Rafiki yangu mpendwa,
Aliyekuwa mtabe na jenerali wa kivita wa nchini Ufaransa, Napoleon Bonaparte amewahi kunukuliwa akisema; “A leader is a dealer in hope”.
Kwa tafsiri rahisi ya Kiswahili alimaanisha KIONGOZI NI MUUZA MATUMAINI.

Nimekuwa nakutana na kauli hiyo mara kwa mara, lakini sijawahi kuitafakari kwa kina.
Ni mpaka siku chache zilizopita nilipojiuliza kwani hii kauli ina maana gani hasa na nawezaje kuitumia kwenye yale ninayofanya.

Tafakari hiyo ilinipa nafasi ya kuona nguvu kubwa mno iliyo kwenye kauli hiyo na moja kwa moja ikapelekea kuifanya kuwa moja ya  vyeo ninavyojitambulisha navyo.

Nimekuwa najitambulisha kama;
1. Daktari wa binadamu kwa sababu ni taaluma yangu na ninatibu.
2. Kocha wa mafanikio ambapo nafanya kazi kwa karibu na wale wanaotaka kufanikiwa.
3. Mwandishi kwa sababu kila siku naandika na nimeandika vitabu 15 na vinaendelea.
4. Mjasiriamali kwa sababu natafuta suluhisho la changamoto mbalimbali ambazo watu wanakabiliana nazo.
Na sasa utambulishi mpya ni;
5. Muuza Matumaini, kwa sababu ndiyo kitu kinachoweza kuleta mabadiliko makubwa kwa wengine.

Nini maana ya kiongozi ni muuza matumaini?

Kauli ya Napoleon kwamba kiongozi ni muuza matumaini ina maana kubwa sana.
Ni kauli ambayo Napoleon aliishi katika kampeni zake za kivita, ambapo aliweza kupata ushindi mkubwa hata alipokuwa na jeshi dogo.
Napoleon aliwashangaza wengi enzi zake maana aliweza kuendesha kampeni nyingi za kivita na kupata ushindi hata kama maadui walikuwa wamemshinda kwa kila kitu.

Siri yake kubwa ilikuwa ni kuwapa matumaini wanajeshi wake. Aliamini watu wakiwa na matumaini, watapambana kufa na kupona mpaka wapate kile wanachotaka.
Hivyo pamoja na mipango mizuri aliyokuwa nayo, bado alijua bila kuwapa matumaini wapiganaji wake, asingeweza kushinda.
Hivyo aliweka kazi kubwa kwenye kuwajaza matumaini wapiganaji wake, kitu kilichowasukuma sana.

Vita na hata mafanikio ni udanganyifu.

Sun tzu ambaye alikuwa mwandishi wa mbinu za kivita wa China ya kale kwenye kitabu cha The Art of War aliandika; Msingi wa vita ni udanganyifu, unapokuwa unaweza kushambulia mfanye adui aone huwezi. Unapokuwa mbali mfanye adui aone uko karibu. Na unapokuwa karibu, mfanye adui aone uko mbali.

Hii ni namna nyingine ya kuangalia kazi ya kiongozi kwenye kuwaongoza watu wake kufika wanakotaka, kwa kuyatumia vizuri.
Hii ni njia nyingine ya kuyaangalia matumaini, kuwafanya watu waone kile chenye manufaa kwao na kinachowapa motisha na siyo kile kilichopo na kinachowakatisha tamaa.

Hivyo pia ndivyo safari ya mafanikio ilivyo, lazima uamini kwamba utafanikiwa na kuweza kufanya makubwa hata kama hujui hilo litatokeaje.
Mafanikio ni zao la matumaini, ni zao la imani ambayo mtu anakuwa nayo kabla ya mengine yote.

Simba na kondoo.

Mbabe mwingine wa kivita  Alexander the Great amewahi kunukuliwa akisema; “Siogopi kundi la simba wanaoongozwa na kondoo mmoja, bali naogopa kundi la kondoo wanaoongozwa na simba mmoja.”

Hii ni njia nyingine ya kuangalia nguvu ya matumaini kwenye ushindi wa jambo lolote lile, hasa kuanzia kwenye uongozi.
Simba na na ukali wao wote, wakiongozwa na kondoo wanaishia kuwa kama kondoo na hawawi na madhara.
Kondoo na upole wao, wakiongozwa na simba wanakuwa na ukali kama wa simba na kuwa na madhara makubwa.

Matumaini yana nguvu mno kwenye ushindi wa aina yoyote ile. Ndiyo yanamsukuma mtu kuendelea kupambana hata kama hakuna njia inayoonekana mbele. Lakini kwa mapambano, njia inafunguka.

Kwa nini nimechagua kuwa MUUZA MATUMAINI?

Nimekuwa natoa huduma ya Ukocha na kufanya kazi kwa karibu na wale wenye kiu ya mafanikio makubwa kwa muda sasa.
Katika safari hii nimekuwa najaribu njia mbalimbali, lakini kuna njia moja ambayo nimekuwa naona ina matokeo makubwa zaidi.

Njia hiyo ni kumpa mtu matumaini, kumfanya ajiamini na kujikubali mwenyewe.
Njia hii ina nguvu kubwa sana ya kumsukuma mtu kufanya makubwa kuliko anavyoweza kudhani mwenyewe.

Matumaini yanamkutanisha mtu na bahati.

Kipindi cha nyuma nilikuwa siamini kwenye bahati. Niliamini juhudi pekee ndiyo zinampa mtu mafanikio.
Lakini kadiri ninavyojifunza na kuyaelewa mafanikio, naona wazi kwamba kila aliyefanikiwa kuna bahati alikutana nayo kwenye safari yake ya mafanikio.

Lakini sasa, bahati hiyo haikumkuta akiwa amelala kitandani, bali ilimkuta akiwa kwenye mapambano.
Hivyo kadiri unavyokaa kwenye mapambano kwa muda mrefu bila kukata tamaa, ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi nzuri ya kukutana na bahati.

Na hapo ndipo matumaini yanapokusaidia kupata bahati, ukiwa na matumaini, utaendelea kupambana hata kama huoni mbele, utaendelea kuweka juhudi. Na kwa wakati usiotegemea, fursa kubwa zinafunguka mbele yako.

Kwa mimi kukuuzia matumaini, nitakusaidia ubaki kwenye mapambano kwa muda mrefu zaidi, kitu kinachokuweka kwenye nafasi ya kukuta na bahati.

Sikuuzii matumaini hewa.

Watu wengi ambao wamekuwa wakihamasisha kwenye mafanikio, wamekuwa wanawapa watu shauku kubwa na kuwaonyesha kwamba wanaweza kufanikiwa na kufanya makubwa.
Watu wanatoka wakiwa na moto mkubwa, lakini hamasa wanayokuwa nayo haidumu, siku chache wanarudi kwenye mazoea yao ya awali.

Mimi sikuuzii matumaini ya aina hiyo, ndiyo nitakubaliana na wewe kwamba chochote unachotaka kinawezekana, lakini nitataka kitu kimoja kwako, UTENGENEZE MCHAKATO wako wa mafanikio na uufuate kila siku.

Matumaini ninayokuuzia mimi siyo ya kukupa tu hamasa, bali kukufanya ukae kwenye mchakato wako kwa muda mrefu iwezekanavyo.
Unapofanya kazi na mimi, kikubwa ninachotaka kwako ni mchakato unaofanyia kazi.
Sijali sana kuhusu matokeo unayopata,  najali zaidi mchakato unaofanyia kazi.

Ninajua na nina uhakika kwamba ukiwa na mchakato unaofanyia kazi, hata kama hutapata unachotaka, hutabaki pale ulipo sasa.

Ukiniambia unataka kuwa bilionea, nakujibu inawezekana kabisa, kisha tunaweka mchakato wa kufanyia kazi ili kufikia hilo.

Ukiniambia unataka kuandika kitabu nakujibu inawezekana, kisha tunaweka mchakato wa kuandika kila siku mpaka ukamilishe kitabu.

Ukiniambia unataka kuanzisha au kukuza biashara yako, nakujibu inawezekana, kisha tunaweka mchakato utakaofanyia kazi.

Njoo kwangu na chochote kikubwa unachotaka na nitakujibu bila ya shaka kwamba kinawezekana,  na hatutaishia hapo, bali tutaweka mchakato unaopaswa kufanyia kazi kila siku ili iwezekane.
Na ushirikiano wangu na wewe ni kwenye huo mchakato.
Kama hakuna mchakato unaofanyia kazi, sina namna ya kukusaidia, matumaini nitakayokuuzia hayatakuwa na manufaa kwako.

Kama unataka kufanya makubwa, na upo tayari kufanyia kazi mchakato, njoo tufanye kazi pamoja.

Watu wengi ni wakatishaji tamaa.

Kwenye jamii zetu, watu wengi mno ni wakatishaji tamaa.
Waambie watu ndoto zako kubwa na watakuambia huwezi, watakupa kila aina ya ushahidi kwamba haiwezekani.

Hivyo kuna fursa kubwa kwa wanaoweza kuuza matumaini ya kweli, matumaini yanayomwezesha mtu kufanyia kazi mchakato sahihi.
Na hiyo ndiyo fursa ambayo mimi naifanyia kazi, ndiyo maana nimejipa cheo kabisa, cha muuza mtumaini.

Tumaini kuu ninalokuuzia.

Kuna tumaini moja kuu ambalo nakuuzia, ambalo ukilipokea, kulikubali na kuliamini, utafanya makubwa kwenye maisha yako.

Tumaini hilo ni KILA KITU KINAWEZEKANA.
Kitu chochote kile unachotaka, ambacho hakipingani na kanuni za asili kinawezekana.
Hata kama hakuna ambaye ameshaweza kufanya, kinawezekana na wewe unaweza kuwa wa kwanza kukifanya.

Nakuuzia tumaini hilo kuu na mchakato wa kulifanyia kazi ili uweze kupata chochote unachotaka.

Njoo ununue matumaini kwangu.

Rafiki, kama umeielewa vizuri dhana hii ya kuuza matumaini, nakukaribisha uje kununua.

Unachohitaji ili uweze kununua matumaini ninayouza ni kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA na kufanyia kazi kwa umakini yale yote ninayoshirikisha.

Kama tayari upo kwenye KISIMA CHA MAARIFA basi kazi yako ni moja, kufanyia kazi yale ninayoshirikisha.
Kuleta kwangu ndoto zako kubwa ulizonazo, kisha tutengeneze mchakato utakaoufanyia kazi kila siku huku nikikufuatilia kwa karibu.

Kama bado hujawa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA karibu ujiunge leo, tuma ujumbe kwa wasap kwenda namba 0717 396 253 wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA na nitakupa maelekezo ya kujiunga.

Katika kupokea cheo hiki kipya nilichojipa, leo natoa zawadi kwa atakayejiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Kama bado hujajiunga, wasiliana nami sasa hivi kuna zawadi kubwa kwako ukijiunga leo.
Kama una mtu wa karibu ambaye ungependa apate zawadi hii, mtumie ujumbe huu na achukue hatua.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.
http://www.somavitabu.co.tz

Moja ya tumaini ninalokuuzia kwa uhakika ni kuhusu nguvu kubwa iliyo ndani yako. Kuna nguvi ya kutenda miujiza mikubwa ndani yako. Pata kitabu hiki na ujue jinsi ya kuitumia. Wasiliana na 0752 977 170 kukipata kitabu.