Karibu rafiki yangu mpendwa kwenye makala hii ya ushauri wa changamoto mbalimbali zinazotuzuia kufanikiwa.
Penye changamoto ndiyo penye ushindi mkubwa kwa sababu wengi huwa wanapakimbia.

Hivyo ukiwa imara na kuweza kuzikabili changamoto mbalimbali na kuzivuka, utaweza kufanya makubwa na kufanikiwa kwenye eneo unalofanyia kazi.

Makala hizi za ushauri zinakupa silaha ya kuweza kukabili kila changamoto na kuishinda ili uweze kupiga hatua kubwa.

Leo tunakwenda kuangalia changamoto ya kutokuijua vizuri biashara unayotaka kufanya, kukosa mtandao mzuri (connection) kwenye biashara hiyo na pia kukosa mtaji wa kuanza.
Kwa kuweza kuyakabili hayo, mtu unaweza kujifunza, ukawajua watu sahihi na ukajua wapi unapoweza kuanzia.

Msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusu changamoto hii alikuwa na haya ya kueleza;
“Dr. Makirita, natamani sana kuanza kufanya biashara ya madini aina ya dhahabu. Changamoto inayonikabili ni mtaji wa uhakika pamoja na wapi pa kuanzia (connection). Naomba msaada, nifanyeje ili nifikie leno langu langu la kufanya biashara hii ambayo ninaipenda sana?” – Alfred M. M.

Kwa maelezo ya msomaji mwenzetu Alfred, kuna changamoto au vikwazo vitatu vinavyomkabili na hapa tutapata ushauri wa jinsi ya kuvivuka vyote.

Changamoto ya kwanza; kuijua biashara.

Alfred anatuambia anatamani sana kufanya biashara ya dhahabu, lakini hajui wapi pa kuanzia.
Kwa maelezo haya tunapata mwanga kwamba mwenzetu anaitamani biashara hiyo kwa yale anayosikia au kuona kwa nje, hajui nini hasa kinachoendelea kwenye biashara hiyo.
Huenda amesikia watu wakitajirika kwenye biashara hiyo na hilo likampa hamasa ya kuingia.

Hakuna ubaya wowote wa kuhamasika kufanya kitu, ila kabla hujaweka rasilimali zako kubwa kwenye kitu husika, ni vyema ukaingia kwanza na ukajionea yaliyo ndani.
Kwa sababu yale unayoona kwa nje mara zote huwa ni tofauti kabisa na kinachoendelea ndani.

Kila biashara ukiiangalia kwa nje utaona ni rahisi kufanya, utaona ina wateja wengi, utaona ina faida kubwa na ya uhakika na utaona haina changamoto kubwa.
Ni mpaka uingie ndani ndiyo utaona jinsi mambo yalivyo tofauti kabisa na ulivyodhani awali.

Hatua ya kuchukua hapa ni kufanya kazi kwenye aina ya biashara unayotaka kuanza. Kwa mwenzetu anayetaka kufanya biashara ya dhahabu ni kwenda kufanya kazi kwenye biashara ya aiba hiyo.
Kama anataka kufanya kwa ngazi ya uchimbaji basi akafanye kazi migodini. Kama kwa ngazi ya uwakala wa kununua na kuuza basi afanye kazi kwa wanaofanya hivyo.

Omba kufanya kazi hata kama ni bure au unalipwa kidogo na ukishapata nafasi hiyo jifunze kwa kina sana kuhusu biashara hiyo. Jua kila kinachoendelea kwenye biashara hiyo, jua jinsi faida inavyopatikana, jua hasara zinakujaje na jua changamoto zote kubwa.

Kwa kuwa ndani ya biashara ya aina hiyo utaona uhalisia ambao hapo awali hukuwa unauona na inaweza kupelekea hata ukabadili mawazo yako baada ya kuona huwezi kukabiliana na yale yanayoendelea kwenye biashara hiyo.

Kwa biashara yoyote unayotaka kufanya na hujui uanzie wapi, anza kwa kutafuta kazi kwenye aina hiyo ya biashara na tumia kazi hiyo kujifunza biashara hiyo kwa kina.

Changamoto ya pili; kuwa na mtandao sahihi.

Kitu kingine ambacho mwenzetu anakosa ni mtandao sahihi (connection) wa kushirikiana nao katika kufanya biashara hiyo.

Kwenye biashara, haijalishi sana unajua nini, bali unamjua nani. Kwa kuwajua watu sahihi unaweza kurahisisha sana baadhi ya mambo unayoyafanya.
Watu ni moja ya nyenzo muhimu ya kufanikiwa kwenye biashara.

