Karibu rafiki yangu mpendwa kwenye makala yetu ya ushauri wa changamoto mbalimbali zinazotuzuia kufanikiwa. Hapa unaeleza changamoto ambayo ni kikwazo kwako na mimi Kocha wako nakupa ushauri wa hatua sahihi za kuchukua.

Kwenye ushauri wa leo tunakwenda kujifunza maamuzi sahihi ya kuchukua kati ya kuendelea na elimu na kuingia kwenye ujasiriamali.

Msomaji na rafiki yetu Ephraim ametuandikia haya kulingana na changamoto hiyo;

Nina miaka 23 nimehitimu kidato cha 6 sikubahatika kupata mkopo, nyumbani wananitaka niende VETA ila mimi natamani niwe mjasiriamali (nifuge kuku) kipi unanishauri? – Ephraim E.

Rafiki yetu Ephraim pamoja na wengine wanaoweza kuwa na changamoto kama hii, ushauri wangu ni huu; FANYA VYOTE KWA PAMOJA.

Endelea na elimu huku pia ukifanya ujasiriamali.

Nakushauri ufanye yote kwa pamoja kwa sababu hizi;

1. Umri wako bado ni mdogo hivyo una muda na nguvu za kutosha kupambana na yote. Lakini pia kama nilivyoandika kwenye kitabu cha UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA, kila mmoja wetu anatumia asilimia 40 tu ya uwezo na nguvu zake, ina maana tuna zaidi ya asilimia 60 hatutumii. Una akiba ya kutosha ya kufanya vyote kwa pamoja.

2. Elimu ya VETA inakwenda kukupatia ujuzi ambao utautumia maisha yako yote na haikuzuii kufanya ujasiriamali pia. Huenda hata ukatumia elimu hiyo kufanya ujasiriamali wako kwa ubora zaidi. Wanasema ujuzi hauozi, hivyo usiache kuupata. Muhimu chagua kusoma kitu ambacho unakipenda na unaweza kujiajiri katika kukifanyia kazi, usisome kwa lengo la kusubiri upate ajira, utakuwa umepoteza muda na fedha.

3. Aina ya ujasiriamali uliochagua kufanya, yaani kufuga kuku ni kitu ambacho hakihitaji uwepo wako muda wote na pia kinahitaji muda uanze kuvuna. Unapofanya ufugaji unahitaji kupata muda wa asubuhi wa kukagua banda la kuku na kujua maendeleo yao, kuweka chakula na maji na kisha kuendelea na mambo mengine huku ukitenga muda wa mchana na jioni kuwaangalia tena. Huwezi kushinda kwenye banda la kuku siku nzima kwa sababu ni mfugaji. Hivyo una muda mwingi, unataka uutumie kufanya nini? Tumia muda huo kupata ujuzi na maarifa zaidi.

Hatua za kuchukua.

Baada ya kuamua kwamba utafanya vyote kwa pamoja, chukua hatua mara moja.

1. Jua ni aina gani ya kuku utakaoanza kuwafuga, utafugia wapi na utaanza na kiasi gani na lini. Kuwa na mpango kamili na ufanyie kazi.

2. Chagua ni fani gani unayokwenda kusomea VETA, jua fani ambayo utapenda kuifanyia kazi maisha yako yote kisha chagua kuisomea hiyo, pata taarifa zaidi kuhusu fani hiyo na jua wakati gani unaanza.

3. Pata maarifa zaidi kuhusu ufugaji wa kuku, maendeleo binafsi na mafanikio. Soma vitabu na hapa hakikisha unasoma vitabu hivi vitatu; ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA na UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA. Kupata vitabu hivyo wasiliana na 0752 977 170.

4. Jitoe kweli kufikia mafanikio makubwa na usikubali kurudisha nyuma au kuangushwa na chochote.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp