Rafiki yangu mpendwa,
Jana nilishirikisha kuhusu kukosekana kwa uwajibikaji kama moja ya sababu ya kwengi kushindwa kufikia mafanikio wanayotaka.

Na nikatoa fomu ya kujaza kwa wale wanaotaka kuingia kwenye mfumo wa uwajibikaji.

Nimepokea maombi mengi sana ya watu waliojaza fomu hiyo kwa siku moja tu.
Hicho ni kiashiria ni kwa namna gani hili ni tatizo na watu wapo tayari kulitatua.

Nilijua ni wachache watakaoomba nafasi hiyo ili tuweze kuanza pamoja baada ya SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2021.
Lakini waombaji wamekuwa wengi.

Lakini pia uzoefu wangu unanionyesha hili siyo mara ya kwanza kutokea.
Kila ninapotoa huduma mpya, wengi huomba kuipata, lakini ninapowapa nafasi hawaitumii kweli.

Wanakuwa hawajajitoa kweli kuhakikisha wanaitumia nafasi hiyo kupiga hatua kubwa kwenye maisha yao.
Na hilo hupelekea wengi kuishia njiani, kitu kinachofanya juhudi nyingi ninazokuwa nimeweka kuwa zimepotea bure.

Safari hii nakwenda kufanya tofauti, ili wale kweli wanaoipata nafasi hii wawe ni walio sahihi na wanufaike nayo kweli.

Nakwenda kusitisha baadhi ya vitu ninavyofanya, ili niweke muda na nguvu nyingi kwenye hii huduma ya uwajibikaji na tulete matokeo makubwa kwa kila anayepata nafasi hiyo.

Na kabla hujaendelea kusoma, nikuahidi tu, hii huduma ni ngumu kuliko huduma yoyote ambayo nimewahi kuitoa.
Na ni huduma ambayo ninakushauri usijiunge nayo kama hujajitoa kweli kweli kufanikiwa.

Kama kuna kitu chochote kinaweza kukuzuia, mfano kama kuna ratiba ya mkutano wa pamoja ambao unakutaka usafiri mkoa mmoja kwenda mwingine na kukawa na kikwazo kinachokuzuia kusafiri, hii huduma haikufai.

Yaani unahitaji uipe huduma hii na biashara unayoingia nayo kwenye huduma hii kipaumbele cha kwanza. Uwe tayari kuahirisha mengine yote kwa ajili ya hii huduma na biashara yako.

Rafiki, kama kwa kusoma tu hapo juu unaona ni kitu ambacho hukiwezi, basi ishia tu hapa. Haimaanishi kwamba hufai au huwezi kufikia mafanikio. Utaendelea kupata huduma nyingine nyingi nzuri ninazozitoa.

Na kama unaona haikufai kwa sasa kutokana na hali fulani uliyopo, ila baadaye itakufaa, tunza huu ujumbe na utakapokuja kuwa tayari nijulishe.

Baada ya hayo naamini sasa nimebaki na wale wenye kiu ya kweli ya kufika ngazi za juu mno za mafanikio.

Maelezo haya tu hayatoshi kuwachuja wale wasio sahihi.
Kwa uzoefu wangu kuna watu hamasa huwa zinawaingia kwa muda mfupi, halafu baadaye wakitulia hamasa hizo zinapotea.

Nimeandaa mchujo mkali sana wa kuwapata watu sahihi wa huduma hii.
Ndiyo, mchujo huo ni mkali, una hatua mbalimbali za kupitia ili kweli uipate hii huduma.

Hivyo kwa mwezi mmoja unaokuja, nitafanya zoezi la mchujo wa wale wanaoomba huduma hii.

Kabla sijakupa zoezi zima la mchujo, niitambulishe huduma kwa ufupi.
Mengi zaidi utayapata utakapopata nafasi.

Huduma inakwenda kwa jina la KISIMA CHA MAARIFA BILLIONAIRES CLUB.

Ni huduma maalumu kwa wale ambao wamejitoa kweli kweli kwamba ije mvua lije jua, kama wapo hai, watapambana kufikia ubilionea.

Huduma hii inakwenda kuchukua nafasi ya KLABU ZA KISIMA CHA MAARIFA ambazo tayari zilikuwepo na kuzifanya kuwa bora na zenye tija zaidi.

Rafiki, kuutamka ubilionea ni kitu rahisi na kila mtu anaweza kufanya hivyo.
Lakini kuufikia ubilionea ni kitu kigumu mno, mno, mno. Lakini uzuri ni kitu kinachowezekana, ila kinamhitaji mtu ajitoe sana.

Rafiki, tambua wazi kwamba mafanikio siyo ubilionea pekee na huhitaji kuwa bilionea ndiyo uwe na uhuru wa maisha.

Hivyo huu ni mchezo tunaocheza kwa ajili ya fedha tu, kujisukuma kutoa kila kilicho ndani yetu kwa manufaa makubwa ya wengine wengi.
Ndiyo maana mchujo wa hii huduma unakwenda kuwa mkali, kwa sababu inataka mtu ujitoe kweli kweli.

Kila klabu itakuwa na watu watano walio maeneo ya karibu, ambao kila mmoja atakuwa mjumbe kwenye biashara za wengine na kuweza kuwajibishana vizuri.

Kila klabu zitakutana kila robo mwaka na kila mwanaklabu atawasilisha maendeleo ya biashara yake pamoja na kuweka mikakati anayokwenda kufanyia kazi.
Mikutano itakuwa inafanyika kwenye eneo la biashara la mmoja wa wanaklabu au eneo la karibu na itakuwa inazunguka kwa kila mwanaklabu.

Na kila klabu itakuwa na akaunti ya pamoja ya benki ambapo kila mwanaklabu anaweka michango ambayo lengo lake kuu ni kuwa chanzo cha mtaji ndani ya klabu.

Faida za huduma hii ni nyingi, lakini sita kubwa kabisa ni hizi;

Moja ni MASTER MIND GROUP hili linakwenda kuwa kundi dogo la watu mnaozungumza lugha moja na kuona makubwa ambayo walio kwenye jamii hawawezi kuyaona.
Katika kukutana kama kundi, mawazo mapya na makubwa yanazaliwa na kuboreshwa ili yaweze kuwa na tija.
Hili linakwenda kuwa kundi pekee unaloweza kuliamini kwa asilimia 100 na pia linalokuamini na kukuelewa kwa asilimia 100.
Ni kundi litakalokuambia ukweli kama ulivyo hata kama unakuumiza, lengo siyo kukukatisha tamaa, bali kuhakikisha unauona ukweli ambao mara nyingi siyo rahisi kuuona hasa pale hisia zinapokuwa zimekutawala.
Kwa kuwa ndani ya kundi hili, utaepuka makosa mengi ambayo umekuwa unayafanya kwenye maisha na biashara zako.

Mbili ni BOARD OF DIRECTORS.
Kwenye hii huduma unaingia na biashara moja ambayo ina uwezo wa kukua bila ukomo na hata baadaye kuuzwa au kuingia kwenye soko la hisa (kuwa kampuni ya umma).
Hiyo ndiyo safari ya kuelekea kwenye ubilionea na ndiyo mabilionea wote wameipitia, kukuza makampuni na kuyauza (Acquisition) au kupeleka kwenye soko la hisa (IPO).
Hizo ndiyo njia pekee kwa mtu anayeanzia chini na ambaye harithi utajiri anaweza kuzitumia.
Lakini ukweli ni huu, ni njia ngumu mno, mno, mno kuipita, hasa kwenye mazingira yetu.
Kuna mchakato mkubwa wa kutengeneza mpaka biashara ifike kwenye hatua hizo.
Makampuni makubwa yana faida ya kuwa na bodi ya wakurugenzi ambao ndiyo wanaleta uwajibikaji mkubwa na kuisukuma biashara kukua.
Lakini wale wanaoanzia chini inakuwa vigumu kupata nafasi ya aina hiyo.
Na hicho ndiyo unakwenda kupata kwenye KISIMA CHA MAARIFA BILLIONAIRES CLUB, maana wenzako ulionao kwenye huduma hii wanakwenda kwa BOARD OF DIRECTORS kwenye biashara unayoingia nayo kwenye huduma hii kama njia yako ya kuelekea kwenye ubilionea.
Utawajibika kwa bodi hiyo ambayo haitakuwa tayari kupokea sababu, bali inapokea matokeo ya hatua zilizochukuliwa.
Utawapata watu sahihi wanaokusukuma ili uweze kukua zaidi kwenye biashara yako na kufikia lengo.