Njia bora ya kupata watu sahihi ni kupitia kufanya kazi kwenye biashara husika na kisha kuwasaidia wengine pale wanapokwama.
Angalia ni changamoto ipi kubwa inayowakabili wengine kwenye biashara hiyo, kisha nenda hatua ya ziada katika kuwasaidia kuitatua.

Watu watafurahishwa na uwezo wako wa kuwasaidia kutatua changamoto zao kubwa na watakutegemea kwa kiasi kikubwa.
Pia watakuwa tayari kukupa fursa mbalimbali, zitakazokuwezesha kupiga hatua kubwa.

Watu wengi wanashindwa kujenga mtandao mzuri kwa sababu wamekuwa omba omba sana. Mtu akikutana na aliyepiga hatua zaidi yake, anachokimbilia ni kuomba asaidiwe kitu fulani.
Watu waliofanikiwa wameshachoka kuombwa vitu mbalimbali hivyo na wewe unapoenda kuomba kitu kwao, wanakukwepa kama ukoma.

Wewe kuwa tofauti, usiende kuomba, bali nenda ukatoe. Mwangalie aliyefanikiwa, angalia changamoto kubwa kabisa zinazomkabili na kisha nenda kwake na pendekezo la kumsaidia kutatua.
Wala hata usimuombe kutatua, nenda ukiwa na suluhisho tayari, ni yeye tu kutumia.
Ukiweza kufanya hivyo, utajenga mahusiano mazuri sana na wale waliopiga hatua kubwa.

Katika kujenga mtandao mzuri, usiangalie tu unapata nini, bali angalia unatoa nini. Kadiri unavyotoa vitu vyenye thamani kubwa, ndivyo wengine wanavyokuwa tayari kushirikiana na wewe.

Changamoto ya tatu; mtaji wa kuanza.

Mtaji huwa inatajwa kama kikwazo kwa wengi kuingia kwenye biashara, lakini hakina uzito kana wengi wanavyoeleza.

Ukifanyia kazi changamoto ya kwanza, kwa kufanya kazi kwenye biashara husika, sehemu kubwa ya kile unacholipwa weka akiba ambayo hutaigusa kabisa na hiyo itakuja kuwa mtaji wako.

Ukifanyia kazi changamoto ya pili, kwa kujenga mtandao sahihi kwenye biashara hiyo, utakuwa umejenga mtaji mkubwa mno.
Kwani wale unaowasaidia na wakakuamini sana, watajua kweli umejitoa kutoa thamani kubwa.
Wakiona na juhudi unazoweka pamoja na uelewa mkubwa ulionao kwenye biashara hiyo, watakuona wa tofauti.

Hapo sasa unaweza kuwapa wazo la wao kuongiza faida zaidi kwa kushirikiana na wewe.
Unaweza kuwaonesha fursa ya kukuza zaidi biashara yao kwa kufungua tawi eneo ambalo haipo. Lakini kwa kuwa hawana muda wa ziada, wewe ndiye ufungue tawi hilo na mshirikiane kama wabia.

Kama umeonesha uwezo mkubwa kwenye kufanya kazi zako, kama umekuwa unawasaidia kwenye changamoto zao mbalimbali na kama umekuwa unatoa thamani kubwa, hawawezi kukataa pendekezo lako.

Tatua changamoto hizo tatu kwa jinsi tulivyoshauriana hapa, weka juhudi kubwa na jipe muda na utaweza kupata kile unachotaka.
Muhimu sana ni kuwa tayari kutoa thamani kubwa sana kwa kila nafasi unayopata, ujenge sifa ya mtu mwenye uelewa, juhudi na aliye tayari kwenda hatua ya ziada katika kukamilisha majukumu yake.

Rasilimali muhimu.
Katika kufanyia kazi ushauri huu, kuna rasilimali muhimu sana unapaswa kuwa nazo.
1. Kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA ambacho kitakuwezesha kujua jinsi ya kuanzisha na kukuza biashara yako.
2. Kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA ambacho kitakuwezesha kuweka akiba kama sehemu ya kukusanya mtaji.
Kupata vitabu hivyo viwili wasiliana na 0752 977 170
3. Kitabu cha TABIA ZA KITAJIRI ambacho kitakuwezesha kutoa thamani kubwa zaidi, kipate hapa; www.bit.ly/somavitabuapp
4. Kuwa kwenye kundi la KISIMA CHA MAARIFA, ukiwa kwenye kundi hilo, tutashirikiana kwa karibu katika kulifikia lengo hilo. Kujiunga tuma ujumbe kwa wasap kwenda namba 0717 396 253

Fanyia kazi haya uliyojifunza hapa kwenye makala hii ili uweze kuyaishi maisha yako.
Kama una changamoto inayokuwa kikwazo kwa mafanikio yako, unaweza kupata ushauri kwa kujaza fomu hii; http://bit.ly/ushauri

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.