Mpendwa rafiki yangu,

Kinachowafanya watu wachoke ndoa zao ni kuvumilia maisha ya ndoa badala ya kuishi na kufurahia ndoa zao. Wako watu ambao wanafikiri labda watakuja kuwa na kipindi cha pili cha maisha ya ndoa kwa sasa wako kipindi cha kwanza ngoja waendelee kuvumilia tu.

Sasa ile hali ya kuvumilia ndiyo inawafanya watu wachoke, wanaisubiria kila siku labda kesho mambo yatakua mazuri lakini hakuna mabadiliko yoyote yale.

Shabaha yetu ya leo ni kutaka kujua kitu pekee ambacho unaweza kumwachia mwenza wako afanye vile anavyotaka.

Najua hapa ni kilio kwa watu ,wengi wako ambao wameingia kwenye ndoa na ndoto zao zikapotea kama mshumaa kwenye upepo.

Wako ambao wanahangaika kuwanyoosha wenza wao lakini wanashindwa, mtu amezaliwa, amejenga tabia yake zaidi ya miaka 30 wewe unataka uiondoe ndani ya mwaka.

Kama tunavyochukua muda kujenga tabia, ndivyo ilivyo hata katika kuvunja tabia. Matokeo ya yale wanayofanya wanandoa kwa sasa ni zile tabia ambazo walijijengea wakati wakiwa wanakua hivyo ili abadilike aendane na tabia unayotaka wewe itachukua muda kidogo.

Lakini tuachane na hayo ya tabia, kitu ambacho nakusihi umwachie mwenzako wako afanye vile anavyotaka ni kwenye ndoto yake.

Kuolewa au kuoa siyo ndiyo mwisho wa ndoto yako. Kila mtu amezaliwa na ndoto na kusudi lake hivyo unatakiwa kuwa nyota ya matumaini kwenye ndoto ya mke au muwe wako.

Tunatofautiana katika ndoto hata katika kusudi la maisha. Wewe kama unajua mwenza wako anataka kua mtu fulani hata usimkataze, bali mshike mkono kwa kuwa sauti ya matumaini kwake, muoneshe njia ili aweze kupita na kisha kufanikiwa.

Kabla hujaolewa au kuoa ulikuwa na ndoto zako nyingi tu, sasa usijifiche na kusema eti ndoa imekuwa kikwazo cha wewe kutokufikia malengo yako.

Tena ukiwa kwenye ndoa ni rahisi sana kupata hamasa ya kufika kule unakotaka kufika huku ukiwa na mtu wako wa karibu mnaosaidiana na kufarijiana pale mambo yanapokuwa ndivyo sivyo.

Wako baadhi ya wanandoa wanaishi kama mtu na kijakazi wake. Una kuta mke au mume hana kauli juu ya mwenzake, yeye ni ndiyo mzee tu, anakuwa anaishi maisha ya utawala wa kiimla ndani ya ndoa.

Tena na hizi likizo za bila malipo, watu wako nyumbani hawana tena pa kwenda huenda mwingine alikuwa akitoka ndiyo anapata faraja lakini sasa akimuona mke au mume wake hana amani.

Hao ni watu waliokiri mbele ya Mungu kuwa watapendana katika hali zote. Lakini sasa wanaishi maisha ya ndoa kama vile kijakazi na mkuu wake.

Kila mtu anao uhuru wa kuishi vile anavyotaka. Usiwe kikwazo kwa mwenza wako kumzuia kutofikia ndoto yake.

Ili mwenza wako afanikishe ndoto yake, hatoweza peke yake bali atahitaji watu lazima atachangamana na watu maana kile ambacho tunakitafuta wala hakipo mbinguni kipo hapa hapa duniani kwa watu.

Sasa wako ambao hawataki wenza wao watoke, wala kuhusiana na watu wengine sasa kwa mtindo huu unafikiri atafanikiwa na wewe hutaki ahusiane na watu? Acha wivu wa kijinga.

Kila mtu akiishi kusudi lake ndani ya ndoa mtaheshimiana sana na kila mtu atakuwa na hamasa kwa sababu mnashirikiana kwenye kusudi.

Mwachie uhuru mwenza wako aweze kupambana, na uzuri ni kwamba mwenza wako akifanikiwa matunda yanakua kwa wote. Mko wa moja kwa lengo la kusaidiana na siyo kuoneshana ubabe nani yuko juu zaidi.

Wengine wanayo nadharia kuwa ni vibaya kupitwa na wenza wao kipato, ndiyo maana wengine hutumia hiyo kama njia ya kujilinda anajua akimwachia uhuru atamzidi. Kama mko kwenye ndoa kumzuia mwenzako asipambane na maisha akusubirie wewe tu huo ni ujinga, vipi kama wewe siku moja haupo duniani?
Muda mzuri wa kujiandaa na vita ni wakati vita havijatokea.

Hatua ya kuchukua leo; Ewe mwanandoa, mwachie uhuru mwenza wako aishi vile anavyotaka apambane kutimiza ndoto yake.
Kua kwenye ndoa siyo ndiyo kuzika ndoto zako, bali pambana kutimiza ndoto yako kwani siku ukifa nani atakulilia? Kama usipofanya mambo makubwa leo ukiwa hai utafanya lini? Amka ishi ndoto yako.

Kwahiyo, wanandoa mume waelewa, muelewe mwe

nzako anataka nini na kuwa nyota ya matumaini kwake kufanikisha ndoto yake.
Kama havunji sheria za ndoa mwache apambane kutimiza ndoto zake.

Ishi maisha ya uaminifu na uadilifu kwenye ndoa yako kiasi kwamba hata wale ambao hawajafunga ndoa wavutiwe na maisha yenu ya ndoa.

Maisha ya ndoa yanahitaji kazi na usadaka. Hakuna maisha ya ndoa bila kujitoa hivyo jitoe sadaka kwa manufaa ya ndoa yako.

Makala hii imeandikwa na
Mwl. Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa
http://kessydeo.home.blog vitabu na kwenye klabu yake ya
MIMI NI MSHINDI. Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.
Rafiki na mwalimu wako,
Mwl, Deogratius kessy
0717101505/0767101504
deokessy.dk@gmail.com //kessydeoblog@gmail.com
Asante sana