Karibu rafiki yangu mpendwa kwenye makala ya ushauri wa changamoto inayokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Changamoto huwa hazikomi kwenye maisha, unapotatua moja unakaribisha nyingine. Hivyo kama ambavyo nimekuwa nakuambia usizikimbie changamoto,  badala yake zitatue na songa mbele.

Kuna wakati unaweza kukutana na changamoto na kuona ni kubwa sana kwako, huku ukijiambia huna namna ya kufanya. Hapa ndipo unapohitaji ushauri wa watu wengine, ambao wanaona changamoto yako kwa namna tofauti na unavyoiona wewe. Hapo ndipo mimi rafiki na kocha wako ninapopata nafasi ya kukushauri kwenye changamoto mbalimbali zinazokukwamisha.

Kwenye makala hii tunakwenda kupata ushauri wa jinsi ya kukabiliana na ushindani wa bei pale unapokuwa unafanya biashara kwa mtaji mdogo. Hii ni changamoto ambayo siyo tu imewakwamisha wengi, bali pia imeua biashara za wengi.

Watu wengi wamekuwa wanaingia kwenye biashara kwa kuanza na mtaji kidogo (kitu ambacho ni kizuri kabisa) lakini wanapojipoteza pale wanapoingia kwenye ushindani na biashara ambazo zina mtaji mkubwa na za muda mrefu. Leo utakwenda kujifunza hatua za kuchukua ili kuweza kuiokoa biashara yako isipotezwe kwenye ushindani wa bei.

Kabla ya kuangalia yale unayopaswa kufanya kwenye changamoto hii, tusome maoni ya rafiki yetu aliyetuandikia kuhusu hili.

Biashara yangu nauza viatu (sendo) za kike, changamoto kubwa kangu ni kuwa na mtaji mdogo na ushindani mkubwa uliopo katika eneo husika la biashara ni ushindani wa bei (kupunguza bei) je nifanyeje kukabiliana na changamoto hizi? – Justine J. M.

Kama alivyotuandikia rafiki yetu Justine, ushindani wa bei umekuwa ndiyo kaburi la biashara nyingi ndogo na mpya. Wengi wanaoingia kwenye biashara hufikiri kupunguza bei ndiyo kuwavutia wateja, lakini kutokana na udogo wa mitaji yao, njia hiyo inawaingiza kwenye hasara kubwa na kupelekea biashara kufa.

ushindani.jpg

Zifuatazo ni hatua za kuchukua ili kukabiliana na ushindani wa bei pale unapofanya biashara kwa mtaji mdogo.

Moja; cheza mchezo wako mwenyewe.

Kama unataka kupata ushindi kwenye eneo lolote la maisha yako, basi unapaswa kucheza mchezo wako mwenyewe. Hii ina maana kwamba unapaswa kutengeneza mchezo wako, kujiwekea sheria zako mwenyewe, kisha kucheza mchezo huo. Ukiingia kucheza mchezo wa wengine, ambao wameutengeneza wao na kuweka sheria zao, huwezi kushinda, maana wao ndiyo wanaoujua mchezo huo kuliko wewe.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye biashara, haijalishi unafanya biashara gani, unapaswa kucheza mchezo wako mwenyewe. Hapa unapaswa kupanga ni aina gani ya biashara unaifanya na utaifanya kwa njia zipi. Tengeneza njia zako mwenyewe, ambazo zinatumia uwezo ulio ndani yako na aina ya wateja unaowalenga, kwa kile unachouza. Jiwekee sheria zako mwenyewe na kisha endesha biashara yako kwa sheria hizo.

Chagua kufanya biashara ya tofauti, ambapo sheria yako kuu kwenye ushindani siyo bei, bali utofauti. Usishindane kwa kupunguza bei, bali shindana kwa kutoa kitu ambacho biashara nyingine hazitoi. Kwa maneno mengine, usikazane kuwa bora zaidi ya wengine, bali kazana kuwa tofauti na wengine.

Hakikisha kuna kitu ambacho wateja wanakipata kwenye biashara yako, ambacho hawawezi kukipata kwenye biashara nyingine yoyote. Inaweza kuwa aina ya bidhaa unazouza, inaweza kuwa aina ya huduma wanayoipata. Ni lazima uwe na kitu ambacho wateja wanakipata kwako tu na hawawezi kukipata kwa wafanyabiashara wengine.

Kama kwenye biashara unayoifanya huwezi kutengeneza kitu cha aina hiyo, ushindani wa bei hauwezi kukuacha salama. Usitegemee utoe kile ambacho kinaweza kupatikana kwa wengine, halafu wateja waje kununua kwako kwa bei juu wakati wanaweza kupata kwingine kwa bei ya chini.

Kumbuka ubinafsi ni asili yetu binadamu, huwa tunaangalia maslahi yetu kwanza kabla ya kitu kingine. Hivyo hakikisha kwenye biashara yako kuna kitu unachowapa wateja wako, kinachowanufaisha na hawawezi kukipata sehemu nyingine. Kwa kuwa na kitu hicho, watakuwa tayari kuja kununua kwako kwa bei ya juu kuliko kwenda kwa wengine wanaouza kwa bei ya chini.

SOMA; Kama Unataka Maisha Mazuri Shindana Na Mtu Huyu Mmoja Tu, Wengine Wote Achana Nao.

Mbili; anza na wateja sahihi.

Kuna wateja ambao wanachoangalia ni bei tu, na wapo wateja ambao wanachoangalia ni thamani wanayoipata. Ni vigumu sana kumshawishi mteja anayeangalia bei rahisi kuona thamani.

Hivyo kabla hujaweka nguvu zako kwenye ushawishi au mengine yoyote, anza na wateja sahihi. Jua kwanza kinachomsukuma mteja kununua ni bei au thamani.

Kama kinachomsukuma mteja kununua ni bei peke yake, usipoteze hata muda wako, kwa sababu atakwenda kule ambapo anapata kwa bei ya chini. Lakini unapokutana na mteja ambaye anaangalia thamani anayoipata, hapo una nafasi ya kumshawishi kulipa zaidi ili apate thamani zaidi.

Wateja wa thamani siyo wengi, lakini wale wachache unaowapata watakufanya ufurahie kuifanya biashara yako, maana huwa ni waelewa na hawakusumbui sana.

Wateja wa bei rahisi huwa ni wengi, lakini pia ni wasumbufu. Unaweza kuwapunguzia bei na bado wakaona umenufaika zaidi na hivyo kutaka zaidi kutoka kwako.

Kwa biashara unayofanya, chagua aina ya wateja unaotaka kwenda nao, kisha tafuta aina hiyo ya wateja. Wanapokuja wateja wanaoangalia bei tu, waeleze thamani unayotoa na kama bado wanasisitiza kwenye bei, unaweza kuwaelekeza wapi pa kupata kwa bei wanayotaka wao, lakini pia waoneshe nini watakosa kwa kuangalia bei pekee.

Tatu; kuwa karibu zaidi na wateja wako.

Biashara ndogo huwa zinazishinda biashara kubwa kwenye eneo hili, uwezo wa kuwa karibu na wateja. Biashara kubwa zinahudumia watu wengi, hivyo huwa hazihangaiki na mteja mmoja mmoja, hivyo mteja hawezi kupata upekee kwenye biashara kubwa.

Ila kwenye biashara ndogo, kwa sababu wateja ni wachache, ni rahisi kumpa kila mteja upekee anaostahili. Ni rahisi kumjua kila mteja na matakwa yake, hivyo wajibu ni kumtimizia mteja yale anayotaka kwa namna yake mwenyewe.

Kosa kubwa ambali wafanyabiashara wengi wadogo huwa wanafanya ni kufanya biashara zao ndogo kama vile ni biashara kubwa, kitu ambacho kinawagharimu sana.

Kuwa karibu zaidi na wateja wako, wasiliana nao mara kwa mara, jua matukio mbalimbali kwenye maisha yao, mfano siku zao za kuzaliwa, watu wao wa karibu na kadhalika. Kisha watumie salamu au jumbe mbalimbali katika siku zao hizo muhimu.

Tumia kila fursa kuwapa wateja wako upekee, uwafanye wajisikie vizuri wanapokuja kwenye biashara yako ambapo wanalipa zaidi kuliko wanavyojisikia wanapokwenda kwenye biashara kubwa ambapo wanalipa kidogo.

SOMA; Anza Kabla Hujawa Tayari; Ushauri Muhimu Kuhusu Biashara Kwa Wale Wanaopanga Kuingia Kwenye Biashara Lakini Wanaahirisha.

Nne; wafuate wateja kule walipo.

Njia nyingine ya kuongeza thamani kwa wateja wako ili wawe tayari kulipa zaidi kwako ni kuwafuata kule walipo. Sasa hivi watu hawana muda, hivyo wanapenda sana pale biashara inapowafuata wao kule walipo. Lakini pia uaminifu umekuwa mdogo, hivyo watu wengi huhofia kuagiza vitu ambavyo hawajaviona.

Wewe kwa kuwa na biashara ndogo, una nafasi ya kujenga uaminifu na wateja wako na kisha kuwafanya waweze kuagiza kile unachouza popote walipo na wakapelekewa. Hii inawafanya wateja wawe tayari kulipa zaidi, kwa sababu imewapunguzia usumbufu na upotevu wa muda kutoka walipo na kwenda kutafuta wanachotaka.

Biashara ndogo inaweza kuwafikia wateja kule walipo kwa ufanisi zaidi kuliko biashara kubwa, hivyo tumia vizuri nafasi hiyo.

Tano; wekeza zaidi kwenye biashara yako.

Unapomtaka mteja alipie zaidi kile anachonunua kwako, ambacho anaweza kukipata kwa bei ya chini sehemu nyingine, lazima utengeneze mazingira ambayo yatamfanya mteja aone anastahili kulipa zaidi. Mfano ukinunua soda ya cocacola kwenye duka la mtaani utalipa shilingi mia tano, lakini soda hiyo hiyo ukiinunua hotelini utalipa shilingi elfu mbili. Ukiwa hotelini hutalalamika kwa nini uuziwe soda ya mia tano kwa shilingi elfu mbili, kwa sababu kuna mazingira yanayokufanya uone kulipa elfu mbili ni halali. Unakuwa umekaa eneo zuri na tulivu, unahudumiwa na watu wanaokujali na kadhalika.

Hivyo pia ndivyo unavyopaswa kufanya kwenye biashara yako, fanya uwekezaji unaoipa biashara yako thamani zaidi kuliko washindani wako. Kuna kitu kidogo sana unaweza kukifanya kwenye eneo lako la biashara na likawafanya watu waipe thamani kubwa. Kitu hicho ni mwonekano wa eneo la biashara, linapaswa kuwa safi na lililopangiliwa vizuri. Mtu akifika kwenye eneo hilo anaona utofauti mkubwa, na ndani yake anakuwa tayari kulipa zaidi.

Wewe mwenyewe ni shahidi, huenda umewahi kufika kwenye eneo la biashara, na kwa jinsi lilivyo na mwonekano mzuri, ukajua utatozwa gharama kubwa, lakini ulipotozwa gharama za kawaida ukashangaa. Hiyo ndiyo hali unayopaswa kuileta kwenye biashara yako pia, kufanya uwekezaji unaowaandaa wateja kuwa tayari kulipa zaidi.

Mwonekano na mpangilio wa eneo la biashara, vifaa unavyotumia na huduma unayowapa wateja wako vinapaswa kuwa vya viwango vya juu sana kiasi cha mteja kuona kama anakuibia pale unapomtajia bei. Na kumbuka hapa utakuwa unawalenga wateja sahihi na siyo wale wanaoangalia bei ya chini pekee.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kulipwa Kwa Kutumia Bidhaa Au Huduma Unayoipenda Na Kuikubali.

Rafiki, hizo ndizo hatua tano za kuchukua ili kuweza kukabiliana na ushindani wa bei pale unapofanya biashara kwa mtaji kidogo. Kama ulivyoona, kuna mengi ya kufanya kuliko kuingia kwenye ushindani wa moja kwa moja kwenye bei, ambao utakuumiza sana.

Nimalizie kwa kukuambia hili rafiki yangu, kama upo kwenye biashara ambayo kitu pekee unachoweza kujitofautisha nacho ni kupunguza bei, basi upo kwenye biashara ambayo siyo sahihi. Kwa sababu kuna wengine wapo tayari kupunguza bei zaidi yako, na wakiwa na mtaji mkubwa kuliko wewe, watapata faida kwa kuuza kwa wengi zaidi kuliko wewe unayeuza kwa wachache.

Hivyo fanyia kazi haya matano uliyojifunza, na mengine yanayoendana na hayo, lakini siyo kupunguza bei. Na kama biashara haina namna nyingine bali bei basi achana nayo na nenda kwenye biashara sahihi, ambapo unaweza kutengeneza mchezo wako mwenyewe na kuucheza vizuri.

Karibu rafiki ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA, programu maalumu ya mafunzo na ukocha ninayoitoa kwa wale ambao wanapenda kupiga hatua zaidi kwenye maisha yao. Kupitia programu hii kila siku unajifunza na kupata hamasa ya kupiga hatua zaidi. Pia kuna mafunzo ya semina mbalimbali kwenye maeneo ha fedha na biashara, ambayo yatakupa maarifa na hatua za kuchukua ili uweze kufanikiwa zaidi. Kupata maelekezo ya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tume ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap kwenda namba 0717396253 na utapewa maelekezo. Karibu twende pamoja kwenye safari hii ya mafanikio.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania