Sikiliza hapa;
Rafiki yangu mpendwa,
Mafanikio ni mchezo mmoja mkubwa sana, ambao una washiriki wengi, lakini wachache sana ndiyo wanaopata ushindi. Na hao wanaopata ushindi siyo kwa sababu wamepata upendeleo fulani, bali kwa sababu wanaijua kanuni ya ushindi ya mchezo wa mafanikio.
Kila mchezo una kanuni zake, ambazo mtu lazima azizingatie ndiyo aweze kupata ushindi. Cha kushangaza, watu wengi wanashiriki kwenye mchezo wa mafanikio bila kuzijua kanuni zake. Matokeo yake ni wanahangaika sana, lakini wanajikuta wamebaki pale pale.
Kwenye barua hii nakwenda kukushirikisha kanuni rahisi sana ya mchezo wa mafanikio, kanuni inayoonyesha wazi jinsi ambavyo kila mtu anaweza kufanikiwa. Japo, mwisho wa siku ni wachache wanaofanikiwa kweli, kwa sababu ndiyo wanaojua na kuifanyia kazi kanuni hiyo.
Matumaini yangu ni wewe rafiki yangu utaipokea kanuni hii na kuifanyia kazi kwa uhakika, ili uweze kuyabadili maisha yako kwa namna ambavyo umekuwa unapanga kwa muda mrefu.

1. Tiketi Ya Kuingia Kwenye Mchezo Ni Kuwa Tayari Kuweka Kazi.
Kama ilivyo kwenye michezo mingine, ni lazima upite hatua za kufuzu kuingia kwenye mchezo husika. Kwenye mchezo wa mafanikio, wengi hata hawajafuzu kuingia kwenye mchezo, hivyo wamebaki kuwa mashabiki, wakikosoa wale wanaopambana uwanjani.
Unafuzu kuingia kwenye mchezo wa mafanikio pale unapokuwa tayari kuweka kazi. Unapoanza kuchukua hatua kwenye malengo na mipango ambayo umejiwekea, hapo unakuwa umeingia kwenye mchezo.
Unaweza kuona kigezo cha kufuzu ni kidogo sana, lakini utashangaa jinsi ambavyo watu wengi wanashindwa kufuzu. Hiyo ni kwa sababu watu wengi wanapenda kuweka malengo na mipango, ila hawana utayari wa kuchukua hatua kwenye mambo wanayopanga.
Kwa wewe kuanza kuchukua hatua, unakuwa umejitenga na kundi kubwa la watu ambao wanapanga tu bila kuchukua hatua. Kwa kuendelea kufanya licha ya kukutana na vikwazo na changamoto, unakuwa kweli umedhamiria kupata ushindi.
Wasiofuzu kucheza huwa ni wazuri kwenye ushabiki. Ni wakosoaji wazuri wa wale wanaofanya. Wana ushauri mwingi wa namna gani watu wanapaswa kufanya, ushauri ambao wao wenyewe wameshindwa kuufanyia kazi.
Kama ambavyo kwenye michezo ya kawaida, mashabiki hudhani wanajua vizuri namna mchezaji angepaswa kucheza uwanjani ili ashinde, wakati wao hata uwanjani hawawezi kuingia, ndivyo mchezo wa mafanikio ulivyo. Wale ambao hawapo kwenye mapambano ya kufanikiwa ndiyo huwa wakosoaji na washauri wakubwa kwa wale wanaofanya.
Wajibu wako ni kuwa kwenye uwanja wa mapambanao. Na hujaingia kwenye uwanja huo kwa kubahatisha, unajua nini hasa unachotaka na unakipataje. Weka kichwa chako chini na pambana kupata ushindi. Wanaokukosoa na kukushauri nini unapaswa kufanya, usikubali wakuyumbishe. Kama wanayosema yangekuwa yanafanya kazi, tayari wangekuwa wanayafanyia kazi wao wenyewe.
2. Unawashinda Asilimia 50 Kwa Kufanya Kazi Kwa Juhudi Kuliko Wote.
Kufanya kazi kunakuingiza kwenye uwanja wa mapambano. Ambapo unaenda kukutana na wengine ambao nao wamejitoa kupambana ili kupata ushindi. Hao siyo mashabiki walio nje ya uwanja wakikosoa na kushauri, ni watu ambao tayari wanafanya kama wewe.
Hawa wataonekana kuwa ushindani kwako, wakitishia kuchukua ushindia ambao unaupambania. Kama ni biashara, siyo mashabiki ambao kila siku wanasema watafanya biashara, bali ni ambao wameshaanza kufanya biashara, ambayo na wewe unaifanya. Hivyo wanalenga wateja ambao na wewe unawalenga.
Hilo linakuweka kwenye ushindani, kwa sababu wote mpo kwenye uwanja na mnapambana kupata ushindi. Japokuwa wengi wanaweza kukutisha na kukufanya uone safari ni ngumu, wengi ni wepesi sana kuwashinda.
Unachohitaji ni kuweka tu kazi kwa juhudi kubwa kuliko wote walio kwenye mchezo ambao upo. Hakikisha hayupo mtu mwingine anayesifika kwa kuweka juhudi kubwa kwenye kila unalofanya kama wewe. Wewe unapaswa kuwa ndiyo kipimo cha kuweka kazi kwa juhudi kubwa.
Kwa kuweka tu kazi kwa juhudi, unawashinda asilimia 50 ya watu waliopo kwenye mchezo. Kwani hao, pamoja na kwamba wanafanya, hawajajitoa hasa kuweka kazi kwa juhudi ili kupata ushindi. Wanafanya kwa mapenzi na hobi, au kwa sababu ndivyo walivyozoea kufanya.
Wewe unapoingia na kufanya kwa viwango vya juu, unawapita wengi ambao wanafanya kwa mazoea. Unapoenda hatua ya ziada kwenye kila unachofanya, unakuwa mbele ya wengi ambao hawatimizi hata kiwango cha chini kinachohitajika.
Yaani hata kama wewe ni mgeni kwenye eneo husika, kuweka kazi kuliko wengine wote kutakuweka mbele ya wale ambao wamekuwepo kwenye mchezo huo kwa muda mrefu.
Habari njema ni kwamba kuweka kazi kwa juhudi ni kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wako. Huhitaji kuwa na kitu chochote cha ziada ndiyo uweze kuweka kazi. Ni wewe kuchagua kuweka kazi, kuifanya hiyo kuwa kipaumbele chako cha kwanza na kuachana na usumbufu unaokutoa kwenye mchezo uliochagua.
Usitishwe na ushindani unaouona kwenye mchezo wako, wewe chagua kuweka kazi kwa juhudi kuliko wengine wote walio kwenye mchezo huo na nusu utawaacha nyuma yako.
Kwenye #BaruaYaKocha kuna ngazi nyingine tatu za ziada kwenye kanuni hiyo ya ushindi kwenye safari ya mafanikio. Soma barua hiyo kuzijua ngazi hizo.
Isome barua hapa; #BZK063; Hii Kanuni Inaonyesha Kwa Nini Kila Mtu Anaweza Kushinda, Japo Wachache Tu Ndiyo Wanaoshinda Kweli.