Karibu tena rafiki yangu kwenye makala ya ushauri wa changamoto mbalimbali ambazo zinakuwa kikwazo kwenye safari yetu ya mafanikio. Kama ambavyo tunajua, safari ya mafanikio siyo rahisi, mambo huwa hayaendi kama tunavyopanga, vikwazo na changamoto ni sehemu ya safari hii. Hivyo ili kufanikiwa, lazima tuwe tayari kukabili na kutatua changamoto hizo na siyo kuzikimbia.

Leo tunakwenda kupata ushauri wa jinsi ya kuwashawishi watu kujiunga na biashara ya mtandao (network marketing), ili uweze kufanikiwa kama unaifanya biashara hiyo.

NETWORK MARKETING

Kabla hatujaingia kwa kina kwenye ushauri huu, tusome maoni ya wasomaji wenzetu ambao wametuandikia kuomba ushauri kwenye hilo.

Habari, changamoto ni kubwa mno ninafanya network marketing nina mwaka mmoja sasa. Changamoto ni kupata watu maana wanahitaji mimi nipeleke watu wawili sema nimepeleka mmoja na huyo mmoja ameshaanza kutengeneza timu naye. Sasa bado mmoja ambao bado naendelea kutafuta sasa sijui nitumie mbinu gani maana naona watu wengi wananipiga vita sana. – Ernest A.

Changamoto yangu  naomba kujuzwa ni kwa jinsi gani naweza kuwashawishi wanafunzi wenzangu kwenye biashara ya network marketing ili niweze kufanikiwa nikiwa kama mwanafunzi. – Hance A. M.

Tumesoma jinsi wenzetu wanavyokwama kuwashawishi watu kujiunga na biashara hii ya mtandao, hali ndivyo ilivyo kwa wengi, na hivyo leo tunakwenda kushirikishana mambo muhimu ya kuzingatia ili uweze kuwashawishi watu kujiunga na pia kufanikiwa kwenye biashara hii.

Moja; biashara ya mtandao ni nzuri.

Biashara ya mtandao ni mfumo wa biashara ambapo mtu unakuwa msambazaji wa bidhaa za kampuni fulani na kulipwa kamisheni kulingana na bidhaa unazonunua wewe na wale ambao wamejiunga kupitia wewe. Biashara hii inategemea mtandao wako binafsi, wa watu unaowajua na mnaoheshimiana, ambao ukiwaambia kitu chenye manufaa wanakifanyia kazi.

Hii ni biashara nzuri sana kuanza kwa watu ambao wanapenda kuongeza kipato chao lakini kuingia kwenye biashara za kawaida ni changamoto kwao. Biashara hii imepunguza changamoto nyingi za biashara za kawaida. Kwa mfano huhitaji mtaji mkubwa kuanza, huhitaji kuwa na eneo la kufanyia biashara na wala huhitaji vibali mbalimbali. Mengi yanafanyiwa kazi na kampuni mama, wewe ni kutumia bidhaa na kuwaalika wengine nao watumie na kisha kulipwa kamisheni yako.

Waajiriwa, wanafunzi na watu wengine ambao tayari wana kitu kingine wanafanya, biashara hii ni nzuri kwao kuongeza kipato, kwani unaweza kuifanya kwa muda wako wa ziada. Na hata kama tayari unafanya biashara nyingine, unaweza pia kufanya biashara ya mtandao, kama umekutana na kampuni nzuri ambayo bidhaa zake unazitumia na zina manufaa kwako.

Kuielewa vizuri biashara hii ya mtandao ni hatua ya kwanza kwenda kuifanya kwa mafanikio makubwa.

Mbili; anza kuwa mtumiaji wa bidhaa husika.

Kosa kubwa ambalo watu wengi wanafanya wanapoingia kwenye biashara ya mtandao, wanaangalia faida ya kifedha watakayoipata kwa kufanya biashara hiyo. Na ndiyo maana ushawishi unaegemea zaidi kwenye fedha. Lakini watu wanapojiunga, ndiyo wanakutana na ukweli kwamba kupata fedha siyo rahisi kama walivyodhani, na hapo wengi hukata tamaa na kuona wamedanganywa au kutapeliwa.

Sababu ya kwanza kabisa kwako kujiunga na biashara yoyote ile ya mtandao ni wewe uwe mtumiaji wa bidhaa za kampuni hiyo na ziwe na manufaa kwako. Kwa kuwa mtumiaji wa bidhaa, kisha zikakupa manufaa ni rahisi kuwashawishi wengine nao watumie ili wapate manufaa kama uliyoyapata wewe.

Fikiria labda ulikuwa na shida ya ngozi ambayo inakusumbua kwa muda mrefu, ukakutana na biashara ya mtandao yenye bidhaa nzuri kwa ngozi, ukatumia bidhaa hizi na shida yako ikaisha. Watu wataanza kukuuliza umefanya nini, na hapo utawaeleza kuhusu biashara hiyo, na wale wenye shida kama yako watapenda kujiunga.

Pia unapotumia bidhaa hizo na kunufaika nazo, ni rahisi kuwashawishi watu kwa mifano kabisa, na kuwaonesha jinsi wewe ulivyonufaika na biashara hiyo.

Kuwa mtumiaji wa bidhaa za kampuni ya biashara ya mtandao unayojiunga nayo ni hitaji muhimu katika kujenga ushawishi, huwezi kuwashawishi watu kwa kitu ambacho hukielewi, hukipendi na hukiamini. Hivyo ili kuelewa, kupenda na kuamini biashara ya mtandao unayoifanya, anza kuwa mtumiaji wa bidhaa hizo.

SOMA; USHAURI; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kujua Biashara Ya Mtandao Iliyo Sahihi Na Kuepuka Kutapeliwa.

Tatu; biashara hii haimfai kila mtu.

Kosa jingine kubwa linalofanywa na wale wanaojiunga na biashara ya mtandao na linawapelekea kukata tamaa na kushindwa ni kutaka kila mtu awe mteja wa biashara hiyo. Kwanza kabisa unapaswa kujua hakuna biashara yoyote ile duniani ambayo mteja wake ni kila mtu, kila biashara ina aina ya wateja ambao inawalenga.

Kadhalika biashara ya mtandao, hakuna ambayo inamlenga kila mtu, bali kila biashara ina aina ya wateja ambao inawalenga.

Hivyo unapaswa kujua biashara unayofanya wewe inawalenga wateja wa aina gani, kisha kuongea na wengi wenye sifa hizo.

Ni kujidanganya na kujiandaa kushindwa, kwenda kumshawishi mtu anunue kipodozi cha elfu 30 wakati hela ya kula hana. Lazima uwajue watu sahihi wa kuwashirikisha biashara yako ambao ukiweka ushawishi mzuri wanao uwezo wa kujiunga.

Sifa kuu mbili za kuzingatia katika kuchagua watu wa kuwashirikisha biashara ya mtandao niuhitaji na uwezo.

Kwenye uhitaji unaangalia wale ambao wana matatizo au changamoto ambazo bidhaa za kampuni hiyo zinaweza kutatua. Mtu mmoja amewahi kusema, kama mtu anazama kwenye maji, huna haja ya kumshawishi kununua boya la kumwokoa, akiliona analichukua mara moja. Hivyo angalia ni watu gani ambao wana tatizo ambalo linaweza kutatuliwa na bidhaa za biashara unayofanya kisha waoneshe jinsi matatizo yao yatatatuliwa na hao utaweza kuwashawishi kujiunga.

Kwenye uwezo, lazima uangalie kwa kipato cha mtu huyo kama anaweza kumudu kununua bidhaa za kampuni husika. Kwa sababu kama hana uwezo, hata umshawishi namna gani, hawezi kujiunga. Na hata kama utamsukuma sana akajiunga, bado hatakuwa na manufaa, kwa sababu anapaswa kuwa mteja endelevu, anayenunua kila mwezi ili wewe unufaike.

Usipoteze nguvu zako kuhangaika na kila mtu, weka vigezo vya uhitaji na uwezo, kisha chagua watu wote ambao unawajua wana uhitaji na uwezo wa kumudu gharama za biashara hiyo, kisha weka juhudi zako katika kuwashawishi hao na wengine wote achana nao.

Nne; waoneshe watu manufaa watakayopata.

Kwa asili, sisi binadamu ni wabinafsi, huwa tunaweka mbele maslahi yetu kuliko ya wengine. Hivyo njia bora ya kuwashawishi watu kufanya kitu chochote, ni kuwaonesha jinsi ambavyo watanufaika kwa kufanya kitu hicho.

Kwenye biashara nyingi za mtandao, wamekuwa wanaonesha eneo moja tu la fedha, kwamba ukijiunga halafu ukaunganisha watu wawili utapata kiasi hiki, wale wawili nao waileta watu wawili wawili kipato chako kinafika hapa. Hesabu huwa zinaenda hivyo mpaka kufika mamilioni ya fedha, na hapo mtu anahamasika kweli.

Lakini inapokuja kwenye uhalisia, inachukua muda sana mpaka kufikia mamilioni hayo ambayo watu wameahidiwa, mwanzoni mambo huwa magumu, na wengi wanapokutana na ugumu huu wanakata tamaa na kuacha.

Wewe waoneshe watu manufaa, siyo tu ya kifedha, bali ya kutumia bidhaa na hata kushiriki mafunzo mbalimbali yanayohusu biashara hiyo. kadiri unavyowaonesha watu manufaa mengi na wao wenyewe wakaanza kuyaona mapema, ndivyo wanavyoshawishika kujiunga na haya kuendelea na biashara hiyo.

Muhimu sana ni usidanganye na wala usizidishe chumvi, sema ukweli kama ulivyo. Wengi wamekuwa wanazidisha chumvi kwa lengo la kuwahamasisha watu, lakini hilo huwageuka na watu kuwachukulia kama matapeli.

Tano; jenga timu nzuri.

Mafanikio kwenye biashara ya mtandao yapo kwenye timu, na siyo kwenye kuunganisha watu wengi kama ambavyo wengi wamekuwa wanashawishiwa na kufanya.

Haijalishi umeunganisha watu wengi kiasi gani, kama baada ya kujiunga hawanunui tena bidhaa huwezi kunufaika. Unanufaika pale mtu anapojiunga na kila mwezi kuendelea kununua bidhaa, huku naye pia akiunganisha wengine ambao nao wananunua bidhaa.

Hivyo badala ya kuhangaika na watu wengi, chagua wachache ambao wana sifa ulizoweka, kisha washawishi wajiunge na wakishajiunga endelea kuwa nao karibu mkijenga biashara pamoja. Ukiwasaidia nao kuwaunganisha watu wengine zaidi ili nao wanufaike.

Kwa kifupi, unapaswa kuhakikisha kila unayemuunganisha anafanikiwa, maana yeye akifanikiwa, basi na wewe umefanikiwa.

Biashara ya mtandao haihitaji ubinafsi kabisa, ni biashara ya ushirikiano, biashara ya kufanya kazi kama timu, hivyo weka nguvu zako kwenye timu.

Sita; jipe muda.

Kwa kiwango cha chini kabisa, itakuchukua angalau miaka miwili mpaka uweze kuingiza kipato cha uhakika kupitia biashara yako ya mtandao. Achana na yeyote anayekuambia utakuwa tajiri haraka kupitia biashara ya mtandao, huenda hajui ukweli au anakudanganya kwa makusudi.

Inahitaji muda kujenga timu sahihi, inahitaji muda kuielewa biashara na kuwaelewa watu unaowashirikisha, inahitaji muda kuifunza zaidi kuhusu biashara.

Jipe muda, sahau hadithi za mamilioni kwa muda mfupi na pia usiwadanganye watu kwamba watafanikiwa haraka.

Hii ni biashara kama biashara nyingine, mwanzoni unafanya uwekezaji mkubwa, baadaye ndiyo unavuna matunda ya uwekezaji wako. Hivyo kama hujipangi kufanya kwa muda mrefu, ni bora hata usiingie kwenye biashara hii.

Saba; soma kitabu cha IJUE BIASHARA YA MTANDAO.

Nimechambua kwa kina sana kuhusu biashara hii kwenye kitabu nilichoandika kinachoitwa IJUE BIASHARA YA MTANDAO (NETWORK MARKETING).

Kwenye kitabu hiki nimeeleza mfumo wa biashara hii na njia mbalimbali za kulipwa.

Nimeeleza jinsi ya kuzitambua kampuni sahihi na kampuni za kitapeli.

Nimeeleza jinsi ya kuchagua kampuni sahihi kwako ya kujiunga nayo.

Nimeeleza mambo muhimu ya kuzingatia ili ufanikiwe kwenye biashara hii, mengi zaidi ya haya uliyojifunza hapa.

Pia yapo mengine mengi unayopaswa kujua kuhusu biashara hii, yote hayo unayapata kwa shilingi elfu 5 tu (5,000/=) ambayo ndiyo gharama ya kitabu hicho.

Kupata kitabu hicho, ambacho ni softcopy na kinatumwa kwa email, lipa tsh elfu 5 kwenda namba 0717 396 253 au 0755 953 887 kisha tuma email yako na utatumiwa kitabu.

Unaweza kupata mafanikio makubwa kwenye biashara ya mtandao kama utaujua msingi wa biashara hii na njia sahihi za kuifanya. Fanyia kazi haya uliyojifunza hapa na pia soma kitabu cha IJUE BIASHARA YA MTANDAO kujifunza mengi zaidi.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

NETWORK MARKETING