Rafiki yangu mpendwa,
Nimekuwa nakusisitiza sana hili; rafiki wa kweli ni kazi.

Kazi ndiye rafiki anayeweza kukutoa popote ulipo sasa na kukufikisha popote unapotaka kufika.

Kazi ni rafiki ambaye ukimpenda anakupenda bila kinyongo chochote.

Kazi ni rafiki ambaye hatakuonea wivu pale unapokuwa umefanikiwa sana.

Hivyo ipende kazi, hiyo ndiyo hatua ya kwanza na ya msingi kabisa ya kufika kwenye mafanikio makubwa.

Na hili lieleweke wazi, ninaposema kazi simaanishi ajira, bali chochote unachofanya ambacho kinatoa thamani kwa wengine.

Sasa tumeshamuona rafiki wa kweli ni kazi, lakini mbona bado zipo kazi ambazo hata tukijilazimisha kuzipenda hatuzipendi?
Mbona zipo kazi ambazo licha ya malipo kuwa mazuri hatupati msukumo wa kuzifanya vizuri?

Majibu ni kwa sababu kazi zote hazilingani. Siyo kila kazi inaweza kupendeka na wewe na ukaweza kuifanya kwa viwango vya juu na kufanikiwa.

Kuna sifa kuu tano ambazo kazi yoyote inapaswa kuwa nazo ili iweze kukuridhisha, uipende kweli, uifanye kwa viwango vya juu na uweze kufanikiwa.

Hapa tunapata nafasi ya kujifunza sifa hizo na jinsi ya kuzijenga kwenye chochote tunachofanya, ili urafiki wetu na kazi uwe wa kudumu na wenye manufaa makubwa.

Sifa ya kwanza; UMUHIMU.

Umuhimu wa kile unachokifanya unachangia sana namna ambavyo utakifanya.
Kama kazi unayoifanya ni muhimu, kwa maana kwamba inatoa thamani kwa wengine na kuleta mchango mkubwa, utasukumwa sana kuifanya.
Pale unapoona wengine wakinufaika moja kwa moja na kile ulichofanya, unaridhika na kusukumwa kufanya zaidi ili wengi zaidi wanufaike.

Hatua ya kuchukua; kwa chochote unachofanya, angalia kinawanufaishaje wengine. Ona jinsi maisha ya wengine yanakuwa bora kwa kile unachofanya na utasukumwa kukifanya zaidi.
Kama huoni hilo kwenye kile unachofanya, ni wakati wa kutafuta kitu kingine cha kufanya.

Sifa ya pili; UMILIKI.

Kujiona ukimiliki kile unachofanya kunakupa msukumo wa kukifanya vizuri na kwa ubora pia.
Hapa unaona kabisa unaacha alama yako kwenye kile unachofanya, watu wanajua kabisa hii kazi ameifanya fulani.
Kadiri unavyoweka hisia zako na kujali kwenye kile unachofanya, ndivyo unavyosukumwa kukifanya bila ya kuchoka.
Maana haiwi tena kazi, bali inakuwa njia ya wewe kujitambulisha.

Hatua ya kuchukua; jimilikishe kila unachofanya kwa kujua ni alama unayoacha. Hata kama ni kazi ya kuajiriwa, usifanye kama mwajiriwa, bali ifanye kama wewe ndiye unayeimiliki.

Sifa ya tatu; UHURU.

Uhuru wa kufanya maamuzi kwenye kile unachofanya kuna mchango mkubwa kwenye namna utakavyokifanya.
Kama unaamua mwenyewe kile unachofanya na namna utakavyokifanya unakuwa na msukumo zaidi wa kukifanya. Maana unajua kwa nini unafanya.
Lakini kama umepangiwa tu kufanya au unalazimika kufanya, hutapata msukumo mkubwa wa kufanya au kufanya kwa ubora.

Hatua ya kuchukua; jijengee uhuru kwenye kile unachofanya. Hakikisha wewe ndiye unayeamua nini unafanya na kwa wakati gani na ujisukume kufanya. Kama unapangiwa tu cha kufanya, ni wakati wa kutafuta kingine.

Sifa ya nne; UTOFAUTI.

Mazoea yanachosha sana kwenye kazi. Kama unafanya kitu kile kile kwa kurudia rudia unafika mahali na kujikuta unafanya bila hata ya kufikiria.
Hilo linaondoa ubunifu na ile shauku ya kuendelea kufanya.
Hupati msukumo mkubwa wa kufanya maana unajua hakuna kitu cha tofauti.

Hatua ya kuchukua; endelea kujifunza na kujaribu vitu vipya kwenye kile unachofanya. Hilo litakuwezesha kuleta utofauti na kufanya makubwa.

Sifa ya tano; MREJESHO.

Kama unafanya tu kitu na hakuna anayekupa mrejesho wa namna ya kukiboresha zaidi, unajikuta ukifanya kwa mazoea na hilo kuathiri ufanyaji wako.
Wakati mwingine utakazana kufanya lakini matokeo yanakuwa tofauti na ulivyotegemea, unarudia na mambo yanakuwa vile vile.
Unapaswa kupata mrejesho wa namna ya kuboresha zaidi kile unachofanya, kutoka kwa wale wanaokipokea au wale ambao ni wazoefu zaidi yako.

Hatua ya kuchukua; tengeneza njia nzuri ya kupata maoni na mrejesho wa kuboresha zaidi kile unachofanya kutoka kwa wale wanaonufaika nacho na wale waliobobea zaidi yako.

Ukiweza kujenga sifa hizi tano kwenye kazi yoyote unayofanya, haitakuwa tena kazi kwako, bali itakuwa sehemu ya maisha yako na utafanya kwa ubora wa hali ya juu sana.

Usiichukulie kazi kama kazi tu, ichukulie kama rafiki wa kweli na hakikisha sifa hizo tano zipo kwenye kazi unayoifanya, ipe kipaumbele kikubwa na pambana kuzalisha thamani kubwa kwa wengine.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani
www.somavitabu.co.tz

Kama umeajiriwa na kazi unayofanya haikuridhishi, unaweza kuanza kujenga biashara ya pembeni ukiwa kwenye hiyo kazi na ukawa na kitu kinachokuridhisha. Pata na usome kitabu cha BIASHARA NDANI YA AJIRA na utaweza kufanya hivyo. Wasiliana na 0752 977 170 kupata kitabu.