Rafiki yangu mpendwa,

Ipo taarifa moja ya kusikitisha sana kuhusu biashara, ambayo watu wengi waliopo kwenye biashara hawaijui wala kuielewa.

Taarifa hiyo ni kwamba, biashara nyingi hazitengenezi faida. Wafanyabiashara wengi wapo kwenye biashara kwa miaka mingi, wakijituma na kujitesa sana, lakini mwisho wa siku hawawezi kuiona faida halisi ambayo imetokana na biashara zao.

Hali hii ndiyo imekuwa inasababisha biashara nyingi kushindwa kukua, licha ya wafanyabiashara kujituma sana na kufanya mauzo makubwa, faida halisi imekuwa haionekani.

profit first formula

Mike Michalowicz, mwandishi wa kitabu kinachoitwa Profit first : transform any business from a cash-eating monster to a money-making machine, ametuonesha jinsi ambavyo biashara nyingi zimekuwa dubwana ambalo linakula fedha bila ya kuridhika, kitu ambacho kinapelekea biashara zisiweze kuzalisha faida. Kwenye kitabu hiki, Mike ametushirikisha mfumo rahisi sana wa kutumia ili kuweza kuiona faida halisi kutoka kwenye biashara yako, mara moja na siyo kusubiri miaka mingi ijayo.

Mike anaifananisha biashara na mnyama ambaye mtu unakuwa umeanza kumfuga akiwa mdogo sana, na hivyo hakuwa na madhara yoyote kwako. Lakini kadiri mnyama huyo anavyokua, anaanza kuwa na madhara kwako, anakula wanyama wengine wadogo wadogo na kuzidi kuwa mkubwa. Na mwisho kabisa, anakuja kukula wewe ambaye ndiye umemlea tangu akiwa mdogo.

Angalia maisha ya wafanyabiashara wengi yanavyoendana na mfano huo. Mtu anaiona fursa ya kuanza biashara eneo fulani, anaianza biashara hiyo, ikiwa ndogo kabisa. Kipindi cha mwanzo cha biashara mtu anajibana sana, fedha ni ngumu na hivyo anaiweka kwenye maeneo muhimu pekee. Mtu anajituma sana kipindi hicho na karibu kila kitu kwenye biashara anakifanya mwenyewe.

Kwa juhudi hizi kubwa za mwanzo, na kujibana sana, biashara inaanza kukua. Lakini kwa sababu mfanyabiashara ana ndoto za biashara hiyo kuwa kubwa zaidi, haondoi faida kutoka kwenye biashara hiyo, badala yake anaendelea kuiwekeza zaidi. Lakini changamoto inaanzia pale ambapo hakuna mpango sahihi wa kuiwekeza faida hiyo.

SOMA; Tano Za Juma Kutoka Kitabu TRACTION; Get A Grip On Your Business (Maeneo Sita Ya Kuzingatia Ili Kufanikiwa Kwenye Biashara).

Kinachotokea kinakuwa ni ukuaji usio na mpangilio wa biashara, kadiri fedha inavyopatikana, ndivyo matumizi yake yanayotengenezwa. Matumizi yanakuwa makubwa kuliko mapato, na yanaendelea kukua kadiri mapato yanavyoongezeka.

Hapa sasa ndipo biashara ndogo ambayo mtu aliianzisha kwa nia njema inageuka kuwa mnyama asiye na huruma na anayekula kila kitu. Kila fedha inayoingia kwenye biashara inatafunwa na biashara hiyo, matumizi yanazidi kuwa makubwa na faida haionekani kabisa. Mfanyabiashara anajaribu kila mbinu, kufanya kazi muda mrefu zaidi, kuajiri watu wengi zaidi lakini hayo yote bado hayasaidii.

Biashara hiyo inamletea msongo kwenye maisha yake, inaharibu mahusiano yake, afya yake na utulivu wake wa ndani. Kadiri biashara inavyoendelea kukua ndivyo inavyozidi kutengeneza hasara na mwisho inaishia kufa, ikiwa imeshaharibu kila kitu kwenye maisha ya mfanyabiashara huyo.

Mike anatuambia maisha ya biashara hayapaswi kuwa hivyo, maisha ya biashara yanapaswa kuwa mazuri na yenye kufurahia, yanayokupa uhuru wa kuwa na maisha unayoyataka. Na kwenye kitabu chake cha Profit First, kama lilivyo jina, anatufundisha jinsi ya kutengeneza faida kwanza kutoka kwenye biashara yako.

Kanuni ya uhasibu iliyopitwa na wakati.

Sababu kubwa ya kwa nini biashara nyingi hazitengenezi faida kama anavyotuambia Mike ni matumizi ya kanuni ya uhasibu ambayo imepitwa na wakati.

Kanuni hiyo inasema hivi; MAUZO – MATUMIZI = FAIDA.

Kanuni hiyo inaleta matatizo kwenye biashara kwa sababu inaanza kuangalia maeneo mawili ambayo siyo sahihi. Inaanza kuangalia mauzo na matumizi, kabla ya kuangalia faida.

Hivyo kinachotokea ni hiki, kila mara biashara inapoingiza fedha kupitia mauzo, kinachoanza kufikiriwa ni matumizi kwanza na hayo yakishaisha ndiyo mfanyabiashara anaangalia kama kuna faida imebaki. Sasa kama unaijua fedha vizuri, unajua kwamba matumizi huwa hayaishi, kama fedha zipo basi huwa hazikosi matumizi.

Mtu anapoona biashara haitengenezi faida, anakazana kuongeza mauzo, mauzo zaidi yanaleta fedha zaidi, ambazo zinazalisha matumizi zaidi na faida kuzidi kuwa kidogo. Hapa ndipo wafanyabiashara wengi wanapokuwa wamekwama wasijue jinsi gani ya kutengeneza faida kutoka kwenye biashara zao.

Mike anatuelewesha hili vizuri kwa kutumia mfano wa dawa ya meno. Anasema unapokuwa na dawa mpya ya meno, unaiminya na kutoa dawa nyingi kuweka kwenye mswaki wako. Kama kwa bahati mbaya dawa uliyoweka imeanguka chini, unabonyeza na kutoa nyingine bila ya shaka. Lakini kadiri kichupa chako cha dawa ya meno kinavyoisha, ndivyo matumizi yako yanapungua. Inafika siku dawa imeisha kabisa kwenye kichupa, lakini unataka kupiga mswaki, basi hapo ndipo unapata ubunifu wa hali ya juu, unaibonyeza chupa hiyo kwa ustadi wa hali ya juu, kwa kuanzia chini kabisa, kupanda nayo kidogo kidogo mpaka kufika juu, na hapo unapata dawa kidogo ambayo unaipakaza kwenye mswaki wako na kuendelea na zoezi la kusafisha meno. Katika kipindi cha uhaba wa dawa kama hivyo hakuna hata tone moja la dawa linalopotea.

Toothpaste full
Wakati chupa ya dawa ya meno imejaa unatumia kwa wingi mpaka kupoteza
toothpaste empty
Wakati dawa imeisha unatumia kwa uangalifu mkubwa.

Hivi ndivyo biashara zilivyo pia, fedha inapokuwa inapatikana, matumizi yanakua yenyewe. Lakini fedha inapokuwa ngumu, matumizi yanashuka. Kwa kifupi mfanyabiashara atajipanga jinsi ya kuendesha biashara yake kulingana na fedha inayopatikana. Kama fedha ni nyingi matumizi yanakuwa makubwa, kama fedha ni kidogo matumizi yanapungua pia.

Kanuni ya zamani ya uhasibu haifanyi kazi kwa sababu matumizi huwa hayana ukomo.

Ndiyo maana hata mfanyabiashara anapofanyiwa mahesabu ya biashara yake na mhasibu, kisha kwenye taarifa ya fedha akamwambia kwa mwaka huu umeingiza faida kiasi fulani, huwa anabaki kushangaa, kwa sababu akiangalia faida hiyo haioni. Kwenye namba za kihasibu biashara inakuwa imezalisha faida, lakini kwenye uhalisia, faida hiyo mfanyabiashara haioni, hawezi kuzishika fedha au kuonesha kwenye akaunti na kusema hii ndiyo faida halisi niliyotengeneza kwenye biashara yangu.

SOMA; Amri Kumi (10) Za Biashara Ambazo Hupaswi Kuzivunja Kama Unataka Kufanikiwa.

Kanuni mpya ya kihasibu inayoleta faida kwenye biashara.

Mike anatushirikisha kanuni mpya ya kihasibu ambayo inakuwezesha wewe kuiona faida halisi ya biashara yako.

Kanuni hiyo inasema hivi; MAUZO – FAIDA = MATUMIZI.

Kanuni ni ile ile, ila kilichobadilika ni vipaumbele. Kwa kanuni hii mpya, baada ya biashara kufanya mauzo, kinachofanyika ni kuondoa faida kwanza kabla ya kufanya matumizi. Kwa njia hii, ni rahisi kuiona faida yako halisi iko wapi.

Kanuni hii mpya inaondoa ile hali ambayo tumeiona ya matumizi kukua kulingana na kipato kilichopo. Kama kwa kila kipato unaondoa kwanza faida kabla hujatumia, kile kiwango kinachobaki unakitumia kwa uangalifu mkubwa. Kwenye mfano wetu wa dawa ya meno, ni wakati ambapo dawa imeisha kwenye chupa na hivyo huwezi kuipoteza kabisa.

profit first accounts

Jinsi ya kutekeleza mpango wa faida kwanza kwenye biashara yako.

Kwa kuwa tumeshaona kwamba ukisubiri matumizi yaishe ndiyo ubaki na faida kwenye biashara yako huwezi kuona faida kamwe, tunapaswa kuwa na njia ya kuiondoa faida kwanza kabla matumizi hayajaanza.

Na hapa mwandishi anashauri njia bora ya kufanya hili, ambalo ni kufungua akaunti tofauti ya faida. Akaunti hii inahifadhi zile fedha ambazo ni faida kutoka kwenye biashara yako. Masharti ya akaunti hii ni kwamba haiguswi kabisa, haupaswi kuondoa fedha kwenye akaunti hii na kuiweka kwenye matumizi yoyote yale.

Hivyo mwandishi anatuambia, kupitia benki ambayo ndiyo una akaunti kuu ya biashara yako, fungua akaunti nyingine ambayo ndiyo itakuwa inatunza faida yako.

Kwa kuanzia, mwandishi anasema kila kiwango cha fedha kitakachoingia kwenye biashara yako kama mauzo, unapaswa kukata asilimia moja ya kiwango hicho cha fedha na kuiweka kwenye akaunti ya akiba. Haijalishi ni mauzo ya nini na kiasi gani, fedha ikishaingia tu kwenye akaunti kuu, asilimia moja inakatwa na kuwekwa kwenye akaunti ya faida.

Hii ni hatua ya kwanza kuchukua na unayopaswa kuchukua mara moja, hii haihitaji kujipanga au kusubiri.

Wakati zoezi hilo la kuwa na akaunti mpya limekamilika na asilimia moja ya mauzo yote inakwenda huko, una kazi ya kujua kiwango chako cha faida kwenye biashara yako.

Hapa unapaswa kujua kwa mauzo unayofanya, ni asilimia ngapi ndiyo faida yako kama utaondoa yale matumizi ya msingi kabisa. Ukishajua kiwango chako cha faida, hicho ndiyo utakachokuwa unakiondoa kwenye mauzo yako na kutunza kwenye akaunti yako ya faida kwanza. Mfano kama umegundua kiwango chako cha faida ni asilimia 10 ya mauzo, basi kila unapofanya mauzo, ondoa asilimia 10 na iweke kwenye akaunti ya faida kwanza. Ukifanya hivi kwa muda, labda miezi mitatu, sita au mwaka, utajionea mwenyewe faida halisi ambayo biashara yako itakuwa imetengeneza.

Vipi kama fedha iliyobaki haikidhi matumizi?

Najua unatikisa kichwa na kukubali kwamba njia hii itakuwezesha kuiona faida kwenye biashara yako, lakini najua kuna swali moja bado linakutatiza kwenye akili yako. Swali hilo ni vipi kama fedha inayobaki baada ya kuondoa faida haitoshi kukidhi matumizi ya biashara yako? Na hapo ndipo pazuri na panapokupa mwanga, kwa sababu hilo linaonesha kwamba biashara hiyo ina matumizi makubwa kuliko mapato yake.

