Habari njema Matajiri Wawekezaji,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo ya uwekezaji kutoka kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU. Lengo letu ni kujenga utajiri na uhuru wa kifedha kupitia uwekezaji wa kiasi kidogo kidogo, kwa muda mrefu bila kuacha.

Kwa masomo ambayo tumeshayapata mpaka sasa kuhusu utajiri na uwekezaji, tunaona wazi kabisa kwamba kila mtu, bila ya kujali ni kipato kiasi gani anaingiza, anaweza kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yake.

Tumejifunza jinsi ambavyo nguvu kubwa ya uwekezaji ipo kwenye muda na siyo kiasi. Na kwenye muda ni pale uwekezaji unapofanyika kwa msimamo bila ya kuingiliwa.

Kwa mfano kwa kiasi cha chini cha kuweka pembeni elfu 1 tu kwa siku na kuwekeza, ambapo kwa mwezi itakuwa elfu 30, hivi ndivyo utajiri unavyokua kwa vipindi tofauti;

Mwaka mmoja = 376,967.04

Miaka 5 = 2,323,112.17

Miaka 10 = 6,145,349.37

Miaka 20 = 11,282,858.99

Miaka 30 = 22,029,779.80

Miaka 40 = 45,135,747.91

Miaka 50 = 95,837,170.70

Hiyo ina maana, mtu akianza kuwekeza akiwa na umri wa miaka 20 au 30, anapofika miaka 70 au 80 anakuwa amekusanya utajiri wa Tsh milioni 95, hapo ni kwa kiwango kidogo sana, ambacho kila mtu anaweza. Na ni zaidi ya mafao ambayo mtu anaweza kuingiza kwenye kima cha chini cha mshahara.

Swali la kujiuliza ni kwa nini watu wengi hawafanyi uwekezaji, ambao upo ndani ya uwezo wao na una manufaa makubwa?

Jibu ni kukosa msimamo kwenye kuwekeza kwa muda mrefu bila kuacha.

Watu wengi huwa ni wepesi kwenye kuanza kufanya kitu, lakini kuwa na mwendelezo kwa muda mrefu, huwa hawawezi.

Watu huwa wanachoshwa haraka na kitu ambacho hakiwapi msisimko na kwenye maisha kitu cha muda mrefu hakiwezi kuwa na msisimko endelevu.

Usumbufu wa maisha pia huwa unawaondoa watu kwenye yale ya msingi wanayopaswa kufanya, ambayo hayaonekani kuwa na uharaka.

Hiyo ndiyo maana ni vigumu sana kwa mtu kuweza kufanya uwekezaji kwa muda mrefu na uendelevu bila kuacha.

SOMA; 3280; Kwa msimamo bila kuacha.

Kuna njia mbili za kuvuka changamoto hiyo;

Njia ya kwanza ni ya kufanya moja kwa moja.

Kwa njia hii, unaweka mfumo wa kufanya uwekezaji moja kwa moja. Njia hiyo inazuia udhaifu wako usikukwamishe kwenye uwekezaji.

Njia hii inafanya kazi pale kunapokuwa na njia za kuitekeleza, mfano kuweza kuweka maelekezo kwenye akaunti ya benki kufanya makato na kupeleka sehemu nyingine.

Kwa uwekezaji mkuu tunaofanya wa UTT AMIS, bado hakuna njia ya moja kwa moja ya kutoa kwenye mifumo mingine ya fedha tunayotumia. Hasa fedha za kwenye mitandao ya simu ambazo ndiyo wengi tunatumia.

Njia ya pili ni kutumia uwajibikaji wa kundi.

Kwa njia hii, unakuwa ndani ya kundi ambalo unaahidi kufanya kitu na kutoa ushahidi ndani ya kundi hilo.

Hiki ndiyo tunachofanya kwenye programu ya NGUVU YA BUKU, kwa kuwa ndani ya kundi ambalo lina watu wengine ambao nao wanafanya uwekezaji, unaahidi kufanya uwekezaji bila kuacha.

Ili njia ya uwajibikaji wa kundi ifanye kazi kwako, lazima kuwe na madhara unayoyapata pale unaposhindwa kutekeleza kama unavyoahidi. Madhara yanaweza kuwa chochote ambacho kitakuumiza na hivyo kusukumwa kufanya kukiepuka.

Pamoja na kuwa kwenye kundi, kama kufanya au kutokufanya hakuna tofauti yoyote, hutaweza kufaidi ile dhana ya kubanwa ili ufanye. Lazima kuwe na kitu kinachokusukuma ufanye bila kuacha kwa sababu usipofanya kuna madhara.

Kwa kuwa umeipata nafasi ya kuwa kwenye kundi, tumia uwajibikaji wa kundi ili ufanye uwekezaji kwa muda mrefu bila kuacha na uweze kunufaika sana.

Tayari unajua kwamba uwekezaji una manufaa, na tayari ipo ndani ya uwezo wako kuwekeza, hata kwa kiasi kidogo kabisa, usikubali tena kujikwamisha wewe mwenyewe.

Hata kama umepoteza miaka mingi bila kuanza uwekezaji, sasa umeshajua, hivyo wekeza kwa ukubwa kadiri ya unavyoweza ili kufidia muda ambao umepoteza huko nyuma.

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo, ushirikishe yale uliyojifunza kwa kujibu maswali yafuatayo;

1. Je ulishawahi kusikia kuhusu uwekezaji huko nyuma lakini hukuanza? Nini kilikuzuia? Na je uliwahi kuanza uwekezaji huko nyuma lakini ukaishia njiani? Nini kilipelekea uishie njiani?

2. Ni kwa namna gani kuwa kwenye programu hii ya NGUVU YA BUKU kumekuwezesha kuwekeza kwa msimamo bila kuacha? Nini kimebadilika na kukuwezesha kuwekeza kwa mwendelezo?

3. Nini ahadi yako kwenye kundi hili la NGUVU YA BUKU kuhusu kuwekeza kwa msimamo bila kuacha kwa miaka 10 ambayo tumejipa? Unachagua kupata adhabu gani pale unapoacha kuwekeza kama ulivyo mpango wa NGUVU YA BUKU?

4. Karibu uulize swali lolote ulilonalo kuhusu somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU.

Shirikisha majibu ya maswali hayo kama uthibitisho wa kusoma, kuelewa na kuwa tayari kutekeleza ili kujenga utajiri na uhuru wa kifedha.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.