Rafiki yangu mpendwa,

Tafiti za kibiashara zinaumiza na kusikitisha. Tafiti hizi zimekuwa zinaonesha kwamba asilimia 80 ya biashara zinazoanzishwa huwa zinakufa ndani ya miaka mitano. Na hata zile ambazo hazifi ndani ya miaka hiyo mitano, miaka mitano mingine nusu yake zinakuwa zimekufa.

Kwa namba rahisi kuelewa ni kwamba, kama mwaka huu 2019 zimeanzishwa biashara 10, basi mpaka kufika mwaka 2024 biashara 8 kati ya hizo kumi zitakuwa zimeshakufa na kufungwa. Kufika mwaka 2029 katika zile biashara 10 zilizoanzishwa, ni moja pekee ndiyo inakuwa na mafanikio.

Hali hii ipo kwenye kila aina ya biashara, kwenye kila uchumi na kila nyakati. Haijalishi ni biashara ya sekta gani, haijalishi kama uchumi ni mzuri au mbaya, biashara nyingi zinazoanzishwa zinaishia kufa.

Swali kubwa ambalo wengi wamekuwa wanajiuliza bila ya kupata majibu ni nini kinasababisha kiwango hiki kikubwa cha biashara kufa? Kama tulivyoona, siyo aina ya biashara na wala siyo hali ya uchumi. Hivi ni viti viwili ambavyo vimekuwa vinalaumiwa sana.

mafanikio biashara.jpg

Ukweli ni kwamba, biashara zinafanikiwa au kufa kulingana na misingi ya uendeshaji wa biashara hizi. Ipo misingi sahihi ya kuendesha biashara ambayo ikifuatwa biashara yoyote ile haiwezi kufa, haijalishi ni aina gani ya biashara au uchumi ni mgumu kiasi gani. Na kama misingi hiyo haitafuatwa, basi biashara lazima ife, hata kama ipo kwenye sekta nzuri na uchumi ni mzuri.

Waandishi na wafanyabiashara wazoefu, Norm Brodsky na Bo Burlingham kwenye kitabu chao kinachoitwa STREET SMARTS wametushirikisha AMRI KUMI ZA BIASHARA ambazo kila mfanyabiashara anapaswa kuzifuata kama anataka kufanikiwa. Amri hizi zimegusa misingi yote muhimu ya biashara, ambayo ikifuatwa lazima biashara ifanikiwe, na ikivunjwa, hata moja tu, biashara itakufa.

Kwenye makala hii tunakwenda kujifunza amri hizo kumi za biashara kama ambavyo Norm ana Bo wametushirikisha kwenye kitabu chao. Karibu ujifunze amri hizi kumi na uziweke kwenye matendo ili biashara yoyote unayofanya au utakayokwenda kuanzisha isife.

AMRI YA KWANZA; NAMBA NDIZO ZINAENDESHA BIASHARA, KAMA HUJUI KUZISOMA, UNARUKA UKIWA KIPOFU.

Kitu cha kwanza unachopaswa kujua pale unapoingia kwenye biashara ni kwamba, biashara yako siyo wewe. Biashara yako ni kiumbe tofauti kabisa na wewe, ambacho kina maisha yake na mahitaji yake ya msingi. Jinsi ya kujua mahitaji hayo ya msingi ya biashara unapaswa kuzijua vizuri namba za kibiashara.

Kwenye biashara, namba ndiyo zinapima uhai wa biashara hiyo, utaijua hali ya biashara kwa kuangalia namba za biashara hiyo, na siyo mwonekano au bidhaa na huduma zilizopo. Namba hizi ndiyo zinakuonesha kama biashara inakua au inakufa, kama biashara inatengeneza faida au hasara na kama biashara inaweza kumudu gharama mpya unazotaka kuingia.

Zipo namba nyingi za kuangalia kwenye biashara, lakini zile muhimu zaidi ni mtaji unaozunguka, manunuzi, mauzo, gharama za uendeshaji wa biashara, faida ghafi na kamili, idadi ya wateja waliohudumiwa, idadi ya wateja wapya wanaokuja kwenye biashara, mali za biashara, madeni na mikopo.

