Hakuna mtu ambaye anaweza kuandika bango mlangoni kwake na kusema hapa kwangu ni salama hakuna matatizo. Mimi sijawahi kuona nyumba ya namna hiyo je wewe umewahi kuiona?

Kila mtu unayemwona unaweza kusema hana shida lakini ukweli ni kwamba kila mtu huwa ana matatizo yake yanayomsumbua. Hakuna mtu ambaye hana matatizo, kila mtu kuna changamoto anapitia.

Usianze kulalamika kuwa mahusiano yako yamekuwa magumu kwa sababu watu wanaweza wakakucheka kama unalalamika mahusiano yamekuwa yana changamoto je ni mahusiano ya nani ambayo hayana changamoto?

Sisi binadamu ni viumbe ambao tuna asili ya udhaifu. Abraham Lincoln aliyewahi kuwa raisi wa Marekeni aliwahi kusema, kama ukitafuta ubaya kutoka kwa mtu tegemea kuupata. Na kweli, ukitafuta ubaya kwa utaupata kwa sababu kila mtu ana mazuri na mabaya yake.

Kama uko kwenye mahusiano yoyote yale, nakusihi sana jihusishe na watu kwa sababu unajua unanufaika nao kwa kitu fulani na kuwa nao kwa sababu hiyo na kazi ya kuanza kuangalia madhaifu ya mtu siyo kazi yako utajikuta huna mtu.

Mtakatifu mama Theresa aliwahi kusema, kama unawahukumu watu utakosa muda wa kuwapenda. Tafadhali rafiki yangu, usiwahukumu watu maana ukiwahukumu utashindwa kuwapenda tena.

Wapende watu kama walivyo, angalia ile faida unayopata kutoka kwako na nufaika nao. Kuhusu tabia yake na madhaifu yake mwache nazo kwani wewe siyo kiranja wa dunia wa kusema kwamba umekuja duniani kumaliza udhaifu wa watu. Waache watu kama walivyo, nufaika na kile ambacho unakipata kutoka kwao na mabaya yao waachie wewe fuata yale mazuri yaliyokushawishi kuwa nao.

Kwenye mahusiano huwa tunakoseana kwa mengi. Huwa tunajeruhiana kwa mengi. Inafikia mahali tunashindwa kuendelea na mahusiano tuliyokuwa nayo. Lakini ni kitu ambacho hakiwezekani kwa binadamu kuishi bila kuhusiana na watu. Kila binadamu yuko kwenye mahusiano kadiri ya vinasaba.

Kwa kuwa katika mahusiano yetu tunakutana na changamoto nyingi mpaka wakati mwingine zinatupausha na ngozi zetu zinaonekana kusinyaa, leo nimekuandalia mafuta ambayo ukiwa unayatumia kwenye mahusiano yako yatakusaidia na kukufanya uwe una nawiri muda wote na ngozi yako kuonekana nyororo.

Mafuta hayo siyo mafuta mengine zaidi ya msamaha. Msamaha ndiyo mafuta ya mahusiano yetu.

Pale unapojikuta umeuziwa, umeumizwa, umekerwa au sitofahamu yoyote ile kwenye mahusiano yako na wale unaojihusisha nao dawa yake ni msamaha.

Samehe ili mahusiano yaendelee. Unaposamehe unakuwa unasamehe kwa faida yako mwenyewe na siyo wala siyo ya mtu mwingine. Wale ambao wamekukosea huenda hata hawajali wanaendelea na maisha yao ili na wewe usikwame samehe kutoka moyoni usiwe na kinyongo tena juu ya watu.

Ukiwa kwenye mahusiano yoyote yale, kila siku lazima unatakiwa kusamehe kwa sababu wako watu ambao watakufanyia tofauti na vile unavyopenda wewe.

Ukiwa ni mtu wa kukasirika kwenye mahusiano uliyonayo utakuwa ni mtu wa kukasirika kila siku. Jifunze kupotezea, usibaki na maumivu yaendelee kukutafuna wakati unao uwezo wa kusamehe.

Hatua ya kuchukua leo; nenda kawapake mafuta wale wote waliokukosea na wale uliowakosea kwa njia ya msamaha wa kweli.

Msamaha wa kweli ndiyo mafuta ya mahusiano. Usikubali ngozi yako ipauke wakati mafuta ya mahusiano yapo. Ni kitendo cha wewe kuamua kusamehe tu na kuwafutia deni wale wote ambao wamekuudhi na uendelee na maisha yako.

Makala hii imeandikwa na
Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali.

Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa
http://kessydeo.home.blog vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI. Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,
Mwl, Deogratius kessy
0717101505/0767101504
deokessy.dk@gmail.com //
Asante sana