Tatu ni FINANCIAL ACCESS.
Ili uweze kuikuza biashara mpaka ifikie kiwango cha kuiuza au kuipeleka kwenye soko la hisa, unahitaji kiasi kikubwa sana cha mtaji.
Mtaji huo huwezi kutegemea faida inayopatikana kwenye biashara.
Badala yake unapaswa kutumia nyenzo (leverage), yaani kutumia fedha zisizokuwa zako, kuzizalisha zaidi na kuiwezesha biashara kukua.
Fedha hizo unaweza kuzipata kwa njia mbalimbali, kama mikopo (loans), ruzuku (grants) na wawekezaji (investors).
Kwa mazingira yetu, kupata kiwango kikubwa cha fedha kwa ajili ya ukuaji wa biashara siyo zoezi rahisi.
Lakini pia unapopata kiwango kikubwa cha fedha, bila ya uwajibikaji mzuri ni rahisi kutumia tofauti na mipango na hilo likaleta matatizo zaidi.
Kwa kuwa ndani ya kikundi, itarahisisha upataji wa kiwango kikubwa cha fedha na pale unapokipata kukitumia kwa uwajibikaji mkubwa ili kiweze kuleta matokeo mazuri.
Ndani ya kikundi kutakuwa na mpango wa kuweka akiba kwa pamoja na akiba hiyo kukopeshwa kwa wanachama kwa utaratibu ambao umewekwa. Hili litatengeneza fursa ya kupata mikopo yenye masharti nafuu, na kwa sababu mnajuana kama kikundi, fedha zinakuwa salama.

Nne ni SUPPORTIVE SERVICES.
Biashara siyo kisiwa, ili ifanikiwe inahitaji huduma mbalimbali ambazo ni muhimu.
Kuna uhitaji mkubwa wa huduma za kisheria katika mambo mbalimbali yanayoendelea kwenye biashara.
Kuna uhitaji wa huduma za kihasibu katika uendeshaji wa biashara.
Kuna uhitaji wa huduma mbalimbali za kibenki.
Kwa kuwa ndani ya hii huduma unapata watu wa uhakika wa kukupa huduma hizo za msingi na nyinginezo.

Tano ni PHILANTHROPY.
Lengo la kuwa bilionea siyo kwa sababu unayataka sana hayo mabilioni, bali kwa sababu unataka kuacha alama kwenye jamii, kupitia mchango chanja unaoutoa kupitia kile unachofanya, lakini pia kupitia matumi  sahihi ya fedha unazokuwa umezikusanya.
Huduma itakuwa na mfumo mzuri wa kutoa misaada kwa jamii, misaada yenye tija na inayoleta mabadiliko ya kudumu.
Misaada ambayo inamfundisha mtu jinsi ya kuvua samaki badala tu ya kumpa samaki.
Kutoa msaada wa chakula kwa watoto yatima ni msaada mzuri, lakini kuboresha huduma kama za elimu au afya ni msaada unaoleta matokeo ya muda mrefu na kwa wengi.
Ukiwa peke yako unaweza kuwasaidia yatima chakula na mavazi, ukiwa na wengine mnaweza kujenga shule au hospitali ambayo itawasaidia wengi kwa kipindi kirefu.

Sita ni STARTUP TOWN.
Kuna wazo nimekuwa nalo kwa muda mrefu, la kuwa na mji maalumu wa kijasiriamali, mji ambao unatengeneza fursa kwa yeyote anayeweza kujituma.
Nchi nyingi zina miji ya aina hiyo na imechochea sana ubunifu na ukuaji wa kiuchumi.
Hapa Tanzania tuna ardhi kubwa mno ambayo bado haijatumiwa.
Kuna mamilioni ya heka za ardhi ambayo hayajatumiwa kabisa.
Vipi kama tukapata angalau hela elfu moja tu na tukaweza kuanzisha mji wa tofauti na wa kipekee ambao utakuwa kitovu cha teknolojia na ujasiriamali?
Ni kitu kinachowezekana kabisa.
Hiki ni kitu tunaweza kukifanyia kazi kupitia klabu ya mabilionea.

Rafiki, unajionea mwenyewe jinsi mambo hayo yalivyo makubwa kabisa na ambayo kwa sasa unaweza kuona hayawezekani.
Ila mimi binafsi nilishafuta msamiati wa haiwezekani.
Najua inawezekana, ila inahitaji watu waliojitoa kweli na ambao hawawezi kuzuiwa na chochote.

Je wewe ni mmoja wa watu hao?
Kama jibu ni ndiyo, basi karibu kwenye mchujo.
Kama nilivyoeleza hapo juu, mchujo ni mkali, ili tuweze kupata watu waliojitoa kweli kupata nafasi hii na kuitendea haki.

Mchujo utakuwa na hatua tatu;

Hatua ya kwanza ni kujaza fomu yenye maswali ya kina kukuhusu wewe na biashara yako.

Hatua ya pili ni mahojiano ya kina kwa wale ambao wamevuka mchujo wa fomu.
Kama hutavuka mchujo utapewa sababu na hatua za kuchukua kama kweli unaitaka nafasi.

Katika hatua hizo mbili watapatikana wale wanaokidhi vigezo vya kupata huduma hiyo na kisha kukutana pamoja kwa ajili ya taratibu mbalimbali za kuanza huduma.

Mchakato utakwenda kwa ratiba hii.

1. Kujaza fomu ya maelezo ya kina yanayohitajika kwenye huduma hii, kuanzia tarehe 20/08/2021 mpaka tarehe 31/08/2021. Kujaza fomu fungua; https://bit.ly/kisimainfo

2. Mchujo wa maelezo ya fomu kuanzia tarehe 01/09/2021 mpaka tarehe 10/09/2021.

3. Mahojiano ya kina na waliovuka mchujo kuanzia tarehe 11/09/2021 mpaka tarehe 20/09/2021.

4. Kupewa taarifa kwa waliopata nafasi pamoja na kufahamishwa wanakikundi wenzake tarehe 21/09/2021 mpaka tarehe 30/09/2021.

5. Kukutana pamoja kwa walioingia kwenye huduma, tarehe 18/10/2021, baada ya SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2021 itakayofanyika Dodoma.

Rafiki, kama umesoma na kuona huiwezi huduma hii, usivunjike moyo, karibu tuendelee na huduma nyingine ninazotoa ambazo unaweza kuzifanyia kazi kweli kweli.

Na kama umesoma na kuona upo tayari kwa hili, upo tayari kujisukuma kweli na kufanya makubwa,  basi umefika penyewe.
Chukua hatua sasa, kwa kujaza fomu ya taarifa zako kwa kufungua kiungo hiki; https://bit.ly/kisimainfo

Rafiki yako na mshirika wa karibu katika safari ya kuelekea kwenye ubilionea,
Muuza Matumaini Dr Makirita Amani.

Kama bado hujathibitisha kushiriki SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2021 fanya hivyo sasa ili usikose nafasi hii ya kipekee.