Karibu mwanamafanikio kwenye makala ya leo ya ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa. Changamoto huwa hazikosekani, ukitatua moja inakuja nyingine. Hivyo kama unataka mafanikio makubwa, usitamani changamoto zote zifutike, bali jijengee uwezo wa kukabiliana na kila aina ya changamoto.

Kwenye ushauri wa leo tunakwenda kujifunza jinsi unavyoweza kukuza mtaji wa biashara yako, hasa pale unapoanza na mtaji kidogo.

Mtaji ni moja ya rasilimali zenye uhaba mkubwa kwenye biashara, hivyo kama mfanyabiashara unahitaji kuwa na mkakati sahihi wa kutumia mtaji ulionao lakini pia kuukuza ili biashara iweze kukua.

kuza mtaji.jpg

Kabla hatujaona ni njia zipi unaweza kutumia kukuza mtaji wa biashara yako, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuomba ushauri kwenye hili.

Mie Nashukuru wateja ninao na biashara yangu inanipa faida na kumbukumbu zote za biashara naziandika ndio maana natambua maendeleo ya biashara yangu tokea nilipo anza mpaka sasa ila biashara yangu ni mpya ina miezi mitatu na nusu mpaka sasa.

Lakini changamoto yangu kuwa wateja wanahitaji huduma nyingi sana kwangu na pia ni za muhimu sana kuwepo ofisini kwangu lakini mtaji wangu ni mdogo, nimejaribu kuomba msaada wa watu wanipe kampani ya kifedha lakini sijapata pia niliamua mpaka niuze kiwanja changu ili niongeze huduma ofisini lakini sijafanikiwa mpaka sasa Kupata mteja na bei niliyoiweka sio kubwa ila hali ya uchumi za watu sio mzuri nafikiri, naomba ushauri nifanye nini hili niweze kutoka katika changamoto hiyo maana wateja ninao ila huduma ndio ndogo. – A. O. Bakar

Kama alivyotuandikia mwenzetu, kuna changamoto kubwa mbili hapo;

Changamoto ya kwanza ni jinsi ya kupangilia mtaji kidogo uliopo.

Na changamoto ya pili ni jinsi ya kukuza mtaji huo mdogo.

Zifuatazo ni hatua za kuchukua katika kukabiliana na changamoto hizo.

Moja; pangilia mtaji wako vizuri.

Kwa kuwa mtaji wa biashara yako ni mdogo na mahitaji ya wateja ni wengi, hatua ya kwanza na muhimu kuchukua ni kupangilia mtaji huo vizuri. Anza kwa kuweka vipaumbele sahihi kwenye biashara yako. Jua zile bidhaa au huduma ambazo zina uhitaji mkubwa kwa wateja wako, zinatoka haraka na pia faida yake ni nzuri. Kisha peleka mtaji kwenye bidhaa au huduma hizo.

Usipokuwa na mipango mizuri kwenye mtaji kidogo ulionao, unajikuta umeutumia kununua mali ambazo hazitoki haraka, hivyo ukawa umeukwamisha mtaji kwenye biashara. Unakuwa hauzunguki na hivyo hauzalishi faida.

Unapofanya biashara kwa mtaji kidogo, mtaji huo unapaswa kuwa unazunguka mara zote, maana hiyo ndiyo njia pekee mtaji huo unaweza kukua zaidi.

SOMA; Sababu Tano Kubwa Zinazozuia Biashara Nyingi Kukua Na Jinsi Ya Kuondoka Kwenye Mkwamo Wa Kibiashara.

Mbili; sehemu kubwa ya faida rudisha kwenye biashara.

Kwa kuwa mtaji ni kidogo, hatua ya kwanza kuukuza ni kwa kurudisha faida kwenye biashara hiyo. unapopata faida usitumie yote, badala yake rudisha sehemu kubwa ya faida hiyo kwenye biashara yako.

Kama utaweza, usiitegemee biashara yako kuendesha maisha yako kwenye hatua za awali, yaani miezi 6 mpaka mwaka au miaka miwili. Huu ni wakati ambapo biashara inahitaji kukua zaidi.

Sasa kama wewe utakuwa unaondoa fedha kwenye biashara katika kipindi hicho cha awali, utakuwa kikwazo kwa ukuaji wa biashara hiyo.

Kama biashara unayofanya ndiyo njia pekee kwako kuingiza kipato, basi jiwekee utaratibu kabisa kipato chako kitatoka sehemu ya faida na jua ni asilimia ngapi ya faida hiyo.

Kujilipa kwa asilimia kunakusukuma kuuza zaidi ili upate faida zaidi.

Tatu; jenga uhusiano mzuri na wasambazaji na utumie kupata mali.

Wale wanaokuuzia au kukusambazia bidhaa unazouza kwenye biashara yako, ni watu ambao unaweza kuwatumia vizuri na biashara yako ikapata mali hata kama huna mtaji. Unachohitaji ni kujenga nao mahusiano mazuri, kwa kuwa mwaminifu kiasi cha wao kuwa tayari kukupa mali bila ya kulipia.

Ukishajenga uaminifu huo, wape pendekezo lako, waoneshe kwamba una soko lenye uhitaji mkubwa, lakini unachokosa ni mtaji wa kuchukua mali za kutosha. Hivyo kama wakikupa mali, una uhakika wa kuuza na kuwalipa.

Ukiwa na mahusiano mazuri na wasambazaji wako, na ukaweza kuwaonesha soko ulilonalo, hutakosa ambao watakuwa tayari kufanya kazi na wewe. Na usiseme haiwezekani kabla hujajaribu, lifanyie kazi hilo na utashangaa jinsi litakavyokuwa na msaada.

Nne; jenga uhusiano mzuri na wateja na utumie kupata fedha.

Wateja wako pia ni sehemu nzuri ya kupata fedha unazoweza kutumia kama mtaji wa biashara. Wateja wanakuja kwako wakiwa na mahitaji ambayo wewe huna, kwa sababu mtaji wako hautoshelezi kununua.

Kwa kuwa na mahusiano mazuri na wateja, unaweza kuwashawishi wakulipe kwanza kisha waje kuchukua bidhaa au huduma yao wakati mwingine. Hapo utatumia fedha walizokulipa kwenda kununua bidhaa wanayotaka na kisha kuwaletea.

Unahitaji kujenga mahusiano mazuri na wateja wako, yaliyosimama kwenye uaminifu ili waweze kukubali kukupa fedha zao kabla. Lakini hilo linawezekana, jaribu na utaona matokeo yake.

Namba tatu na namba nne vinahitaji ujenge uaminifu mkubwa na usio na shaka, hivyo hakikisha unaepuka kufanya chochote kitakachotia doa kwenye uaminifu wako.

SOMA; Anza Kabla Hujawa Tayari; Ushauri Muhimu Kuhusu Biashara Kwa Wale Wanaopanga Kuingia Kwenye Biashara Lakini Wanaahirisha.

Tano; tafuta wawekezaji kwenye biashara yako.

Unapowaomba watu wakuchangie fedha za mtaji wa biashara yako wanakuwa wazito kwa sababu hakuna watakachonufaika nacho.

Jua hili, kila mtu ni mbinafsi, anaangalia nini anapata yeye kwanza kabla hajafanya chochote. Kwa kuwaomba mtaji, hakuna wanachokwenda kupata, hivyo hawapati msukumo wa kukupa mtaji unaotaka.

Kama unataka kupata mtaji kwa wengine, badili mfumo. Acha kuwaomba wakuchangie na wakaribishe wawe wawekezaji. Tengeneza mpango mzuri wa biashara yako, ukionesha kiasi cha fedha unachohitaji na jinsi kitakavyotumika pamoja na faida itakayozalishwa. Kisha chagua watu wachache na washirikishe mpango huo.

Ukiwa umepangilia vizuri na kuwaonesha manufaa watakayoyapata kwa kuweka mtaji kwenye biashara yako, utashangaa jinsi wengi watakavyokuwa tayari kuwekeza kwenye biashara yako, kwa kuwa kuna manufaa watakwenda kuyapata.

Ukitumia njia hii ya kutafuta wawekezaji unahitaji kuwa makini katika matumizi ya mtaji unaopata kwa sababu una gharama, wale waliowekeza wanataka kupata faida na siyo hasara.

Sita; mengineyo.

Hapa kuna mambo mengine ya kuzingatia katika kukuza mtaji wa biashara yako;

  1. Epuka kuchukua mkopo kwenye hatua za awali za biashara, hii ni kwa sababu mkopo utakutaka uanze kufanya marejesho wakati bado biashara yako haijasimama vizuri.
  2. Epuka kuweka kila bidhaa ambazo wateja wanaulizia, siyo kila bidhaa inayouliziwa unaweza kuiweka, badala yake fanya tathmini kabla ya kuweka mtaji kidogo kwenye bidhaa yoyote ile.
  3. Kuwa na subira, japo unaweza kuwa na mipango mikubwa ya kufanikiwa kwenye biashara yako, unahitaji subira, mambo huwa hayatokei haraka, jipe muda kuielewa biashara yako kwa mtaji kidogo ulionao kabla hujawa na mtaji mkubwa.

Fanyia kazi haya uliyojifunza ili unapoanza biashara kwa mtaji kidogo uweze kupangilia vizuri mtaji huo na biashara iweze kukua zaidi.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania