Rafiki yangu Mpendwa,

mtu yeyote akiniambia amejaribu kila kitu ila hajapata matokeo, ndani yangu najiambia anadanganya.

Naweza nisimwambie wazi, lakini hakuna namna naweza kuamini mtu amejaribu kila kitu na asipate matokeo. Hakuna namna.

Ambacho najua ni mafanikio yanataka mtu awe msumbufu sana, awe mkaidi, aliyeshindikana. Ndiyo namna pekee ya kupata matokeo machache ambayo wengi wanayataka lakini hawayapati.

Wewe unadhani kwa nini pamoja na watu wengi kutaka mafanikio makubwa na uwezekano wa kila mtu kufanikiwa, bado ni wachache sana wanaofanikiwa?

Watu watatoa sababu nyingi, lakini iliyo sahihi ni moja tu, anayepata mafanikio ni yule anayeyataka kweli, ambaye hawezi kuzuiwa na chochote.

Sasa hayo si ni maneno mengine tu ya kusema lazima mtu awe mbishi? Agome kabisa kukosa kile ambacho anakitaka.

Kwenye hii #BaruaYaKocha naenda kukufundisha tabia mbaya kidogo, tabia ya ubishi na ukaidi, tabia ya kutaka jambo lako na kutokukubali kuyumbishwa kwa namna yoyote ile. Uko tayari?

1. Mara Zote Kuna Njia.

Ni rahisi watu kusema wanataka mafanikio na wamepambana kuyapata ila wameyakosa. Watakuonyesha vitu ambavyo wamejaribu na hawajapata matokeo. Na hapo wanakuwa wamekubali kwamba wameshindwa.

Lakini unapoangalia kwa karibu, unaona kabisa walichofanya ni kile ambacho wamezoea kufanya, na ambacho kila mtu anafanya. Ni vigumu sana mtu kupata matokeo ya tofauti kwa kufanya kile ambacho amezoea kufanya.

Kwa chochote ambacho mtu anataka kufanya, huwa kuna njia ya kufanya na kupata. Hata kama ni kikubwa na kigumu kiasi gani, njia ipo. Mara nyingi sana njia hiyo huwa siyo ya wazi, lakini ipo. Na yeyote atakayepambana aipate njia hiyo, anaipata.

Ni vile watu siyo wabishi kiasi cha kutosha, wakikutana na ugumu wanaona ndiyo mambo yote yameshindikana hapo. Lakini kama watu watakataa kukosekana kwa njia, lazima njia itafunguka mbele yao.

Unahitaji ubishi kuamini kwamba njia ipo hata kama huioni. Huhitaji ushahidi au uthibitisho wowote kwamba njia ipo, wewe unahitaji kuwa tu mbishi. Kwa sababu kutakuwa na njia au itajitengeneza mpya.

Swala ni hakuna kukubali kuishia njiani, ni kuendelea kwenda, mguu moja mbele ya mwingine. Ni kutafuta njia au kutengeneza njia, hakuna mbadala wa hilo.

2. Kuwa Kiziwi Wa Kuchagua.

Unaweza ukawa umefungua hii barua na kusema; ‘Ah, kuwa mbishi tu, mbona rahisi hiyo!’ Jibu ni siyo rahisi. Maana siyo ubishi huo unaofikiria wewe.

Ubishi ninaokuambia hapa ni wa kubishana na kivuli chako mwenyewe. Sijui kama unaelewa vizuri hapo, lazima uwe na ubishi kwenye vitu ambavyo watu wataona mboka kama havina maana hivi.

Kwa sababu hivyo ndiyo vitu ambavyo vitakupa matokeo makubwa unayoyataka. Vitu vyenye maana ambavyo umehangaika navyo havijakupa matokeo makubwa. Sasa ni wakati wa vitu ambavyo watu watakuambia havina maana.

Moja ya ubishi ninaotaka uwe nao ni wa kuwa kiziwi wa kuchagua. Hapa unachagua baadhi ya maneno ambayo wewe utakuwa huyasikii kabisa. Maneno yoyote ambayo yanakwamisha wewe kupata unachotaka, hayo chagua kutokuyasikia kabisa.

Watu watasema hayo maneno, lakini wewe utakuwa hujayasikia. Ndiyo utakuwa umeyasikia, lakini utaendelea kama vile hujasikia chochote kabisa.

Unaweza kuona hiki ni kitu kidogo, lakini kina nguvu sana. Chukua mfano unamshawishi mteja anunue bidhaa yako, halafu akakujibu kwamba bidhaa yako siyo bora na haitaki. Unajisikiaje? Kama binadamu lazima hilo litakuuma, utaacha kuuza sifa na manufaa ya bidhaa hiyo na kuanza kupinga au kutoa ufafanuzi wa kile kilichosemwa.

Chukua mfano huo huo, unamuuzia mchina, ambaye anakujibu hivyo hivyo kwa kichina, lakini wewe huelewi hata neno moja la kichina. Wakati yeye anakazana kukuambia bidhaa yako ni mbaya na haitaki, wewe unadhani anasema ameipenda na anaulizia bei. Mchina anakazana kukuambia hataki, wewe unakazana kumpa sifa na manufaa.

Katika kueleza kwako, huenda ukataja kitu ambacho kitabadili maamuzi yake, kwa sababu umeendelea kueleza sifa na manufaa, kwa kina zaidi. Lakini pale uliposikia maneno ya kukatisha tamaa, ulihama kutoka kueleza chenye manufaa na kuanza kujitetea.

Hicho ndiyo namaanisha kwenye kuchagua kuwa kiziwi. Sijui utafanyaje, lakini mimi nataka wewe usisikie neno lolote linalokukwamisha kwenye jambo unalotaka. Yaani hata yasemwe maneno gani, wewe baki kwenye programu yako.

Kama umepanga kumshawishi mtu kwenye kitu fulani, na kabla hata hujaanza anakushambulia kwa mambo mbalimbali, hilo halipaswi kubadili chochote kwenye huo mpango wako. Atamaliza kushambulia halafu atashawishiwa. Hata neno moja hujalisikia. Alikuwa anaongea kichina. Sasa anatakiwa asikilize kilicho sahihi.

Unaweza huo ubishi? Unaona kwa nini umekuwa unakwama?

Kuna watu wanajua jinsi ya kukutoa kwenye reli kirahisi. Wanajua kabisa wanachofanya, wanakubadilishia mada ili utoke kwenye kitu ambacho upo. Wewe komaa hapo, usisikie kingine ila kile tu kinachokupa unachotaka.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK098; Mafanikio Yanataka Uwe Mbishi Sana, Hakuna Kinachokuja Kirahisi.