Rafiki yangu mpendwa,
Kitu kimoja kinachowatofautisha wale wanaopata mafanikio makubwa na wanaoshindwa ni malengo.

Wanaofanikiwa wanajua ni nini hasa wanachotaka na watakipataje na kila siku wanakipambania mpaka wakipate. Hawakati tamaa licha ya kukutana na magumu mbalimbali.

Wanaoshindwa hawajui nini hasa wanachotaka, wapo wapo tu na kila wakati wanakimbizana na mambo mapya yanayowavutia.

Malengo ndiyo yanamfanya mtu aamue nini hasa anachotaka, anakipataje na hatua za kufanyia kazi kila siku ili kupata anachotaka.

Hapa kwenye malengo watu wana changamoto nyingi, hawajui jinsi ya kuweka malengo sahihi na hata wakiyaweka hawawezi kuyafanyia kazi.

Kwenye makala hii ya ushauri tunakwenda kujifunza jinsi ya kuweka malengo makubwa na kuyafanyia kazi mpaka kuyafikia.

Kabla hatujaangalia hatua unazopaswa kuchukua kwenye eneo la malengo, tupate maoni ya mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili.

“Ninakuwa na malengo makubwa ila nashindwa kuanza kuyafanyia kazi na hatimaye najikuta nabaki kuyabadilisha kadri siku zinavyoenda” – Gamalieli J. M.

Ili kuweka malengo makubwa na kuweza kuyafikia, fuata hatua hizi.

I Jua kwa hakika nini unataka.
Sababu kubwa ya watu kutokupata wanachotaka ni kwa sababu hawajui wanachotaka.
Unaweza kushangaa hilo linawezekanaje, lakini ndiyo uhalisia.
Watu wengi huwa wana matamanio tu, wanatamani kupata mambo makubwa.
Malengo ni kuamua kwa hakika nini unataka, siyo unachotamani, bali unachotaka.

II Jiambie kwamba lazima utapata unachotaka.
Wapo wanaojua kile hasa wanachotaka, lakini wanaishia kujiambia watajaribu au kama watapata sawa na kama hawatapata sawa.
Hakuna aliyewahi kupata makubwa kwa kufikiri kizembe hivi.
Wewe jiambie ni lazima utapata kile unachotaka, kama tu utaendelea kuwa hai.
Ahadi yako na nafai yako ni kwamba utapata kile unachotaka au utakufa ukiwa unakipambania.
Kata shauri kabisa ukijua hakuna kurudi nyuma.

III Uwe unaweza kupima kile unachotaka.
Changamoto nyingine kwenye malengo ni watu kushindwa kupima. Wanajiambia tu wanataka makubwa, lakini hawawezi kupima ni makubwa kiasi gani.
Chochote ambacho hakiwezi kupimwa hakina nafasi ya kuboreshwa zaidi.
Hivyo hakikisha malengo yako yanapimika.
Badala ya kujiambia unataka fedha nyingi au utajiri mkubwa, jiambie kiasi kabisa cha fedha au utajiri unaotaka kuwa nao.

IV Chukua hatua ndogo ndogo kufanyia kazi lengo.
Kwa kuwa tayari unaweza kulipima lengo, anza kuchukua hatua ndogo ndogo ili kulifikia.
Ndiyo lengo lako ni kubwa, ila ligawe kwenye hatua ndogo ndogo unazoweza kufanyia kazi kila siku.
Hata kama ni kiasi kidogo sana unafanyia kazi, kwa kufanya hivyo kila siku bila kuacha hata moja, utapata matokeo ambayo ni makubwa mno.
Usikubali siku iishe hujafanyia kazi lengo lako hata kwa hatua ndogo.

V Lifanye lengo kuwa kipaumbele cha kwanza kwako.
Kwa lengo lako kubwa, ambalo ndiyo lenye nguvu ya kuleta matokeo makubwa kwenye maisha yako, ndiyo linapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza kwako.
Usihangaike na mambo mengine yanayoondoa muda, nguvu na umakini wako kwenye lengo lako kuu.
Usiruhusu usumbufu wa mambo mengine kuwa kikwazo kwako.
Kila siku fanyia kazi kipaumbele cha kwanza kwako ambacho ni lengo lako kuu.

VI Jua kwa nini uteseke ili kufikia lengo hilo.
Unapokuwa na malengo makubwa, jua umechagua mateso. Utakutana na changamoto kubwa katika kufanyia kazi malengo hayo. Utapitia mateso ya kila aina. Kwa nini uko tayari kupitia yote hayo?
Kama huna kwa nini kubwa inayokusukuma, hutafika mbali na malengo yako makubwa, utakata tamaa na kuishia njiani.
Kwa nini inaweza kuwa ni kuacha alama kubwa, kuwaonyesha wengine inawezekana, kuwasiadia wengine wenye uhitaji au kupata kile unachotaka sana.
Ijue kwa nini yako kubwa na kila mara jikumbushe ili usiishie njiani.

VII Kuwa na mtu wa kukusimamia na kukuwajibisha.
Sisi binadamu kwa asili ni wavivu, wazembe na tunaopenda kufanya vilivyo rahisi. Kwa sifa hizo huwezi kufikia malengo yako makubwa.
Unahitaji mtu ayakayekufuatilia kwa karibu, kukusimamia kwenye malengo yako makubwa na kukuwajibisha pale unapokwenda nje ya malengo yako.
Ukiwa mwenyewe ni rahisi kupotea, ukiwa na anayekusimamia kwa karibu hatokuacha upotee.
Unahitaji menta, kocha au mshauri wa karibu katika kuyafanyia kazi malengo yako makubwa.

VIII Jifanyie tathmini mara kwa mara.
Japo unachukua hatua ndogo ndogo kila siku ili kuyafikia malengo yako, unapaswa kujua kama kweli uko kwenye njia sahihi au la.
Utalijua hilo kupitia kujifanyia tathmini mara kwa mara.
Kila siku jifanyie tathmini ya ilivyoenda na namna ulivyoyafanyia kazi malengo yako.
Kila wiki jifanyie tathmini ya hatua ulizopiga.
Kila mwezi pia fanya tathmini na kila mwaka jitathmini.
Ni kupitia tathmini ndiyo unapata picha ya wapi unaelekea.

IX Usibadili malengo, badili mipango.
Kama lengo lako ni kutoka Dar kwenda Arusha, ukafika stendi ya mabasi na kuambiwa mabasi yote yamejaa, hupaswi kubadili lengo la safari, bali unapaswa kubadili usafiri unaotumia.
Kadhalika kwenye malengo ndivyo ilivyo, unapokutana na vikwazo na changamoto, hata ziwe kubwa kiasi gani, usibadili lengo, wewe badili mpango unaofanyia kazi katika kufikia lengo hilo.
Njia moja ikijifunga usione ndiyo mwisho, angalia, zipo njia nyingine nyingi tu unaweza kutumia kufikia lengo.

X Andika lengo lako kubwa kila siku.
Tafiti mbalimbali zilizofanywa kwenye malengo zinaonyesha kitendo tu cha kuandika malengo, kinaongeza uwezekano wa kuyafikia kwa asilimia 42.
Tumia nguvu hiyo ya kuyaandika malengo ili uhakikishe unayafikia.
Ianze kila siku kwa kuyaandika malengo yako makubwa.
Na unapokutana na ugumu, vikwazo au changamoto zozote zinazotaka kukukatisha tamaa, rudia kuyaandika malengo yako.
Unapoyaandika malengo yako unayapa kipaumbele cha kwanza kwenye akili yako na hilo linakufanya uzione fursa za kuweza kuyafikia.

Rasilimali muhimu za kukusaidia kuweka na kufikia malengo.
1. Pata na usome kitabu cha MIMI NI MSHINDI, kukipata ingia kwenye app ya SOMA VITABU; www.bit.ly/somavitabuapp
2. Jiunge na KISIMA CHA MAARIFA ambapo utapata mwongozo wa karibu wa kujua kusudi lako na kuwa na ndoto kubwa unazofanyia kazi.
Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA wasiliana na namba 0717 396 253

Fanyia kazi haya uliyojifunza kwenye hii makala ili uweze kujiwekea malengo makubwa na kuyafikia.
Kama una changamoto inayokuwa kikwazo kwa mafanikio yako, unaweza kupata ushauri kwa kujaza fomu hii; http://bit.ly/ushauri

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.
www.somavitabu.co.tz