Habari rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye makala ya ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa ambapo leo tunakwenda kushauriana jinsi ya kutengeneza hadhira na kuwafikia wengi kupitia utoaji wa mafunzo.

Nianze kwa kukupongeza kama umechagua kutoa mafunzo ya aina yoyote ile kwa wengine, kwa sababu ni kitu kinachohitaji moyo kweli kweli. Kama hujajitoa kweli, utaishia njiani.

Sisemi hili kukukatisha tamaa, bali kukuonesha uhalisia ulivyo. Nilikuwa nawasiliana na mmoja wa watu ninaowakochi, ambaye aliniambia maamuzi yake ya kuacha mpango wa mafunzo aliokuwa anaendesha. Nilipomuuliza sababu akanijibu anaona watu hawapo makini, anaweka nguvu kubwa lakini watu hawathamini.

Nilimtaka asikate tamaa na kuacha, badala yake aendelee, ila aboreshe namna anavyofanya na achague watu sahihi wa kuwahudumia. Kupitia mpango huu wa ushauri, mwenzetu mwingine naye aliomba ushauri kwenye hili, hivyo naona ni eneo ambalo wengi wanahitaji mwongozo.

Hivyo kwenye makala ya leo nitakwenda kushauri hatua sahihi za kuchukua kulingana na uzoefu nilionao kwenye hili.

Kabla hatutajifunza hatua za kuchukua, tusome aliyotuandikia msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili;

Nina youtube channel ya motivational videos, ina mwaka mmoja na miezi mitatu, na nimefikisha subscribers 132. Changamoto nilikuwa nahitaji ushauri namna ya kupata subscribers zaidi na kuwafikia watu wengi katika kuelimisha Kupitia youtube. – Hosea J. S.

Anachokipitia Hosea ni ambacho kila ambaye amewahi kutoa mafunzo kwa watu amewahi kukipitia. Wengi walikata tamaa walipofika hapo, lakini wachache waliendelea na kuweza kuwasaidia wengi pamoja na wao kujenga jina na kuingiza kipato pia.

Inaweza kuwa unatoa mafunzo kwa njia ya maandishi, sauti au video, lakini yote yana msingi mmoja, changamoto zinazofanana na hivyo hatua za kuchukua zinafanana.

Kitu kimoja ninachopenda kueleza kabla hatujaingia kwenye hatua za kuchukua ni ugumu wa sekta hii ya kutoa mafunzo au biashara ya maarifa. Wakati naanza kuandika miaka karibu 10 iliyopita, watu waliniambia blogu za mafunzo Watanzania hawasomi, wanataka tu blogu za udaku. Ilikuwa inahamasisha kweli kuandika udaku upate wasomaji wengi, lakini nilikataa, nilichagua kile ninachoona nipo tayari kukiandika hata kama silipwi, nikajenga hadhira ndogo na kukua nayo.

Katika zama hizi, hali ni ngumu zaidi, kwani mitandao ya kijamii imewavuruga wengi, wengi wapo kwenye usumbufu na wanataka vitu laini laini vya kusisimua akili, wengi wako bize na instagram na facebook kiasi kwamba hawana muda wa kusoma, kusikiliza au kuangalia mafunzo yako.

Hivyo kama umechagua kweli kuingia kwenye tasnia hii ya biashara ya maarifa, lazima ujue unakabiliana na changamoto kubwa ya kupata umakini wa watu na hivyo uwe na mpango bora wa kuwapata wale walio sahihi kwako.

Baada ya utangulizi huo, sasa tuingie kwenye hatua za kuchukua.

Moja; Chagua unaowalenga.

Hatua ya kwanza kabisa kwenye biashara ya maarifa ni kuchagua watu gani unaowalenga na maarifa unayoandaa na kutoa.

Ndiyo unatoa maarifa ya hamasa, lakini je unataka kuhamasisha watu gani? Unataka kuhamasisha wanafunzi wafaulu? Au wafanyakazi wapige hatua? Au wafanyabiashara wakue zaidi kibiashara.

Kamwe usijidanganye kwamba mafunzo yako yanamlenga kila mtu, kwa kuanza na kila mtu unakuwa huna unayemlenga kabia. Utatoa mafunzo ya wazi ambayo hayamlengi yeyote na hivyo hakuna atakayekuwa anakufuatilia.

Nakumbuka wakati naanza kufanya biashara hii ya mafunzo, nilijifunza kuhusu kutengeneza msomaji unayemlenga, kumpa sifa anazokuwa nazo. Nilifanya zoezi hilo na mpaka sasa sehemu kubwa ya wasomaji wanaonifuatilia wanaingia kwenye sifa zile kwa kiasi kikubwa.

Jua kabisa maarifa yako yanawalenga watu gani, ili unapoyatoa yawe yanaenda kwao moja kwa moja badala ya kuwa ya wazi kwa wote. Cha wote siyo cha yeyote.

Mbili; Jua changamoto zao kubwa.

Ukishachagua watu unaowalenga kwenye maarifa unayotoa, jua changamoto yao kuu.

Kila mtu kwenye maisha kuna changamoto anakabiliana nayo, inayomzuia asipige hatua.

Nilianza utaratibu huu wa kuandika makala za changamoto mwezi May 2014 na niliandaa fomu ya watu kujaza kuhusu changamoto zao. Mpaka sasa nimepokea changamoto 874 (angalia picha).

Japo sijazijibu zote na nyingine zinajirudia, lakini unaweza kuona ni jinsi gani nina uwanja mpaka wa kujua watu wanasumbuka na nini na hivyo kuandaa maarifa ya kuwasaidia kuvuka changamoto zao.

Hivyo lazima uwe na njia ya kujua wale unaowalenga wana changamoto gani. Inaweza kuwa kupitia maoni wanayoyatuma wanaposoma, kuangalia au kusikiliza mafunzo yako, inaweza kuwa yale wanayokutafuta uwasaidie na kadhalika.

mwanzo wa fomu, tarehe ya kwanza kupokea changamoto ni 04/05/2014
fomu mpaka kufikia tarehe 14/01/2021

Tatu; Wape maarifa ya kuvuka changamoto hizo.

Baada ya kujua changamoto kuu za wale unaowalenga, sasa mafunzo yote unayoyaandaa yanapaswa kuwa ya kuwasaidia kuvuka changamoto hizo.

Jua watu hawana muda kabisa, na hawaji kusoma kwa sababu umeandika, bali wanakuja kusoma kwa sababu wana changamoto, wana maumivu ambao hawawezi kuendelea nayo.

Hivyo kama unakuwa na maarifa yenye manufaa kwao, watakuja kuyapata ili waweze kuondokana na changamoto zao.

Kitu kingine kikubwa nilichojifunza wakati naingia kwenye tasnia hii ni kuhakikisha kwa kila mafunzo unayoandaa, kuna hatua ya mtu kuchukua, hata kama ni ndogo, lakini itakayompa matokeo tofauti.

Kuna ambao watafurahia tu kujifunza na kufurahia, hao huwezi kuwategemea sana, lakini wale watakaojifunza na kuchukua hatua kisha wakapata matokeo tofauti, unaweza kuwategemea kuwa wataenda na wewe kwa muda mrefu, watajifunza, watakulipa na wataleta watu wengine.

Hivyo andaa mafunzo yenye hatua za mtu kuchukua ili kuondoka kwenye changamoto zinazomkabili, kadiri anavyopata matokeo mazuri ndivyo atakavyoendelea kuwa na wewe.

Nne; Tengeneza mfumo wa watu kujiunga ili kupata maarifa zaidi.

Usijenge nyumba kwenye kiwanja cha kukodi, naweza kusema hili ni jambo nililojifunza kwenye hii tasnia na ambalo limekuwa na manufaa makubwa mno kwangu.

Iko hivi rafiki, unapotoa mafunzo kupitia mitandao ya kijamii, pale siyo kwako, hivyo chochote unachofanya huko, hakipo kwenye udhibiti wako. Unaweza kuwa na wafuasi wengi kwenye mtandao ya kijamii kama instagram, facebook, youtube na twitter, lakini jua mitandao hiyo ina nguvu ya kukufungia kwa sababu yoyote ile na ukapoteza kila kitu. Kama unafuatilia yanayoendelea duniani unajua raisi wa Marekani anayemaliza muda wake, Dinald Trump amefungiwa kabisa na mitandao mikubwa, pamoja na kuwa na mamilioni ya wafuasi kwenye mitandao hii.

Nilipojifunza dhana hii ya kutokujenga nyumba kwenye kiwanja cha kukodi, niligawa majukwaa kwenye sehemu tatu;

Sehemu ya kwanza ni mitandao ya kijamii, hii niliita ni kijiwe, unaweza kukutana na mtu kijiweni mkaongea mengi, lakini kile kijiwe siyo chako na mtu huyo anaweza asiwe rafiki kwako, mnakutana tu.

Sehemu ya pili ni blogu unayoimiliki mwenyewe, hii niliita nyumbani, mtu unayemkaribisha nyumbani kwako ni rafiki na unamwamini na yeye anakuamini zaidi ya yule mnayekutana naye kijiweni.

Sehemu ya tatu ni mfumo wa email (email list), hii niliita chumbani, mtu unayemruhusu kuingia chumbani kwako ni unayemuamini kweli kweli, na yeye anakuamini kweli kweli na kuwa tayari kufanya yale unamwambia.

Hivyo nikawa nashauri watu hili, kama upo kwenye mitandao ya kijamii, lengo lako siyo kujenga hadhira kule, lengo lako ni kuileta hadhira kwenye blogu yako. Na watu wakishafika kwenye blog, washawishi wajiunge kwenye email list yako.

Mitandao ya kijamii huimiliki, lakini blog ni yako, hata wakitaka kuifungia, bado unaweza kuipakua na usipoteze chochote. Email list ndiyo mali yako zaidi, maana hapo wasomaji wako wanakupa taarifa zao na mawasiliano yao, email na namba za simu. Hata kama jukwaa unalotumia kuendesha mfumo wa email watataka kukufungia, unapakua taarifa za wasomaji wako na kwenda nazo kwenye jukwaa jingine.

Nimekuwa naeleza hili na nimeandika kitabu kinachoitwa JINSI YA KUTENGENEZA PESA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, ambacho nashauri kila anayejihusisha na utoaji wa mafunzo kwa aina yoyote ile akisome.

Pamoja na kushauri hilo kwa kina, bado wengi wamekuwa hawalipi uzito, sasa hivi nimeona watu wanafanya kosa kubwa zaidi, wanaandaa mafunzo na kuyatoa kwa njia ya wasap status, kitu ambacho siyo kibaya, ila mafunzo hayo yanapotea kila baada ya masaa 24, huoni ni kazi bure.

Nirudie msisitizo ambao nimekuwa natoa, kama unajihusisha na utoaji wa maarifa, iwe ni kwa kuandika, sauti au video, hakikisha unakuwa na hatua zote tatu, unatumia mitandao ya kijamii kuwaleta watu kwenye blog kisha kwenye blog unawapeleka kwenye email list yako na huko kwenye email ndiyo mambo mazuri yanaendelea.

Kama bado hujasoma kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA PESA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, kipate na ukisome leo, tuma ujumbe kwenda namba 0717396253 wenye jina la kitabu hicho ili ukipate.

Tano; Waombe wawakaribishe na kuwashirikisha wengine.

Wale ambao watakuwa wanajifunza kwako na kurudi mara kwa mara watakuwa wanakutumia shuhuda na kukushukuru jinsi ambavyo maarifa waliyopata kwako yamewasaidia.

Washukuru kwa hilo na wape ombi moja muhimu, wakusaidie kuwakaribisha wengine ambao nao wanaweza kunufaika kama wao.

Kuna njia mbili za kupata wateja wapya, kwa wewe kuwatafuta au kuwatumia wateja ulionao kuleta wateja zaidi.

Njia ya kutumia wateja ulionao huwa ina nguvu kubwa, kwa sababu mtu anayeambiwa na mtu wake wa karibu na anayemuamini aje kwako kujifunza, atazingatia zaidi kuliko akisikia wewe ukijinadi.

Kwa kila mfuatiliaji uliyenaye, lenga kupata watu wengine angalau kumi na kisha kuwa na njia mbalimbali za kuwashawishi walete wafuatiliaji zaidi. Hiyo ndiyo njia nzuri na ya uhakika ya kukuza hadhira yako.

Kuna njia nyingine za matangazo, unaweza kuzitumia lakini kwa uzoefu wangu huwa hazileti watu ambao ni bora.

Sita; Endelea kutoa kazi bora zaidi.

Kosa moja kubwa la kuepuka kwenye biashara ya maarifa ni ‘kukopi na kupesti’. Kama unachukua maarifa ya watu wengine na kuyafanya kama yako halafu unategemea upate wasomaji wanaokuamini na kuwa tayari kukufuatilia unajidanganya.

Unaweza kuwadanganya watu kwa muda, lakini baadaye watajua na hilo litakuwa anguko lako.

Kwa maarifa yoyote uliyochagua kutoa, toa mapya na halisi kabisa, kwa namna unavyoona wewe ni sahihi. Weka utu na upekee wako kwenye maarifa unayoyatoa kwa kuzingatia kuwasaidia watu kutatua changamoto zao.

Toa maarifa ambayo watu hawawezi kuyapata kwingine kule isipokuwa kwako tu na hicho ndiyo kitawafanya waendelee kuja kwako.

Na usihofie watu kuiba maarifa yako na kuyatumia kama yao, wewe toa kazi halisi, kazi bora na wale wanaokopi wanakutengenezea wateja wa baadaye, kuna siku watajua chanzo na kuja kwenye chanzo.

Saba; Tengeneza mfumo wa kuingiza kipato.

Nimalizie hatua ya mwisho ya kuchukua katika biashara hii ya maarifa, ambayo nimeona wengi wakifanya makosa makubwa hapa.

Wengi huingia kwenye biashara hii kama hobi, wanatoa maarifa kwa sababu ndiyo kitu wanapenda. Lakini kadiri wanavyokwenda wanajenga hadhira kubwa ambayo inataka mtu aipe vitu zaidi na zaidi. Mtu anajikuta akiendelea kutoa, mpaka inafika mahali anakuwa anatumia muda mwingi kuihudumia hadhira kuliko uwezo wake.

Lakini ubaya anakuwa ameizoesha hadhira hiyo kupata huduma bure kutoka kwake. Siku akipata wazo la kuitaka hadhira ilipie, inamuona kama mtu mwenye tamaa na hapo mtu anaogopa kuitaka hadhira imlipe, anaishia kuitumikia bure, kitu kinachokuwa kinamuumiza.

Usifanye kosa hili, wakati unaanza weka kabisa mfumo wa hadhira kukulipa. Yagawe maarifa unayotoa kwenye makundi mawili, kuna kundi la maarifa ambayo unayatoa bure kabisa halafu kuna kundi la maarifa ambayo ili mtu ayapate anapaswa kulipia.

Na watu wajue tangu mwanzo, mtu anapojifunza na kufurahia kisha kukutafuta akitaka zaidi, mwambie ndiyo yapo zaidi, lakini unalipia kiasi fulani kupata zaidi. Hapo unaijenga hadhira yako mapema kulipia ili kupata zaidi.

Kama umeshachelewa, tayari una hadhira kubwa na hukuweka mfumo wa kulipwa, anza sasa. Endelea na mpango wa maarifa ya bure unayotoa lakini anza mpango mwingine wa maarifa ya kulipia na ieleze hadhira yako kwamba kama kuna wanaotaka kujifunza zaidi basi kuna maarifa ya kulipia.

Andika vitabu kulingana na maswali yanayoulizwa sana na mtu anapokuomba ushauri kwenye eneo husika basi mwambie asome kwanza kitabu ulichoandika. Andaa kozi za kufundisha mtandaoni na mtu kulipia kujifunza. Kuwa na blog au kundi ambalo ili mtu aingie lazima alipe. Njia ni nyingi, angalia hadhira yako inataka nini zaidi, kuwa na viwango vya juu vya maarifa hayo na kiasi cha ada ambacho hadhira yako itamudu na weka mpango huo.

Rafiki yangu mpendwa, umejifunza mengi hapa kuhusu uendeshaji wa biashara ya maarifa, nihitimishe kwa kukuambia kitu kimoja, unaweza kuona kama soko la biashara hii limejaa na watu ni wengi, lakini mimi nimekuwa kwenye biashara hii kwa muda nakuambia kitu kimoja, soko halijajaa, fursa bado ni nyingi mno. Wengi wanaofanya biashara hii hawaifanyi kibiashara bali wanafanya kwa hobi. Watu wana changamoto nyingi ambazo wanakosa maarifa sahihi kuzitatua. Ukichagua unaowalenga na kujua changamoto zao kisha kuwaandalia maarifa bora ya kuzitatua huku ukijipa muda wa kujenga hadhira yako, kuna fursa kubwa.

Nikutakie kila la kheri kama tayari upo kwenye tasnia hii na nikukaribishe kama ndani yako una ujumbe ambao unasukumwa kuutoa na uko tayari kuweka kazi. Maana kingine kinachowaangusha wengi ni kufikiri ni njia ya haraka ya kupata fedha. Kwa uzoefu wangu binafsi, ndiyo watu watakuwa tayari kukulipa kiasi kikubwa ili wajifunze, lakini haitakuja haraka, imenichukua zaidi ya miaka mitano mpaka kuweza kuwatoza watu ada za juu kwenye mafunzo mbalimbali. Na hiyo yote ni kwa sababu nimekuwa naisaidia hadhira yangu kupiga hatua na kadiri wanavyopiga hatua wanaweza kumudu gharama zaidi.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp