#TANO ZA JUMA #15 2019; Ijue Asili Ya Binadamu, Sheria 18 Za Asili Ya Binadamu, Hatua 3 Za Kutawala Hisia Zako, Hisia Na Fedha Haviendani Na Wanachoonesha Watu Ndiyo Walichokosa.

Rafiki yangu mpendwa,

Hongera sana kwa juma hili la 15 la mwaka huu 2019, nina imani limekuwa juma bora sana kwako, ambalo umejifunza mengi, kufanya mengi na kuweza kujiandaa vyema kwa juma linalokuja.

Nachukua nafasi hii kukukaribisha kwenye makala ya tano za juma, ambapo nakushirikisha mambo matano muhimu ya kufanyia kazi ili maisha yako yaweze kuwa bora sana.

Juma hili la 15 tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kitabu kinachoitwa The Laws of Human Nature ambacho kimeandikwa na Robert Greene. Robert Green pia ni mwandishi wa vitabu maarufu kama 48 Laws of Power na Mastery, Green amekuwa na uandishi wa kipekee ambapo amekuwa akiangalia wale waliofanya makubwa kwenye historia au kushindwa vibaya na kuondoka na somo la kipi cha kufanya au kuacha kufanya.

laws of human nature

Kwenye kitabu chake cha Laws of Human Nature, Green ametupa sheria 18 za kuijua asili ya binadamu, akitupa mifano halisi iliyowahi kutokea kwa watu waliozingatia sheria hizi na wakafanikiwa au walizipuuza na kushindwa.

Laws of Human Nature ni kitabu ambacho kila mtu anapaswa kukisoma kwa sababu kimeeleza asili yetu binadamu tulivyo bila ya kuficha chochote. Tunaziona zetu halisi na hata za wengine, tunajifunza udhaifu mkubwa uliopo ndani yetu ambao unatufanya kushindwa kwenye mengi na pia tunajifunza jinsi ya kuvuka udhaifu tulionao ili tuweze kuwa na maisha bora na ya mafanikio.

Karibu kwenye tano za juma, tujifunze asili yetu, tujijue vizuri ili tuweze kuishi kwa ukamilifu na kutumia uwezo mkubwa uliopo ndani yetu kufanya makubwa zaidi.

#1 NENO LA JUMA; IJUE ASILI YA BINADAMU.

Asili ya binadamu ni kitu ambacho kila mmoja wetu angepaswa kuwa anakijua, kwa sababu ni kitu kinachotuhusu sisi wenyewe. Lakini jambo la kushangaza ni kwamba, hili ni eneo ambalo hatuna uelewa kabisa. Kwa kifupi hatujijui sisi wenyewe na wala hatuwajui wengine. Tunaishi maisha yetu kama watalii ambao wamejikuta kwenye miili yetu na tunaendeshwa tu na hisia bila ya kukaa chini na kufikiri kwa kina haya maisha yanatupeleka au tunayapeleka wapi.

Kitu kimoja ambacho kinatuzuia tusiijue asili yetu ni ubishi wetu, hatutaki kukubali kwamba hatujijui. Mfano najua unaposoma hapa unakataa kwamba wewe siyo mmoja wa wasiojijua, kwamba wewe unajijua vizuri.

Kama ndivyo nikuulize swali moja, je umewahi kuweka malengo na mipango mizuri, labda unajiambia kesho utaamka mapema na kutekeleza majukumu yako. Hiyo kesho muda wa kuamka unafika, lakini huamki, hata unapoamka unashindwa kutekeleza yale uliyopanga? Je unafikiri nini kinakwenda kinyume na malengo na mipango yako? Kama hujui basi huijui asili yako.

Kitu kingine; je umewahi kujiambia hutafanya kitu fulani, labda kumsema mtu vibaya, au kujihusisha na mahusiano fulani, au kudanganya. Lakini unakuja kujikuta umefanya, unapojiuliza unasema shetani alikupitia? Kama ndiyo basi jua huijui asili yako.

Cha mwisho muhimu zaidi; umewahi kumwamini mtu fulani, labda ni mwenza wako, au mtu unayefanya naye biashara, au kiongozi fulani, kwa nje anaonekana ni mwaminifu kabisa na unaweza kumtetea kwamba hawezi kufanya kitu cha ajabu. Lakini siku unakuta amefanya kitu ambacho hukutegemea afanye, unashtuka kwamba hukutegemea afanye hivyo. Kama umewahi kukutana na hali kama hii, basi huijui kabisa asili ya binadamu. Maana kama ungekuwa unaijua, ungeona dalili za yeye kufanya hivyo mapema kabla hajafanya. Kwa sababu kwanza, watu huwa hawafanyi kitu mara moja pekee, na pili watu wanaweza kuficha siri kwenye maneno, lakini matendo na lugha ya mwili inaeleza wazi kabisa.

Rafiki, kwa jinsi tunavyoona makosa tunayoyafanya kila siku kwenye maisha yetu, kuanzia kwetu wenyewe na hata kwa wale wa karibu yetu, suluhisho ni moja, tunapaswa kujifunza na kujua asili ya binadamu. Kwa sababu ni uelewa huo pekee utakaotuwezesha kujijua wenyewe, kujua uimara na udhaifu wetu na kupiga hatua. Pia tutaweza kuwajua wengine vizuri, kuelewa uimara na udhaifu wao, kuwajua mapema watu ambao ni matatizo na hata kuona vitu ambavyo watu wanaficha tusione.

Mwandishi Baltasar Gracian amewahi kunukuliwa akisema, watu wanatumia muda mwingi kujifunza tabia za wanyama na mimea, badala ya kutumia muda huo kujifunza tabia za binadamu ambao wanaishi nao kila siku! Kama anavyotuambia Baltasar, tukiweka nguvu zetu katika kujifunza tabia za watu, tutaweza kuwa na maisha bora na mahusiano mazuri na wengine.

Kwenye kitabu chake cha 48 Laws Of Power, Robert Green anasema, mahusiano ya binadamu yanahusisha kusema uongo na kudanganya, anasema kitu pekee kinachotutofautisha sisi binadamu na wanyama wengine ni uwezo wetu wa kusema uongo na kudanganya kwa vitendo.

Kama hivi ndivyo watu walivyo, unaweza kuona ni jinsi gani kutokuijua asili ya binadamu kunavyokugharimu. Hivyo amua leo kwamba utaweka kipaumbele kwenye kujifunza asili na tabia za binadamu, ili ujijue vizuri wewe mwenyewe na uwajue wengine pia.

Na sehemu sahihi ya kuanzia elimu yako ya kuijua asili ya binadamu ni kwenye kitabu hiki cha The Laws of Human Nature.

#2 KITABU CHA JUMA;  SHERIA 18 ZA ASILI YA BINADAMU.

Rafiki yangu mpendwa,

Kama nilivyokueleza hapo juu, juma hili tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kitabu kinachoitwa The Laws of Human Nature ambacho kimeandikwa na Robert Greene. Kitabu hiki kimeshiba kweli kweli, kimechambua kwa kina sana sheria 18 za asili ya binadamu, na kwenye kila sheria kuna mfano wa watu waliotumia au kupuuza sheria hiyo na matokeo waliyopata.

Katika uchambuzi huu, nakwenda kukushirikisha sheria hizi 18 za asili ya binadamu na hatua za kuchukua kwenye kila sheria ili uweze kuwa na maisha bora.

SHERIA YA KWANZA; KUTOKUFIKIRI.

Huwa tunadhani ya kwamba tunadhibiti mwenendo wa maisha yetu, kwa kupanga na kufikiri kila hatua tunayopiga kwenye maisha. Lakini ukweli ni kwamba, hatufanyi maamuzi yetu kwa kufikiri, badala yake tunafanya kwa hisia.

Kwa sehemu kubwa tunaendeshwa na hisia na siyo kufikiri. Tunaweza kujidanganya kwamba tunafikiri, lakini huwa tunafanya maamuzi kwa hisia kwanza kisha baadaye tunayahalalisha kwa kufikiri.

Tunapaswa kuondokana na hali hii ya kuongozwa na hisia na kuanza kufikiri kwa kina kwenye kila maamuzi unayofanya. Tunapaswa kujilazimisha kuona vitu na hali kama zilivyo na siyo kwa jinsi tunavyotaka kuona.

Hili siyo jambo ambalo linakuja kirahisi kwetu sisi binadamu, bali ni jambo ambalo tunapaswa kujifunza na kufanyia kazi. Inawezekana kama tutajipa muda katika kufikiri, kuepuka kufanya maamuzi ya haraka na kuacha kuangalia wengine wanafanya nini.

SHARIA YA PILI; MAJIVUNO.

Huwa tuna tabia ya kujivuna, kujiona sisi ni bora kuliko watu wengine. Hali hii ya majivuno inatofautiana baina ya watu, kuna ambao wanajiona wao ndiyo wa muhimu zaidi kuliko wengine. Tunataka dunia nzima ituzunguke sisi, kila mtu atusikilize sisi na hata tunapokuwa kwenye mazungumzo na watu wengine, tunajisifia zaidi sisi kuliko wengine.

Kwa vyovyote vile, majivuno siyo mazuri kwenye maisha, kujiona sisi ni wa maana na muhimu kuliko wengine kunaharibu mahusiano yetu na watu wengine.

Njia pekee ya kuondokana na majivuno ni kuwa na utu na uelewa kuhusu wengine. Kujua na kuonesha kila mtu ni muhimu na kujali hali na hata maoni ya wengine. Kuacha kujiongelea wewe mwenyewe na kuwapa watu nafasi ya kujiongelea wao pia.

Pia epuka sana wale watu ambao wamezama kwenye majivuno kiasi kwamba hawajali kabisa kuhusu wengine. Hawa ni watu ambao wameshapotea na hawawezi kurudi tena kwenye uhalisia, kuhangaika nao utaishia kuumia mwenyewe.

SHERIA YA TATU; BARAKOA.

Binadamu tuna tabia ya kuvaa barakoa (masks) ambazo zinatuonesha kuwa watu wazuri na wanaojali. Kwa nje tunaonekana ni wastaarabu, waaminifu, na tunaojiamini. Lakini ndani mambo ni tofauti kabisa. Hivi ndivyo binadamu tunavyodanganyana kila siku, hivyo kama utafanya maamuzi kuhusu mtu kwa mwonekano wa nje, jua utaishia kufanya makosa makubwa kwenye maisha yako. Kile unachoona nje, siyo uhalisia wa mtu, bali sanamu ambayo mtu ameitengeneza uione.

Jifunze kuona nyuma ya sanamu ambazo watu wamevaa, jifunze kuangalia zaidi ya mwonekano wa nje. Kwenye kila sanamu ambayo mtu amevaa, kuna ufa ambao unaonesha uhalisia wa mtu huyo. Watu huwa wanaonesha matendo na hisia zao kwa njia ambayo siyo ya moja kwa moja. Kama utakuwa makini utaweza kuona kile ambacho watu wanaficha.

Kwa upande wa pili, kwa kuwa watu wanakuhukumu kwa mwonekano wako wa nje, basi unapaswa kujijengea mwonekano ambao ni bora. Jijengee mwonekano ambao utaleta kuheshimika na kuaminika kwa wale unaotaka wafanye hivyo. Lakini usifanye hivyo kwa kudanganya tu, bali fanya ikusaidie katika kuboresha mahusiano na ushirikiano na wengine.

SHERIA YA NNE; TABIA.

Unapochagua mtu wa kushirikiana naye kwenye jambo lolote, ni rahisi sana kushawishika na maneno na mwonekano wa mtu. Lakini vitu hivyo ni rahisi kukudanganya na kukupoteza. Watu wanaweza kuahidi na kujisifia watakavyo, wanaweza kutengeneza mwonekano mzuri wa nje na ukakushawishi sana.

Kuujua ukweli kuhusu watu ili uweze kufanya maamuzi ya kushirikiana nao, angalia tabia za watu, hasa tabia za nyuma. Angalia mwenendo wao wa maisha, mambo ambayo wamewahi kukamilisha na waliyowahi kushindwa. Angalia kipindi ambacho wamekutana na magumu, waliwezaje kuyavuka. Angalia mahusiano yao ya nyuma na watu wengine.

Tabia za mtu za nyuma zinamweleza yeye kwa ukweli kuliko sifa anazokuambua kwa mdomo. Hili ni muhimu sana kuzingatia pale unapochagua mtu wa kumwajiri au kuajiriwa naye, pia unapochagua mtu wa kufanya naye biashara. Mfano kama mtu anakuambia ni mchapa kazi, lakini ukiangalia kwenye historia yake ya nyuma alishafukuzwa kazi maeneo matatu tofauti, haijalishi atakupa sababu gani, ana tatizo.

Tabia za watu huwa zinajirudia, na huwa zimejichimbia ndani kabisa kwenye mfumo wao wa maisha, hivyo kabla hujafanya maamuzi kuhusu mtu, angalia kwanza tabia zake, kwa yale yanayoonekana na siyo anayokuambia.

SHERIA YA TANO; TAMAA.

Kanuni kuu ya uchumi ni hii, kadiri kitu kinavyokuwa kigumu kupatikana, basi thamani yake inakuwa kubwa zaidi. Hivi ndivyo binadamu tulivyo, huwa tunathamini sana kile ambacho tunajua hatuwezi kukipata kwa urahisi. Ndiyo maana vitu vinavyopigwa marufuku ndiyo vinakuwa na thamani kubwa na watu wanakuwa tayari kuvipata kwa gharama kubwa.

Tumia sheria hii katika kuongeza thamani yako binafsi na ya kazi au biashara yako. Kwenye thamani yako binafsi jifunze kutokuonekana sana na kutokupatikana kirahisi. Kama watu wanajua unapatikana muda wowote na kwa urahisi, hawakuthamini sana. Lakini wanapojua kwamba upatikanaji wako ni mgumu, watakuthamini zaidi. Hata pale wanapoweka mipango, wataanza kukuuliza kwanza kabla hawajapanga. Lakini unapopatikana kirahisi, wanapanga na kukupa taarifa.

Kwenye kazi na biashara yako, toa huduma ambayo hakuna mwingine anayeweza kuitoa, ambayo watu wanaipata kwako tu, na watu watathamini sana kile unachofanya. Zalisha thamani kubwa sana kiasi kwamba hata wale wanaoshindana na wewe wanaacha kushindana na badala yake wanakusifia.

SHERIA YA SITA; UPOFU.

Ni kawaida kwa sisi binadamu kuona kile ambacho kipo mbele yetu kwa wakati husika, lakini kushindwa kuona kile kilicho mbele zaidi kwa wakati ujao. Ndiyo maana watu hawawezi kuweka akiba ya muda mrefu, kwa sababu wanaangalia zaidi raha ya sasa kuliko furaha ya baadaye.

Tabia hii ya upofu, ya kuona pale ulipo na kutokuona mbele imekuwa chanzo cha matatizo makubwa sana kwa wengi. Ukiacha hilo la kushindwa kujiwekea akiba na hata kuwa na malengo, utapeli mwingi huwa unafanywa kwa wale ambao hawawezi kuona mbele. Ukiangalia mambo mengi ambayo watu wanatapeliwa nayo, ni tamaa ya kupata matokeo ya haraka sasa, bila ya kujiuliza madhara ya baadaye.

Kuepuka kutapeliwa na hata kutengeneza matatizo kwenye maisha yako, ondokana na upofu ambao unao. Acha kuangalia sasa na muda mfupi, angalia muda mrefu ujao. Kila unachotaka kufanya sasa, angalia madhara yake kwa muda mrefu ujao.

Pia jiwekee malengo ya muda mrefu, ambayo utayagawa kwenye muda mfupi. Kila mara jikumbushe malengo hayo, na kabla hujafanya kitu chochote kipya, jiulize kwanza kama kinachangia wewe kufikia malengo yako.

SHERIA YA SABA; KUJIHAMI.

Ni asili ya binadamu kutaka kuona na kuamini kwamba anayaendesha maisha yake kwa maamuzi na machaguo yake mwenyewe. Hivyo huwa tuna tabia ya kujihami pale tunapogundua kwamba kuna watu wanatulazimisha tufanye maamuzi fulani. Mfano pale ambapo watu wanatulazimisha tubadili tabia zetu, ndiyo tunahakikisha tunaziimarisha ili tusionekane sisi ni dhaifu kwenye maisha yetu.

Hivyo kama unataka watu wachukue hatua fulani, kama unataka watu wabadilike, njia pekee ya kufanya hivyo ni kuwafanya waone wamechagua kufanya hivyo wenyewe na siyo kulazimishwa na wengine. Wafanye waone wanafanya maamuzi kwa maoni yao wenyewe na wataondoa kabisa hitaji la kujihami.

Njia za kukuwezesha kufikia hilo ni kuwa msikilizaji mzuri, kuwasifia watu kwenye yale maeneo ambayo wako vizuri na kuwafanya wajiamini, hasa kwenye yake maeneo ambayo hawajiamini. Ukiweza kuwapa watu hali ya kujiona wanafanya maamuzi wenyewe, wataondokana na hali ya kujihami na wataweza kufanya kile unachotaka wafanye, bila ya kuwalazimisha.

SHERIA YA NANE; MTAZAMO.

Kila mmoja wetu anaiona dunia siyo kama ilivyo, bali kama alivyo yeye. Tunaweza kusema tunaiona dunia kupitia miwani ambayo ina rangi fulani, hivyo tunachoona siyo rangi ya dunia, bali rangi ya miwani tuliyovaa. Miwani ambayo kila mmoja wetu amevaa ni mtazamo ambao tunao.

Mtazamo ulionao ndiyo unakufanya uione dunia jinsi unavyoiona. Kama tuna mtazamo wa hofu na kushindwa, tutaona nafasi za kushindwa kwenye kila tunachokutana nacho. Lakini kama tuna mtazamo wa kujiamini na kufanikiwa, tutaona nafasi za kufanikiwa kwenye kila jambo.

Unapaswa kuujenga mtazamo unaoendana na yale maisha ambayo unayataka, kuacha kujihujumu mwenyewe kwa mitazamo uliyonayo sasa na kutengeneza mtazamo unaokufanya uone kile unachotaka.

Jijengee mtazamo chanya, mtazamo wa kujiamini, mtazamo wa inawezekana na mtazamo wa mafanikio, na kwenye kila jambo utaona njia ya kufanikiwa.

SHERIA YA TISA; UKANDAMIZAJI.

Kwa asili sisi binadamu tuna nafsi zaidi ya moja. Hii tunayoonekana nayo kwa nje ni moja ya nafasi nyingi tulizonazo. Huwa tuna tabia ya kuipa nafsi moja nafasi ile ambayo tunataka kuonekana nayo, na kukandamiza nafsi nyingine ambazo hatutaki zionekane. Lakini hili limekuwa na madhara makubwa kwetu, zile nafsi ambazo tunazikandamiza zisionekane, huwa hazifi, badala yake zinakuwa na nguvu zaidi, na zinapopata nafasi ya kujionesha, zinakuja zikiwa na nguvu kubwa zaidi.

Hapa ni pale unapofikiri unajijua vizuri au unamjua mtu vizuri, lakini anapokutana na changamoto kubwa anabadilika kabisa, anafanya mambo ambayo hukutegemea afanye. Jua hapo ile nafsi ambayo imekuwa inakandamizwa imepata nafasi ya kujionesha. Wengine wanaweza kusema kila mtu ana shetani au mzimu ndani yake, kwa jinsi ambavyo nafsi hizi zina nguvu.

Ili kuepuka kukutana na madhara ya kukandamiza nafsi zako nyingine, tambua kila nafsi iliyopo ndani yako na ijumuishe kwenye nafsi yako kuu na utakuwa na nafsi yenye nguvu sana. Angalia kila hisia iliyopo ndani yako, hisia za hasira, hisia za wivu, chuki, tamaa na nyingine, hizi zinawakilisha nafsi nyingine iliyopo ndani yako. Badala ya kukandamiza hisia hizi, ona ni kwa namna gani unaweza kuzitumia kwa upande chanya.

SHERIA YA KUMI; WIVU.

Ni asili yetu binadamu kujilinganisha na wengine hasa wale ambao ni wa karibu kwetu, ndugu, wafanyakazi wenzetu na wengine wanaotuzunguka. Kwa baadhi hali hii inaleta hamasa ya kupiga hatua zaidi, lakini kwa wengine hali hii inazalisha hisia za wivu. Huwa tunaona wale waliofanikiwa kuliko sisi ni kwa sababu wana bahati, au hawajakutana na magumu tuliyokutana nayo sisi, au wamependelewa na sababu nyingine kama hizi. Ni vigumu sana kukubali kwamba wale tulioanza nao na wakafanikiwa kuliko sisi wamefanya hivyo kwa juhudi zao.

Unapaswa kuondokana na hisia hizi za wivu, kwa kuacha kujipa sababu za wengine kufanikiwa, badala yake angalia kile walichofanikiwa na pata hamasa ya kufanikiwa zaidi. Muhimu ni usijilinganishe, unapowaangalia wengine, waangalie kwa lengo la kujifunza na siyo kujilinganisha, hakuna anayeweza kulingana na wewe.

Kitu kingine epuka sana kuibua wivu kwa wengine, kuwa mwangalifu pale unapojisifu kwa mafanikio yako. Siyo kila mtu atafurahia mafanikio yako, wengi wanaweza kukuchekea na kukupongeza, lakini kwa ndani wanaumia na wakafanya kitu cha kukukwamisha au kukurudisha nyuma. Usiwe mtu wa kuimba mafanikio yako kwa kila mtu, utakaribisha wivu usio na sababu.

SHERIA YA KUMI NA MOJA; UKOMO.

Ni asili yetu binadamu kujisahau pale tunapofanikiwa. Tunapopata mafanikio makubwa tunajiona tuna uwezo mkubwa wa kufanya chochote. Na hii imekuwa sababu ya wengi kushindwa sana baada ya kupata mafanikio kidogo. Mtu anaanzisha kitu kimoja, kinafanikiwa sana na kuanza kujiona anaweza kufanya chochote. Tunasahau kwamba tuna ukomo wa uwezo wetu kwenye vitu gani tunaweza kufanya.

Kingine muhimu zaidi ni kwamba huwa tunaamini mafanikio tunayoyapata ni kwa juhudi zetu wenyewe na hivyo tunaweza kurudia tena kupata mafanikio hayo. Lakini ukweli ni kwamba kuna vitu vingi vinachangia mafanikio yetu, ambavyo haviwezi kujirudia vyote kwa pamoja. Mfano mazingira, hali ya hewa, hali ya uchumi na hata bahati, vina mchango mkubwa kwenye mafanikio unayopata.

Hivyo unapopata mafanikio yoyote, acha kujiangalia wewe kama ndiye chanzo kikuu cha mafanikio na angalia vitu vyote vilivyochochea mafanikio hayo. Pia acha kujiona kwamba unaweza kufanya chochote na ukafanikiwa kwa sababu tu umefanikiwa kwenye kitu kimoja. Kaa kwenye eneo ambalo una uimara na acha kujihusisha na maeneo ambayo huyajui kwa undani na huna uzoefu nayo.

Tumekuwa tunaona sana hili kwenye biashara, mtu anaanzisha biashara moja, inafanikiwa anajiona anajua sana biashara na anaweza kufanikiwa kwenye biashara yoyote, anashawishika kuingia kwenye biashara asiyoijua ila kwa kuwa ina faida kubwa anaona atanufaika kirahisi, na anakwenda kushindwa vibaya.

SHERIA YA KUMI NA MBILI; JINSI.

Binadamu tuna mgawanyiko wa aina mbili na katika makundi mawili. Mgawanyiko huo ni wa jinsi (gender) na jinsia (sex). Kwa mgawanyiko wa jinsia tuna wanaume (male) na wanawake (female), na mgawanyiko huu upo kwenye majukumu ya uzazi baina ya mwanamke na mwanaume. Mgawanyiko mwingine ni wa jinsi, hii ni nafsi ambayo ipo ndani ya mtu, kuna jinsi ya kiume (masculine) na jinsi ya kike (feminine).

Japokuwa mtu anaweza kuwa na jinsi a moja tu, yaani mwanamke au mwanaume, wote tuna jinsi mbili ndani yetu, jinsi ya kike na jinsi ya kiume. Kama wewe ni mwanaume basi ndani yako kuna jinsi ya kike na kama wewe ni mwanamke basi ndani yako kuna jinsi ya kiume. Jinsi ambayo tunajulikana kwayo ni ile ambayo inatawala nafsi yetu kwa ujumla, lakini haimaanishi ile jinsi nyingine haipo. Na ukitaka kuona hili vizuri, ukiangalia utaona kuna wanawake ambao wana tabia za kiume na wanaume ambao wana tabia za kike zaidi. Hivyo ndivyo jinsi inavyofanya kazi.

Unachopaswa kufanya ni kutambua jinsi ya pili iliyopo ndani yako, ambayo umekuwa unafanya kazi kubwa ya kuikandamiza, na kuitumia ili uwe bora zaidi. Haimaanishi ujibadili jinsi, badala yake uweke ushirikiano kwenye jinsi zote mbili ulizonazo. Mfano jinsi ya kiume inaamini kwenye matumizi ya nguvu na jinsi ya kike inaamini kwenye ushirikiano. Ukiweza kuweka vitu hivyo kwa pamoja, nguvu na ushirikiano, utaweza kufanya makubwa sana.

SHERIA YA KUMI NA TATU; KUSUDI.

Tofauti yetu binadamu na wanyama ni hii, wanyama wanazaliwa wakiwa tayari wana kusudi la maisha yao, kuishi na kuzaliana, hivyo mazingira yao yanawapa nafasi ya kutimiza kusudi hilo. Lakini sisi binadamu tunazaliwa tukiwa hatujui kusudi la maisha yetu, kipindi chote cha utoto tunawategemea wazazi kwa maisha yetu. Lakini tunapofika utu uzima ndipo sasa kila mtu anapaswa kujua kusudi lake na kulifanyia kazi.

Na hili ndiyo zoezi gumu kuliko yote kwetu sisi wanadamu, kwa sababu watu wengi wamekuwa wanaenda maisha yao yote, wasijue kusudi lao ni nini. Wanafanya kile ambacho kila mtu anafanya lakini mwisho wa siku hawajisikii ukamilifu ndani yao. Wanajaribu mambo mengi kwenye maisha lakini hawapati ridhiko.

Unapaswa kulijua kusudi la maisha yako, na kupeleka nguvu zako zote kwenye kufikia kusudi hilo. Kadiri unavyojua kusudi hili mapema na kuacha kupoteza muda, ndivyo unavyoweza kuwa na maisha bora.

Katika kutambua kusudi lako, kwanza jua wewe ni wa kipekee, hakuna anayefanana na wewe na hivyo hakuna anayeweza kukuambua kusudi lako ni lipi. Pili angalia ni vitu gani vinakupa msukumo mkubwa kutoka ndani yako, vitu ambavyo unavijali hasa na kuwa tayari kuvifanya hata kama hakuna anayekulipa. Hapo ndipo kusudi lako lilipo, ifanye kuwa kazi ya maisha yako na weka juhudi zako zote kwenye kufanyia kazi kusudi lako.

SHERIA YA KUMI NA NNE; KUIGA.

Huwa tunafikiri kwamba tunafanya maamuzi yetu wenyewe, lakini uhalisia ni kwamba huwa tunaathiriwa sana na wengine. Tunapokuwa ndani ya kundi lolote lile, maamuzi yetu yanaathiriwa na kundi hilo. Kwa kifupi tunapokuwa ndani ya kundi huwa tunaiga yale ambayo watu wengine kwenye kundi hilo wanafanya.

Na kuona hili kwa vitendo, tembelea maeneo ya kazi au biashara, utagundua maisha ya watu wanaofanya kazi au biashara pamoja yanafanana sana. Hata maisha nje ya kazi hizo, bado yanakuwa hayatofautiani. Hii ni kwa sababu maamuzi ya wengine kwenye kundi yanatuathiri sana, na tunajikuta tukiamini na kufanya kile ambacho wengine kwenye wanafanya.

Jukumu lako ni kuhakikisha huruhusu kundi lolote ulilopo kuathiri fikra na maamuzi yako. Kuwa ndani ya kundi, lakini inapofikia kufanya maamuzi fikiria nje ya kundi hilo. Kwa kufanya hivi, utaweza kufikia maamuzi bora kwako na siyo kuiga kundi.

SHERIA YA KUMI NA TANO; UONGOZI.

Ni asili ya binadamu kupenda kuongozwa, tangu enzi na enzi tumekuwa na mifumo mbalimbali ya uongozi, kuanzia kwenye familia, ukoo, kabila, ufalme nchi na mpaka dunia. Binadamu huwa hatujiamini sisi wenyewe, hivyo huwa tunatafuta mtu wa kumwamini atuongoze. Pale ambapo tumefika njia panda na hatujui nini cha kufanya, tunamwangalia kiongozi kama mwongozo wetu.

Hivyo kama unataka kuwa kiongozi bora kwenye maisha yako, unapaswa kujua hitaji hili la watu la kuongozwa.

Majukumu makuu unayopaswa kuyafanyia kazi kama kiongozi ni kuwa na maono makubwa, kuweka mbele vipaumbele vya wengine na kuimarisha ushirikiano baina ya watu.

Majukumu hayo ni magumu kwa sababu kama kiongozi huwezi kumridhisha kila mtu, lakini pale unapojiamini kama kiongozi na kuwa na msimamo wengi watakuheshimu. Wapo watakaokuchukua na kutoka kukuona ukianguka, lakini inapofanyia kazi majukumu hayo makubwa wanakuheshimu zaidi.

Elewa hitaji hili la binadamu kuongozwa na kuwa kiongozi bora popote unapokuwa.

SHERIA YA KUMI NA SITA; SHARI.

Ni asili yetu binadamu kutaka kupata kile tunachotaka, kwa namna yoyote ile. Kama tutakikosa kwa njia za kawaida basi tutajaribu kukipata kwa njia za shari. Kila mmoja wetu ana hali ya ushari ndani yake, hali ya kuwa tayari kutumia nguvu kupata kile ambacho anataka. Katika jamii zetu, watu huficha ushauri wao kwenye mwonekano na tabia za nje. Mfano mfanyabiashara anaweza kuonekana anajali sana wateja na hata kutoa misaada, lakini anawaumiza sana wengine kwenye kufanya biashara yake.

Tunapaswa kutambua hali hii ya ushari ndani yetu na kuigeuza kuwa nguvu yenye manufaa. Kuepuka kuwaumiza wengine pale ambapo tunakazana kupata kile tunachotaka.

Pia tunapaswa kuelewa ushari ulio kwa wengine, hasa wale ambao wanaficha ushari kwa mwonekano laini unapoingia kwenye maeneo yao unakoma. Kuna watu kwa nje ukiwaona unawaona watakatifu sana, lakini utakapoingia kwenye anga zao ndiyo utajua kwamba ni watu washari na wakatili sana. Watu hawa kwa kiingereza wanaitwa PASSIVE AGGRESSIVE. Jamii zetu kwa sasa zimejaa watu wa aina hii, unapaswa kuwatambua haraka na kujiepusha nao, kwa sababu ukishaingia kwenye anga zao, hawatakuacha salama.

SHERIA YA KUMI NA SABA; VIZAZI.

Dunia inaenda kwa mzunguko wa vizazi, na hivyo watu kwenye jamii wanatofautiana kulingana na rika na vizazi vyao. Katika kila wakati, tangu kuwepo kwa binadamu hapa duniani, wazee wamekuwa wanalaumu vijana, utasikia kauli kama vijana wa siku hizi hawafai, hawana maadili yetu. Vijana hao nao wakifikia uzee wanalaumu vijana wanaokuja.

Tunachopaswa kuelewa ni kwamba kila kizazi kina vitu vyake ambavyo inavijali, na vinatofautiana. Hivyo badala ya kulaumu kizazi kwa vitu inavyojali zaidi, angalia hali ya kizazi husika. Tabia za kizazi zinatengenezwa zaidi na matukio ambayo wanakutana nayo wakati wanafikia ujana. Mfano kizazi cha sasa, ambacho kimefikia ujana wakati wa mapinduzi ya kiteknolojia, kinaonekana kuwa na upungufu mkubwa kwenye mahusiano ukilinganisha na vizazi vya nyuma, lakini hii ni hali ambayo wamekutana nayo. Kadhalika vizazi vinavyokuja vitaonekana kuwa na mapungufu yake.

Unachopaswa kuelewa ni kwamba vizazi vinabadilika, jamii haiwezi kubaki vile ilivyo, kila rika jipya linapofikia ujana linakuja na mambo yake, likifika uzee, wanakuja vijana wengine na mambo yao. Aina ya miziki, mitindo ya nguo, vyakula na hata mahusiano yanatofautiana baina ya kizazi na kizazi.

SHERIA YA KUMI NA NANE; KIFO.

Binadamu ndiyo viumbe pekee ambao tunajua kwamba tutakufa, tunajua kwamba haya maisha tuliyonayo kuna siku yatafika tamati, kwa wengi hatujui ni lini, lakini uhakika ni kila mtu atakufa. Cha kushangaza, sisi binadamu tumekuwa tunaendesha maisha yetu tukikwepa kukikabili kifo. Tunaishi kama vile tutaishi milele, hatufikirii kwamba leo inaweza kuwa siku yetu ya mwisho. Kwa kupweka kukikabili kifo, tunapoteza muda kwenye mambo yasiyo muhimu, tunaahirisha kufanya mambo na kuchelewa kuchukua hatua tukiona muda upo wa kutosha.

Unapaswa kukikabili kifo kila siku, unapaswa kujikumbusha kwamba muda pekee ulionao ni sasa, na huenda leo ikawa siku yako ya mwisho. Kwa kujikumbusha hivi, utaweka juhudi zako kwenye yale muhimu, hutaahirisha lolote na chochote unachopanga utakikamilisha kwa haraka.

Wale wanaokutwa na magonjwa ambayo yana muda mfupi wa maisha kama saratani, huwa wanapata nguvu kubwa ya kufanya yale muhimu kwenye maisha yao. Zipo hadithi za watu walioambiwa wana miezi sita tu ua kuishi, na ndani ya miezi hiyo sita wakafanya makubwa kuliko walivyofanya kwa miaka zaidi ya 30 au 40 waliyoishi.

Tumia nguvu hiyo kubwa iliyolala ndani yako kwa kujikumbusha kwamba kifo unatembea nacho na utaweza kufanya makubwa sana kwa muda mfupi.

Rafiki, hizi ndizo sheria 18 za asili ya binadamu, sheria ambazo unapaswa kuzielewa vizuri na kuzitumia kwenye kila siku ya maisha yako. Kama ambavyo umejifunza, sheria hizi zinakuhusu wewe na wale ambao unajihusisha nao kila siku. Kadiri unavyozielewa na kuziishi, ndivyo maisha yako yanakuwa bora na mahusiano yako na wengine kuwa vizuri.

#3 MAKALA YA JUMA; HATUA 3 ZA KUTAWALA HISIA ZAKO.

Rafiki,

Sisi binadamu ni viumbe wa kihisia, sehemu kubwa ya maamuzi yetu tunayafanya kwa kusukumwa na hisia. Lakini kama ilivyo kwenye mambo mengi, tumekuwa tunajidanganya kwamba tumefikia maamuzi yetu kwa kufikiri. Kumbe ambacho tunafanya ni tunafikia maamuzi kwa hisia, halafu tunayahalalisha kwa kufikiri.

Kama unataka kufanya maamuzi bora kwenye maisha yako, ambayo yatakuletea matokeo bora, lazima uweze kutawala hisia zako na kufikiri kwa kina.

Kwenye makala ya juma, kutoka kwenye kitabu cha Laws of human nature, nimekushirikisha hatua tatu za kukuwezesha kutawala hisia zako, kufikiri kwa kina na kufanya maamuzi sahihi. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hiyo, isome sasa hapa; Hatua Tatu Za Kukuwezesha Kutawala Hisia Zako Na Kufikiri Kwa Usahihi Ili Kuepuka Kufanya Maamuzi Mabovu. (https://amkamtanzania.com/2019/04/12/hatua-tatu-za-kukuwezesha-kutawala-hisia-zako-na-kufikiri-kwa-usahihi-ili-kuepuka-kufanya-maamuzi-mabovu/)

Hakikisha unasoma makala hiyo na kufanyia kazi yale unayojifunza ili uweze kuboresha ufanyaji wako wa maamuzi. Kwa sababu ukishatetereka kwenye maamuzi, mengine yote yanaanguka.

#4 TUONGEE PESA; HISIA NA FEDHA HAVIENDANI.

Mwaka 1719 mfanyabiashara wa Uingereza, John Blunt (1665–1733), ambaye alikuwa mmoja wa wakurugenzi wa kampuni iliyoita South Sea Company alikuwa akifikiria njia ya mkato ya kupata fedha nyingi zitakazomwezesha kuwa milionea kwa ulaya nzima kwa kipindi hicho. Alipata wazo, serikali ya Uingereza ilikuwa na deni kubwa ambalo haiwezi kulipa. Hivyo akaja na mpango wa kampuni yake kununua deni hilo la nchi, kisha nchi kuwa inailipa kampuni hiyo riba. Watakachofanya wao kama kampuni ni kuligeuza deni hilo kuwa hisia na kuuza kwa wananchi.

Wenye uelewa wa mambo ya fedha na sheria za uchumi waliona udhaifu kwenye mpango huo, lakini kwa ushawishi wa Blunt pamoja na uhitaji mkubwa wa serikali kuondokana na deni hilo, walikubaliana na mpango huo. Basi mchakato ulifanyika na deni likageuzwa kuwa hisa na kuanza kuuzwa kwenye siko la hisa la London. Kwa ushawishi wake mkubwa na kutoa matarajio makubwa ya baadaye, watu wengi walikimbilia kununua hisa hizo. Hisa zilianza kuuzwa kwa bei ya euro 100 kwa hisa moja, lakini ndani ya mwezi mmoja bei ilikuwa imekua mara mbili, kufika euro 200 kwa hisa.

Mmoja wa watu waliochangamkia fursa hii ya uwekezaji ni mwanasayansi Isaack Newton, aliweza kununua hisa za thamani ya euro 7,000 lakini baada ya kufikiria kwa kina, aliona kampuni hiyo haina uzalishaji wowote wa kulipa hisa hizo, bali ulikuwa ni mchezo wa upatu. Hivyo baada ya wiki chache aliuza hisa zake na kupata euro 14,000 mara mbili ya kiasi alichowekeza.

Lakini muda uliendelea kwenda na bei ya hisa ilizidi kupanda, ikafikia mpaka euro 400 kwa hisa moja. Newton alishawishika kwa ukuaji huu na kuwekeza euro 20,000 lakini muda mfupi baadaye kampuni hiyo ilivunjika na kusababisha hasara kubwa kwa wengine, ikiwepo yeye Newton kupoteza fedha zake. Baada ya hili, Newton alisema ‘I can calculate the motion of heavenly bodies, but not the madness of people’ akimaanisha anaweza kukokotoa mienendo ya sayari mbalimbali lakini siyo ukichaa wa watu.

Tunaona jinsi ambavyo hisia zilimwingiza mwanasayansi na mmoja wa watu wenye akili sana kuwahi kuwepo hapa duniani, ambaye ametupatia sheria tatu za mwendo ambazo ndiyo zinatumika kwenye maeneo mbalimbali. Lakini aliporuhusu hisia kumtawala katika kufanya maamuzi ya fedha zake, alipata hasara.

Tukiangalia kwenye mambo yote ambayo watu wanapata hasara kwenye fedha, chanzo kimekuwa ni kuruhusu hisia zitawale maamuzi tunayofanya. Hata michezo mbalimbali ya upatu ambayo imewapa hasara wengi, ukiiangalia kwa kufikiri kawaida unaona kabisa ina shida. Lakini unapoona wengine wanapata faida, unaweka akili pembeni na kwenda kwa hisia zako.

Kama kitu siyo sahihi, hupaswi kufanya, haijalishi kama kila mtu anafanya au wapo wanaopata faida. Siyo sahihi, ni swala tu la muda kabla hakijaanguka. Hivyo mara zote tumia fikra zako na weka hisia pembeni inapokuja kwenye maamuzi ya fedha zako.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; WANACHOONESHA WATU NDIYO WALICHOKOSA.

“When people overtly display some trait, such as confidence or hypermasculinity, they are most often concealing the contrary reality.” ― Robert Greene

Ipo kanuni rahisi sana ya kujua  kile ambacho watu wanakificha, ambacho ndiyo udhaifu wao. Kanuni hiyo ni kuangalia kile ambacho watu wanalazimisha kuonesha kwa nje.

Ukiona mtu analazimisha kuonekana anajiamini sana basi jua hiyo hajiamini. Ukiona mtu anajilazimisha kufurahi basi jua ana huzuni. Ukiona mtu anakazana kuonekana kwa nje kwamba ni tajiri basi jua ni masikini.

Binadamu tuna tabia ya kuficha madhaifu yetu kwa kulazimisha kinyume chake kwa nje, lakini hii ni njia ya kujihami na kudanganya wengine.

Hii pia itakusaidia sana kujua wakati watu wanadanganya, kwa mfano kwa watu wako wa karibu, wale ambao unazijua vizuri tabia zao, unapoona ghafla wanakazana kuonesha tabia ya tofauti, jua kuna kitu wamefanya na wanajaribu kukuficha. Kama tulivyojifunza, watu wanaweza kuficha siri wasiiseme kwa maneno, lakini miili yao haiwezi kuficha siri kabisa. Ukiwa mwangalifu utaona jinsi mwili wa mtu unavyojaribu kueleza kila kinachoendelea.

Rafiki yangu mpendwa, nina imani umekuwa mwanafunzi mzuri wa asili ya binadamu, umeanza kupata mwanga wa uimara na udhaifu uliopo ndani yako, umeanza kuona kwa nini baadhi ya watu wanafanya mambo ambayo huyaelewi au hukuyategemea. Wito wangu kwako rafiki ni uendeleze hili, endelea kujifunza asili na tabia za binadamu, maana ndiyo elimu itakayokuwezesha kuwa na maisha bora na kuwa na mahusiano mazuri na wengine pia.

Karibu kwenye channel ya TELEGRAM ya TANO ZA JUMA ambapo nitakushirikisha mafunzo na mifano zaidi kuhusu ASILI YA BINADAMU. Kama bado hujajiunga na channel hii, maelekezo ya kujiunga yako hapo chini. Chukua hatua sasa ili uweze kujijua wewe mwenyewe na kuwajua wengine pia.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu