Rafiki yangu mpendwa,
Kama ambavyo nimekuwa nasisitiza, biashara ndiyo njia ya uhakika ya kutengeneza kipato kisicho na ukomo na kuweza kufika kwenye uhuru wa kifedha.

Hivyo yeyote ambaye anataka kuongeza kipato bila ukomo na kufika kwenye uhuru wa kifedha, hana budi kuingia kwenye biashara.

Lakini hapo kuna changamoto, kuingia kwenye biashara siyo rahisi kama wengi wanavyodhani.
Kuna vikwazo mbalimbali, ambavyo vinawaweka pembeni wale ambao hawajajitoa kweli na kutoa nafasi kwa wale walio tayari kupambana.

Kwenye makala hii ya uchambuzi, tunakwenda kujifunza jinsi ya kuingia kwenye biashara kubwa kwa kuanza na mtaji kidogo.
Msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuomba ushauri kwenye hili, alikuwa na haya ya kusema;

“Nimefikiria kufanya biashara ambayo mtaji wake ni mkubwa wakati mimi nina kiasi kidogo.  Je nikichukua hicho kiasi kidogo nikaamua kufanya biashara ndogo ndogo haitapelekea kuvuruga mipango yangu?” – Gabriel G. A.

Kila anayepanga kuingia kwenye biashara, huwa ana ndoto za kufanya biashara kubwa sana.
Lakini mtu anakuwa anaanzia kwenye mazingira ambayo ndoto hizo kubwa siyo rahisi kuanza nazo.

Wengi wamekuwa wanatumia hicho kama kisingizio, kusema wameshindwa kuingia kwenye biashara kwa sababu hawana mtaji.
Lakini kama ambavyo nimekuwa naandika mara nyingi, kukosa mtaji siyo sababu, bali ni kisingizio.

Kwa kuwa wapo watu wengine ambao wameweza kuanzisha biashara na kufanikiwa sana bila ya kuwa na mtaji, huwezi kutumia hiyo kama sababu, labda kama unataka kujidanganya na kujifariji tu.

Hivyo haijalishi ndoto zako za kibiashara ni kubwa kiasi gani, utaweza kuzifikia kwa kuwa tayari kuanza kidogo na kuanzia chini kabisa.

Unapoanzia chini, wakati mwingine unalazimika kuanza na biashara ambayo ni tofauti na ya ndoto yako. Kufanya hivyo hakuvurugi mipango yako, bali kunakupa darasa kubwa na muhimu mno kwenye safari yako ya kufanikiwa kwenye biashara.

Zifuatazo ni faida za kuanzia biashara chini kuliko ndoto yako.

1. Unapata nafasi ya kujifunza biashara kwa vitendo.
Haijalishi umeitafiti biashara kwa kiwango gani kabla hujaanza, umesoma vitabu vingapi vya biashara na umejifunza kwa wafanyabiashara gani, unapoingia kwenye biashara utakutana na changamoto ambazo hukuzitegemea.
Ni vizuri ukutane na changamoto hizo ukiwa umeanza kidogo na hivyo unakuwa na nafasi nzuri ya kujifunza.
Unajifunza kwa ukaribu mahitaji ya wateja, ubora wa bidhaa au huduma zinazohitajika, ushindani na mengine muhimu.
Usijinyime fursa hii ya kujifunza biashara kwa vitendo unapoanzia chini kabisa.

2. Unajua ni biashara ipi hasa unayoiweza au yenye fursa.
Kuna kauli kwamba mipango siyo matumizi.  Kabla hujaingia kwenye biashara unaweza kupanga mambo mengi uwezavyo, unaweza kuiona biashara ni sahihi kwako na ina fursa nyingi.
Unapoingia kwenye biashara ndiyo unaona mambo ya ndani ambayo hukuweza kuyaona kwa nje.
Unapokuwa ndani ndiyo unagundua ulizokuwa unaona ni fursa siyo fursa, unaona changamoto ambazo kwa nje hukuwa unaziona.
Ni vigumu kujua kama biashara ni nzuri kama bado hajaingia kuifanya. Na wengi wamebadili au kuboresha biashara zao baada ya kuingia.
Hivyo anza kidogo, ili ujifunze na kuona kama kweli hiyo ndiyo biashara ambayo upo tayari kuendelea nayo.

3. Ukipata hasara hupotezi sana.
Kwenye kila biashara, kuna wakati utapata hasara, hasa mwanzoni.
Ukipata hasara wakati mtaji ni mkubwa unapoteza kiasi kingi. Lakini ukipata hasara wakati mtaji ni mdogo, unapoteza kiasi kidogo.
Hivyo unakuwa umejifunza mengi kuhusu biashara kwa gharama kidogo tu.

Haijalishi una ndoto kubwa kiasi gani, ndoto hizo hazitakamilika ukiwa umekaa au kulala, ndoto hizo zitakamilika iwapo utachukua hatua sahihi ya kuzifanyia kazi.
Wewe una malengo ya kuwa na biashara kubwa, anza kidogo.
Anza na biashara hiyo hiyo kwa kiwango kidogo au anza na biashara nyingine unayoweza kuanza nayo kwa hali unayokuwa nayo.

Lengo la kuanza kidogo ni kujifunza biashara kwa vitendo na kuziona fursa sahihi zilizo kwenye biashara husika.
Kadiri unavyokaa kwenye biashara ndiyo unavyoweza kuziona na kuzitumia fursa za kukua zaidi.

Jipatie kitabu hiki cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA uweze kujenga biashara sahihi kwako, kukipata wasiliana na 0752 977 170

Lakini kuna tahadhari kubwa unapaswa kuondoka nayo hapa. Unapoanza biashara kidogo, jizuie sana usifikiri kwa udogo. Kwani fikra zako ndiyo ukomo wako.
Endelea kufikiria biashara kubwa ya ndoto yako, endelea kuaandika malengo yako makubwa na endelea kupata picha ya ukiwa tayari umefika kwenye biashara yako kubwa.

Kwa kuendelea kuzishikilia ndoto zako kubwa, biashara ndogo unayokuwa umeanza nayo inakuwa kama jiwe la wewe kupanda kwenda kwenye biashara ya ndoto yako. Lakini kama utasahau ndoto zako kubwa na kumezwa na biashara hiyo ndogo, utaishia hapo hapo.

Fanyia kazi haya uliyojifunza hapa, ili uweze kuanzia popote ulipo sasa na kufika kwenye biashara ya ndoto zako. Usijicheleweshe, kama alivyowahi kusema Martin Luther King, kama huwezi kuruka kimbia, kama huwezi kukimbia tembea, kama huwezi kutembea tambaa, fanya chochote ila tu usibaki pale ulipo sasa.

Kama una changamoto inayokuwa kikwazo kwa mafanikio yako, unaweza kupata ushauri kwa kujaza fomu hii; http://bit.ly/ushauri

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.
www.somavitabu.co.tz