vigumu kwao kuona majibu rahisi kwenye maswali magumu yanayowasumbua. Wengi wanakuwa na uelewa wa ndani sana kiasi kwamba kila tatizo wanalifikiria kwa juu sana hivyo kushindwa kutumia hali ya kawaida kupata suluhisho.

Kuondokana na hali hii, tumia msaada wa nje. Pale unapokuwa umekwama kwenye tatizo ambalo lipo kwenye eneo lako la ubobezi, omba ushauri kwa wale ambao hawajabobea kwenye eneo hilo. Waliangalia tatizo hilo katika hali ya kawaida, na hapo inakuwa rahisi kwao kuja na jawabu rahisi sana na linalofanya kazi.

Usikubali ubobezi wako uwe kikwazo kwako kupata majibu ya changamoto unazopitia, badala yake tumia msaada wa nje kupata jawabu. Hili ni gumu kwa wengi waliobobea, kwa sababu wanaamini kama wao na ubobezi wao wameshindwa, basi hakuna anayeweza. Lakini hilo ni kosa linalowazuia watu kujifunza na hata kupata majibu ya changamoto wanazopitia.

TISA; KUFIKIRI TOFAUTI.

Tunapokabiliana na hali ambayo hatujaizoea au kuitegemea huwa tunakwama na kushindwa kuja na majibu sahihi. Mara nyingi huwa tunaishia kurudi kwenye kufikiri kwa namna tulivyozoea, ambavyo ndivyo wengine pia wanavyofikiri.

Lakini huu ni wakati mzuri kwetu kufikiri tofauti, kwa kuangalia tatizo kwa namna ya tofauti na kuona kama kuna kitu cha tofauti kinachoweza kufanyika. Lengo lako lisiwe tu kupata matokeo unayotaka, bali kuona kama kuna matokeo mengine yanaweza kupatikana.

Kwa kupeleka umakini wako kwenye matokeo tofauti, unafikiri tofauti na kujaribu vitu tofauti hali inayokuweka kwenye nafasi ya kuja na uvumbuzi au ugunduzi mpya.

KUMI; KUPUMBAZWA NA UZOEFU.

Tafiti zinaonesha, inapokuja kwenye utabiri au makadirio ya vitu vya baadaye, wale ambao wana uzoefu mkubwa kwenye eneo wanalotabiria au kukadiria, wanakosea kuliko wasiokuwa na uzoefu mkubwa. Hii ni kwa sababu wale wenye uzoefu wanakuwa na mambo mengi a kufikiria na kuangalia, kuliko wale ambao hawana uzoefu mkubwa.

Hili ni tatizo jingine kwenye ubobezi, kwa sababu kadiri unavyobobea kwenye kitu kimoja, ndivyo utabiri wako na makadirio yako kwenye kitu hicho yanakuwa mabovu. Kuondokana na hali hii, unapaswa kuwa na uelewa mpana kwenye mambo mengi ili kuweza kufanya maamuzi sahihi.

Pia unaweza kuwatumia watu wenye uzoefu tofauti na wewe na wakakupa maoni yao kabla hujafikia maamuzi. Mfano makadirio ya muda au gharama za miradi mbalimbali huwa yanakuwa chini kuliko uhalisia. Hivyo ni vyema unapofanya makadirio yako, uombe pia wale wasio na uzoefu mkubwa kwenye eneo hilo kufanya makadirio yao pia na kisha kutumia makadirio ya wale wasio na uzoefu. Huwa yanakuwa sahihi au kukaribiana na usahihi kuliko ya wale wazoefu.

KUMI NA MOJA; JIFUNZE KUACHA KIFAA ULICHOZOEA.

Unapokuwa na nyungo, kila tatizo linageuka kuwa msumari. Hii ni dhana ambayo imekuwepo ka muda mrefu ambapo watu hujaribu kufanya kila tatizo liendane na ujuzi au uzoefu walionao, kitu ambacho siyo sahihi.

Unapojikuta kwenye tatizo au changamoto kubwa, kitu cha kwanza unachopaswa kuweka pembeni ni uzoefu wako. Liangalie tatizo kama mtu ambaye hajui kile unachojua sasa, na jiulize chanzo hasa cha tatizo ni nini na njia ya kulitatua ni ipi.

Kama hutaweka pembeni uzoefu wako kwanza, utakimbilia kutatua tatizo kwa njia ambazo siyo sahihi na hivyo hutopata matokeo sahihi.

KUMI NA MBILI; AMUA KUWA MWANAFUNZI WA MAISHA.

Chagua maisha ambayo kila siku kwako inakuwa siku ya kujifunza. Usijifungie kwenye eneo moja, kwa kuendelea kuchimba na kubobea kwenye eneo moja.

Badala yake jifunze kwa upana, jifunze maeneo ya nje ya ujuzi au ubobezi wako. Hayo yote yatakusaidia kufikia maamuzi sahihi pale unapokuwa umekutana na tatizo au changamoto.

Usiwe mtu wa kukariri vitu, badala yake jifunze jinsi ya kufikiri kwa usahihi. Kwa njia hiyo utaweza kujifunza maeneo mengi na kuwa bora zaidi.

Siku utakayojiambia umeshajua kila kitu, ndiyo siku unayoanza kuanguka.

Siku utakayojiambia unachagua kujifunza eneo moja tu ili ubobee zaidi na kuachana na maeneo mengine yote, ndiyo siku ambayo unakuwa umechagua kutokufikiri kwa usahihi.

Kuwa mwanafunzi wa maisha, jifunze kwa upana maeneo mbalimbali na jua kila unachojifunza kina manufaa kwenye maisha yako.

Rafiki, hayo ndiyo mambo muhimu ya kujifunza kuhusu ubobezi kutoka kwenye kitabu cha RANGE. Muhimu ni kwamba hakuna ubaya wowote kwenye kubobea eneo moja, muhimu ni usifanye hivyo mapema, na hata unapobobea, usiyasahau kabisa maeneo mengine. Endelea kujifunza kwa upana na kuwa na uelewa wa mambo mengi maana hayo yote yatakusaidia kwenye kufikia maamuzi sahihi pale unapokuwa umekwama.

Kwenye #MAKINIKIA ya juma tunakwenda kujifunza jinsi ya kukuza uelewa wako kwenye maeneo tofauti badala ya kubobea eneo moja pekee. Kujua jinsi ya kupata #MAKINIKIA soma mwisho wa makala hii.

#3 MAKALA YA JUMA; KUWA NDEGE LAKINI AJIRI VYURA.

Hii ndiyo hadithi ya wengi wanaotoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri.

Mtu ni mfanyakazi mzuri kwenye ajira yake, labda ni mwalimu, daktari, mwanasheria au mhasibu.

Haridhishwi na kipato anachopata kwenye ajira yake, sasa akiangalia na jinsi anavyoweza kufanya kazi yake vizuri, na sifa anazozipata kwa wale anaowahudumia, anajiona kabisa anaweza kwenda kujiajiri na akatengeneza kipato zaidi.

Hivyo anaondoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri, kwenye lile eneo ambalo amebobea. Kama ni mwalimu anaanzisha shule, kama daktari anaanzisha hospitali na kadhalika kwa fani nyingine.

Na hapo ndipo matatizo mapya yanapoanzia, kwanza wanajikuta wanafanya kazi sana. Pili biashara wanazokuwa wameanzisha hazikui kwa kasi, na hii ni kwa sababu muda mwingi wanautumia kwenye kufanya kazi ndani ya biashara hizo badala ya kufanya kazi nje ya biashara na kuzikuza zaidi.

Kwenye makala ya juma la 36 tumejifunza kuhusu sifa za NDEGE na VYURA, na kwamba kama unataka kufanikiwa kwenye biashara, unapaswa kuwa NDEGE, lakini uajiri vyura.

Ili kujifunza kuhusu eneo hilo kwa kina, soma makala hiyo ya juma. Unaweza kusoma makala hiyo hapa; Siri Ya Mafanikio Kwenye Biashara; Kuwa Ndege, Ajiri Vyura.

Endelea kutembelea AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA kila siku, kuna makala nzuri zinawekwa kila siku, za kukuwezesha wewe kupiga hatua zaidi.

#4 TUONGEE PESA; JINSI YA KUEPUKA KUPOTEZWA NA MASHINE.

Hatari kubwa iliyopo kwenye kazi na biashara kwa sasa ni nafasi za watu kuchukuliwa na mashine.

Ilianza kwa kompyuta, ambapo kazi iliyohitaji kufanywa na watu wengi iliweza kufanywa na mtu mmoja kwa kutumia kompyuta. kompyuta zikawa na uwezo mkubwa sana wa kutunza na kukokotoa mambo, lakini zikakosa njia ya kujiendesha zenyewe. Hivyo zikahitaji mtu ambaye anaziongoza kufanya kile ambacho zinapaswa kufanya.

Sasa hivi tatizo limekuwa kubwa zaidi, kwani sasa kuna maroboti (Artificial Inteligence) ambayo yana uwezo wa kujiongoza yenyewe na kutekeleza majukumu yake bila ya kumtegemea mwanadamu. Yaani kwa sasa maroboti hayo yanaweza kufanya kila kitu, kuanzia kutengeneza bidhaa viwandani, kufanya upasuaji wa kitabibu, kuendesha magari na hata kutoa huduma kwa wateja.

Hali hii imeongeza hatari kubwa kwenye soko la ajira na hata fursa mbalimbali za watu kujiajiri na kufanya biashara. Kwa sasa wale wanaoweza, wanapendelea zaidi kutumia maroboti kwenye kazi zao kuliko kuajiri watu.

Njia pekee ya kuzidiwa nguvu na maroboti haya, kuepuka kunyang’anywa nafasi za kazi na mashine hizi, siyo kubobea kama wengi wanavyofanya, bali kuwa na uelewa mpana wa mambo mengi.

Maroboti yamebobea sana kwa sababu yamejazwa kila aina ya taarifa inayohusiana na kitu yanachofanyia kazi. Hivyo huwezi kuyazidi kwa ubobezi. Namna pekee unayoweza kuyazidi maroboti haya ni kutengeneza uelewa mpana ambao unakupa wigo mpana wa kufikiri na kufanya maamuzi sahihi.

Kwa sasa fursa zinakwenda kwa wale ambao wana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi pale ambapo matokeo hayajulikani au hakuna uhakika. Kitu ambacho wabobezi au maroboti hayawezi. Wabobezi na maroboti wanakuwa na taarifa na maarifa mengi ambayo yanafaa kutumia pale matokeo yanapokuwa ni ya uhakika. Lakini kunapokuwa na changamoto ambayo inaondoa uhakika wa matokeo, wabobezi na maroboti yanakwama. Hapa ndipo wale wenye uelewa mpana wanapopata fursa ya kutumia vizuri uzoefu wao katika kufanya maamuzi sahihi.

Kuvuka nyakati hizi ngumu na kuendelea kuwa na kazi au biashara yako, usikimbilie kubobea eneo moja, badala yake jenga uelewa mpana kwenye mambo mengi. Yote yanakuwa na mchango kwako pale mambo yanapokwenda tofauti na inavyotegemewa.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; KITU CHA KUFANYA KABLA YA KUTATUA TATIZO.

“Whether chemists, physicists, or political scientists, the most successful problem solvers spend mental energy figuring out what type of problem they are facing before matching a strategy to it, rather than jumping in with memorized procedures.” ― David Epstein

Matatizo mengi yamekuwa magumu kutatua, au pale mtu anapojaribu kutatua anatengeneza matatizo zaidi kwa sababu wengi hukimbilia kutatua tatizo kabla hata hawajajua tatizo hasa ni nini.

Hivyo kabla hujakimbilia kutatua tatizo, hebu kaa chini kwanza na ulielewe tatizo hasa ni nini, chimbuko lake ni nini na hatua sahihi kuchukua ni zipi ili kutatua tatizo hilo.

Hapa unapaswa kuondokana na ile dhana ya kuwa na nyundo na kila tatizo kuwa msumari. Usikimbilie kutatua kila tatizo kwa kutumia yale uliyokariri. Badala yake pata muda wa kulijua tatizo, kisha kufikiri na kutumia uzoefu wako kuja na jawabu sahihi kwa tatizo hilo.

Wanasema kulijua tatizo ni nusu ya kulitatua. Wengi wanashindwa kutatua matatizo yao kwa sababu hawachukui hata muda kuyajua matatizo hayo. Ondoka kwenye mkumbo huo, usikimbilie kutatua tatizo hata kama linaonekana ni rahisi kiasi gani. Chukua muda wako kulielewa na kulitafakari kabla hujaingia kutatua.

Rafiki, hizi ndizo tano za juma la 36, tumejifunza mengi kuhusu eneo hili la ubobezi. Kazi ni kwako kuchukua hatua ya kuhakikisha unajijengea uelewa mpana kwenye maeneo mengi na siyo kubobea kwenye eneo moja pekee.

Kwenye #MAKINIKIA ya juma hili, tunakwenda kujifunza jinsi unavyoweza kujijengea uelewa mpana wa mambo mbalimbali ili uweze kuondokana na hali ya kubobea eneo moja na kujiwekea ukomo.

#MAKINIKIA yanapatikana kwenye channel ya TANO ZA JUMA iliyopo kwenye mtandao wa TELEGRAM. Kama bado hujawa kwenye mtandao huu, soma maelekezo hapo chini.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu