Kwenye safari ya mafanikio kimaisha hakuna jeshi la mtu mmoja, hakuna anayeweza kufanya kila kitu peke yake.

Hivyo tunategemeana sana, tunahitaji msaada wa watu wengine wengi ili tuweze kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu.

Lakini changamoto ni kwamba, baadhi ya watu waliokusaidia watakufanya uwe mtumwa kwao. Kwa sababu walikusaidia basi watataka kuendelea kukutumia kwa manufaa yao na hilo linakuwa kikwazo kwa mafanikio yako.

Je unawezaje kuondoka kwenye utumwa wa watu waliokusaidia kipindi ambacho ulikuwa na wakati mgumu? Hilo ndiyo tunakwenda kujifunza kwenye makala hii ya ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufanikiwa.

Msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuomba ushauri kwenye changamoto hii, alikuwa na haya ya kusema;

Nimesomeshwa na binamu zangu baada ya kumaliza masomo wakanikabidhi duka tangu  6 Machi 2017 hadi leo nauza duka bila Malipo. Na hapa nilipo nina mke na mtoto wanaishi peke yao. Nikitaka kuondoka nawekewa vikwazo chungu mzima. Nifanyeje naomba ushauri wako. – ELIJAH A. H.

Changamoto aliyonayo mwenzetu Elijah ni changamoto ambayo kila mtu anaipitia kwa namna moja au nyingine. Hii ni kwa sababu jamii zetu zimejengwa kwenye mfumo wa kusaidiana na katika kipindi unapitia magumu, watu wa karibu hawawezi kukuacha uanguke kabisa.

Hivyo kila mtu atachukua hatua kwa namna anavyoweza ili uondoke kwenye magumu. Wengi tumesomeshwa na wazazi na ndugu ambao wengine hawakuwa na uwezo mkubwa. Lakini walijitoa kuhakikisha tunapiga hatua.

Ni hali ya kawaida kibinadamu kulipa fadhila kwa wale waliokusaidia kupiga hatua, kama ambavyo wao walitoa kwako, unakuwa na deni la wewe kutoa kwao au kwa wengine pia.

Lakini hali hii ya kulipa fadhila haipaswi kukufanya kuwa mtumwa, kwani hapo itakuwa imeondoa kabisa ile maana ya watu hao kukusaidia. Kwani wanakuwa wamekusaidia siyo ufanikiwe, bali wakutumie, kitu ambacho siyo sahihi.

Hivyo kwa mwenzetu Elijah na wengine ambao tunapitia changamoto hii, kuna hatua tunazoweza kuchukua na kuitatua ili isiwe kikwazo kwa mafanikio yetu.

Hapa nakwenda kushirikisha hatua tano za kuchukua ili kuweza kuchukua uhuru wako ulioupoteza kwa wale waliokusaidia.

Hatua ya kwanza; jua kwa hakika nini unataka kwenye maisha yako.

Watu wengi wanaishia kuwa chini ya wale wanaowasaidia kwa sababu wao wenyewe hawajui nini wanachotaka. Ipo kauli kwamba usipokuwa na ndoto, basi wengine watakutumia kufikia ndoto zao. Hivyo ndivyo baadhi ya wale wanaokutumia sasa wanavyokuchukulia, wanaona huna kikubwa unachopambana nacho na uko tayari kuwafanyia kazi.

Kaa chini na utafakari nini hasa unachotaka kufanya kwenye maisha yako, ni kwa namna gani unataka maisha yako yawe, ni uhuru upi unaoutaka kwenye maisha.

Amua kile unachotaka na fanya maamuzi kwamba hayo ndiyo maisha yako na hutakuwa tayari kuishi tofauti na hapo.

Hatua hii ni muhimu kwani kwa hatua zitakazofuata zitategemea msingi wako kwenye kile unachotaka, la sivyo utatetereshwa.

SOMA; Hatua Saba (07) Za Safari Ya Shujaa Na Jinsi Ya Kuzitumia Kupata Chochote Unachotaka Kwenye Maisha.

Hatua ya pili; angalia ni kwa kiasi gani unaweza kurudisha fadhila za waliokusaidia huku ukitimiza ndoto yako.

Baada ya ndoto yako kuwa kipaumbele cha kwanza, sasa angalia wale waliokusaidia kwenye maisha na ona ni jinsi gani unawalipa fadhila. Kwa namna yoyote ile, kulipa fadhila hakupaswi kuwa kikwazo kwa ndoto yako.

Fadhila kubwa na ya kwanza unayowalipa wale waliokusaidia ni kuishi maisha ya ndoto yako, kwani msaada wao utakuwa umefanikiwa. Lakini kama hutaishi maisha ndoto yako, hutakuwa na mafanikio unayotaka, msaada wao hautakuwa na manufaa kwako.

Kwa upande wa mwenzetu Elijah, unaweza kupanga kuendelea kuuza duka hilo kwa mwaka mwingine mmoja, lakini katika kipindi hicho unawasaidia kutengeneza mfanyakazi mwingine atakayeendelea kuuza duka hilo, unamjengea uzoefu ambapo ataweza kuendesha biashara vizuri kama wewe baada ya kuwa umeondoka.

Au anaweza kutengeneza ushirikiano mpya, badala ya kuuza bure na kulipwa tu posho, kuweka mpango wa kulipwa mshahara kila mwezi na kiwango cha kulipwa ili kuweza kufanya vitu vingine kulingana na ndoto yako.

Kwa namna ulivyosaidiwa na kile unachotaka kufanya kwenye maisha, kuna fursa mbalimbali za kuweza kulipa fadhila huku pia ukiishi ndoto zako.

Hatua ya tatu; kaa chini na waliokusaidia na waeleze mpango wako na jinsi utakavyowalipa fadhila.

Baada ya kuwa na ndoto yako na mpango wa kulipa fadhila, ueleze kwa wahusika. Waeleze wazi mpango au ndoto yako ni ipi na jinsi gani utaendelea kushirikiana nao. Usiwaeleze kwamba unalipa fadhila, kuna watu hawatajisikia vizuri kuambiwa hivyo.

Waeleze kwamba umefika wakati kwa wewe kupiga hatua zaidi, washukuru kwa namna wamekusaidia na mmeshirikiana na waeleze mtaendeleaje kushirikiana.

Wafanye wajue wazi kwamba huwaambii kuwaomba ruhusa, bali unawapa taarifa ya nini kinakwenda kufanyika.

SOMA; ONDOKA NYUMBANI

Hatua ya nne; tekeleza kile ulichopanga.

Umeshawapa wahusika taarifa sasa kinachofuata ni utekelezaji. Kama nilivyogusia hapo juu, wakati unawaeleza wahusika, wafanye wajue wazi kwamba huwaombi ruhusa, bali unawapa taarifa. Kwamba hakuna kitakachokuzuia kutekeleza kile ulichopanga.

Katika hatua hii tegemea upinzani mkubwa, kulingana na namna watu walivyokusaidia, watakupa mapingamizi mbalimbali. Lakini wewe simama kwenye kile ulichoamua na kitekeleze.

Kuwa tayari kupokea lawama, laana na maneno mengine mabaya, lakini visikurudishe nyuma, kama unachofanya ni sahihi, baadaye watakuja kufurahia maamuzi uliyochukua.

Wapo pia ambao atakuombea ushindwe ili wakuambie huwezi bila wao, jua hilo na jua utashindwa katika baadhi ya mambo, lakini hushindwi kwa sababu ya maombi yao, au kwa sababu ya laana zao, bali kwa sababu ndivyo safari ya mafanikio ilivyo.

Unakumbuka nimekuambia hatua ya kwanza ni muhimu, ndoto yako ndiyo itakayokusaidia kuvuka nyakati hizo ngumu utakazokutana nazo.

Hatua ya tano; isikilize nafsi yako, ina majibu sahihi.

Katika utekelezaji wa hili, kuna wakati utajikuta njia panda, wale waliokusaidia wakikuweka kwenye mtego wa kushindwa kujua nini ufanye. Hapo ndipo unapopaswa kuisikiliza nafsi yako, maana ina majibu sahihi.

Kama wale waliokusaidia hawataki kukuelewa kabisa, huku nafsi yako ikikuambia uende na mpango wako, nenda na mpango wako, hata kama utaitwa usiye na fadhila, jua unafanya kwa nia sahihi ya kuyaishi maisha yako.

Kama wale waliokusaidia ni taasisi ambayo iliingia gharama kukusomesha, huenda wakataka uwalipe gharama zao, kwa kuwa mliingia mkataba, basi kuwa tayari kulipa gharama hizo.

Kwa vyovyote vile, kuwa tayari kulipa gharama ili kupata uhuru wa maisha yako huku ukijua kwamba uhuru huo hautafanya maisha yawe rahisi, bali utakupa nafasi ya kufanyia kazi yale yenye maana zaidi kwako.

Hupaswi kumruhusu mtu mwingine yeyote achukue uhuru wako, hata kama ni mzazi wako, haijalishi alikufanyia nini, ukishakuwa mtu mzima, unapaswa kuwa huru kuyaendesha maisha yako, huo unapaswa kuwa msimamo wako kabla ya mengine yote. Huku ukitumia kila fursa kulipa fadhila ambazo wengine walifanya kwako.

Ukifanya hili kwa nia njema na kuchukua hatua zilizo sahihi, watu watakuelewa na utafanikiwa kwenye maisha yako. Lakini usisubiri mpaka kila mtu akuelewe ndiyo uchukue hatua, wewe chukua hatua sahihi na watu watakuelewa kwa wakati wao wenyewe.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania