“Matatizo yote ya binadamu chanzo chake ni mtu kushindwa kukaa peke yake kwenye chumba bila ya kuwa na kitu cha kufanya.” Hii ni kauli ambayo ilitolewa na mwanahisabati, mwanafalsafa na mwandishi Blaise Pascal mwaka 1654.

Unaweza kusema kauli hiyo ni ya zamani na haina ukweli kwenye zama tunazoishi sasa. Lakini utakuwa umekosea sana, kwa sababu utafiti uliofanyika mwaka 2014, umeweza kudhibitisha kauli hiyo.

Mwaka 2014 kulifanyika utafiti ambapo watu walipewa jukumu moja tu, kukaa kwenye chumba peke yao na kufikiri. Chumba hicho hakikuwa na kitu chochote kile, bali nyaya za umeme ambazo mtu akizishika anapigwa shoti na kuumia.

Kabla ya kuingia kwenye chumba hicho, watu waliulizwa kama wapo tayari kushika nyaya hizo za umeme na kupigwa shoti, wote walisema hawapo tayari kuzishika. Hivyo waliwekwa kwenye chumba hicho na kuachwa, kwa dakika 15 mpaka 25 bila ya kitu cha kufanya, bali kufikiri tu.

Baada ya kuachwa kwenye chumba hicho kwa muda, asilimia 67 ya wanaume na asilimia 25 ya wanawake walizishika nyaya za umeme na kupigwa shoti. Tena wengine walifanya hivyo zaidi ya mara moja. Waendeshaji wa utafiti huu walijumuisha kwamba, watu huwa hawapo tayari kukaa bila ya kuwa na kitu cha kufanya, watafanya hata kitu kinachowadhuru lakini siyo kukaa kwa upweke.

Rafiki, hili halishangazi, kwa sababu zama tunazoishi sasa, ni zama zenye kelele ya kila aina. Simu janja tunazotembea nazo kila mahali, ni chanzo kikuu cha usumbufu kwenye maisha yetu. Ukiwa umekaa karibu na mtu na simu yake ikaita, utaangalia na yako pia. Ukipata dakika chache za kuwa mpweke, haraka sana utakimbilia kuangalia simu yako, kuingia mitandaoni, kufuatilia habari na kadhalika.

stillness is the key.jpg

Matatizo makubwa uliyonayo kwenye maisha yako, ni matokeo ya kushindwa kukaa peke yako kwenye eneo tulivu na kufikiria bila ya kuwa na usumbufu wa aina yoyote ile. Huu ni ukweli ambao wengi hawajawahi kupata nafasi ya kuujua, lakini wewe umepata nafasi hiyo leo, hivyo itumie vizuri.

Ipo nguvu moja kubwa sana iliyopo ndani yako, ambayo ukiijua na kuanza kuitumia, utaweza kutatua kila aina ya tatizo ulilonalo, itaweza kuzuia usitengeneze matatizo mapya na itakuwezesha kuwa na maisha bora na yenye utulivu mkubwa. Nguvu hiyo ni muhimu sana kwenye zama tunazoishi sasa, zama ambazo tumezungukwa na usumbufu mpaka kwenye vitanda vyetu.

Hivi unaweza kuamini kwama zaidi ya asilimia 90 ya watu wanalala na simu zao, tena zikiwa wazi na hivyo kuruhusu usumbufu wowote kuwafikia, hata kama wamelala? Na je unajua asilimia zaidi ya 80 ya watu kitu cha kwanza wanachofanya wanapoamka ni kuangalia simu zao, kujua nini kimeendelea duniani ili wasipitwe?

Unaweza kuona hayo ni maendeleo, lakini kwa hakika siyo maendeleo, ni kinyume kabisa na maendeleo, ni mtu kujirudisha nyuma, kwa sababu mtu anaianza siku akiwa amevurugwa badala ya kuianza siku kwa utulivu ambao utamwezesha kufanya makubwa.

Nguvu kubwa ambayo unakwenda kujifunza hapa ni UTULIVU, kuweza kukaa peke yako eneo tulivu na kufikiri, bila ya kuruhusu usumbufu wowote ukuondoe kwenye utulivu wako. Hii ni nguvu kubwa mno, ambayo tayari ipo ndani yako, unachopaswa kujua ni jini ya kuifikia na kuanza kuitumia.

SOMA; Siri Pekee Ya Mafanikio Ambayo Hakuna Anayekusisitizia Kama Siri Nyingine.

Mwandishi Ryan Holiday kwenye kitabu chake kipya kinachoitwa STILLNESS IS THE KEY amejadili kwa kina sana kuhusu dhana hii ya UTULIVU, ametuonesha jinsi ambavyo ni muhimu, jinsi ambavyo viongozi wakubwa, watu wa dini, falsafa na hata waliofanikiwa sana waliweza kutumia nguvu hii ya utulivu kufanya makubwa.

Ukiangalia Falsafa zote kubwa duniani na hata wanafalsafa wakubwa, walikuwa na utaratibu wa kutenga muda wa kukaa peke yao bila ya kuruhusu usumbufu wowote na kufikiri kwa kina.

Hata kwenye dini kubwa duniani, mfano Ukristo, Uislamu na Ubudha, wale ambao dini hizi zimeanzishwa kupitia wao, walipenda kupata muda ya kuwa peke yao. Yesu (Ukristo), Mohamad (Uislamu) na Gautama (Ubudha) katika vipindi vyao, walikuwa na utaratibu wa kuyaacha mazingira yao, kuwaacha wafuasi wao na kwenda milimani au msituni peke yao na kupata muda wa kuwa tulivu, kufikiri na kutafakari kwa kina. Ni katika nyakati hizo za UTULIVU na kutafakari ndipo viongozi hao waliweza kupata ufunuo na uamsho ambao umekuwa msingi wa dini hizo.

Nguvu hii pia ipo ndani yako, lakini umeidumaza kwa sababu kila siku umekuwa unakimbia mazingira yanayokuacha wewe na fikra zako tu.

Kwenye kitabu chake Ryan anatuambia UTULIVU ni ufunguo wa vitu vingi sana kwenye maisha, baadhi ya vitu hivyo ni kama;

Kufikiri kwa umakini na kwa ufasaha.

Kuweza kuuona mchezo mzima pale unapokuwa na ushindani.

Kufanya maamuzi magumu.

Kudhibiti hisia zako.

Kuweza kuyajua malengo sahihi kwako.

Kuweza kukabiliana na hali zenye msongo mkubwa.

Kuweza kuimarisha mahusiano yako na wengine.

Kujijengea tabia bora.

Kuongeza ufanisi na uzalishaji wako.

Kuweza kufurahia hali unayopitia, bila ya kujali ni hali gani.

Utulivu ni ufunguo wa kila kitu kwenye maisha, hakuna kitu chochote ambacho ufunguo huu hauwezi kufungua pale kinapokuwa kimefungwa.

Kama unataka kuwa mzazi bora, msanii bora, mfanyakazi bora, mfanyabiashara mwenye mafanikio, mwekezaji mkubwa, mwanamichezo mkubwa, mwanasayansi bora au hata kuwa mtu bora, ufunguo pekee unaoweza kuutumia kufika huko ni UTULIVU.

Jijengee tabia ya kuwa na muda wa utulivu kwenye kila siku yako, muda ambao unakaa wewe peke yako na mawazo yako, na hakuna usumbufu wowote unaokuwa karibu na wewe katika wakati huu.

Hili ni zoezi gumu sana katika zama hizi, lakini linawezekana kama ukiamua, anza na muda mdogo kama wa dakika 15 mpaka 30, kisha endelea kuongeza muda huo kadiri unavyokwenda. Mwanzoni litakuwa zoezi gumu sana, utakapokaa tu utaanza kufikiria vitu vingi ambavyo ungeweza kuwa unafanya, mambo mazuri yanayoendelea mtandaoni ambayo yanakupita, lakini usiruhusu hayo yakuondoe kwenye utulivu wako.

Anza zoezi hili na utaona jinsi ambavyo maisha yako yataanza kubadilika na kuwa tulivu na bora zaidi. Msongo utapungua, wasiwasi na mashaka ya kupoteza vitu yataondoka kabisa na utajiona unayaendesha maisha badala ya maisha kukuendesha wewe.

Kwenye uchambuzi wa kitabu cha juma hili, tutakwenda kujifunza kwa kina kutoka kwenye kitabu hiki cha STILLNESS IS THE KEY, tutaona jinsi ya kupata utulivu wa AKILI, ROHO na MWILI, kuna hatua mbalimbali za kuchukua ili kupata utulivu kwenye maisha yetu kwa kuanzia maeneo hayo matatu yanayotengeneza utu wetu.

Kupata uchambuzi huu, jiunge sasa na channel ya SOMA VITABU TANZANIA, kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania kisha bonyeza JOIN na utakuwa umejiunga. Kwa kujiunga utaweza kupata vitabu na chambuzi zake na kujifunza ili uweze kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania