Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu kinachoitwa The Four Agreements: A Practical Guide To Personal Freedom kilichoandikwa na Miguel Ruiz

Hiki ni kitabu kinachotupa mwongozo wa jinsi ya kufikia uhuru binafsi kwenye maisha yetu kwa kufuata misingi minne ambayo mwandishi ametushirikisha. Misingi hiyo minne ni rahisi na ipo ndani ya kila mmoja wetu kufanyia kazi na akaweza kuwa na maisha bora.

Changamoto nyingi tunazokutana nazo kwenye maisha huwa zinaanza na sisi wenyewe, kwa kukosa misingi sahihi ya kufuata. Tunaweza kuona wengine ndiyo wamesababisha na kuwalaumu, lakini kama tukiangalia vizuri, tutagundua matatizo ni yetu wenyewe.

Kwa kujua misingi tunayokwenda kujifunza hapa, tutaweza kuzipunguza changamoto nyingi kwenye maisha yetu, tukawa na maisha tulivu na ambayo ni bora.

Kuhusu mwandishi.

Don Miguel Ruiz (kuzaliwa Agosti 27, 1952) ni mwalimu wa kiroho na mwandishi mashuhuri wa vitabu vya kiroho na maendeleo binafsi. Mafunzo ya Miguel yanatokana na falsafa ya Toltec ambayo asili yake ni nchini Mexico.

Kwa zaidi ya miongo mitatu, Miguel amekuwa akiwafundisha na kuwaongoza watu kufikia uhuru binafsi na maisha ya furaha na upendo kupitia kazi zake.

Kuhusu Toltec

Kitabu cha THE FOUR AGREEMENTS kimeandikwa kutokana na Falsafa ya Toltec. Hii ni falsafa ya kale ya nchini Mexico ambayo ilikuwa ikitumiwa kama mwongozo wa maisha. Kupitia falsafa hii, watu waliweza kupata mwongozo wa kuishi kijamii na kiroho. Lengo kuu la falsafa hii ilikuwa kumwezesha mtu kufikia uwezo wa uungu ulio ndani yake.

Kwa miaka mingi falsafa hii imekuwa ni siri kati ya walimu wanaoifundisha na wanafunzi wanaojifunza. Kutokana na nguvu kubwa ambayo falsafa hii inayo, watu wa nje walioijua waliitumia vibaya na hilo lilipelekea walimu wa falsafa hiyo kuzidi kuificha na kuitoa kwa siri, kwa wale tu ambao wanaweza kuitumia vizuri.

Mwandishi wa kitabu hiki, Miguel Ruiz ni mmoja wa wale waliojifunza falsafa hii ya Toltec na kuweza kuiishi na kunufaika nayo na kupitia kitabu hiki anakwenda kutushirikisha misingi ya falsafa hiyo ambayo tukiifanyia kazi tutakuwa na maisha bora pia.

Maarifa ya falsafa ya Toltec yanayokana na ukweli ambao unatokana na asili na ambao kila jamii na falsafa ya kale zilikuwa zinasimamia kwa namna tofauti. Japokuwa Toltec siyo dini, lakini inaheshimu mafundisho yote ya kiroho ambayo yalikuwa yanatolewa na walimu mbalimbali wa kiroho ambao dini mbalimbali zimeanzishwa kupitia wao.

Falsafa ya Toltec ni mwongozo wa kiroho kwa wale wanaotaka kuwa na maisha huru, yenye furaha na upendo.

UTANGULIZI WA KITABU.

Mafundisho mbalimbali ya kiroho na kidini yamekuwa yanatuambia tumeumbwa kwa mfano wa Mungu. Hili ni funzo kubwa ambalo watu wamekuwa hawalipi uzito unaostahili. Kama umeumbwa kwa mfano wa Mungu, maana yake ndani yako unazo sifa za uungu. Kila unachokiona ni mfano wa Mungu, na hivyo kila kitu ni Mungu.

Hii ni hatua ya kwanza na ya muhimu kwako kufikia uhuru binafsi kwenye maisha yako, kwa kutambua kwamba wewe ni mfano wa Mungu, na hivyo wewe ni Mungu.

Dunia nzima ni kitu kimoja na wote tunaunganishwa pamoja na nguvu inayoendesha ulimwengu ambayo ni mawimbi ya mwanga. Nguvu ya mwanga ndiyo inayotuunganisha pamoja na ndiyo inayotengeneza uhalisia. Kile unachokiona ni mwanga ulioakisiwa kuna kwenye macho yako, kama kusingekuwa na mwanga, usingeweza kuona chochote.

Kwa kutambua hili, unapata uhuru mkubwa kwenye maisha yako na kuondoka kwenye vifungo vya hofu ambavyo wengi wamefungwa. Dini na imani nyingine zimekuwa zinawafanya watu kuishi kwenye hofu badala ya kuwafanya wawe huru. Kwa kuujua ukweli kuhusu wewe na kila kilichopo duniani, inakufanya wewe kuwa huru.

Wengi hawawezi kuelewa hili, kwa sababu haliwezi kueleweshwa wala kufundishwa. Wanaolielewa hili ni wale wanaopitia hali inayowasukuma kuuona ukweli wa maisha na dunia kwa ujumla wake. Na kwa kuwa wengi wamekuwa wanaishi kwa hofu maisha yao yote, ni vigumu sana kuuona ukweli huu.

Ukimuambia mtu kwamba wewe ni Mungu, atakuona ni kichaa, umechanganyikiwa au umeingiwa na pepo mbaya. Lakini huo ndiyo ukweli, kila mtu ni Mungu kwa sababu ana nguvu ya uungu ndani yake. Binadamu na vyote vilivyo duniani ni kitu kimoja, tunaunganishwa na nguvu na tofauti tuliyonayo ni mtetemo wa mawimbi ya nguvu ndani yetu. Wale wenye mtetemo wa juu wa mawimbi ndiyo wanaokuwa huru na kufanya makubwa.

Kinachotufanya tusione uungu wetu na kufikia uhuru na uwezo wa kufanya makubwa ni wingu zito ambalo limetufunika. Wingu hilo linatokana na maisha ambayo tumekuzwa nayo, miiko ambayo tumewekewa na hofu ambazo tumejengewa. Tukiweza kuondoa wingu hilo, tunakuwa huru na kuweza kutumia nguvu kubwa iliyo ndani yetu.

Kwa kujua maazimio manne tunayokwenda kujifunza kwenye kitabu hiki, tutaweza kuondokana na wingu hilo, kuwa huru na kufanya makubwa kwenye maisha yetu.

Karibu kwenye uchambuzi.

Uchambuzi wa kitabu hiki utakuwa na sehemu mbili.

Sehemu ya kwanza itakuwa na utangulizi, ndoto ya dunia na maagano mawili ya mwanzo.

Sehemu ya pili itakuwa na maagano mawili ya mwisho na jinsi ya kutumia falsafa ya Toltec kufikia uhuru wa maisha.

Karibu kwenye uchambuzi tujifunze na kupata mwongozo wa kufikia uhuru binafsi kwenye maisha yetu.

Kupata uchambuzi wa kina wa kitabu hiki pamoja na vitabu vingine vizuri jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.