Namba hizi unapaswa kuwa unazitengeneza wewe mwenyewe kama mfanyabiashara kila siku, kila wiki na kila mwezi. Usisubiri mpaka wahasibu wakupe namba za mwisho wa mwaka, mpaka kufika wakati huo utakuwa umeshachelewa sana kujua biashara inaendaje.

Kwenye programu ya ukocha wa biashara ninayoendesha, inayoitwa LEVEL UP, kuna namba 11 za kibiashara ambazo kila mshiriki lazima aziripoti kwenye biashara yake kila wiki. Namba hizi zimewezesha biashara nyingi sana kujijua zilipo na kuweza kukua zaidi.

Nina zawadi ya mwongozo wa namba hizi kwako, ni chati yenye namba husika, ambayo unaweza kuichapa na kuwa unaijaza kwenye biashara yako kila wiki. Kama utapenda kupata zawadi hii tuma email kwenda maarifa@kisimachamaarifa.co.tz sema NAOMBA CHATI YA NAMBA ZA BIASHARA.

SOMA; Njia Kumi (10) Za Kupata Mpenyo Ambao Utaiwezesha Biashara Yako Kukua Na Kufikia Mafanikio Makubwa.

AMRI YA PILI; FEDHA NI NGUMU KUPATA NA RAHISI KUTUMIA. PATA FEDHA KABLA HUJAZITUMIA.

Watu wengi wamekuwa hawaelewi thamani ya fedha wanapoingia kwenye biashara. Kama wangekuwa wanaelewa, wasingepoteza fedha kununua vitu vya anasa kama samani za ofisi, kulipa gharama kubwa kwenye mapambo na matumizi mengine yasiyo na tija kwa biashara.

Unapoingia kwenye biashara, jukumu lako la kwanza na muhimu sana ni moja, kupata mteja ambaye atalipia huduma au bidhaa unayouza. Hivyo chochote kinachotaka kutumia fedha yako, lazima kiwe kinachangia kumleta mteja kwenye biashara yako. Kama hakichangii basi kinaweza kusubiri kwanza.

Usianze matumizi ya anasa kwenye biashara kabla biashara haijatengeneza faida. Hapo utakuwa unatumia mtaji wa biashara yako kwa mambo yasiyo muhimu na mwisho biashara inakufa.

Tengeneza kwanza fedha, yaani faida, na ukishapata faida basi wewe mwenyewe utachagua uitumieje. Lakini kama biashara haijatengeneza faida, huna anasa ya kununua chochote unachojisikia kununua.

AMRI YA TATU; FAIDA GHAFI NDIYO NAMBA MUHIMU KULIKO ZOTE.

Watu wengi wanapoingia kwenye biashara, huwa wanakazana na namba moja pekee, huwa wanafikiri hiyo ndiyo namba inayopima mafanikio ya biashara. Lakini wengi wamekuwa wanashindwa kwenye biashara licha ya kufanya vizuri kwenye namba hiyo moja.

Namba moja ambayo wengi wanaizingatia sana ni MAUZO. Na inaleta mantiki kabisa, kwamba kadiri unavyouza ndivyo fedha zinavyoingia kwenye biashara na ndivyo biashara inafanikiwa! Si ndiyo? Kama ndivyo unavyofikiri basi jua unaelekea kubaya.

Umewahi kuwasikia wale watu wanaosema kwamba kuna chuma ulete? Kwamba wanauza sana lakini fedha hawazioni, bidhaa na huduma zinatoka sana lakini faida hakuna? Basi hao ndiyo wamekutana na tatizo la kuweka mkazo kwenye mauzo.

Kuuza sana siyo kiashiria cha kufanikiwa kwenye biashara, biashara nyingi huwa zinauza sana lakini zinakufa. Hii ni kwa sababu mauzo hayo yanakuwa yanafanyika kwa hasara. Na mtu hajui kwa sababu hana namba za biashara anazozifuatilia.

Namba muhimu kwako kufuatilia kwenye biashara yako ni FAIDA GHAFI. Faida ghafi unaipata kwa kuchukua mauzo na kutoa gharama za mauzo. Mauzo ni yale yote yaliyofanyika kwenye biashara, na gharama za mauzo zinahusisha gharama zote zilizohusika kwenye bidhaa au huduma iliyouzwa pekee. Hapa huhusishi gharama za kuendesha biashara.