Hivyo kazi yako kubwa kama mfanyabiashara ni kupitia matumizi yote ya biashara na kuchagua yapi ya msingi yanayoweza kuendelea na yapi yanaweza kupunguzwa na/au kufutwa kabisa kwenye biashara yako.

Kumbuka sisi binadamu na hasa wafanyabiashara, ni wazuri sana kwenye kutumia kile kinachopatikana. Hivyo utakapoanza kuondoa biashara kwanza, utajifunza ni yapi matumizi ya msingi na kutimiza hayo na kuachana na yale yasiyo ya msingi.

Unaifanyia nini faida yako na baada ya muda gani?

Swali jingine ambalo watu wamekuwa wanajiuliza ni hili, mpango huu unatuambia tuweke faida kwenye akaunti tofauti na tusiitoe kabisa, je unaitumia faida hiyo kufanya nini na kwa wakati gani?

Na jibu liko wazi, utaamua mwenyewe utumieje faida halisi uliyoipata kwenye biashara yako. Lakini jilipe faida hii kila baada ya miezi mitatu, chukulia ni kama umewekeza kwenye kampuni iliyopo kwenye soko la hisa ambayo inatoa gawio kila robo mwaka. Faida unayokuwa umeitenga ndiyo gawio lako.

Mwandishi anashauri matumizi sahihi ya faida halisi ya biashara yako kuwa kama ifuatavyo. Unachukua nusu ya faida hiyo na kufanya matumizi binafsi, hapo usiihusishe kabisa na biashara yako. Nunua chochote unachopenda au fanya matembezi yoyote unayotaka, haya ndiyo matunda ya biashara yako umeanza kuyavuna, yafurahie.

Nusu ya faida iliyobaki hiyo unaweza kuiacha kama fedha ya dharura au kuirudisha kwenye biashara kama ongezeko la mtaji. Mwandishi anashauri utengeneze kwanza kiwango cha kutosha cha akiba ya dharura, hii ni fedha inayoiwezesha biashara kujiendesha kwa angalau miezi mitatu hata kama mauzo yapo chini kabisa. Kiwango hicho cha dharura kikishakamilika, basi faida ya ziada inarudi kwenye biashara kama ongezeko la mtaji.

SOMA; Njia Kumi (10) Za Kupata Mpenyo Ambao Utaiwezesha Biashara Yako Kukua Na Kufikia Mafanikio Makubwa.

Hatua za kuchukua leo.

Umeshajifunza jinsi ambavyo unaweza kuiona faida halisi ya biashara yako, kilichobaki ni wewe kuchukua hatua ili kuondoka kwenye mtego ulionasa sasa kibiashara. Najua biashara yoyote unayoendesha sasa inakupa shida sana kuiona faida halisi. Leo hii, nenda kwenye benki ambayo ndipo akaunti yako ya biashara ipo, kisha omba kufungua akaunti nyingine mpya, ambayo siyo rahisi kuondoa fedha. Kisha weka mfumo wa benki kufanya makato ya moja kwa moja kwenye kila kiwango cha fedha kinachoingia kwenye akaunti yako kuu na kupeleka kwenye akaunti mpya. Unaweza kuweka kiwango cha asilimia moja au asilimia nyingine ambayo umeipata kwa kukokotoa kiango halisi cha faida kwenye biashara yako.

Chukua hatua hiyo muhimu sana leo, na kuanzia miezi mitatu ijayo utakuwa unachekelea, kwa sababu kwa mara ya kwanza utaweza kuiona faida halisi ya biashara yako.

Kwenye makala ya TANO ZA JUMA namba 38 la mwaka huu 2019, tunakwenda kujifunza mengi zaidi kutoka kitabu hicho cha PROFIT FIRST. Tutajifunza aina nyingine nne za akaunti unapaswa kuwa nazo, jinsi ya kupunguza gharama za kuendesha biashara yako na kuweza kukuza zaidi faida kupitia biashara hiyo. Usikose makala hiyo ya TANO ZA JUMA kama kweli unataka kuwa na biashara inayozalisha faida na siyo matatizo.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

WhatsApp Image 2019-07-13 at 18.40.50