Maisha ni shule isiyo na ukomo, kila siku tuko darasani mpaka siku tunayoondoka hapa duniani.

Changamoto tunazokutana nazo kwenye maisha ni madarasa kwenye hii shule, ukitatua changamoto moja unakuwa umevuka kwenda darasa jingine. Usipotatua changamoto hiyo utaendelea kurudia darasa hilo.

Hivyo hata siku moja usifikirie utakuwa na maisha ambayo hayana changamoto, ukitatua moja, inakuja nyingine, mambo yataenda hivyo mpaka utakapoondoka hapa duniani.

Ni kwa sababu hii mimi rafiki yako nimekuwa nakuandalia makala hizi za ushauri wa changamoto mbalimbali zinazokuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Lengo ni kukujengea uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali ili zisiwe kikwazo kwako.

elimu fedha 2

Leo tunakwenda kupata ushauri kuhusu kuwakimbia wazazi ambao wanakuwa kikwazo kwako kufikia mafanikio. Hili ni jambo gumu hasa ukizingatia umuhimu wa wazazi, lakini hakuna kinachopaswa kusimama kati yako na mafanikio yako.

Kabla hatujaangalia hatua za kuchukua kwenye hili, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuomba ushauri kwenye hili.

“Changamoto ya kubanwa na wazazi kutofanya mambo yangu kama mimi afu kutopewa uhuru wa kukaa na mke wangu baada ya kuoa yaani nakaa kwa baba na mama.” – Daniel L. M.

Kama alivyotuandikia msomaji mwenzetu, anapitia changamoto ya kushindwa kuishi maisha yake kwa uhuru kwa sababu bado yuko kwa wazazi wake. Hivyo kikubwa ambacho tunakwenda kumshauri hapa ni jinsi ya kuwakimbia wazazi wake bila ya kuharibu mahusiano yao.

Kevin O’Leary, Mwekezaji wa nchini Canada, huwa ana misimamo mikali sana kwenye biashara na uwekezaji, huwa siyo mtu wa kubembeleza, bali hueleza ukweli kama ulivyo.

Kwenye moja ya mahojiano yake, Kevin aliulizwa iwapo atawaachia watoto wake utajiri alionao (ambao unakadiriwa kuwa bola milioni 400, karibu tsh trilioni moja).

Kevin alijibu ameingia makubaliano na watoto wake kwamba atawalipia kila kitu mpaka mwaka wa mwisho wa chuo. Wakishahitimu chuo basi hawatapata tena hata senti kutoka kwake, lazima waende kupambana kuanzisha maisha yao wenyewe na siyo kutegemea utajiri wa baba yao.

Huu ndiyo umekuwa mtazamo wa matajiri wakubwa katika zama hizi, hasa baada ya kuona watoto wa matajiri wa kipindi cha nyuma wakiharibika kwa kubweteka na utajiri wa wazazi wao.

Nimeanza na funzo hili kutoka kwa Kevin kwa sababu naona ndiyo tatizo ambalo msomaji mwenzetu analo. Bila hata kuuliza kwa undani, uwezekano mkubwa ni kwamba msomaji anaishi kwenye familia yenye uwezo na ana utegemezi mkubwa kwa wazazi wake, kitu ambacho wazazi hao wanakitumia kumpangia ni jinsi gani aishi maisha yake.

Ukizingatia msomaji huyu kwamba tayari ana mke, lakini bado anaishi kwa wazazi na hayupo huru, inazidi kuonesha ni jinsi gani amekuwa na utegemezi kwa wazazi hao.

Hivyo ushauri ni huu, ambao nimewahi kuutoa tena huko nyuma, ONDOKA NYUMBANI na leo naongeza kitu kingine, WAKIMBIE WAZAZI WAKO.

SOMA; ONDOKA NYUMBANI

Wazazi wako wanakupenda sana, walikuzaa, wakakulea, wakakusomesha mpaka sasa umekuwa mtu mzima. Ni watu ambao unapaswa kuwaheshimu sana, lakini upo usemi kwamba mtoto kwa wazazi huwa hakui. Hali hiyo ya kutokukua inakuwa kubwa zaidi pale unapokuwa na utegemezi kwa wazazi hata kama umeshakuwa mtu mzima.

Hivyo ondoka nyumbani, wakimbie wazazi wako na nenda kaanzishe maisha yako. Kama huna pa kuanzia nenda kaanzie sifuri kabisa, na jua wazi kwamba mambo yatakwenda kuwa magumu, jua utapitia kipindi kigumu, lakini utajifunza na kuwa imara kuliko ulaini ulioutengeneza kwa kuwa chini ya wazazi wako.

Kuhusu utaondokaje, waeleze wazazi wako wazi kwamba kwa sasa unaona umefika wakati wa wewe kwenda kupambana na maisha mwenyewe. Washukuru kwa kila kitu, na waambie mtaendelea kuwa karibu, lakini hapo nyumbani unaondoka na kwenda kuyaanza maisha yako.

Muhimu kabisa ni kwamba, usiwaombe fedha za kwenda kuanzisha maisha yako, na hata unapoondoka, hata kama kuna siku utalala njaa, lala njaa na usijaribu kurudi kwa wazazi wako kuomba akupe chakula au fedha.

Unapochagua njia hii jua umejitoa kupambana, kukabiliana na kila ugumu wa maisha. Na kitu kimoja ninachoweza kukuhakikishia ni kwamba, pamoja na magumu utakayopitia, hutakufa, badala yake utakuwa imara na kuweza kuyakabili maisha yako.

Iwapo unajiambia huwezi kuondoka bila kuwaomba fedha za kwenda kuanza maisha, au kama utapata shida utarudi kuwaomba fedha basi nikuambie kitu kimoja, hujawa tayari kuondoka nyumbani, hivyo kaa hapo kwa adabu na fuata kila wazazi wako wanakuambia.

Kuondoka nyumbani na kuwakimbia wazazi wako ni kwa wale ambao wameshachoshwa na kupangiwa jinsi ya kuendesha maisha yao na wako tayari kulala njaa siku kadhaa kuliko kula vizuri huku wakipangiwa waendesheje maisha yao.

SOMA; Barua Ya Wazi Kwa Vijana Wanaokwenda Kuanza Maisha Ya Kujitegemea Kwa Mwaka Huu 2016.

Ushauri wangu kwa vijana wote huwa ni huu, kijana yeyote ambaye ameshahitimu masomo yake, hapaswi kukaa nyumbani kwa wazazi wake, hata kama hajapata kazi. Wazazi wako wamepambana mpaka umefikia kuhitimu, sasa ondoka na kapambane na maisha, ukiangalia wazazi wako, utagundua walianza maisha kwa umri mdogo kuliko wao. Hata kama mambo ni mazuri kiasi gani hapo nyumbani, usibweteke.

Kwa wale ambao hawajapata nafasi ya kuendelea na elimu za juu, umri wa miaka 21 ndiyo nimekuwa nautumia kama ukomo wa kuwa chini ya wazazi. Ukishavuka umri huo na husomi, ondoka nyumbani na achana na wazazi, nenda kafanye chochote, pambana kuyajenga maisha yako.

Mambo mawili muhimu ya kuzingatia kwenye ushauri huu;

  1. Wazazi hawatakubaliana na wewe kirahisi utakapoamua kuondoka nyumbani, hivyo ukishafanya maamuzi haya hakikisha unayasimamia kweli, watakupa kila aina ya sababu, watakuamba nyumba ni yako, kwa nini uondoke, na mengine. Lakini usidanganyike na hadithi hizo, ondoka na nenda kayaanze maisha yako. Wanaweza kukasirishwa na hilo, lakini utakapopambana na kujenga maisha yako, watakuja kukuelewa na watakuheshimu sana.
  2. Hili la kuondoka nyumbani na kuachana na wazazi haliwezi kuwa sawa kwa wote. Kuna wale ambao wazazi wao wanawategemea zaidi wao, huwezi kuondoka na kuwaacha wazazi wako katika kipindi ambacho wanakutegemea zaidi wewe. Lakini hata kwenye hali hii, hakikisha hawaingilii maisha yako, una wajibu wa kuwasaidia, lakini pia unapaswa kuyaishi maisha yako. Hivyo unapaswa kuwaeleza wazi ni maisha ya aina hani unayotaka kuyajenga na nini ungependa kutoka kwao.
  3. Kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA kinapaswa kuwa mwongozo wako mkuu kwenye maisha yako mapya. Utakwenda kupitia changamoto nyingi na wajibu wako mkubwa ni kujijengea uhuru wa kifedha, utakapoanza na msingi sahihi, utakusaidia sana. Kwenye kitabu hicho utajifunza jinsi ya kukuza kipato, kupunguza matumizi, kuweka akiba na kuwekeza. Bila ya msingi sahihi kifedha, utajikuta unajutia maamuzi yako ya kuondoka nyumbani na hatimaye kurudi kwa aibu. Kupata nakala ya kitabu hiki piga simu au tuma ujumbe kwenda namba 0752 977 170.

Hakuna mtu yeyote au kitu chochote kinachopaswa kuingia kati yako na maisha uliyochagua, wazazi wanaweza kutumia nguvu yao kukufanya uendelee kuwa chini yao, kitu ambacho kitakuwa kikwazo. Achana nao na nenda yakaanze maisha yako, pambana bila ya kuwategemea na utakapofanikiwa, kila mtu atakuheshimu.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania