Ili uweze kuishi maisha ya mafanikio, ni muhimu kwako kuishi maisha ambayo yanaendana mkabala na kile unachokihitaji katika maisha yako na sio kinyume chake. Haiwezekani kwako ukafanikiwa kama utaendelea kuishi kiholela, kuishi maisha ambayo hayakufikishi kwenye ndoto na malengo yako uliyojiwekea, halafu ukawa unadai mafanikio hiyo itakuwa sawa na kujidanganya wewe mwenyewe.
Ni muhimu sana kujua na kutambua kuwa ili tuweze kufanikiwa ni lazima kuacha tabia zetu za kale zilizotukwamisha na kufanya mambo ambayo yatatufikisha kwenye mafanikio ya kweli na sio kuturudisha nyuma. Unapofanya mambo haya, utajikuta unafanikiwa kwa sababu yatakupa hamasa ya kusonga mbele zaidi. Kama unafanya  mambo haya katika maisha yako, ni lazima ufanikiwe.

1. Kama unaishi kwa mipango na malengo. 
Mafanikio katika maisha yako yanajengwa kwa kuwa na mipango imara unayojiwekea kila wakati na hayaji hata kidogo kwa bahati mbaya. Watu wengi huwa hawana mipango ya kuwaongoza na kutegemea mafanikio, ambayo kiuhalisia hawawezi kuyapata. Kama wewe ni mtu wa kujiwekea mipango na malengo katika maisha yako ni lazima ufanikiwe. Huu ndio ukweli ambao huwezi kuupinga, utayafikia mafanikio yako tu kama utachukua hatua muhimu ya kujiwekea mipango na malengo yako.

SOMA; Jinsi Ya Kuweka Malengo Utakayoyafikia.

   
 
2. Kama unaianza siku yako mapema.
Utakuwa unauwezo mkubwa wa kujenga mafanikio makubwa katika maisha yako, kama utakuwa unaishi maisha ya kuanza kuipangilia siku yako mapema kila siku. Utaweza kufanya hili kama utakuwa unamudu kuamka asubuhi na mapema na kuweza kutafakari na kupitia malengo ya maisha yako na kuweza kujua wapi umefikia na wapi unapoelekea. Unapoamka asubuhi na mapema akili yako inakuwa imetulia na inakuwa na uwezo mkubwa wa kutafakari tofauti na muda mwingine.

SOMA; Saa Moja Ya Maajabu Maishani Mwako.

3. Kama unamahusiano mazuri na wengine. 
Kuna wakati katika maisha yako ili uweze kufanikiwa ni lazima uwe na mahusiano mazuri na watu wanaokuzunguka. Unaweza ukawa na pesa lakini haziwezi kukusaidia kama utakuwa unaishi na watu wanaokuzunguka vibaya. Watu hawa mara nyingi ndio watakusaidia wewe kukupa taaarifa sahihi zitakazo weza kukufanikisha kwa kile unachofanya. Kumbuka, tunaishi katika ulimwengu wa taarifa, kwa kadri unavyojua taarifa sahihi ndivyo unavyozidi kufanikiwa. Kama una mahusiano mabovu itakuwa ngumu kwako kupata taarifa sahihi za kukufanikisha.

SOMA; Haijalishi Unajua Nini Bali Unamjua Nani.

4. Kama utaishi maisha ya kuwasadia wengine. 
Utaweza kufikia mafanikio makubwa sana katika maisha yako kama utakuwa unawasidia wengine nao kufikia mafanikio yao. Simaanishi uwe unatoa pesa tu ndio ieleweke umetoa msaada, hapana. Ipo namna nyingi ambapo unaweza ukafanya hili hata kwa kutoa msaada wa mawazo na mchango wako kwa jamii huo nao ni msaada tosha wa kuweza kuisadia jamii unayoishi. Kama unajua unaishi maisha ya kuwasadia wengine kwa namna moja au nyingine ili waweze kufikia ndoto zao, mafanikio kwako ni lazima.

SOMA; Vitu Vitatu Ambavyo Ukivitoa Utawasaidia Wengi Na Hutopungukiwa Navyo.

5. Kama utaishi bila ya kukata tamaa mapema. 
Kati ya kitu ambacho hutakiwi kukipoteza katika safari ya mafanikio ni matumaini ya kile unachokifanya. Unapokosa tumaini katika maisha yako, hakuna tena kinachoendelea kwako, mwisho wa siku utajikuta unakata tamaa na kupoteza kila kitu. Kumbuka, katika maisha yetu hatufanikiwi sana sio kwa sababu tunaweza sana au sio kwa sababu hatukutani na vikwazo na majaribu, hapana. Tunafanikiwa kwa sababu ya kuwa na nguvu ya kuvumilia kila aina ya changamoto tunazokutana nazo. Kama unaishi kwa uvumilivu kuelekea katika ndoto zako, mafanikio kwako ni lazima.

SOMA; Kabla Hujakata Tamaa Kwa Wazo Lako Kubwa.

6. Kama unaishi kwa kung’ang’ania ndoto zako. 
Ili uweze kufikia mafanikio unayoyataka unalazimika kujifunza kuwa king’ang’azi wa ndoto zako na kuhakikisha mpaka zinatimia. Usiache kitu chochote kikakuzuia kuelekea kwenye malengo na mipango yako. Hapa inatakiwa kujifunza kuwa mbishi kwa kufanya lolote lile linawezekana mpaka kuona malengo yako yanatimia. Kama kuna wakati unaona maisha yako yamepinda na hayako sawa kama unavyotaka na wewe unalazimika upinde ili mwende sawa, vinginevyo utaendelea kulaumu maisha magumu. Hakikisha unang’ang’ania ndoto zako mpaka unaona matokeo unayoyataka.

SOMA; Mambo 15 YaKung’ang’ania Bila Kujali Watu Wanasema Nini.

7. Kama utakuwa na nidhamu binafsi. 
Hiki ndicho kitu muhimu unachotakiwa kuwa nacho ili uweze kufanikiwa. Bila kuwa na nidhamu binafsi hauwezi kufanikisha kitu chochote katika maisha yako. Hii ni tabia ya kujifunza ambayo inauwezo wa kukufanya ukafikia mafanikio makubwa unayoyataka katika maisha yako. Watu wengi wameshindwa kufikia mafanikio makubwa kwa yale wanayoyafanya kwa sababu ya kukosa nidhamu binafsi katika maisha yao. Kujifunza zaidi kwa undani juu ya  nidhamu binafsi, hakikisha unajiunga leo  na KISIMA CHA MAARIFA.

SOMA; Kama Umekosa Tabia Hii Moja, Sahau Kuhusu MAFANIKIO MAKUBWA.

8. Kama utajifunza kusema HAPANA. 
Wapo watu ambao katika maisha yao ni watu wakukubali kila kitu hata kwa mambo yanayowaumiza wao wenyewe. Kama unataka kufanikiwa katika maisha yako jifunze kusema HAPANA kwa mambo ambayo unaona hayawezi kukusaidia. Unapojifunza kusema HAPANA sio lazima kwa mambo mabaya tu, hata kwa mambo mazuri jifunze kusema HAPANA  kama yapo nje ya malengo yako. Sio kila kitu unatakiwa kukifanya katika maisha yako hata kama ni kizuri. Jifunze kusema hapana utafanikisha mambo mengi katika maisha yako.

SOMA; Mambo 30 Ya Kusema Hapana Mwaka Huu 2015…

9. Kama unatunza muda wako vizuri. 
Maisha yako yatakuwa ya mafanikio sana kama unatunza muda wako vizuri. Muda katika maisha yako ni kila kitu. Unaweza ukapoteza pesa katika maisha yako ukazipata lakini sio muda ukipotea  umepotea. Kwa kadri unavyotunza na kutumia muda wako vizuri unakuwa unauwezo mkubwa wa kufikia mafanikio yako makubwa unayoyataka. Mafanikio yote yaliyopo kwenye maisha yako yamefungwa kwenye muda. Kama unaishi maisha ya kupoteza muda sana ujue ndio unapoteza mafanikio yako siku hadi siku.

SOMA; Hivi Ndivyo VituVinavyokupotezea Muda Sana Katika Maisha Yako.

10. Kama unaishi maisha bila ya kulaumu. 
Watu wengi wanashindwa kufanikiwa kutokana na kuwa na tabia ya kulaumu sana wengine kuwa ndio wamesababisha maisha yao yawe magumu. Unapolaumu unakuwa unashindwa kuchukua jukumu zima la kuwajibika juu ya maisha yako. Ili uweze kufanikiwa na kufikia ndoto zako acha kulaumu, chukua hatua juu ya maisha yako.

SOMA; Hiki Ndicho Kitu Kinachokupotezea Mafanikio Makubwa Unayoyataka Katika Maisha Yako.

Nafasi ya kufanikiwa na kujenga mafanikio unayoyataka katika maisha yako unayo, chukua hatua juu ya maisha yako na fanya mambo hayo ili yakuletee mafanikio makubwa unayoyahitaji.

Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kujifunza na kuboresha maisha yako kila siku.

Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatemblea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika kila siku.

IMANI NGWANGWALU,

0713048035/dirayamafanikio@gmail.com