Juma lililopita nilipata nafasi ya kutafakari maisha ya aliyekuwa mwanzilishi wa shirika la kitawa la wafransiscan ndugu Fransisco wa Asizi.

Kama unavyojua kwenye maisha hakuna maisha magumu kama ya kuishi na watu. Kama wale unaokutana nao tu kwenye maeneo ya kazi, biashara n.k kuishi nao ni kazi vipi mtu ambaye sasa anaomba ndugu wa kuishi nao maisha ya kijumuiya?

Pata picha maisha ya ndoa unakutana na mtu ukubwani ambaye tayari ameshakuwa na tabia zake na unaishi naye. Na ni mtu mmoja lakini changamoto za hapa na pale hazikosekani. Vipi yule mtu anayeishi na watu wengi katika maisha ya kijumuiya kwa mfano, maisha ya kitawa? Wanawezaje kuishi maisha ya kijumuiya na kukabiliana na magumu yote ya kitabia?

Ndugu Francisco wa Assisi, baada ya kuanzisha shirika lake la kitawa na watu kuwa wengi alipiga magoti na kumuamba Mungu; na sala yake ilikuwa ya kinyenyekevu sana. “Bwana umenipa ndugu, naomba unipe hekima ya kuishi nao.” Hii ndiyo ilikuwa sala ya ndugu Fransisco wa Asizi.

Kwa kuwa na sisi tunaishi na watu ni vema tukaomba hekima ya kuishi na wale ambao tunaishi nao.

Kwa mfano, kama uko katika maisha ya wito wa ndoa, sala yako iwe hivi, “Bwana umenipa mke/mume naomba unipe hekima ya kuishi naye” Kwa sala hii itakusaidia kupata hekima ya kuishi na mwenza wako. Maana usipokuwa na hekima ya kuishi na mke au mume uliyenaye utayaona maisha ya ndoa ni mateso, badala ya kufurahia wewe utakua unavumilia maisha ya ndoa.

Kama una watoto, kila siku sali sala hii ya kuomba hekima, “Bwana umenipa watoto, naomba unipe hekima ya kuwalea vema”

Kwenye kazi au biashara, omba hekima pia, ” Bwana umenipa kazi, biashara naomba unipe hekima ya kuwahudumia wateja wangu vizuri” ni katika kuwahudumia wateja wetu vizuri ndipo na sisi tunapokea haki yetu.

Eneo la muda, omba hekima pia, Bwana umenipa muda, naomba unipe hekima ya kutumia muda wangu vizuri. Tatizo siyo muda, tatizo ni matumizi mabaya ya muda. Usipoweza kutumia rasilimali muda vizuri, utakua ni masikini wa kila kitu, kwanini uwe masikini wakati unao muda wa kutengeneza utajiri?

Eneo la fedha, shukuru kwa fedha unazopata lakini pia omba hekima ya kutumia fedha ulizonazo vizuri.
Kwenye eneo la fedha kama huna hekima ya kutumia fedha ulizonazo vizuri utapotea haraka kwenye hii dunia.

Kama una kipaji, omba hekima ya kutumia kipaji chako vizuri.
Na utafanikiwa sana pale utakapotumia kipaji chako vizuri.

Hakuna mtu aliyewahi kufanikiwa kama mfalme Suleiman, Yeye aliomba hekima na maarifa ya kumwezesha kutumia vizuri vile ambavyo alikuw navyo. Hata wewe katika maisha yako, uwe mtu wa kujifunza kwa watu waliofanikiwa kwenye maisha.

Utaweza kupata hekima katika maeneo haya matatu;

Moja, kusali, kushukuru na kufanya tahajudi. Hapa unakuwa vizuri kiroho na kujiunganisha na asili na Mungu wako.

Mbili, kusoma vitabu kulingana na eneo unalotaka kuwa bora. Hapa utapata maarifa ya kukuwezesha kuwa bora.

Tatu, kujifunza kwa watu wenye hekima jinsi walivyofanya au wanavyofanya mambo yao. Watu waliyofanya kwenye eneo ambalo wewe hujafanikiwa wana maarifa na hekima ambayo wewe huna hivyo ni muda wako sasa kuchukua hatua.
Hapa tunao watu waliokuwa na hekima sana kama mwanafalsafa Socrates, pale unapokuwa unakwama au njia panda hebu jiulize Socrates alifanyaje ni moja ya ushauri aliowahi kutoa mwanafalsafa Epictetus.

Hatua ya kuchukua leo; chochote kile ulichonacho omba hekima ya kukitumia vizuri kile ulichonacho.
Tumia mfano wa sala hizo hapo juu kuomba hekima ya kutumia vizuri kile ulichonacho au kuishi vizuri na wale watu wa karibu kwako.

Mwisho, ukiishi kwa utii, nidhamu, uadilifu na kujituma bila kwenda kinyume na sheria ya asili utakuwa ni mtu wa hekima sana. Na ukishakuwa na hekima lazima utafanikiwa sana kwenye maisha yako.

Makala hii imeandikwa na
Mwl. Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali.

Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa
http://kessydeo.home.blog ,vitabu nakwenyeklabu yake ya MIMI NI MSHINDI. Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,
Mwl. Deogratius kessy
0717101505//0767101504
deokessy.dk@gmail.com //
Asante sana