Kila mmoja wetu bila ya kujali kipato chake anaweza kuwa tajiri kama ataweza kufuata sheria hii moja ambayo ni rahisi sana. Japokuwa ukisikia neno kuwa tajiri unaona kama ni kitu ambacho sio kizuri, maisha yako yote unahangaika ili uwe tajiri au ufikie uhuru wa kifedha. Na kwa kuwa umeshachagua kuwa WORLD CLASS PERFORMER tayari umeshajihakikishia kuwa tajiri. Nasema umeshajihakikishia kwa sababu unapofanya kitu kwa upekee na utofauti una nafasi kubwa sana ya kufikia mafanikio makubwa.

Sasa leo tutaangalia sheria moja rahisi sana ambayo itakuwezesha kufikia uhuru wa kifedha na kuwa na maisha mazuri. Sheria hii kama nilivyosema hapo juu ni rahisi sana na inaweza kutumiwa na mtu yeyote bila ya kujali kipato chake au hata elimu yake. Kwa kujifunza sheria hii na kuanza kuitumia mara moja miaka michache ijayo utaona mabadiliko makubwa sana.

Sheria hii inasema tumia kidogo ukilinganisha na kile unachopata.

Ni sheria rahisi sana, imekuwepo toka enzi na enzi lakini bado imekuwa ni ngumu sana kuifuata. Kila mtu anajua kwamba ni muhimu kutumia kidogo zaidi ya unachopata na kile kinachobaki unaweka akiba. Lakini maisha ya sasa ambapo mtu anaweza kukopa yanarahisisha sana mtu kuweza kutumia zaidi ya kile anachopata. Pia maisha haya yaliyojaa mashindano yanamfanya mtu kufanya matumizi makubwa zaidi ya kipato chake.

Sasa leo tutajadili hili na sio kwamba nitakukataza usifanye matumizi kwa fedha zako bali nitakuonesha njia nzuri ya kufanya matumizi yako.

Hatua mbili za kutekeleza sheria hii kwenye maisha yako.

Hatua ya kwanza; Jua ni kiasi gani cha fedha unapata kila mwezi.

Kabla hujaweka utaratibu wa kutumia kidogo zaidi ya unachopata, ni vyema kujua ni kiasi gani unapata. Kujua ni kiasi gani unapata kaa chini na ujue vyanzo vyako vya mapato na uandike ni kiasi gani unapata kila mwezi. Kama vipato vya kila mwezi havilingani, chukua wastani wa vipato vya miezi michache iliyopita au chukua kipato kidogo.

Hatua ya pili; Weka kiwango cha juu cha matumizi.

Baada ya kujua ni kiasi gani cha fedha unachopata kila mwezi, weka kiwango cha juu cha matumizi unayoweza kufanya kwa mwezi mzima. Kiwango hicho kiwe chini ya kipato chako. Katika hatua hii kuna mambo mengi sana itabidi uyabadili. Unaweza kufanya mabadiliko mawili makuu;

1. Kupunguza matumizi yako.

Hapa utabadili kabisa mfumo wako wa maisha, kama ulikuwa unafanya starehe inabidi kupunguza sana au kuacha kabisa, kama ulikuwa unafanya manunuzi holela ya vitu ambavyo sio vya lazima inabidi kuacha kabisa. Kwa hatua hii unahakikisha matumizi ya fedha unayofanya ni yale ambayo ni ya muhimu kabisa kwa maisha kuendelea.

2. Ongeza kipato chako.

Kama matumizi yako yote ni ya msingi na bado yanazidi kipato chako chaguo pekee ulilonalo ni kuongeza kipato chako. Kila mtu anaweza kuongeza kipato chake tofauti na kilivyo sasa. Kama umejiajiri au unafanya biashara unaweza kujifunza mbinu bora zaidi za kukuza kipato chako na kuanza  kuzitekeleza. Kama umeajiriwa unaweza kufanya kazi kwa ubunifu zaidi ili kuongeza uwezo wako wa kulipwa zaidi au kutafuta kitu cha ziada cha kufanya ambacho kitakupatia kipato zaidi. Usiseme huna muda wa kufanya kitu cha ziada kutokana na kazi uliyonayo sasa, maana kwa siku yenye masaa 24, unafanya kazi masaa 8 na unalala masaa 8 sasa niambie hayo mengine 8 unayatumia kufanya nini?

Kwa vyovyote vile utakavyofanya hakikisha unatumia kidogo ukilinganisha na kile unachopata. Kaa chini leo na ufanye kazi yako ya kujua ni kiasi gani unapata na kiasi gani utatumia. Anza utekelezaji huo mara moja. Najua unaweza na najua miaka michache ijayo hali yako ya kifedha itakuwa nzuri sana.

Nakutakia kila la kheri katika mipango yako ya kufikia uhuru wa kifedha.

TUKO PAMOJA.