Wazazi wamekuwa ni watu wa kutafuta ukamilifu kwa watoto. Ukamilifu huo wanautafuta utafikiri nao wazazi ni wakamilifu.

Usitafute ukamilifu kwa watoto au mtoto uliyenaye kwa kumlinganisha na mwingine. Mbona huyu hafanyi kama yule, au yule hafanyi kama huyu.

Watoto hawafanani kama yalivyo majina yao. Kila mmoja ana upekee wake, hivyo wewe kama mzazi tambua upekee wa kila mtoto na mwimarishe pale ambako anapapenda.

Usimlazimishe mtoto kupenda unachopenda wewe, Kama kitu kimo ndani yake atakifanya tu na kipo nje yake hatokifanya. Mpe mtoto uhuru wa kuchagua na afanye kile anachopenda, usimchagulie mtoto awe nani mwache aamue mwenyewe ndiyo ataweza kufanya vizuri.
Watu wote wanaofanya vizuri sana kwenye kile wanachofanya ni wale ambao wanafanya kile wanachokipenda.

Tumepewa akili ya kufikiri, lakini uwezo wetu wa kufikiri uko tofauti kwa kila mtu. Wako ambao wanaelewa haraka na wako ambao hawaelewi haraka hivyo hao wote unapaswa kuwapokea kama walivyo. Hakuna mtoto anayependa awe na uelewa wa chini bali naye anapenda awe na uelewa wa hali ya juu. Unapokutana na mtoto ambaye uwezo wake uko chini ni nafasi kwako kumsaidia kisaikolojia na endapo ukimsaidia vizuri hatokusahau kwa msaada wako.

Watoto wako tofauti, kuna wengine wanapenda kusoma sana, kuna wengine wanapenda kazi za mikono hivyo wapokee kadiri ya kile ambacho wanakipenda wao.

Huu siyo muda wa kutafuta ukamilifu kwa mtoto. Mwache mtoto ajaribu vitu vingi kadiri awezavyo na mpe nafasi ya kukosea kwani maisha ndivyo yalivyo kuna muda mwingine atashinda na kushindwa hayo yote ni sehemu ya maisha.

Mfundishe mtoto kukosa, siyo kila anapotaka kile anachotaka unampa. Wewe mzazi utaweza kufanya hivyo lakini dunia haiko hivyo mzoeshe mtoto kuishi maisha yoyote yale ambayo ataweza kukutana nayo katika maisha yake. Maisha ya kupata na kukosa na siyo kila siku ni kupata tu.

Hatua ya kuchukua leo; Wafundishe watoto kukosa, usitafute ukamilifu kwa watoto wadogo kwani bado wako katika hatua ya kujifunza na wasaidie pale wanapohitaji msaada wako kama mzazi lakini wasaidie kwa lugha ya upendo.
Yeyote anayehudumiwa kwa upendo anapokea vizuri ile huduma unayompa na lazima itamsaidia kwenye maisha yake.

Kwahiyo, zawadi pekee ambayo utaweza kumpa mtoto wako ni kumlea vizuri. Mpe mtoto malezi bora ambayo hatoweza kuyapata sehemu nyingine yoyote ile duniani.
Malezi bora yatamwezesha mtoto kuishi maisha yoyote yale.

Ukawe na siku bora sana rafiki yangu.

Makala hii imeandikwa na Mwl. Deogratius Kessy ambaye ni mwalimu, mwandishi na mjasiriamali.

Unaweza kuendelea kujifunza kutoka kwake kupitia vitabu na makala anazoendelea kuandika kupitia mtandao wake wa Kessy Deo http://kessydeo.home.blog

Au unaweza kuwasiliana naye kwa namba zifuatazo //0717101505//0767101505
deokessy.dk@gmail.com
Asante sana na Karibu sana.