Mpendwa msomaji na mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA karbu kwenye huu utaratibu wa kujijengea tabia za mafanikio. Katika utaratibu huu kila mwezi tunajadili tabia moja muhimu ili kuweza kufikia malengo tuliyojiwekea na kufanikiwa. Ni ukweli usiopingika kwamba mafanikio hayaji kwa bahati mbaya. Mafanikio yanatengenezwa kidogo kidogo kulingana na tabia za mtu.

Tatizo kubwa linalosababisha watu wengi hawafanikiwi ni kukosa tabia za mafanikio. Mtu anaweza kuwa na malengo mazuri, kufanya kazi kwa bidii ila kwa kukosa tabia muhimu za mafanikio akashindwa kufikia malengo aliyojiwekea.

Mwezi huu wa sita tutajadili na kujijengea tabia ya kujisomea na kujifunza binafsi. Hii ni tabia huhimu sana ili kuweza kufikia mafanikio kwenye jambo lolote unalofanya. Kama ilivyo utaratibu wetu katika kujenga tabia, kila siku ya jumanne kunakuwa na makala moja inayozungumzia tabia tunayojenga kwenye mwezi husika na mwisho wa makala kunakuwa na zoezi la kufanya.

Katika utaratibu huu wa kujisomea kila wiki nitakuwa natoa kitabu kimoja cha kujisomea na kutoa mchanganuo wa jinsi ya kusoma kitabu hiko. Kwa hiyo mpaka tunamaliza mwezi huu utakuwa umesoma vitabu vinne kama utakuwa unazingatia mafundisho haya. Kama ukiweza kusoma vitabu hivi maisha yako yatabadilika kwa kiwango kikubwa sana kwani vitabu nitakavyotoa ni vitabu vya kubadili mitazamo na fikra hasi juu ya maisha.

Kabla hatujaanza naomba nitoe ushahidi wangu mwenyewe ni jinsi gani tabia ya kujisomea ilivyoboresha maisha yangu.

Mwaka 2011 nilijikuta katika wakati mgumu sana kwenye maisha yangu baada ya kusimamishwa chuo kikuu kwa muda usiojulikana. Baada ya kupewa barua ya kuondoka chuoni haraka, niliingia mtaani nikiwa sina mbele wala nyuma. Lakini kwa kuwa nilishazoea kujishughulisha kwa shughuli mbalimbali nilianza kujishughulisha mtaani ili maisha yaweze kuendelea.

Mwanzoni mwa mwaka 2012 niliamua kuanza kujifunza vitu vya ziada ili niweze kuongeza ufahamu wangu na fursa za kutengeneza kipato cha ziada. Kwa kuwa nilikuwa mpenzi na mtumiaji mkubwa wa kompyuta niliamua kujifunza IT(Information Technology). Nadhani unajua kozi hii inafundishwa vyuoni, tena sana sana vyuo vikuu, lakini mimi nilianza kujifunza mwenyewe kwa kutumia kompyuta yangu na mtandao wa intanet. Nilidownload vitabu vya pdf, video na material mengine muhimu kwa ajili ya kujifunza mambo haya. Baada ya miezi sita nilikuwa nimeshajifunza vitu vifuatavyo; Website designing, Graphics design na Java programing. Kwenye Graphics design nilijifunza kutumia adobe photoshop, adobe dreamweaver, adobe fireworks na adobe illustrator.

Baada ya hapo nikajifunza sales na marketing. Nilijifunza kwa kusikiliza vitabu na kusoma vitabu zaidi ya kumi vinavyohusiana na sales na pia vinavyohusiana na marketing. Kupitia ujuzi wa sales niliojifunza nilielewa ni jinsi gani ulimwengu wa biashara unavyokwenda na ni vitu gani vinawafanya watu kununua au kutonunua bidhaa. Pia kwenye marketing nilijifunza mbinu mbalimbali za kutafuta masoko ya bidhaa au huduma yoyote, jinsi gani ya kuweza kutengeneza soko hata sehemu ambayo inaonekana haiwezi kuwa na soko. Nilijifunza kwa nini baadhi ya bidhaa zinafanikiwa sana sokoni na kwa nini bidhaa nyingine zinashindwa kuhumili mkikimkiki wa soko.

Wakati huo huo nikawa najisomea na kusikiliza vitabu vya maendeleo binafsi(personal development). Hivi viliniwezesha kubadili mtazamo wangu na kuniwezesha kujiamini na kuweza kufanya kile nachofikiria kufanya bila ya kuogopa pale wengine wanaponikatisha tamaa. Hapa nimesikiliza na kusoma zaidi ya vitabu mia moja kutoka kwa wahamasishaji maarufu kama Antony Robins, Zig Zigler, Brian Tracy, Les Brown, Earl Nightngale, Robert Kiyosaki, Donald Trumph, John Maxwell, Napoleon Hill na wengine wengi.

Pia nikajisomea na kujifunza kuhusu uongozi, kitu ambacho bado naendelea kujifunza mpaka sasa. Katika kujifunza mambo ya uongozi nimejua ya kwamba kwenye kila nyanja ya maisha wanaofanikiwa ni wale wenye tabia za uongozi. Wanaokuwa wazazi bora, wafanyabiashara bora, wanaofanikiwa kwenye ujasiriamali na hata wafanyakazi bora wote wanasifa moja ya kuwa na tabia za uongozi.

Pia nimejifunza na naendelea kujifunza uandishi wa makala bora na vitabu.

Mwaka 2012 nilikuwa nasoma vitabu vingi niwezavyo ndani ya muda wowote ninaokuwa nao, hivyo kwa mwaka ule nilisoma na kusikiliza vitabu zaidi ya 120.

Mwaka 2013 nilipanga kusoma vitabu viwili kila wiki na kwa mwaka huo nilisoma na kusikiliza vitabu zaidi ya 70.

Mwaka huu 2014 nimepanga kusoma kitabu kimoja kila wiki na ni wiki chache ambazo sikumaliza kusoma kitabu.

Tabia hii ya kujisomea imenisaidia nini?

Labda unajiuliza kwa kusoma mavitabu yote haya nimefaidika nini? Jibu ni kwamba maisha yangu nayaendesha kwa ujuzi nilioupata kutokana na kujisomea vitu hivi mbalimbali. Kuanzia katikati ya mwaka 2013 mpaka sasa na kuendelea sehemu kubwa ya kipato cha kuendesha maisha yangu na familia yangu nakipata kwa ujuzi niliojifunza kutokana na kujisomea.

Nafanya biashara za kawaida, biashara za kwenye mtandao wa intanet(intanet marketing), naendesha blog nne, natengeneza na kurekebisha blogs na website na pia nafanya shughuli nyingine mbalimbali. Yote haya sikuwahi kufundishwa na mtu yeyote, hata kuwasha kompyuta sikuwahi kufundishwa. Ni tabia yangu ya kupenda kujisomea ndiyo iliyoniwezesha kufanya yote haya.

Hata wewe unaweza kunufaika na tabia hii.

Nakueleza yote haya ili kama na wewe ukipenda kuboresha maisha yako uweze kujijengea tabia ya kujisomea na kujifunza wenyewe.

Hata wewe unaweza kunufaika sana na tabia hii ya kujisomea kama utaweza kuijenga kwako.

Kwa kuwa hii ni tabia hivyo inahitaji kujengwa. Inawezekana unapenda sana kujisomea ila kila ukijaribu unashindwa. Au unapenda kujisomea ila unaona huna muda wa kutosha kufanya hivyo.

Katika ulimwengu wa sasa ambapo ajira zimekuwa ngumu kupatikana na hata kufanya ni muhimu sana kujifunza vitu vya ziada.

Nakutakia kila la kheri kwenye harakati zako za kuboresha maisha yako.

TUKO PAMOJA.