Rafiki yangu mpendwa,
Miaka elfu 5 iliyopita, binadamu aliyekuwa porini akiwinda au kukusanya chakula, aliposikia kishindo alianza kukimbia mara moja.
Hakusubiri aone kishindo hicho ni cha nini, hatua ya kwanza ilikuwa kukimbia ili kuokoa uhai.

Wakati mwingine kishindo kilikuwa ni cha hatari, kama wanyama wakali. Lakini wakati mwingine kishindo hakikuwa cha hatari, kama tawi la mti uliovunjika.
Lakini binadamu hakutaka kichukua hatari ya kusubiri aone ni nini, cha kwanza ilikuwa ni kuhakikisha anakuwa salama.

Na hivyo ndivyo jamii ya binadamu imeweza kupitia magumu na hatari mbalimbali, lakini mpaka sasa jamii hii ipo.
Ni kwa sababu ndani yetu binadamu tuna mfumo wa kutusukuma kuchukua hatua za tahadhari pale tunapoona kuna hatari, hata kama hatujui hatari hiyo ni nini.

Na katika kuchukua hatua hizo, mwili hupata nguvu za ziada ambazo mtu anaweza kuzitumia kufanya makubwa kuliko alivyozoea.
Kama umewahi kufukuzwa na mbwa au mnyama mwingine mkali, huenda uliweza kuruka ukuta au kupanda mti, kitu ambacho ukiambiea urudie tena huwezi.

Uliweza kufanya hivyo kwa sababu mwili wako ulitengeneza msongo mkubwa, ukazikusanya nguvu zote za mwili kwa ajili ya kupambana au kukimbia. Ni uwezo huu wa kujenga msongo ndiyo umeiwezesha jamii ya binadamu kuvuka magumu mengi na kuwepo mpaka sasa.

Lakini pia uwezo huo umekuwa kikwazo kwa wengi kuwa na maisha bora.
Kwanza kabisa, hatupo kwenye zile hatari za zamani ambapo tunazungukwa na wanyama wakali au hatari za aina hiyo.
Lakini hali yetu ya mwili kutengeneza msongo haijaondoka.
Hivyo tumekuwa tunatumia hali hiyo ya mwili kutengeneza msongo kwenye mambo mengine.

Kwa mfano unapaswa kuongea mbele ya watu, mwili wako unatengeneza msongo kama vile uko kwenye hatari kubwa.
Au umechelewa kazini, au bosi wako amekuambia nina kikao na wewe.
Au umemsalimia mtu na hakuitika.
Mambo hayo yote ni ya kawaida kabisa, lakini mwili wako utajenga msongo kama vile uko kwenye hatari kubwa.

Na msongo huo huwa hauji bila madhara. Unapokuwa kwenye msongo huwezi kufikiri vizuri, mwili unakusukuma kupambana au kukimbia.
Unapokuwa kwenye msongo nguvu zote za mwili zinaenda kwenye kupambana au kukimbia, hivyo majukumu mengine muhimu ya mwili hayapati nguvu, moja wapo ni mfumo wa kinga.

Watu wanaokuwa na msongo muda mwingi huwa hawana kinga nzuri ya mwili, wanapata maradhi mara kwa mara na matatizo ya akili pia.

Japo tunaishi kwenye mazingira salama mno ukilinganisha na watangulizi wetu, bado miili yetu inaishi kama enzi hizo.
Ukienda na mwili jinsi ulivyo, hutaweza kufanya makubwa kwenye maisha yako, kwa sababu kila wakati utakuwa kwenye msongo ambao utakuathiri sana.

Hapa kuna zoezi la upumuaji unaloweza kufanya na likaluondoa kwenye msongo wowote unaoweza kuwa nao.
Kwa kufanya zoezi hili, unautuliza mwili, unatudisha nguvu ya maamuzi kwenye fikra zako na kuacha kupoteza nguvu kwa hatari zisizo na msingi.

Kwa nini zoezi la kupumua?
Zoezi la kupumua lina nguvu ya kukupa utulivu mkubwa kwa sababu unapokuwa kwenye msongo upumuaji wako hubadilika sana.
Huwa unapumua kwa haraka na juu juu, hivyo mwili ukiona unapumua hivyo, unazidi kutengeneza msongo.

Lakini pia unapopumua kwa haraka, hupati hewa ya kutosha ya oksijeni ambayo inatumika kuunguza chakula ili upate nguvu.
Unapopumua kwa kina, unasaidia mwili kupata hewa ya kutosha ya oksijeni, kuweza kuunguza vizuri chakula na kupata nguvu za kutosha, hasa kwenye ubongo ambao unahitaji nguvu nyingi kufanya maamuzi.

Njia ya kwanza; 5 × 5 × 5.
Njia ya kwanza ya kufanya zoezi la pumzi ni ya tano mara tano mara tano.
Kufanya zoezi hili toa hewa yote kwenye mapafu yako.
Kisha vuta pumzi kwa kuhesabu mpaka tano.
Shikilia pumzi kwa kuhesabu tena mpaka tano.
Kisha toa pumzi kwa kuhesabu mpaka tano.
Rudia zoezi hilo mara nne na utaona mabadiliko makubwa kwako.
Msongo uliokuwa nao utaondoka, utapata utulivu mkubwa na utaweza kufikiri vizuri.

Zoezi hili unaweza kulifanya ukiwa popote, pale tu unapojisikia msongo ndani yako, fanya zoezi hili. Pale unapotaka kufanya maamuzi muhimu lakini unakuwa na hofu, fanya zoezi hilo.

Njia ya pili; 4-7-8
Njia ya pili ya kufanya zoezi la upumuaji ni 4-7-8.
Vuta pumzi kwa kuhesabu mpaka nne,
Shikilia pumzi kwa kuhesabu mpaka saba.
Kisha toa pumzi kwa kuhesabu mpaka nane.
Rudia zoezi hilo kwa jumla ya mara nne kwa wakati mmoja.
Zoezi hili linakupa utulivu mkubwa wa kiakili, linakuwezesha kufikiri kwa kina, kufanya maamuzi sahihi na kuchukua hatua sahihi.

Njia ya tatu; Pumzi na matembezi.
Njia ya tatu ya kufanya zoezi la pumzi ni kufanya pamoja na matembezi.
Wakati mwingine msongo unakuwa mkubwa kwa sababu ya eneo unalokuwepo.
Unapotoka kwenye eneo hilo na kufanya matembezi hasa kwenye maeneo ya asili, unapata utulivu mkubwa.
Wakati unafanya matembezi hayo, unafanya na zoezi la pumzi pia.
Unaweza kufanya pumzi ya 5×5×5 au 4-7-8, lakini huhesabu, badala yake unatumia hatua.

Kwenye 5×5×5 unavuta pumzi kwa hatua tano, unashikilia pumzi kwa hatua nyingine tano na kutoa pumzi kwa hatua tano pia.
Kwenye 4-7-8 unavuta pumzi kwa hatua 4, unashikilia kwa hatua 7 na kuitoa kwa hatua 8.

Ukifanya zoezi la pumzi na matembezi kwa pamoja, unapata manufaa makubwa kwenye kutuliza akili yako na pia kwenye kuja na ubunifu wa kipekee.

Pumzi ni silaha unayoihitaji sana kwenye zama hizi ambazo tunatengeneza msongo mkubwa kwa mambo yasiyo na tija kabisa.
Jizoeshe kufanya mazoezi haya ya pumzi hata kama huna msongo, ili unapokuwa na msongo iwe rahisi kwako kuyafanya.

Na pale unapokuwa na maamuzi yoyote muhimu ya kufanya, usiyafanye kabla ya kufanya zoezi la pumzi mara kadhaa.
Ni baada ya kufanya zoezi la pumzi ndiyo unaweza kuwa na utulivu mkubwa wa kufikiri kwa kina na kufanya maamuzi sahihi.

Rasilimali muhimu za kukusaidia kwenye msongo.
Kwa kuwa tumeona msongo kuwa changamoto kwa wengi na kwa kuwa mazingira yanachochea sana hali ya msongo, unahitaji kuwa na rasilimali muhimu za kupambana na hali hiyo.
Hapa kuna rasilimali kubwa mbili unazopaswa kuwa nazo.
1. Kitabu cha UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA. Kwenye kitabu hiki kuna tahajudi ya hatua sita ambayo ina nguvu ya kukupa utulivu mkubwa na kuvuta kwako chochote unachotaka.
2. Kitabu cha EPUKA UTUMWA WA KIDIJITALI, kwenye kitabu hiki unajifunza jinsi ya kuondoka kwenye uraibu wowote ule na pia kuepuka matumizi ya mitandao ya kijamii ambayo ni chanzo kikuu cha msongo kwa sasa.
Pata leo vitabu hivi kwa kuwasiliana na 0752 977 170 na utatumiwa au kuletewa kitabu popote ulipo Tanzania na Afrika Mashariki.

Usikubali msongo uendelee kuwa kikwazo kwenye utulivu wa maisha yako.
Usikubali wengine waendelee kukuweka kwenye msongo ili ufanye makosa na wao wanufaike.
Fanya zoezi la pumzi tulilojifunza hapa na uweze kuwa na utulivu mkubwa kwenye maisha yako.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.