Rafiki yangu mpendwa,

Sisi binadamu ndiyo viumbe hai pekee ambao tunazaliwa tukiwa hatujakamilika na kuwa na maandalizi sahihi ya kukabiliana na mazingira yetu.

Swala akizaliwa, masaa machache baadaye anakuwa tayari kukimbia wanyama wakali na kuokoa maisha yake, lakini sisi binadamu tunapozaliwa, tunakuwa hatuna uwezo wowote wa kukabiliana na mazingira yetu.

Inatuchukua muda mrefu kujifunza mpaka kuwa tayari kuyakabili maisha yetu sisi wenyewe. Na hii ni kwa sababu nguvu yetu sisi binadamu ipo kwenye akili zetu, tofauti na wanyama wengine. Sisi binadamu ndiyo viumbe hai pekee ambao tunaweza kufikiri na kupanga mambo, wanyama wengine wanaendeshwa tu na hisia au mazingira yao.

Pamoja na uwezo huu mkubwa ambao sisi binadamu tunao, ni wachache sana ambao wameweza kuutumia, kufikiri na kufanya maamuzi sahihi kwao, wengi wamekuwa wakifanya kile ambacho wengine wanafanya.

Pia licha ya kutumia muda mwingi kujiandaa kukabiliana na mazingira, watu wengi bado wanayaendesha maisha yao bila ya kujijua wao wenyewe au kuyaelewa maisha yao.

Na sehemu kubwa ambayo watu wengi wanashindwa ni kwenye kujua maana ya maisha yao na kusudi la wao kuwa hapa duniani.

life meaning.jpg

Maana na kusudi la maisha ndiyo vitu vyenye nguvu kubwa sana kwa maisha ya kila mtu, lakini ni wachache sana wanaopata nafasi ya kuvijua. Wengi wanaishia kuwa na maisha ya kawaida, kwa sababu hakuna mtu anayeweza kumwambia mwingine maana na kusudi la maisha, hivi ni vitu ambavyo mtu mwenyewe anavitambua kutoka ndani yake.

Sasa kwa kuwa wengi hawatumii akili zao kufikiri wao wenyewe, badala yake wanaangalia kile ambacho wengine wanafanya na wao kukifanya, hawapati nafasi ya kujitambua na kujua maana na kusudi la maisha yao.

Leo wewe rafiki yangu unakwenda kuondokana na hali hiyo, kupitia makala hii, utakwenda kujifunza njia tatu za kujua maana na kusudi la maisha yako. Kupitia njia hizi tatu, utaweza kuyatafakari maisha yako, kujitambua wewe mwenyewe na kuweka vipaumbele sahihi kwenye maisha yako.

Viktor Frankl, aliyekuwa daktari bingwa wa magonjwa ya akili na mmoja wa watu waliopitia mateso makali wakati wa vita kuu ya pili ya dunia, aliandika kitabu kinachojulikana kama MAN’S SEARCH FOR MEANING. Kwenye kitabu hiki, ambacho kinashirikisha historia fupi ya mateso yake pamoja na tiba ya kisaikolojia kupitia maana (logotherapy), Frankl ametushirikisha njia tatu za kujua maana na kusudi la maisha.

Karibu tujifunze njia hizi tatu na jinsi tunavyoweza kuzitumia na kuyafanya maisha yetu kuwa bora zaidi. (Kupata uchambuzi kamili wa kitabu cha MAN’S SEARCH FOR MEANING Fungua; https://www.t.me/somavitabutanzania)

NJIA YA KWANZA; KAZI YA KIBUNIFU.

Njia ya kwanza ya kujua maana na kusudi la maisha yako ni kupitia kazi ya kibunifu, kazi ambayo unaifanya kutoka ndani ya moyo wako na yenye manufaa makubwa kwa wengine. Kazi hiyo unakuwa unaipenda sana kiasi kwamba uko tayari kuifanya hata kama hakuna anayekulipa. Ukiwa unafanya kazi hiyo akili yako yote inakuwa kwenye kazi hiyo kiasi kwamba unaweza kusahau hata kula.

Kama umewahi kukutana na hali kama hii kwenye maisha yako, basi jua hapo ndipo maana na kusudi la maisha yako lilipo. Haijalishi kazi hiyo ni ya kuajiriwa, kujiajiri au biashara, kama tu unavutiwa kufanya kitu na upo tayari kukifanya muda wote, basi hicho ni kitu chenye maana kubwa kwako na ndiyo kimebeba maana ya maisha yako.

Wale wote ambao wameibadili dunia kupitia gunduzi mbalimbali walizofanya, siyo kwa sababu walikuwa wanataka kulipwa au kuonekana, bali ni kwa sababu walipenda sana kile walichofanya. Wengi walipingwa, kukosolewa na kukatishwa tamaa, lakini hawakusikiliza chochote, maana ndani yao walishajitoa kweli na walikuwa wakifurahia sana wanachofanya.

Jiulize katika mambo yote unayofanya kwenye siku yako na ambayo umewahi kufanya siku za nyuma, ni kipi ambacho umekuwa unavutiwa sana kukifanya, kile ambacho unaona mchango mkubwa unaotoa kwa wengine na upo tayari kukifanya muda wote.

Jibu hili lazima lianzie ndani yako, watu kwa nje wanaweza kukuona uko vizuri kwenye eneo fulani, lakini ni wewe pekee unayeweza kujua ndani yako kama kitu kinakupa msukumo mkubwa wa kukifanya au unakifanya tu ili uonekane au ulipwe. Kile ambacho unapata msukumo mkubwa wa kukifanya kutoka ndani yako, ndiyo kimebeba maana ya maisha yako na ndipo kusudi la maisha yako lipo.

Kujua maana na kusudi la maisha kupitia kazi, jiulize ni kitu gani unapenda sana kufanya ambacho kina manufaa kwa wengine na upo tayari kukifanya hata kama hakuna anayekulipa. Ukishakijua, kipe muda zaidi na angalia namna unavyoweza kukigeuza kuwa kitu kikuu unachofanya kwenye maisha yako, yaani kiwe ndiyo njia ya wewe kuingiza kipato na hapo utaweza kuwa na maisha bora sana.

NJIA YA PILI; MTU AU WATU UNAOWAJALI.

Njia ya pili ya kujua maana na kusudi la maisha ni kupitia mtu au watu ambao mtu unawajali, kwa maneno mengine ni kupitia upendo wako kwa mtu au watu wengine.

Upendo una nguvu kubwa sana, hasa pale unapokuwa upendo wa kujitoa kweli kwa ajili ya mtu au watu wengine. Upendo unakupa nguvu ya kufanya makubwa kwa ajili ya wengine na kukuondoa kwenye ubinafsi.

Watu wengi wanakuwa na maisha yasiyo bora kwa sababu wana ubinafsi, wanajali mambo yao zaidi na hawana watu ambao wamejitoa kuhakikisha wanakuwa bora.

Unapokuwa na watu ambao unawapenda na kuwajali kweli, ambao upo tayari kufanya lolote ili kuhakikisha maisha yao yanakuwa bora, unapata maana na kusudi la maisha yako. Hapa msukumo unakuwa siyo fedha, bali kuona wengine wakiwa vizuri, wale unaowajali.

Hili ndiyo linawafanya baadhi ya watu kuchukua kazi ambazo hazina malipo makubwa, lakini zenye msaada mkubwa kwa wengine. Mfano mtu anayechagua kuwasaidia yatima au watu wenye mazingira magumu, hapati fedha nyingi, lakini anapata kuridhika kwa jinsi anavyofanya maisha ya wengine kuwa bora.

Au mtu anayebeba jukumu la kuhakikisha familia yake au wale wanaomtegemea wanakuwa na maisha bora, atajisukuma kwa kila namna kuhakikisha anatimiza hilo.

Kujua maana na kusudi la maisha yako kupitia upendo, jiulize ni watu gani unaowapenda sana, ambao upo tayari kufanya lolote kwa ajili yako na watumie hao kuyapa maisha yako maana na kuwa na kusudi unalofanyia kazi, ambalo ni kuhakikisha watu hao wananufaika na uwepo wako.

Hapa pia tunaweza kuchanganya njia ya kwanza na ya pili na tukapata maana kubwa ya maisha yetu, kwa kuwa na watu ambao tunawajali, na kitu ambacho tunapenda kufanya, kisha kufanya kitu hicho kwa ajili ya wale ambao tunawapenda.

NJIA YA TATU; MATESO.

Njia ya tatu ya kujua maana na kusudi la maisha yako ni kupitia mateso. Buddha aliwahi kusema, maisha ni mateso na kila mtu kuna mateso anayopitia kwenye maisha yake, wenye nacho wanateseka na kile walichonacho, na wasiokuwa nacho wanateseka kwa kile wanachokosa.

Watu wengi wamekuwa wanalalamikia mateso wanayopitia na kutafuta watu wa kuwalaumu au kuwalalamikia kwa mateso hayo wanayopitia kwenye maisha yao. Lakini licha ya kufanya hivyo, bado mateso hayo yanaendelea kuwaandama na hilo hupelekea wengi kukata tamaa na maisha.

Ambacho wengi hawajui ni kwamba, mateso wanayopitia yanaweza kuwa maana na kukupa kusudi la maisha yao.

Kujua maana na kusudi la maisha yako kupitia mateso, angalia yale mateso unayopitia na usiangalie tu upande wa mateso, bali angalia mateso hayo yanakuja na kitu gani kwako. Utaona mateso hayo yanakuandaa kuwa bora zaidi au yanakufundisha kuwa mvumilivu au yanakupa nafasi ya kuwajua watu vizuri.

Kwa vyovyote vile, mateso unayopitia kwenye maisha yana maana fulani kwako na hata kwa wengine pia. Hata unapompoteza mtu wa karibu na uliyempenda sana, ukiangalia kwa upande mwingine, jambo hilo lina manufaa kwako, linaweza kuwa linakufundisha upendo wa kweli, kujali watu wakati bado wapo hai na hata kuwa mvumilivu pale unapopoteza kile unachokijali sana.

Pale unapokutana na ugumu, changamoto, vikwazo au mateso kwenye maisha yako, usiyakimbie wala kulalamika, badala yake jiulize hilo ulilokutana nalo limekuja na manufaa gani kwako? Na mara zote utaona manufaa, ambayo yatayafanya maisha yako kuwa na maana na kufanyia kazi hicho unachopitia kinakuwa ndiyo kusudi la maisha yako.

Rafiki, kwa pamoja, njia hizi tatu zinaweza kuungana na kutuwezesha kutengeneza maana na kusudi la maisha yetu kama ifuatavyo; kuna kitu ambacho unapenda sana kukifanya, hivyo unakifanya kwa ajili ya wale unaowapenda na kuwajali sana na magumu unayokutana nayo kwenye maisha yako, yanakusukuma zaidi kufanya kitu hicho.

Kaa chini na orodhesha vitu hivyo vitatu; kazi unayopenda kufanya, watu unaowajali sana, mateso unayopitia kwenye maisha yako, kisha viweke pamoja na hapo utakuwa na maisha yenye maana na kuwa na kusudi linalokusukuma kuamka kila siku na kwenda kuendelea na mapambano.

Kujua maana na kusudi la maisha yako ndiyo hitaji la kwanza na muhimu kama unataka kufanikiwa. Tumia njia hizi tatu tulizojifunza hapa kutengeneza maana na kusudi la maisha yako.

Kupata uchambuzi kamili wa kitabu cha MAN’S SEARCH FOR MEANING, ambapo utajifunza mateso ambayo watu walipitia wakati wa vita ya pili ya dunia pamoja na jinsi maana ya maisha inavyoweza kuwa tiba ya magonjwa ya akili, karibu ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA, kwa kufungua; https://www.t.me/somavitabutanzania kisha kubonyeza JOIN CHANNEL. Kwa kujiunga na channel hiyo utapata chambuzi za vitabu vingine vingi.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania