Rafiki yangu mpendwa,
Kila ninapopata nafasi ya kushauri au kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara, huwa nawauliza kama wanajua dhumuni na malengo ya biashara zao.

Majibu ambayo huwa napata yanaonesha wazi kwamba wengi hawajui tofauti ya dhumuni na lengo la biashara zao.
Wengi hujiona wapo kwenye biashara ili wapate faida.

Ni fikra na mtazamo huo ndiyo vimekuwa kikwazo kwa ukuaji wa biashara zao. Kama biashara inachoangalia ni kuingiza faida pekee, lazima itapoteza wateja kwa kiasi kikubwa sana.

Dhumuni la biashara linapaswa kuwa ni kutengeneza na kutunza wateja. Lakini lengo kubwa la biashara linapaswa kuwa kutengeneza faida. Ni kupitia wateja ndiyo biashara inaweza kuingiza faida.
Hivyo kwa kuanza na wateja, biashara itakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutengeneza faida nzuri.

Biashara nyingi huwa zinashindwa kwa sababu hazina wateja wa kutosha kuziwezesha kujiendesha kwa faida. Kwenye makala ya leo ya ushauri wa changamoto tunakwenda kujifunza jinsi ya kutengeneza na kutunza wateja kwenye biashara na iweze kufanikiwa.

Wasomaji wenzetu waliotuandikia kuomba ushauri kwenye hili walikuwa na haya ya kusema;

“Biashara yangu inapoteza wateja kila siku haikui zaidi ya kumaliza pesa zangu za kubrandy nimefungua Min Juice bar huduma na bidhaa tunazozalisha ni nzuri na bora sana lakini tatizo ni nini?” – Victor V. G.

“Sehemu nilipo weka biashara sio chumba cha njee ni ngum kufikiwa na wateja nifanye nini ili niweze kufikiwa na wateja na kujulikana pande zote” – Laban H.

Changamoto hizo mbili linamlenga mteja, moja kupata mteja na ya pili kumtunza asipotee. Tutayajadili haya mawili kwa kina.

Kupata wateja wa biashara.

Ili kupata wateja kwenye biashara yako, lazima kwanza uchague ni wateja wa aina gani unaowalenga, lazima ujue sifa zao kabisa.
Kwa bidhaa au huduma unayouza, jua ni watu gani unaowalenga na jua sifa zao muhimu.
Jua matatizo au mahitaji waliyonayo ambayo biashara yako inatatua.
Jua uwezo wao wa kuweza kumudu gharama ya unachouza.
Jua wanakopatikana na njia gani ya kuweza kuwafikia.

Ukishazijua sifa za wateja wa biashara yako, usiwasubiri waje kwenye biashara, bali wafuate kule walipo.
Uzuri wa zama hizi siyo lazima biashara yako iwe eneo linaloonekana ndiyo ipate wateja.
Kwa kuwa na mkakati mzuri wa masoko unaweza kuwafikia wateja kule waliko, iwe ni ana kwa ana au kwa mawasiliano.
Usifanye biashara kizamani kusubiri waje, bali toka na watafute wateja.
Tayari umeshajua matatizo au mahitaji yao na tayari una suluhisho linalowafaa, ni wewe kuwafikia na kuhakikisha wanajua uwepo wa biashara yako na kushawishika kuja kwenye biashara yako.

Baada ya kuwashawishi wateja na wakaja kwenye biashara yako, unapaswa kuwashawishi wanunue.
Usiwakubalie kirahisi pale wateja wanapokuambua wameshaona na watakuja siku nyingine kununua, hapo wanakukimbia kirahisi.
Washawishi wanunue kwa kuwahakikishia kwamba hawatapoteza fedha zao wanapofanya maamuzi ya kununua.
Kumbuka wateja wako wametafuta fedha zao kwa maumivu na hawapo tayari kutengana nazo kirahisi. Lazima uwape uhakika kwamba wakitumia fedha zao kwenye biashara yako yatakuwa ni matumizi bora kuliko mengine wanayoweza kufanya kwa fedha hizo.

Mjue mteja, mfikie mteja na kumshawishi kuja kwenye biashara na anapofika mshawishi anunue, hizo ni hatua tatu kubwa za kupata wateja kwenye biashara yako.

Kutunza wateja wa biashara wasipotee.

Kama mteja hajanunua kwenye biashara yako, huyo siyo mteja wako. Hata kama amekuahudi atanunua, kama bado hajanunua, usimhesabie ni mteja.
Mteja akishanunua kwako mara moja, ni rahisi kununua tena kwa mara nyingibe kulimo kwa mteja ambaye hajanunua kabisa.
Mteja ambaye ameshanunua, kuna imani ambayo tayari ameshaijenga kwenye biashara.

Wanapokosea wafanyabiashara wengi ni kuhangaika kukimbizana na wateja wapya huku wakiwasahau kabisa wateja ambao tayari walishanunua.
Hii ni sawa na kuacha dhahabu ya uhakika uliyonayo ndani na kwenda kuhangaika kutafuta dhahabu sehemu ambayo huna uhakika nayo.

Sisemi uache kutafuta wateja wapya, ila ninachosema ni juhudi unazoweka kutafuta wateja wapya, weka juhudi za kiwango hicho hicho kuwatunza wateja ambao tayari wameshanunua.
Kuwatunza wateja ambao wameshanunua kwako, zingatia haya muhimu.

Moja ni kuwapatia huduma bora kabisa kwenye biashara yako. Wape wateja wako huduma bora ambazo hawawezi kuzipata sehemu nyingine yoyote. Hilo litawasukuma kurudi tena kwako kwa sababu wanajua watapata ambacho hawawezi kupata pengine.
Kama hakuna tofauti ya wanachopata kwako na wanachopata kwa wengine, hawatajisumbua kurudi tena kwako.

Mbili ni kuendelea kuwasiliana nao mara kwa mara. Kila mteja ambaye ameshanunua kwako, hakikisha unakuwa na mawasiliano yake. Uzuri kila mtu ana njia mbalimbali za mawasiliano, kuanzia namba za simu, barua pepe na mitandao ya kijamii.
Mteja akishanunua kwako hawezi kuwa mgumu kutoa mawasiliano yake, hivyo muombe akupe mawasiliano hayo na yatumie kuwasiliana naye.
Siyo tu unatumia kumtangazia biashara yako, bali kumjulia hali, kumtumia salamu mbalimbali kulingana na sikukuu au matukio mbalimbali.
Kadiri unavyowasiliana na wateja wako, ndivyo wanavyokufikiria wewe na biashara yako na kuja kwako pale wanapokuwa na uhitaji.

Tatu ni waombe wakuletee wateja zaidi. Kama mteja ameridhika na huduma unazompa, na hilo utalijua kwa shuhuda atakazokupa yeye mwenyewe, muombe awaalike watu wake wa karibu nao waje kupata huduma hizo.
Mteja anapochukua hatua ya kuwaalika wengine, yeye mwenyewe ataendelea kuja maana hawezi kuwaleta watu halafu yeye asije.
Kwa kumshawishi na akakubali kuleta wateja zaidi, anakuwa amechagua kuendelea kuwa mteja wako kwa muda mrefu zaidi.
Na mteja anapokuletea wateja zaidi, hakikisha unawapa huduma bora kabisa ili asipoteze imani yake kwa wale aliowashawishi kuja kwenye biashara yako.

Utoaji wa huduma bora na za kipekee, mawasiliano ya mara kwa mara na wateja kukuletea wateja zaidi ni njia bora za kuwafanya wateja kuendelea kuwa kwenye biashara yako.

Kama mfanyabiashara jua dhumuni na lengo la biashara na weka juhudi kubwa kwenye kutafuta wateja wapya wa biashara yako, na juhudi za aina hiyo pia kwenye kuwatunza wateja ambao tayari wameshanunua.
Kwa namna hiyo biashara itakuwa na wateja wengi na kuweza kuingiza faida nzuri.

Rasilimali muhimu kuwa nazo.
Katika kufanyia kazi haya uliyojifunza, kuna rasilimali muhimu unapaswa kuwa nazo.

  1. Kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA kina sura zinazokusaidia kujenga mfumo wa masoko, mauzo na utoaji wa huduma bora kwa wateja.
  2. Kitabu cha TABIA ZA KITAJIRI kinakupa mwongozo wa kuweza kuwasiliana na wateja wako kila siku.
    Kupata vitabu hivyo wasiliana na 0752 977 170
  3. Kwa kuwa ndani ya KISIMA CHA MAARIFA unapata mafunzo na usimamizi kutoka kwa kocha kukuwezesha kuendesha biashara yako vizuri.
    Kupata nafasi kwenye KISIMA CHA MAARIFA wasiliana na 0717 396 253.

Fanyia kazi haya uliyojifunza kwenye hii makala ili uweze kutengeneza wateja wapya na kuwatunza kwa muda mrefu kwenye biashara yako.
Kama una changamoto inayokuwa kikwazo kwa mafanikio yako, unaweza kupata ushauri kwa kujaza fomu hii; http://bit.ly/ushauri

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.