Mpendwa rafiki yangu,

Kama mtoto anaenda shule na kupata elimu ya darasani basi kuna elimu ya ziada ambayo mtoto anapaswa kuipata kutoka kwa wazazi wao au walezi wanaowalea.

Zama tunazoishi mtoto hawezi kuwa bora kwa kutegemea elimu ya darasani tu, lazima kama mzazi uanzishe darasa nyumbani la kumfundisha mtoto stadi mbalimbali za maisha.

Kama mzazi au mlezi, mtoto anapotoka shule jioni na wewe tenga muda wako wa kukaa na mtoto au watoto wako, wafundishe kitu cha ziada baada ya kumaliza kukagua yale aliyojifunza ndani ya siku husika.

Hili darasa unalopaswa kulianzisha nyumbani ni la kumfundisha mtoto kitu cha ziada kinachohusu maisha kiujumla. Viko vitu vingi ambavyo unaweza kumfundisha mtoto na akawa bora sana. Kwa mfano, unaweza kumfundisha mtoto wako hata namna anavyotakiwa kuwa na imani sahihi, maana waswahili wanasema wajinga ndiyo waliwao lakini katika zama hizi watu wasiokua na imani thabiti,ndiyo wanaliwa kila siku, mfundishe namna ya kuwa vizuri kiimani ili asije akaliwa na watu feki katika imani.

Ukijitoa kila siku kumfundisha mtoto wako kitu kipya tofauti na cha darasani atakua vizuri sana. Anza kumfundisha kazi na kumwambia ukweli jinsi dunia inavyokwenda na siyo tu kila siku kumfundisha mtoto mambo ya darasani.

Ukiwa na darasa lako nyumbani hakikisha unamfundisha mtoto kile ambacho hafundishwi shule. Mfundishe namna fedha inavyopatikana, nidhamu yake, nk.

Watoto wengi hawako huru ndiyo maana wanashidwa kugundua vipaji vyao, kupitia vipaji mtoto ndiyo anaweza kuonesha uwezo mkubwa alionao ndani yake. Mwache mtoto awe huru kujaribu kile anachopenda kufanya ili agundue kipaji chake na siyo kumkazania tu elimu ya darasani.

Watoto wengine hawafanyi vizuri sana darasani lakini kama akiweza kugundua kipaji chake kitamsaidia kufanya vizuri darasani, kitaamsha uwezo mkubwa alionao ndani yake.

Hatua ya kuchukua leo; Kama wewe ni mzazi au mlezi jitahidi kuanzisha darasa nyumbani la kumfundisha mtoto wako vitu ambavyo hafundishwi shule.
Mpe elimu ya ziada itakayomsaidia kuwa bora hapo baadaye.

Kwahiyo, mtoto apate elimu ya darasani lakini pia elimu ya nje ya darasa, elimu ya maisha ni muhimu sana. Unaweza kumfundisha mtoto wako namna ya kuvua samaki na siyo kumpa samaki kila siku, yaani hapa unaweza kumfundisha mtoto wako namna hata ya kufanya kazi na kuzalisha fedha.
Mwache mtoto awe huru katika kujaribu vitu mbalimbali hii itamsaidia kujua kipaji chake, mzazi msaidie mtoto kugundua kipaji chake kwani kila mtu huwa anazaliwa na kipaji chake, hivyo uwe msaada wa kukikuza na siyo kukikandamiza.

Makala hii imeandikwa na
Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali.

Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa
http://www.mtaalamu.net/kessydeo , vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI. Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,
Mwl, Deogratius kessy
0717101505/0767101504
deokessy.dk@gmail.com //
kessydeo@mtaalamu.net
Asante sana