Rafiki yangu mpendwa,

Mwanzo wa mwaka wowote ule watu huwa na malengo na mipango mingi mizuri.

Wanakuwa na shauku na hamasa kubwa kwamba huo ni mwaka wao wa kufanya makubwa.

Lakini imekuwa haichukui muda mrefu, watu wanasahau yote hayo na kurudi kwenye mazoea ya zamani.

Hicho ndiyo kimekuwa kifo cha ndoto za wengi na kufanya watu wabaki pale walipo miaka na miaka bila kupiga hatua.

Leo nataka kusema na wale waliopanga kuanza biashara mwaka huu.

Iwe umeweza kuanza kweli au umeshindwa kuanza, kuna mambo matano muhimu kabisa natama uyazingatie kwa mwaka huu mzima na hutabaki pale ulipo sasa.

Moja; mtaji tayari unao.

Kuna kauli fupi sana niliwahi kujifunza mahali ambayo imekuwa majibu sahihi kwenye maeneo mengi.

Kauli hiyo inasema; “Kama huna fedha wekeza muda na kama huna muda wekeza fedha.”

Kauli hiyo ni jibu kwenye kuanza na kukuza biashara pia. Kama huna mtaji fedha, una mtaji muda, mtaji nguvu, mtaji uzoefu na mitaji ya aina nyingine nyingi.

Chagua chochote ulichonacho sasa na kifanye ndiyo mtaji wa biashara yako. Chochote kile, hata wafuasi ulionao kwenye mitandao ya kijamii au namba ulizonazo kwenye simu yako, ni mtaji tosha.

Mbili; anza na kuuza.

Unaweza kuhangaika sana na wazo gani la biashara ni zuri au biashara gani inayolipa.

Hapa pia nataka nikusaidie uokoe muda wako, wazo zuri la biashara ba biashara inayolipa ni mahitaji ambayo tayari watu wanayo.

Hivyo angalia ni vitu gani ambavyo watu tayari wana uhitaji navyo na anza kuwauzia. Usisubiri mpaka uwe na eneo la kufanya hivyo, tumia simu yako, tumia mitandao ya kijamii, nenda mtu kwa mtu au vyovyote vile, muhimu ni uweze kuuza.

Hapa kuna kauli nyingine muhimu itakayokusaidia sana inayosema; “Usitengeneze funguo kisha kutafuta kufuli la kufungua, badala yake tafuta kufuli lililofungwa kisha tengenezea ufunguo”.

Kama huwezi kuwashawishi watu wanunue, haijalishi wazo ni zuri kiasi gani, biashara haiwezi kwenda vizuri.

Tatu; mteja ni mfalme.

Una wafalme wawili kwenye biashara, ambao unapaswa kuwatii wakati wote.

Mfalme wa kwanza ni mteja.
Huyu huwa yuko sahihi mara zote hivyo hakikisha unakwenda naye vizuri.

Wajali sana wateja wako na wape huduma bora kabisa.

Nenda hatua ya ziada kwa kuwapa thamani kubwa kuliko wanavyotegemea.

Hakuna hazina nzuri kwenye biashara kama mteja aliyeridhika, kwa sababu;

1. Mteja aliyeridhika ataendelea kununua. Ni rahisi kumuuzia mteja ambaye alishanunua kuliko mpya.

2. Mteja aliyeridhika atawaambia wengine kuhusu biashara yako. Njia ya wateja kuambiana ina nguvu kuliko njia nyingine yoyote ya masoko.

Mteja ni mfalme, jikumbushe hili kila mara na uwahudumie vizuri wateja wako.

Nne; faida ni mfalme.

Unakumbuka nimekuambia una wafalme wawili kwenye biashara?
Wa kwanza ni mteja na wa pili ni faida.

Faida ni mfalme ambaye unapaswa kumtukuza kwenye biashara.
Maana haijalishi una wateja wengi kiasi gani na unauza kiasi gani, kama hutengenezi faida, biashara itakufa.

Hivyo hakikisha unajua jinsi ya kukokotoa faida kwenye biashara yako na uweze kuiona hiyo faida kweli.

Kama huwezi kukokotoa faida au kama ukiikokotoa haionekani, kuna shida kubwa kwenye hiyo biashara.
Itatue shida hiyo mapema kabla haijaleta majanga makubwa.

Tano; kujifunza ni endelevu.

Kama ulipokuwa shuleni ulisubiri kwa hamu kuhitimu ili uachane na mambo ya kujifunza, jua ulikuwa unajifanganya.

Unapoingia kwenye biashara umeingia kwenye darasa lisilo na ukomo.
Kuna mengi usiyojua ambayo utasukumwa kujifunza.
Na kadiri unavyojifunza ndivyo unaona jinsi gani hujui mengi zaidi.

Kuna maeneo mengi ya kujifunza, lakini haya matatu ni muhimu kama kweli umejitoa kwenye biashara na unataka kufanikiwa;

1. Soma angalau kitabu kimoja kila wiki. Ndiyo, kitabu kimoja kila wiki, umesoma kwa usahihi kabisa.

2. Hudhuria mikutano, semina na mafunzo mbalimbali ya biashara.

3. Kuwa na kocha anayekusimamia kwa karibu kabisa na unayefanya naye kazi kwa muda mrefu.

Mambo hayo matatu siyo lazima, lakini ni ya msingi kabisa kama unataka mafanikio makubwa kwenye biashara.

Kama umeyasoma na kujiambia haya siyawezi, uko sahihi kabisa, maana yake ni kwamba huwezi kupata mafanikio makubwa kwenye biashara.

Kama unakubaliana na hilo hakuna tatizo, endelea na mambo yako ya kawaida.

Lakini kama unataka zaidi, lazima pia uwe tayari kufanya zaidi.

Rasilimali muhimu;
1. Vitabu vya kusoma, ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA na BIASHARA NDANI YA AJIRA kuvipata wasiliana na 0752 977 170.

2. Huduma ya ukocha wa biashara, kuipata wasiliana na 0717396253.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr. Makirita Amani.