Faida ghafi inakuonesha kama biashara inaweza kusimama yenyewe kabla hujaweka gharama zako za kuendesha biashara. Kwa sababu kama hakuna faida ghafi, haijalishi utabana matumizi kiasi gani, bado biashara yako itakufa. Ukishakuwa na uhakika kwamba biashara inatengeneza faida ghafi, basi hapo unajua sehemu ya kujibana ni kwenye matumizi.

AMRI YA NNE; MAUZO HAYAJAKAMILIKA MPAKA ULIPWE.

Kama biashara yako inahusisha kuwapa wateja bidhaa au huduma na wao kulipa baada ya kupokea, usihesabu kama umeuza mpaka pale mteja anapokulipa fedha. Hata kama mteja anakuahidi atalipa kesho na kukupa uhakika, usihesabu kama ni mauzo leo, kwa sababu bado hujapokea fedha hiyo.

Unapompa mteja bidhaa au huduma bila ya kulipa jua kwamba umemkopesha, hapo umetoa fedha kwenye biashara na kumpa mtu mwingine. Usihesabie kamba umeuza, hapo utajichanganya na kuona una mauzo makubwa kumbe siyo sahihi. Pia unapoyaweka vizuri mauzo usiyolipwa kama madeni, unajua kwamba una jukumu la kukusanya madeni hayo kabla hayajageuka na kuwa madeni sugu na yasiyolipika.

Kazana kukusanya madeni yote ambayo yapo kwa wateja wako ili yasomeke kama mauzo kwenye biashara yako. Na unaposema umeuza, hakikisha fedha imeingia kwenye biashara, hakuna fedha basi hayo siyo mauzo.

AMRI YA TANO; MADENI YA MUDA MFUPI YANAPOZIDI MALI ZA MUDA MFUPI, UMEFILISIKA.

Hii ni mari nyingine muhimu inayokutaka wewe uwe unazijua namba zako za biashara vizuri. Watu wengi kwenye biashara huwa wanafikiri kufilisika kwenye biashara ni mpaka pale watakapofunga biashara kabisa, lakini kile ni kitendo cha mwisho tu, kufilisika huwa kunaanza mapema kabla biashara haijafungwa. Ukizijua namba za biashara yako na kuzifuatilia kwa ukaribu, utajua mapema kwamba biashara imefilisika na kuchukua hatua kuinusuru.

Kuna aina tatu za hesabu za biashara unapaswa kuzijua na kuzifuatilia kwa karibu. Aina hizo ni taarifa ya faida na hasara (PROFIT AND LOSS STATEMENT), taarifa ya mzunguko wa fedha (CASHFLOW STATEMENT) na mizania (BALANCE SHEET). Huhitaji kuwa na ujuzi mkubwa wa uhasibu kuelewa na kusoma taarifa hizi, bali unapaswa kuzijua namba muhimu zilizopo kwenye taarifa hizi na zinamaanisha nini.

Kwa mfano, kupima uhai wa biashara yako, unaangalia madeni ya muda mfupi (unayopaswa kulipa ndani ya mwaka mmoja) na mali za muda mfupi (fedha ulizonazo na zilizopo benki pamoja na chochote kinachoweza kukupa fedha taslimu haraka).  Kama madeni unayopaswa kulipa ndani ya mwaka mmoja ni makubwa kuliko kiasi cha fedha unachoweza kuwa nacho ndani ya mwaka mmoja, biashara yako inafilisika.

Kwa kujua hili haraka, utakazana kuongeza kiasi cha fedha unachopaswa kuwa nacho kwa mwaka na huku ukipunguza madeni unayotengeneza. Kama huzijui namba zako hutajua hili mapema na utajikuta imefika siku ya kufunga biashara usijue tatizo limeanzia wapi.

SOMA; Tano Za Juma Kutoka Vitabu Just Run It Na 101 Crucial Lessons They Don’t Teach You In Business School; Mfumo Bora Wa Kuendesha Biashara Na Siri 101 Za Mafanikio Kwenye Biashara.

