Mwaka 2013 mwandishi Neil Gaiman aliandika utangulizi wa toleo la maadhimisho ya miaka 60 tangu kuandikwa kwa kitabu Fahrenheit 451. Katika utangulizi huo, Neil alielezea jinsi kitabu hicho kilivyo na mafunzo ambayo yanaakisi dunia tunayopitia sasa, licha ya kitabu kuandikwa miaka mingi iliyopita.

Neil anasema kuna wakati waandishi huandika kuhusu dunia isiyokuwepo na sababu za kufanya hivyo ni kuangalia mambo yanayoendelea sasa na kisha kuonya watu kwamba kama mambo yataendelea hivyo, basi kutakuwa na madhara. Hivi ndivyo kitabu Fahrenheit 451 kilivyoandikwa, kama tahadhari kwa jamii kwamba kama hali iliyokuwepo wakati huo ingeendelea, basi jamii ingeangamia kwa kukosa maarifa.

Kitabu hiki kiliandikwa katika kipindi ambacho televisheni ndiyo zilikuwa zinaingia na kupata umaarufu mkubwa, watu walitumia muda mwingi kuangalia televisheni kuliko kusoma vitabu na hiyo ndiyo hatari kubwa ambayo mwandishi aliiona.

Katika kipindi hicho cha uandishi pia kuna mambo mengine yaliyokuwa yanaendelea, hasa kwa nchi ya Marekani. Ilikuwa ni baada ya vita kuu ya pili ya dunia ambapo silaha hatari ya bomu ilitumika, ilikuwa ni kipindi ambacho mabadiliko makubwa ya kijamii yalikuwa yanaendelea, lakini pia kulikuwa na vita baridi inayoendelea kati ya Marekani na Urusi.

Haya yote yalimfanya mwandishi kufikiria kwamba kama mambo yangeendelea kwenda kama yalivyokuwa yanaenda, watu kujiburudisha kwa tv badala ya kusoma, watu kukimbizana na raha za muda mrefu badala ya kujua kusudi lao na uhasama baina ya mataifa kuendelea huku baadhi ya mataifa yakipiga marufuku baadhi ya vitabu, basi jamii nzima ingeangamia.

fahrenheit.jpg

Katika kutafakari yale yaliyokuwa yanaendelea kwenye jamii yake, mwandishi Ray Bradbury alijiuliza swali, vipi kama watu wa kuzima moto watafanya kazi ya kuwasha nyumba moto badala ya kuzima moto? Na iwapo vitabu vyote vilivyopo duniani vitachomwa moto, ni kwa namna gani maarifa yataendelea kupatikana?

Kujibu maswali hayo, Ray aliandika hadithi fupi aliyoiita Mzimamoto (The Fireman), baadaye hadithi hiyo ilihitaji kuendelezwa zaidi kwa sababu dunia aliyokuwa ameitengeneza kwenye hadithi hiyo, ilihitaji mengi zaidi.

Ray alipiga simu kwenye kitengo cha zimamoto cha Los Angeles na kuuliza ni joto kiasi gani linahitajika kuchoma karatasi, alijibiwa ni nyuzi joto za Fahrenheit 451 alichukua jibu hilo kama jina la kitabu na hakutaka kujua kama ni kweli au la.

Kitabu cha Fahrenheit 451 kimesomwa na kupendwa na wengi miaka kwa miaka. Wengi wamekuwa wanasema ni kitabu kuhusu udhibiti wa serikali, wengine kuhusu udhibiti wa fikra huku wengine wakisema ni kitabu kuhusu vitabu.

Kupitia kitabu hiki, Ray anatuonesha thamani kubwa iliyopo kwenye vitabu pamoja na umuhimu wa kujali vile vilivyo muhimu kwetu kuanzia kwenye vitabu mpaka kwa watu.

Kwa Nini Kitabu Hiki Ni Muhimu Kwa Zama Hizi.

Unaweza kusema kitabu hiki ni cha zama ambazo zimepita, lakini hakuna wakati ambapo kitabu hiki ni muhimu kwama sasa;

Mwaka 1953 Ray alionya kwamba TV zinakwenda kuharibu watu, mwaka 2020 mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii ndiyo inayofanya hivyo. Watu kwa sasa hawana kabisa muda wa kusoma vitabu, lakini muda mwingi wanautumia kwenye mitandao ya kijamii, ambapo hawajifunzi lolote.

Mwaka 1953 Ray alihofia watu kutafuta raha za muda mfupi kwenye vitu visivyo na maana kwao, badala ya watu kujitambua na kuishi maisha yao, waliishi kwa kuiga yale yanayofanyika kwenye TV. Haihitaji nguvu kubwa kuona jinsi watu wanavyoishi sasa kwa kuangalia wengine wanaishije kwenye mitandao ya kijamii, kitu ambacho siyo maisha halisi.

Wakati Ray anaandika kitabu mwaka 1953 kulikuwa na mvutano baina ya mataifa makubwa mawili, Marekani na Urusi, mwaka 2020 kuna mvutano baina ya mataifa makubwa mawili, Marekani na China.

Hakuna wakati sahihi kama sasa wa kujifunza kupitia kitabu hiki na kuchagua kuchukua hatua sahihi ili maisha yetu yawe na maana na bora kwetu na kwa wengine pia.

Riwaya Kwa Ufupi.

Hadithi ya riwaya hii ya Fahrenheit 451 inamhusu mzimamoto aitwaye Guy Montag ambaye yeye na wenzake kazi yao ni kuchoma nyumba zenye vitabu. Hadithi inaelezea jamii ya kufikirika na ijayo ambapo kuna teknolojia inayozuia nyumba zisiungue, hivyo watu wa zima moto kazi yao inakuwa kuchoma moto vitabu.

Mwanzoni Guy anaifurahia kazi yake kwa sababu ndiyo amekuwa anaifanya na amekula kiapo cha kutekeleza wajibu wake. Lakini siku moja akiwa anatoka kazini, anakutana na binti aitwaye Clarisse ambaye anaonekana kuwa na furaha muda wote. Anamuuliza Guy iwapo anayafurahia maisha yake na kile anachofanya, na hapo ndipo Guy anapata nafasi ya kuyatafakari na kugundua hayafurahii maisha yake.

Anafika nyumbani na kukuta mke wake, Mildred, amekunywa chupa nzima ya dawa kujiua, anaita watu wa dharura, wanamsaidia na anapona, lakini kesho yake mke wake haonekani hata kujali, anaendelea na maisha yake kama kawaida ambayo ni kuangalia TV siku nzima.

Guy anapata nafasi ya kukutana na Clarisse kila anapotoka kazini na wanajadili mambo mbalimbali kuhusu maisha. Anashangazwa na jinsi binti huyo alivyo na uelewa mkubwa kuhusu maisha, ambaye alikuwa akimweleza jinsi familia yao huwa inakaa jioni kujadili mawazo muhimu badala ya kuangalia TV. Siku moja Guy anamtafuta Clarisse na hamuoni, baadaye anakuja kujua kwamba aligongwa na gari na kufariki dunia.

Wakiwa kazini, taarifa ya nyumba yenye vitabu inawafikia na wanaondoka kwenda kuichoma moto. Kufika wanakuta mwanamke mzee ambaye alikuwa ameficha vitabu vingi ndani kwake. Wanafanya utaratibu wa kawaida ambao ni kumwaga mafuta ya taa kwenye nyumba nzima, lakini kabla hawajachoma, wanamtaka mwanamke huyo atoke. Wanamshawishi kwa kila namna ila anagoma, anachagua kufa na vitabu vyake. Nyumba inawashwa moto na mwanamke yule anaungua na vitabu vyake.

Guy anapata nafasi ya kuficha biblia kutoka kwenye vitabu vya mama yule kabla havijachomwa moto. Siku hiyo hakuweza kulala, alitafakari sana kuhusu kazi wanayofanya na kusudi la maisha yake.

Siku iliyofuata hakutaka kwenda kazini, hivyo alimtaka mke wake amuombee ruhusa. Anamweleza mke wake lengo lake la kuacha kazi ya zima moto, kitu ambacho mke wake anakipinga kwa sababu hawataweza kumudu maisha wanayoishi sasa.

Kiongozi wa kikundi chao cha zima moto, Captain Beatty anafika nyumbani kwa Guy na kumshawishi kwamba kazi wanayoifanya ni kazi yenye maana na mchango mkubwa kwa jamii, kwa sababu inazuia mawazo yaliyopo kwenye kitabu yasiifikie jamii. Anamweleza kwamba watu wanaposoma vitabu wanaanza kufikiria na wakishaanza kufikiria wanakosa furaha. Hivyo kwa wao kuchoma vitabu, wanawapa watu nafasi ya kuwa na furaha kwenye maisha yao.

Baada ya kiongozi wake kuondoka, Guy anampa mke wake siri kwamba amekuwa anaficha vitabu kwenye dari lao na kumshawishi waanze kusoma labda watajifunza kitu kitakachowasaidia kwenye maisha. Guy anatoa vitabu hivyo ambavyo ni vingi na wanaanza kuvisoma, lakini hawaelewi. Hawajui waanzie wapi na wasomeje, mke wake anaamua kurudi kuangalia TV, huku Guy akiwa hajui la kufanya.

Guy anakumbuka amewahi kukutana na profesa mstaafu wa Kiingereza aliyeitwa Faber na alichukua namba yake. Anaitafuta na kuwasiliana naye, akijua huyo ndiye mtu pekee anayeweza kumsaidia kwenye kusoma na kuelewa vitabu. Guy anakutana na Faber ambaye anakubali kumsaidia kwenye usomaji.

Guy anarudi nyumbani na kukuta mke wake yuko na marafiki zake wanaangalia TV, mmoja wa marafiki hao anaeleza kwamba mume wake ameitwa jeshini na kwamba vita imekaribia. Guy anaamua kuwasomea ushairi kwa sauti ili wasikie na kuelewa, mmoja wa wanawake hao anaanza kulia kwa kusikia ushairi uliosomwa. Wanawake hao wanapata hasira na kukubali kwamba ni sahihi kwa vitabu kuchomwa maana vinawanyima watu furaha.

Siku inayofuata, Guy akiwa kazini inakuja taarifa ya nyumba yenye vitabu ya kwenda kuchoma. Wanaondoka na wanafika kwenye nyumba husika, ni nyumba ya Guy, mke wake ametoa taarifa kwamba kuna vitabu na hivyo inabidi ichomwe. Wakiwa hapo, Mildred anaondoka na mabegi yake bila kumsemesha. Captain Beatty anamwamrisha Guy achome nyumba yake, anafanya hivyo na mwisho anamchoma yeye pia na kumuua.

Guy anakimbilia kwa Faber ambaye anampa njia ya kutoroka maana kwa wakati huo anatafutwa kila kona. Anamwelekeza wapi pa kwenda ambapo atakutana na watu wengine ambao nao pia wanatafutwa.

Guy anafuata maelekezo hayo, anakutana na kikundi cha watu ambao wameondoka kwenye jamii hiyo, kiongozi wa kikundi hicho anaitwa Granger. Granger anamjulisha kwamba kwenye kikundi hicho kila mtu amekariri kitabu kimoja kwa matumaini kwamba jamii ya sasa itakapoangamia, basi watatumia kumbukumbu zao kutoa maarifa mapya ya kujenga jamii mpya.

Wakiwa kwenye kikundi hicho ambacho kipo nje ya mji, vita inatokea na mji mzima unaharibiwa kwa mabomu. Baada ya vita kumalizika, Guy na wenzake wanarudi kwenye mji kuanzisha jamii mpya kwa maarifa waliyoyakariri.

Wahusika Wakuu

Guy Montag. Huyu ndiye mhusika mkuu wa hadithi, ni mzimamoto ambaye amekuwa anaficha vitabu kitu ambacho ni kinyume na sheria. Anachagua kwenda kinyume na jamii nzima, kitu ambacho kinamfanya awe mhalifu. Mwisho anakuwa mmoja wa wale wanaoijenga jamii mpya kwa maarifa.

Guy anawakilisha wale wanaopambana kuikomboa jamii kupitia maarifa.

Mildred Montag. Huyu ni mke wa Guy, ambaye maisha yake yote anayatumia kwenye TV, anaangalia tv siku nzima na ndugu zake ni watu wa kwenye tv. Anapinga mpango wa mume wake wa kujifunza kupitia kusoma vitabu na anachagua kuripoti kwenye mamlaka ili nyumba yao ichomwe na hapo anamwacha mume wake.

Mildred anawakilisha jamii nzima, ambayo inaishi maisha ya juu juu na haitaki maarifa.

Clarisse McClellan. Huyu ni binti anayeishi jirani na Guy Montag. Ni binti mdadisi na anayeyaishi maisha yake kwa uhalisia, anakataa kuishi kwa mazoea kama wengine na badala ya kujiburudisha kwa TV kama wengine anakaa na familia yake na kujadili mawazo muhimu. Yeye ndiye anayekuwa chache kwa Guy kushika hatamu ya maisha yake.

Clarisse anawakilisha wale ambao wanakataa kuharibiwa na yale yanayoendelea kwenye jamii na kuchagua kuishi maisha yao kwa uhalisia.

Captain Beatty. Huyu ni bosi wa Guy kwenye kazi ya zimamoto. Beatty ni mmoja wa watu waliosoma sana, lakini anakata tamaa na kuona vitabu haviwezi kuwasaidia watu kutatua matatizo yao. Hili linamfanya aunge mkono mpango wa uchomaji vitabu kwa sababu vinawanyima furaha.

Beatty anawakilisha wasomi ambao pamoja na kupata elimu, hawajapata ukombozi hivyo kukata tamaa na kuona elimu haina maana, bora watu wapewe vitu vingine vya kuwafurahisha. Pia anawakilisha mamlaka ambazo zinazuia watu wasipate maarifa.

Professor Faber. Huyu ni profesa mstaafu wa Kiingereza ambaye ana misimamo yake kuhusu umuhimu wa maarifa, lakini anakosa ujasiri wa kuonesha misimamo yake na kuipigania. Anakuwa tayari kumsaidia Guy katika mapambano yake.

Faber anawakilisha wale ambao wanajua kilicho sahihi, lakini hawapo tayari kukisimamia kwa kutokutaka kuingia kwenye matata. Hawa ni wengi kwenye jamii ambao wanakuwa wamechagua kuyaishi maisha yao badala ya kupambana na kile kisicho sahihi.

Granger. Huyu ni kiongozi wa kikundi cha watu walioondoka kwenye jamii kwa sababu hawakukubaliana na kile kinachoendelea. Granger na kundi lake wamekariri maarifa ili kuyalinda yasiharibiwe na baadaye wayatumie kujenga jamii mpya.

Granger na kundi lake wanawakilisha makundi ya watu kwenye jamii ambayo yanapambana kutunza kile kilicho muhimu kisipotee.

Mwanamke mzee. Huyu ni mmoja wa watu ambao nyumba zao zinachomwa moto kwa sababu ana vitabu, lakini yeye anakataa kutoka kwenye nyumba hiyo na kuchagua kufa na vitabu vyake.

Mwanamke huyu mzee anawakilisha wale ambao wamejitoa kupambania kile kilicho sahihi na kuwa tayari kufa kuliko kusaliti misimamo yao, hata kama hawana nguvu ya kupambana, hawakubali kusaliti utu wao.

Kuhusu Mwandishi.

Ray Douglas Bradbury (kuzaliwa Agosti 22, 1920 – kufariki Juni 5, 2012) alikuwa mwandishi wa nchini Marekani.

Ray alikuwa mmoja wa waandishi mashuhuri wa karne ya 20 na 21 ambaye aliandika kazi nyingi za riwaya za kisayansi (science fiction) na hadithi fupifupi.

Ray anajulikana zaidi kupitia riwaya hii ya Fahrenheit 451 (1953), lakini pia ameandika riwaya nyingine kama The Martian Chronicles (1950), The Illustrated Man (1951), na I Sing the Body Electric! (1969).

Katika kazi zake, Ray alikuwa akionesha madhara ya teknolojia mpya iwapo watu watazipokea bila ya kuhoji na kuchagua yenye manufaa na kuacha yasiyo na manufaa.

Karibu kwenye uchambuzi.

Kitabu hiki cha Fahrenheit 451 kina sehemu tatu,

Sehemu ya kwanza tunaona maisha ya kawaida ya Guy katika kazi yake ya kuchoma vitabu. Ni katika sehemu hii ndiyo anapata nafasi ya kuhoji maisha yake na kugundua hayupo njia sahihi.

Sehemu ya pili ni mabadiliko ambayo Guy anapitia kwenye maisha yake, baada ya kumwona mwanamke mzee anakufa na vitabu vyake na kuona anachofanya siyo sahihi. Anaamua kwenda kinyume na misingi ya kazi yake bila ya kificho.

Sehemu ya tatu tunaona magumu ambayo Guy anayapitia kwa kuchagua kuishi maisha yake, mke wake anamsaliti, nyumba yake inachomwa na anakimbia mji. Mwisho mji unaangamia na yeye na wenzake wanarudi kujenga jamii mpya.

Tutapata uchambuzi wa sehemu tatu za kitabu hiki, pamoja na yale ya tunayojifunza na hatua za kuchukua ili maisha yetu yawe bora.

Karibu sana kwenye uchambuzi huu wa kitabu cha Fahrenheit 451.

Kupata uchambuzi wa kitabu hiki na vitabu vingine vizuri, karibu ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.