Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu kinachoitwa Bird by bird : some instructions on writing and life kilichoandikwa na  Anne Lamott.

Anne Lamott (kuzaliwa Aprili 10, 1954) ni mwandishi wa nchini marekani. Amekuwa mwandishi wa miaka mingi, akindika riwaya na vitabu vya kawaida ambavyo vimeshika chati mbalimbali za mauzo duniani.

Kupitia kitabu hiki cha Bird to Bird, Anne anatupa ushauri muhimu kwenye uandishi na maisha kwa ujumla kutokana na uzoefu mkubwa alioupata kwa miaka mingi ambayo amekuwa anaandika.

bird-by-bird1.jpg

Maisha ya uandishi yana changamoto nyingi, bila ya kuwa na msingi sahihi, wengi wamekuwa wanaanguka na kukata tamaa, hasa wanapokutana na changamoto kama mkwamo, kukosolewa na kukataliwa kwa kazi ambayo mtu ameweka nguvu kubwa kuiandaa.

UTANGULIZI.

Anne anatushirikisha kwa ufupi maisha yake na ukuaji wake mpaka kufikia kuwa mwandishi.

Anatuambia anakumbuka akiwa mtoto alikuwa akimuona baba yake akikaa kwenye meza na kusoma na kuandika siku nzima. Alisoma vitabu na majarida mbalimbali huku akiandika vitabu na makala mbalimbali. Kuna kipindi baba yake alisafiri maeneo mbalimbali katika kazi yake ya uandishi. Hili lilimfanya Anne aone jinsi kazi ya uandishi inavyompa mtu uhuru.

Pamoja na kuandika, baba yake Anne pia alikuwa akifundisha wengine uandishi wa kibunifu. Wanafunzi wake walikuwa wafungwa wa gereza la San Quentin ambapo kitu kikubwa alichofundisha ni jinsi mtu anapaswa kuweka umakini kwenye maisha ya kila siku ili kupata vitu vya kuandika. Katika madarasa yake na kupitia maisha yake, Anne alijifunza yafuatayo kutoka kwa baba yake;

  1. Andika kila siku, hata kama ni kwa kiasi kidogo.
  2. Soma vitabu vyote bora kuwahi kuandikwa.
  3. Soma ushairi.
  4. Kuwa halisi, kuwa jasiri na usiogope kukosea.

Anne anaendelea kutuambia kwamba moja ya vitu vilivyomvutia kwenye uandishi ni umaarufu ambao unampa mtu kuwa na maisha yake. Anasema mwandishi anaweza kuwa maarufu kupitia kazi yake, hata kama hakuna ambaye amewahi kumuona. Tofauti na tasnia nyingine kama siasa au muziki, umaarufu unakutaka uwe mbele ya watu. Lakini kwa mwandishi, unaweza kuwa maarufu bila hata kutoka nyumbani kwako.

Anne anatuambia akiwa mtoto, alikuwa akiandika mashairi wakati baba yake anaandika vitabu. Nyumbani kwao vitabu viliheshimika kuliko kitu kingine chochote na hilo lilimfanya apate nafasi ya kusoma vitabu vingi. Mazingira hayo yalimfanya aone kazi ya uandishi ndiyo kitu bora kwake kufanya, kwa sababu inampa uhuru mkubwa.

Pamoja na uhuru ambao aliona baba yake alikuwa nao, lakini changamoto hazikukoma. Kuna changamoto nyingi alizozishuhudia kwenye maisha ya baba yake, ikiwepo changamoto ya kipato, hakuwa anapata kipato cha kutosheleza kutoka kwenye uandishi. Changamoto nyingine ilikuwa ni ulevi hasa wa madawa ya kulevya, ambapo baba yake na marafiki zake ambao ni waandishi walikuwa wakishiriki pamoja kwenye ulevi huo. Changamoto nyingine aliyoiona hasa kwa marafiki wa baba yake ni kujiua, wengi walikuwa wanapatwa na sonona na kuishia kujiua.

Anne anatuambia maisha yake ya utoto hayakuwa kama ya watoto wengine. Wakati watoto wengine wakicheza na kufurahia maisha, yeye alikuwa akisoma vitabu, kitu ambacho kilimpa msongo ndani yake, akijiuliza anawezaje kuandika kama waandishi aliofurahia kazi zao. Hakuwa na marafiki wengi wala kujihusisha na shughuli nyingine za kijamii, yeye alitumia muda mwingi kusoma.

Anne anaendelea kutusimulia kwamba alipofika chuoni, aliendelea na tabia yake ya kujisomea na alipata marafiki ambao pia walikuwa wasomaji. Kupitia marafiki hao alijifunza kuhusu waandishi wengine na kasi yake ya kusoma ilikuwa kubwa. Lakini pia alijaribu mambo mbalimbali kwa kujiunga na vikundi mbalimbali.

Katika kipindi hicho Anne alikuwa akiandika hadithi fupi fupi lakini bado hazikuwa nzuri. Baba yake aliendelea kumpa ushauri muhimu kwenye uandishi, baadhi ya mambo aliyomsisitiza; “Andika kila siku kama mtu anayejifunza kinanda, jipange vizuri upate muda kila siku, fanya kila siku kama deni la heshima na hakikisha unamaliza kila unachoanza. ”

Anne alikazana kuandika kila siku, na kwa kuwa muda wa mchana alikuwa anabanwa, alihakikisha anatenga angalau saa moja kila usiku kuandika. Kilichomsukuma mwanzoni ilikuwa ni hitaji lake la kuchapishwa kwa kazi zake, kwani aliamini akiandika kitabu ambacho kitakubaliwa kuchapwa, basi atakuwa amefikia mafanikio ya juu kabisa kwenye uandishi.

Msukumo wake wa kuandika kila siku ulimfikisha kwenye nafasi ya riwaya yake ya kwanza kukubaliwa kuchapwa. Wakati anasubiria kitabu kitoke, alipata picha kwamba maisha yake yatabadilika sana baada ya kitabu chake kuchapwa. Aliona jinsi ambavyo kitapokelewa na wengi huku akipata sifa na umaarufu. Pia aliona kitauza sana kiasi kwamba hatakuwa tena na changamoto za kifedha.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; THE WAR OF ART: Jinsi Ya Kushinda Vita Ya Ndani Ya Ubunifu.

Lakini hicho siyo kilichotokea, kitabu kilitoka, kilipokelewa vizuri na baadhi ya watu, alipata maoni mazuri na wakosoaji wachache, alialikwa kwenye shughuli mbalimbali zinazohusu vitabu na kupata mahojiano kwenye vyombo vya habari. Baada ya siku chache hali ilirudi kama awali, mategemeo makubwa aliyokuwa nayo hayakutokea na hata kipato hakikuwa kikubwa kama alivyotegemea.

Anne anasema hii ndiyo changamoto kubwa kwenye uandishi, kabla ya kutoa kitabu unakuwa na mategemeo makubwa, lakini kikishatoka ndiyo unakutana na uhalisia, mategemeo yako makubwa hayatimii. Licha ya kuwa mwandishi mzoefu, bado udhaifu huo hajaweza kuuvuka.

Anne anasema amekuwa anawashauri wale wanaopata msukumo wa kuandika waandike, lakini wasiwe na mategemeo makubwa sana kwamba kazi zao zikishachapwa basi watapata kila wanachotaka. Anasisitiza manufaa ya uandishi hayapo kwenye kazi ya mwandishi kuchapwa, bali kwenye zoezi zima la uandishi. Wakati wa kuandika, mwandishi anajifunza mengi na hayo yanampa nafasi ya kujitabua yeye mwenyewe zaidi.

Anne anatuambia tangu amekuwa mtu mzima, amefanikiwa kuwa anaandika karibu kila siku ya maisha yake. Japo uandishi haujampa mafanikio makubwa kifedha, ni kitu ambacho ataendelea kukifanya, na hata angekuwa anayaanza maisha yake upya, bado angeandika.

Anne amekuwa akiendesha darasa la uandishi ambapo amekuwa akifundisha uandishi wa kibunifu kwa wale wanaojifunza kuandika riwaya na hadithi fupi fupi.

Kupitia darasa hilo, Anne amekuwa anawashirikisha wanafunzi wake kila anachojua kuhusu uandishi, kila ambacho kimemsaidia kufanikiwa kwenye uandishi. Anne amekuwa anawafundisha wanafunzi wake vitu ambavyo havifundishwi pengine. Mfano Disemba siyo mwezi mzuri kwenye uandishi na Jumatatu siyo siku nzuri ya wiki kwenye uandishi. Hivyo anawasisitiza waepuke kuanza mipango mikubwa kwenye siku za Jumatatu na kwa mwezi Disemba.

Anapopata nafasi ya kuhojiwa na  waandishi na kuulizwa kwa nini anaandika, Anne huwa anawanukuu waandishi wawili, John Ashbery ambaye hujibu “Kwa sababu nataka kuandika” na Flannery O’Connor ambaye hujibu “Kwa sababu naweza kuandika vizuri.” Na pia Anne huongeza kwamba huwa anaandika kwa sababu haajiriki, ukiacha uandishi, hakuna kitu kingine ambacho anasukumwa kukifanya, hivyo hana budi bali kuandika.

Anne anashirikisha tukio kwenye sinema inayoitwa Chariots of Fire, ambapo mwanariadha Eric anatembea na mmishonari ambaye anamtaka aachane na maandalizi ya riadha kwenye mashindano ya Olimpiki na arudi kufanya kazi ya umishonari kwenye kanisa lake ambapo anapaswa kwenda China kwa huduma hiyo. Eric anamjibu ataenda China kwa sababu ni kusudi la Mungu kwake, lakini kabla hajaenda China, atajiandaa kwa moyo wake wote kwa mashindano ya Olimpiki kwa sababu Mungu pia alimuumba akiwa na kasi ya kukimbia kuliko wengine.

Anne anashirikisha tukio hili kufikisha ujumbe kwamba kila mmoja wetu ana zawadi ndani yake, kuna kitu ambacho kwake ni rahisi kufanya huku wengine ikiwa ni vigumu. Kwenye uandishi, mtu utajua kama una zawadi ya uandishi kama unapenda kusoma na kushirikisha yale unayojifunza.

Anne huwa anawaeleza wanafunzi wake ukweli kwamba nafasi ya kazi zao kuchapishwa na kuwapa mafanikio makubwa kifedha na kuwa na maisha ya mafanikio ni ndogo sana. Hofu, kukosolewa, kukosa fedha na changamoto za mahusiano ni vitu ambavyo mtu anaweza kuwa na uhakika navyo kwenye safari ya uandishi kuliko uhakika wa mafanikio. Lakini pamoja na yote hayo, bado amekuwa anashauri wanafunzi wake waandike kama wana zawadi ya uandishi ndani yao. Anawataka waandike, lakini wasiwe na mategemeo makubwa kupitia uandishi wao, maana mengi wanayotarajia hawatayafikia, hata baada ya kazi zao kuchapwa.

Anne anatuambia wanafunzi wake wamekuwa hawapendi kusikia ukweli huo kuhusu maisha ya uandishi. Hawapendi kusikia pale anapowaambia kwamba ilimchukua kuchapwa kwa vitabu vinne ndiyo akaacha kuhangaika kupata hela ya kula. Hawapendi kusikia kwamba katika wengi wanaoandika, ni wachache ambao kazi zao zitachapishwa, na hata baada ya kazi kuchapisha, bado mafanikio siyo uhakika.

Lakini pia amekuwa anawaambia kwake na marafiki zake, wakati wa kuandika ndiyo wakati wanaojisikia vizuri, wanaona wakiwa na mchango kwenye maisha ya wengine, na hilo linaridhisha kuliko kile mtu anachopata kutokana na uandishi wake. Anne anasema uandishi wa aina hii ni kama kumkamua ng’ombe, maziwa ni mazuri kwa anayeyatumia, huku ng’ombe akijisikia vizuri kukamiliwa. Mwandishi ana kitu kipo ndani yake, anapokitoa kinawanufaisha wengine na kitendo cha kukitoa kinamfanya aridhike.

Kwenye kitabu hiki, Anne anatushirikisha yale yote aliyojifunza kwenye maisha ya uandishi na kupitia kufundisha wengine uandishi. Anatuambia kitabu hiki ni tofauti na vitabu vingine vya uandishi kwa sababu anashirikisha uzoefu wake binafsi na anachoweka hapa ni kila anachojua kuhusu uandishi.

Karibu kwenye uchambuzi.

Kitabu hiki kina sehemu tano;

Sehemu ya kwanza zoezi zima la kuandika. Hapa Anne anatupa mbinu mbalimbali za kutuwezesha kujenga tabia ya kuandika kila siku. Kwenye sehemu hii anatupa msingi imara wa kujijengea ili kuwa waandishi bora.

Sehemu ya pili inahusu mchango wa maisha ya kawaida kwenye uandishi. Kwenye sehemu hii tunajifunza jinsi tunavyopaswa kuweka umakini kwenye maisha yetu na kutumia kila tulichowahi kupitia na tunachopitia sasa kupata vitu vya kuandika. Kwa kuyaishi maisha na kuwa mkweli, hutakosa vitu vya kuandika.

Sehemu ya tatu inahusu jumuia ya uandishi. Hapa Anne anatushirikisha umuhimu wa kuwa na mtu au kikundi cha watu mnaoelewana ambapo mnasaidiana katika uandishi. Hapa tunajifunza jinsi ya kupata watu sahihi wa kupitia na kuhariri kazi zetu za uandishi.

Sehemu ya nne inahusu kuchapwa kwa kazi ya uandishi na sababu nyingine za uandishi ukiacha tu kuchapwa. Hapa Anne anatushirikisha jinsi ambavyo kuchapwa kwa kazi za uandishi hakutaleta matokeo makubwa kama mtu anavyotegemea, lakini pia atatuonesha jinsi zoezi la kuandika lenyewe lilivyo na manufaa kwa mwandishi. Anatufundisha jinsi ya kuwa halisi na kuacha kuiga waandishi wengine.

Sehemu ya tano ni hitimisho la darasa lake la uandishi, yale ambayo anayajumuisha kwenye siku ya mwisho ya darasa ambapo anawaasa wanafunzi wake kuhusu maisha ya uandishi na jinsi yanavyomsaidia mtu kuwa bora zaidi.

Kutakuwa na chambuzi tatu za kitabu hiki, uchambuzi wa kwanza ni huu wenye utangulizi na sehemu ya kwanza, uchambuzi wa pili utakuwa na sehemu ya pili na ya tatu na uchambuzi wa tatu utakuwa na sehemu ya nne na ya tano ya kitabu.

Karibu ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA ili kupata uchambuzi wa kitabu cha Bird to Bird na ujifunze kuhusu uandishi na misingi mingine ya mafanikio kwenye maisha. Kujiunga na channel hiyo fungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania Kisha bonyeza JOIN CHANNEL.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.