Sikiliza hapa;

Rafiki yangu mpendwa,

Leo nakuwa mganga wako, ambaye nakupa dawa ya uhakika ya kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Ukifanyia kazi dawa ninayokupa, mafanikio makubwa yanaenda kuwa kitu cha uhakika kwako.

Hiatakuwa kama utafanikiwa au la, bali itakuwa lini utafanikiwa. Yaani mafanikio makubwa yanakuwa uhakika, ni swala la muda tu.

Lakini kama unavyojua, dawa za waganga huwa zina masharti. Na kadiri unavyotaka matokeo makubwa, ndivyo pia masharti yanakuwa makali.

Na hii dawa ninayokupa ya mafanikio makubwa, ina sharti moja kubwa. Sharti hilo ni lazima utoe kafara. Na kafara unayotakiwa kutoa ni ya uhai.

Kabla hujafikiria nani wa kumtoa kafara, ili upate mafanikio makubwa unayotaka, nikuambie tu wazi, mtu huyo ni wewe mwenyewe.

Unashangaa siyo, kwamba ili ufanikiwe unatakiwa kutoa kafara ya uhai, halafu tena kafara hiyo ni wewe mwenyewe! Ndiyo, ni sahihi kabisa, kwa sababu hiyo ndiyo kafara pekee inayoweza kukupa mafanikio makubwa unayotaka kuyapata.

Imetosha sasa kwenye uganga kwa leo, sasa turudi kwenye sayansi ya mafanikio, eneo ambalo nimebobea kukuongoza vyema wewe rafiki yangu.

Ili upate mafanikio makubwa, ni lazima ufanye mambo makubwa, ya tofauti na ambayo ni hatari. Mambo hayo unayopaswa kufanya, wengi wa wanaokuzunguka hawajawahi kufanya na wala hawathubutu kufanya.

Kwanza utahitajika kufanya kazi kubwa, na ngumu na kwa muda mrefu kuliko ilivyozoeleka. Wakati wengine wanafanya kazi masaa 8 kwa siku kwa siku 5 za wiki, wewe unalazimika kufanya kazi masaa 16 kwa siku, siku 7 za wiki. Kwa hakika hilo halijakaa kiafya kabisa.

Utalazimika kusimamisha kabisa maisha yako ya kijamii uliyozoea. Huwezi kuendelea kuwa kwenye kila kikundi ambacho upo sasa, kwenye kamati mbalimbali, kuhudhuria kila sherehe, kuwa shabiki wa mpira na mengine mengi. Maisha yako yatamezwa na kile unachofanya, kwa sehemu kubwa sana. Sehemu kidogo itakayobaki itakuwa kwa ajili ya familia yako. Hilo halitakuweka kwenye hali ya mahusiano mazuri na watu wengine.

Watu wote wanaokuzunguka watakuambia maisha uliyochagua ni ya hatari. Utaharibu afya yako kwa uchovu na msongo. Utakufa mapema kwa kufanya kazi sana bila mapumziko. Utakuwa mpweke na kupata sonona.

Yote watakayosema ni ya kweli kabisa, wanakuwa sahihi. Na ndiyo maana nimekuambia lazima utoe kafara, na kafara hiyo ni wewe mwenyewe.

Tukirudi kwenye sayansi yetu ya mafanikio, hebu tuuangalie ukweli. Njia ya mwisho ya kila mtu hapa duniani ni nini? Sote tunajua kwamba wote njia yetu ni kifo. Kwa hiyo kila mtu atakufa. Na kuna kitu ambacho kitamuua mtu.

Wapo watakaokufa kwa ajali. Wapo watakaokufa kwa magonjwa. Na wapo watakaokufa kwa uzee. Kuna ubaya gani kwa wewe kuchagua kufa kwa kile kikubwa unachofanya ili kuacha alama kubwa hapa duniani?

Kwa kuwa kifo hakiepukiki, basi ni vyema kuchagua kufa kishujaa kwako. Kwa kufanya mambo ambayo ni hatari, lakini matokeo yake ni makubwa kwenye maisha yako.

Kila kitu kwenye maisha yetu ni hatari. Kuwa hai ndiyo hatari kubwa kwenye maisha, unaweza kufa muda wowote. Huongezi hatari yoyote kwa kuchagua kupeleka maisha yako yote kwenye kile ambacho kitakupa mafanikio makubwa.

Kwenye #BaruaYaKocha nimeshirikisha mahojiano ya mwanzilishi mmoja wa biashara anayefanya kazi siku saba za wiki na kuishi kwenye biashara yake masaa 24. Alipoulizwa achague kati ya kampuni yake kupata mafanikio makubwa sana na afe akiwa na miaka 50 au kampuni yake ishindwe na aishi mpaka miaka 80, alijibu kitu cha kushangaza sana.

Kujua majibu ya mwanzilishi huyo na jinsi ya kuyatumia kwenye safari yako ya mafanikio, karibu uisome barua hapa; #BZK009; Mafanikio Makubwa Ni Kuchagua Kwa Usahihi Kitakachokuua.

Rafiki, kamwe usijizuie kufanya mambo yatakayokupa mafanikio makubwa kwa sababu yana hatari ya kupelekea kifo cha haraka kwako. Kwa vyovyote vile utakufa, ni bora ukafa umefanya mambo makubwa kuliko kuishi maisha duni.

Haya yote hayamaanishi uharakishe kifo chako. Bali usiogope kuchukua hatua kubwa kwa hofu ya kifo. Uzuri ni kwamba, hata kwa kufanya hayo hatari, bado haitaharakisha sana kifo chako ukilinganisha na usingefanya.

Huna kikubwa cha kupoteza, huku ukiwa na kikubwa cha kupata kama utachagua kufanya makubwa kwenye maisha yako.

Kocha