AMRI YA SITA; SAHAU NJIA ZA MKATO, ENDESHA BIASHARA KAMA VILE ITADUMU MILELE.

Kuanzisha na kukuza biashara ni kazi ngumu SANA. Asikudanganye yeyote kwenye hilo. Haijalishi uchumi ni mzuri au mbaya, haijalishi ni aina gani ya biashara, kuna ugumu na changamoto nyingi kwenye kuanzisha na kukuza biashara.

Unahitaji kuwa na bidhaa au huduma bora, kuwa na kitu kinachokutofautisha na washindani wako, kuweza kuwashawishi wateja na kutengeneza nao mahusiano mazuri, kutafuta na kuajiri wafanyakazi wazuri, kusimamia kwa karibu mzunguko wa fedha, kuendelea kujifunza na kuona mabadiliko kabla hayajafika na mengine mengi.

Yote hiyo ni kazi kubwa, sasa kwa kuwa sisi binadamu hatupendi kazi ngumu, huwa tunakimbilia kutafuta njia za mkato. Unaanza kutafuta njia za mkato za kukuza biashara yako haraka kama kuchukua mkopo kabla hujawa tayari, kuajiri kwa kiwango kikubwa kabla ya kuwa na mfumo, kutoa ahadi hewa ili kushawishi wateja kununua na nyingine nyingi.

Chochote unachofanya kama njia ya mkato ya kukuza biashara yako, huwa kinarudi kuiumiza zaidi biashara baadaye. Kila njia ya mkato ina madhara na gharama kubwa kwa biashara yako baadaye. Mkopo unaochukua kabla hujawa tayari unakuja kuilemea biashara na kuleta hasara kubwa. Wafanyakazi unaoajiri kabla ya kuwa na mfumo wanakuwa mzigo mkubwa kwako. Ahadi hewa unazowapa wateja zinawafukuza kabisa.

Endesha biashara yako kama vile itaishi milele, fanya kile kilicho sahihi mara zote, kuwa mvumilivu na usijaribu kufuata njia yoyote ya mkato.

AMRI YA SABA; WAJUE WASHINDANI WAKO WA KWELI NA WAHESHIMU.

Kamwe usimseme vibaya mshindani wako, hasa mbele ya wateja wako. Hili ni kosa ambalo wafanyabiashara wengi huwa wanalifanya, wakiamini litawavutia wateja kununua kwao na siyo kwa washindani wako.

Unapaswa kuwajua vizuri washindani wako wa kibiashara, kujua nini wanatoa na wewe unajitofautishaje nao. Na pale mteja anapokuambia mbona fulani anafanya hivi na wewe hufanyi, usianze kumwambia yule bidhaa au huduma zake siyo nzuri, badala yake mwoneshe nini cha ziada atakachokipata kwako.

Usiwachukie washindani wako wa kibiashara, wana mchango mkubwa sana kwenye mafanikio yako kibiashara, kwa sababu kadiri biashara inavyokuwa na wafanyaji wengi, ndivyo inavyochangamka na kutengeneza wateja wengi.

Hivyo unapokuwa na washindani, kazi yako kubwa ni kuhakikisha unatoa huduma bora kabisa ambazo wateja wako hawawezi kuzipata sehemu nyingine ila kwako pekee.

AMRI YA NANE; KWENYE BIASHARA HAKUNA URAFIKI, BALI KUNA USHIRIKA.

Usifanye biashara na marafiki zako au ndugu zako wa karibu. Ni ushauri rahisi na ambao unatolewa kila mara, lakini wengi hawaufuati na wanaishia kuumia.

Wengi huona kwa nini nisiwaajiri rafiki zangu au ndugu zangu ambao hawana kazi ya kufanya na wakanisaidia kwenye biashara, hawa huishia kuwa wafanyakazi wabovu kabisa kwenye biashara yoyote ile.

Wengi hujiambia badala ya kwenda kununua kwa watu wengine, kwa nini nisinunue kwa rafiki yangu ambaye anauza kile kile ambacho nakipata kwa wengine, ananua na matokeo yanakuwa siyo mazuri.

Unapofanya biashara na rafiki au ndugu, kuna tabia ya kupuuza baadhi ya kanuni au misingi unayoifuata kwenye biashara, na hilo huwa linakuja na madhara baadaye.

Unapofanya biashara na rafiki au ndugu, unakuwa kwenye hatari ya kupoteza vitu viwili, biashara na undugu  pia.

Kumbuka hili muhimu, hakuna urafiki au undugu kwenye biashara, kuna ushirika. Shirikiana na wale ambao hakuna mahusiano ya nyuma yanayokushawishi kukiuka baadhi ya misingi au kanuni za kuendesha biashara hiyo.

AMRI YA TISA; UTAMADUNI NDIYO UNAOENDESHA BIASHARA.

Kila biashara ina utamaduni wake, na baada ya muda utamaduni huo ndiyo unaendesha biashara hiyo. Jinsi wateja wanavyohudumiwa, jinsi watu wanavyotekeleza majukumu yao inatokana na utamaduni uliojengeka kwenye biashara hiyo.

Ni wajibu wako kama mmiliki wa biashara kutengeneza utamaduni mzuri kwenye biashara yako, utamaduni ambao utaiwezesha biashara hiyo kukua zaidi.

Utamaduni wa biashara unahusisha mahusiano baina ya watu kwenye biashara, jinsi ambavyo watu wanatekeleza majukumu yao, vipaumbele ambavyo watu wanakuwa navyo, huduma ambazo wateja wanazipata na kadhalika.

Haya yote unayatengeneza wewe mmiliki wa biashara na kufuatilia kwa makini, kuondoa yale yasiyo mazuri na kuweka yale ambayo ni mazuri.

SOMA; Makosa Haya Matano (05) Pekee Ndiyo Yanayoua Kila Aina Ya Biashara, Yajue Na Yaepuke Ili Biashara Yako Isife.

AMRI YA KUMI; MIPANGO YA MAISHA INAPASWA KUJA KABLA YA MIPANGO YA BIASHARA.

Ni rahisi sana kuweka malengo na mipango mikubwa ya kibiashara, lakini unapokaa na kujiuliza kwa nini unataka kufikia malengo hayo makubwa unakosa jibu la uhakika.

Watu wengi wamekuwa wanapotea kwenye biashara kwa sababu wanaweka malengo ya biashara kabla hawajaweka malengo ya maisha. Wanataka kuwa mabilionea kupitia biashara zao, na hilo linawataka kuweka maisha yao yote kwenye biashara na kusahau vitu vingine vyote. Wanaweza kufikia lengo hilo, lakini maeneo mengine ya maisha yao kama afya na mahusiano yanakuwa yameathirika sana.

Kabla hujaweka lengo kubwa la biashara, anza kwanza na lengo kuu la maisha yako. Jua unataka kuwa na maisha ya aina gani, jua maisha ya mafanikio kwa upande wako yana maana gani.

Ukishajua kwamba unataka nini kwenye maisha yako, hapo sasa unaweza kuitumia biashara yako kuwa na maisha unayoyataka wewe. Lakini ukianza kufikiria unachotaka kwenye biashara pekee, utaishia kuwa na maisha mabovu sana.

Rafiki, hizi ndizo AMRI KUMI za biashara unazopaswa kuzifuata kama unataka kufanikiwa kwenye biashara. Kama unavyoona, ni amri rahisi ambazo hazichagui ni mtu wa aina gani au mwenye elimu gani anayepaswa kuzifuata. Mtu yeyote aliyepo kwenye biashara au anayetaka kuingia kwenye biashara anaweza kufuata amri hizo na akafanikiwa sana. Na kama utavunja amri hizo, hakuna kitakachoweza kukusaidia kufanikiwa kwenye biashara.

Kwenye TANO ZA JUMA hili la 37 tutakwenda kujifunza kwa kina mambo muhimu ya kuzingatia unapoendesha biashara yako ili iweze kufanikiwa kama ambavyo waandishi Norm na Bo wametushirikisha kwenye kitabu chao kinachoitwa STREET SMARTS. Hii ni ile elimu halisi ya biashara ambayo haifundishwi mashuleni au kwenye vyuo vya biashara. Usikose kusoma TANO ZA JUMA hili pamoja na #MAKINIKIA yake.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha