Rafiki yangu mpendwa,
Safari ya kupata mafanikio na uhuru kwenye maisha haijawahi kuwa rahisi.
Ndiyo maana katika wengi sana wanaotaka kufakiwa, ni wachache mno ambao wanayapata mafanikio wanayotaka.
Wengi inabidi wakubaliane na kuridhika na kile wanachopata.

Mafanikio na uhuru siyo kitu ambacho unaweza kupewa na mtu yeyote yule, bali ni kitu unachopaswa kukipambania wewe mwenyewe. Ni vitu unavyopaswa kuvidai na kuvichukua, kwa kuonesha kwamba unaweza kuvihimili.

Kinachowazuia wengi kufanikiwa ni kuwa chini ya wengine ambao wanawageuza kuwa kama watumwa wao. Watu hao hutafuta njia mbalimbali za kuwarubuni walio chini yao ili wasiondoke. Kama usipozijua mbinu hizo na kuzivuka, hutaweza kufanikiwa.

Kwenye makala hii ya ushauri tunakwenda kujifunza jinsi ya kuondoka kwenye utumwa wa kumfanyia kazi ndugu bila ya malipo.
Kabla hatujaingia kwenye mikakati ya kufanyia kazi hilo, tusome maoni ya msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili.

“Nilimaliza kidato cha nne mwaka 2018 matokeo hayakuweza kuniruhusu kuendelea kidato cha tano, maana combination hikublance. Kaka aliniambia atanipeleka chuo, ila alikuja kunigeuka na kusema kusoma sio kupata kazi maana kuna marafiki zake wamesoma ila amewaajiri. Ikanilazimu niingie kwenye biashara zake nakaa dukani kwake bila malipo yoyote zaidi ya nauli ninayopewa. Nashindwa kumwambia hata naomba anilipie ada nikaongeze ujuzi kwenye urembo, nahisi nimekuwa mtumwa. Nimekuwa na ndoto ya kujiajiri mwenyewe niwe na saluni maana ni kitu nakiweza na kukipenda kutoka ndani ya moyo wangu.” – Happy J. M.

Ndugu na watu wengine wa karibu huwa wanakuwa na nia njema ya kutusaidia pale tunapokuwa tumekwama kwenye maisha.
Lakini nia yao njema inaweza kuwa kikwazo kwetu kwa sababu hawajali kile hasa mtu anachotaka.

Na hawajali kwa sababu hawajui, wanaona mtu hawezi kusimama mwenyewe na anahitaji msaada. Wanaangalia ni kwa namna gani wanaweza kumsaidia kwa kile kilicho ndani ya uwezo wao.
Kwa sababu mtu anakuwa hana namna, inabidi akubali kile ambacho anasaidiwa, hata kama siyo alichokuwa anataka.

Wengi hukubali wakijua muda unavyokwenda mambo yatabadilika na waweze kupata kile wanachotaka, lakini hilo halitokei. Wanajikuta wakiwa wamenasa kwenye utumwa ambao hawajui jinsi ya kujinasua.

Hapo ndipo alipo msomaji mwenzetu Happy, ambaye amenasa kwenye biashara ya kaka yake huku ndoto yake ikiwa ni kuwa na biashara yake ya saluni.

Ili kuondoka kwenye utumwa huo, kuna hatua ambazo mtu unaweza kuchukua na kupata uhuru wako.

Moja ni kumweleza anayekusaidia ukweli.

Wakati mwingine unaweza kumlaumu anayekusaidia kwamba anakutumia tu, kumbe yeye wala haoni hivyo. Yeye anaona bado anakusaidia na kwa sababu umetulia anadhani kila kitu kipo vizuri.
Kama kuna kitu hupendezwi nacho juu ya jambo lolote lile, hakuna anayeweza kujua kama hutakisema.

Hivyo hatua ya kwanza ni kukaa chini na ndugu yako kumweleza yaliyo moyoni mwako.
Mweleze ndoto na matarajio yako ni nini na namna gani unaomba akusaidie kwenye hilo.
Unaweza kuona hili ni rahisi, lakini utashangaa jinsi linavyoweza kufanya kazi, hasa unapoeleza vizuri na kwa ushawishi.

Wengi watakusikiliza, kukubaliana na wewe na kuwa tayari kukusaidia kwenye kile unachotaka.
Na kama watakataa, basi nenda hatua inayofuata.

Mbili ni kutaka ulipwe kama wengine wanavyolipwa.

Kama umemweleza mtu kile unachotaka na namna unavyoomba akusaidie na akakataa, hatua inayofuata ni kumwomba akulipe kama wengine wanavyolipwa.
Angalia kazi unayofanya na jiulize angekuwa amemwajiri mtu mwingine angemlipa kiasi gani.
Toa gharama nyingine anazokusaidia kisha mtake akulipe kile kiasi cha ziada ambacho kwa sasa hakulipi.

Kama atakubali kukulipa, weka akiba fedha hizo zote na uje kuzitumia kama sehemu ya mtaji wako pale utakapochukua uhuru wako.
Usitumie kabisa kile atakachokulipa, endelea kama unavyokwenda sasa ili uweze kukusanya mtaji wa kutosha kwenda kufanya kile unachotaka.
Kama atakataa kukulipa, basi nenda hatua inayofuata.

Tatu ni kuwa bora sana kwenye kile unachofanya.

Kama ndugu yako anayekusaidia kwa kukupa kazi ya kufanya ila hakulipi amekataa mapendekezo hayo mawili hapo juu, basi kuna kitu kimoja ambacho wewe mwenyewe hujakiona na unapaswa ukione kama unataka kuwa huru.

Kitu hicho ni hakuna thamani kubwa unayoweka kwenye kile unachofanya. Kwa kifupi umekuwa ni mzigo kwake na hivyo hataki uendelee kuwa mzigo zaidi ya ulivyo sasa.
Hatakuambia hivyo wazi, lakini jinsi anavyokuchukulia, unapaswa kuelewa hilo mwenyewe.

Hakuna mtu aliye tayari kupoteza mtu anayempa thamani kubwa.
Na kama kweli unazalisha thamani kubwa kwa mtu na hakujali, si upeleke thamani hiyo kwa mwingine anayejali?

Hivyo kubali hakuna thamani kubwa unayozalisha na hivyo pambana sana ili uweze kuwa bora kwenye kile unachofanya.
Ukishakuwa bora kabisa, unakuwa na nguvu ya kuondoka hapo kwa ndugu yako na kwenye kufanya kazi mahali pengine ambapo watathamini mchango wako na kuwa tayari kukulipa vizuri.

Na kama unajiona tayari umeshakuwa bora ila ndugu yako haoni thamani yako, ni wakati wa kuondoka kwake na kupeleka thamani yako kwa wengine.
Tafuta sehemu nyingine unayoweza kutoa thamani yako na wakaijali, kisha mshukuru ndugu yako kwa kipindi chote alichokusaidia.

Usiogope kusimamia maslahi yako kwa sababu mtu alikusaidia, kusaidiwa siyo tiketi ya kuwa mtumwa wa mtu. Kusaidiwa ni njia ya kuwezeshwa kusimama ili uweze kuwa vile unavyotaka.
Hivyo endelea kusimamia ndoto zako kubwa na wajulishe wazi wanaokusaidia kile unachotegemea kutoka kwao.
Na kama hawathamini ndoto zako, hulazimiki kuwa chini yao, dunia ni pana hii na fursa ni nyingi. Kama kweli uko vizuri kwenye kile unachofanya, hutakosa fursa za kukuwezesha kusimama na kufikia ndoto zako.

Rasilimali muhimu.

Soma kitabu cha BIASHARA NDANI YA AJIRA ili uweze kujifunza jinsi unavyoweza kuanzisha biashara ya pembeni wakati unaendelea kufanya kile unachofanya sasa.
Hii ni njia nzuri ya kuchukua uhuru wako, kwa sababu utakuwa umejenga kitu cha kukuwezesha kusimama kabla hujaachana na utumwa unaokusumbua.

Kwa bahati mbaya sana, watu huchoshwa na utumwa waliopo na kuamua kuachana nao, kabla hawajajijengea mahali pa kusimama. Kinachotokea ni wanajikuta wakitudi kwenye utumwa tena katika hali mbaya kuliko ya mwanzo.

Wewe usiwe hivyo, anza kujenga kitu cha kusimamia kabla hujaondoka kwenye utumwa wowote unaokusumbua sana.
Kama umeweza kuwa kwenye utumwa huo kwa muda, unaweza kuendelea nao huku ukijenga kitu cha pembeni kutakachokuwezesha kusimama imara pale utakapoondoka kwenye utumwa huo.

Kupata kitabu cha BIASHARA NDANI YA AJIRA wasiliana na 0752 977 170 na utatumiwa au kuletewa kitabu popote ulipo ndani ya Afrika Mashariki.

Fanyia kazi haya uliyojifunza kwenye hii makala ili uweze kuchukua uhuru wako na kuishi kusudi la maisha yako.
Kama una changamoto inayokuwa kikwazo kwa mafanikio yako, unaweza kupata ushauri kwa kujaza fomu hii; http://bit.ly/ushauri

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.