Rafiki yangu mpendwa,
Bill Gates ajaye hataanzisha Microsoft.
Mark Zuckerberg ajaye hataanzisha Facebook.
Elon Musk ajaye hataanzisha Tesla.
Na Bakhresa ajaye hataanzisha Azam.

Lakini ni vitu gani ambavyo watu wapo ‘bize’ kufanya?
Kuiga wale waliofanikiwa, kufanya kama walivyofanya wao wakiona hiyo ndiyo kanuni ya mafanikio.

Kuna vitu ukiiga kwenye maisha unaweza kupata matokeo kama ya wengine.
Kujifunza, afya, mahusiano na kadhalika ni vitu ambavyo unaweza kuiga kwa wengine.

Lakini inapokuja kwenye ujasiriamali, kuiga ni njia ya uhakika ya kushindwa.

Kila wazo la kibunifu la ujasiriamali huwa linatokea mara moja tu, na yule anayelifanyia kazi vizuri wazo hilo na kuteka soko, ndiye anayenufaika zaidi.

Biashara nyingi mpya zimekuwa zinashindwa kwa sababu haziji na wazo lolote jipya na la kibunifu, bali zinaiga wazo ambalo tayari limeshafanyiwa kazi.

Bilionea Peter Thiel kwenye kitabu chake kinachoitwa Zero To One amezigawa biashara mpya katika makundi mawili.

Kundi la kwanza ni biashara zinazotoka sifuri kwenda moja. Hizi ni biashara zinazotokana na wazo jipya kabisa na kuleta uvumbuzi mpya.
Kwa jina jingine anaita hilo ni TEKNOLOJIA.

Kundi la pili ni biashara zinazotoka moja kwenda namba kubwa zaidi. Hizi ni biashara ambazo zinaiga wazo ambalo limeshafanya kazi na kulikuwa zaidi.
Kwa jina jingine anaita hili ni UTANDAWAZI.

Kutoka sifuri kwenda moja ndipo penye manufaa makubwa.
Kutoka moja kwenda namba kubwa zaidi kuna manufaa pia.

Thiel ametumia mfano wa taifa la China, lipo vizuri sana kwenye kuiga vitu vinavyofanyika kwenye taifa la Marekani, ila halipo vizuri kuja na teknolojia mpya.

Ukiangalia mfano wa simu za IPhone, japo kwa sehemu kubwa zinazalishwa nchini China, faida kubwa wanaipata Wamarekani kwa sababu ndiyo wenye hatimiliki ya bidhaa hiyo.

Tutoke kwenye mifano mikubwa na tuje kwenye mifano ya maisha yetu ya kila siku.
Angalia eneo lolote lile, mtu akiona fursa nzuri na kufungua biashara mpya ambayo haikuwepo kabisa, anaanza kupata faida nzuri.

Haichukui muda mrefu unakuta wengi zaidi nao wamefungua biashara ya aina hiyo hiyo, kwenye eneo hilo hilo na wanaanza kunyang’anyana wateja. Inakuwa ndiyo fursa ya moto na hakuna anayetaka kupitwa nayo.

Kinachotokea ni wengi wanaokimbilia kwenye fursa hiyo mpya wanaishia kushindwa vibaya. Wanabaki wakilaumu wamedanganywa kuhusu fikra, badala ya kuona wazi kilichofanya washindwe ni kuiga na kujipeleka kwenye ushindani mkali.

Angalia kwenye kila eneo au fursa mpya ya kibiashara inayokuja, na utaona picha hiyo ikiendelea kujirudia rudia kila wakati.
Lakini bado watu hawakomi.

Na sababu kubwa ni watu kupenda kutafuniwa ili wao wameze tu, hawataki ugumu.

Ingia kwenye mtandao wowote au majadiliano wanayokuwa nayo watu na hutakosa swali hili; biashara gani nzuri naweza kufanya kwa mtaji XXX ambayo haitanisumbua na ina faida kubwa na ya haraka?

Kila ninaposikia swali la aina hiyo au mtu akiomba ushauri kwenye hilo huwa najisikia hata kucheka.
Hivi kweli unafikiri biashara ya aina hiyo ingekuwepo ingekuwa imekaa tu kukusubiri wewe?

Rafiki, tukirudi kwa Peter Thiel na kitabu chake cha Zero To One, anatuonyesha jinsi tunavyoweza kuwa wabunifu na kuzitumia changamoto zinazotuzunguka kuja na mawazo ya kibunifu ya kibiashara.
Kuweza kuja na wazo jipya kabisa ambalo halijawahi kufanyiwa kazi kabisa na hivyo kuwa tofauti.

Lakini je utawazuiaje watu wasiige wazo lako? Maana watu wakiona kitu kinalipa, lazima tu watakiiga.

Kwenye kitabu hicho Thiel anatufundisha kitu kingine muhimu mno ambacho ni kuepuka kushindana. Anasema wazi kwamba kushindana ni kuchagua kushindwa.
Hakuna mashindao ya kibiashara ambayo yamewahi kufaidisha biashara, anayefaidi ni mteja huku biashara zikiumia.

Hivyo anapendekeza mtu unapokuja na wazo la kipekee la biashara, ujijengee ukiritimba (monopoly). Yaani uweze kuhodhi soko lako kiasi kwamba mtu mwingine hapati nafasi ya kuingia.

Kwenye uchumi huria kuhodhi soko ni kitu kinachopewa picha mbaya na kuzuiwa na kila aina ya sheria.
Lakini jua wazi huwezi kupata mafanikio makubwa kibiashara kama hutaweza kulihodhi soko lako.

Yapo mengi mno ya kujifunza kuhusu kuanzisha na kukuza biashara yenye mafanikio kutoka kwenye kitabu cha Zero To One.
Ni kwa sababu hiyo tutakuwa na mjadala wa moja kwa moja wa kitabu hicho kwenye channel ya Telegram ya SOMA VITABU TANZANIA.

Mjadala utafanyika siku ya jumapili ya tarehe 22/08/2021 kuanzia saa mbili usiku saa za Afrika Mashariki.
Kupata nafasi ya kushiriki mjadala huo unapaswa kuwa umejiunga kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA.

Kama bado hujajiunga na channel, wasiliana na namba 0717 396 253 kwa telegram ili uweze kuunganishwa.

Kwa zama tunazoishi sasa, biashara ndiyo njia ya uhakika ya kuingiza kipato na kupata mafanikio makubwa.
Lakini kufanya tu biashara kwa kuiga, ni kujipeleka kwenye shimo la kushindwa.
Karibu kwenye mjadala wa kitabu cha Zero To One ujifunze misingi sahihi ya kuanzisha biashara itakayokuwa ya kipekee na kukufikisha kwenye mafanikio makubwa.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani
http://www.somavitabu.co.tz